WAZIRI MKUU KUZINDUA MRADI WA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI NAFAKA TANZANIA JUMAMOSI 21 APRILI 2018

April 19, 2018

Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Tarehe 21 Apili 2018 atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kuongeza uwezo wa uhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika dhifa itakayofanyika kwenye viwanja vya Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula zilizopo Mtaa wa Kizota eneo la Viwanda Mjini Dodoma.

Mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 55, ambao ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha Dola milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mikataba ya ujenzi ilianza kutekelewa tarehe 9 Disemba 2017 ambapo Mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) huku msimamizi wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandashi wa habari na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba ameeleza kuwa Mradi huo utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa, ujenzi wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni (Babati)-Manyara, Dodoma, Makambako-Njombe, Mbozi-Songwe, Shinyanga, Songea-Ruvuma, Sumbawanga-Rukwa na Mpanda-Katavi.

Baada ya mradi kukamilika Wakala utakuwa umeongeza uwezo wa kuhifahi kwa 250,000 MT zaidi (vihenge vya kisasa 190,000MT na maghala 60,000 MT) jambo ambalo litakuwa chachu na mafanikio yenye tija katika kuunga mkono Juhudi za utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Kupatikana kwa Mradi huo nchini ni jitihada za Serikali ambazo zitapelekea ukuaji wa uchumi nchini na kuchangia kuwezesha Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya Wakala kuweza kuhifadhi akiba ya Chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura kulinganisha na ongezeko la watu nchini.

Hifadhi ya Chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharula kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 2008 Wakala ulipoanzishwa.

Aidha, Zikankuba alisema kuwa technolojia itakayotumika katika ujenzi wa vihenge vya kisasa, itawezesha Wakala kupunguza gharama za uendeshaji; kuhifadhi chakula kwa muda mrefu zaidi; kupunguza upotevu wa zao la mahindi baada ya kuvuna (posthaverst loss), kuongeza soko la mahindi nchini na kuimarisha usalama wa nafaka inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu (Aflatoxin) kwa mahindi yaliyohifadhiwa. Jitihada hizi zinalenga katika kuimarisha uwezo wa Taifa katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.

WAGONJWA WA KIFUA KIKUU WAKIMBILIA KWA WAGANGA WA KIENYEJI WILAYANI MUHEZA

April 19, 2018
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Muheza, Dr Kassim Enzi akizungumza na waandishi wa habari wilayani Muheza
 Mratibu wa Mtandao wa Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Elimu nchini kutoka Asasi ya (INUKA) Tanzania Gaudance Msuya   akizungumza wakati wa mafunzo ya umuhimu wa jamii kupima magonjwa ya kifua kikuu, Saratani ya Kizazi na Tezi Dume.yaliandaliwa na Asasi hiyo ambayo yanawashirikisha viongozi wa kidini,watu maarufu na watumishi wa halmashauri ya wilaya yaMuheza
 Sehemu ya washiriki kwenye mafunzo hayo
Sehemu ya washiriki kwenye mafunzo hayo

WATAALAMU wa Afya wilayani Muheza Mkoani Tanga wamelazimika kubuni mbinu mbadala za kuwafuata wagonjwa wanaougua kifua kikuu kwa waganga wa kienyeji baada ya asilimia kubwa kuonekana kukimbilia kwenye maeneo hayo kusaka matibabu.

Hatua ya wataalamu hao kuwafuata kwa waganga hao imesaidia kubaini idadi ya wagonjwa wanaougua ugonjwa huo ambapo hivi sasa imefikia asilimia 66 kutoka 30 za mwanzo kabla ya kuanza zoezi la kuwafuata na hivyo kulazimika kupata matibabu kwenye vituo vya afya na hospitali

Hayo yalibainishwa jana na Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Muheza, Dr Kassim Enzi wakati akifungua mafunzo ya uhamasishaji watu kupima afya zao yaliyofanyika jana mjini hapa na kuratibiwa na mtandao wa maendeleo ya wanawake,elimu na watoto nchini (Inuka)

Alisema hatua hiyo imetokana na watu wenye magonjwa hayo kukimbilia kwa waganga wa tiba asili badala ya hospitalini na hivyo kutofahamika kwa hali halisi ya ugonjwa huo.

Aidha alisema waligundua kuwepo kwa TB wilayani Muheza kitakwimu “Tuligundua ilikuwa ikionekana ni ndogo lakini kiuhalisia kuna tatizo kubwa kwa kuwa watu wengi wanaougua wanaenda kwa waganga wa tiba asili badala ya hospitali

Alieleza kuwa baada ya kubaini tatizo hilo wataalamu waliunda timu ambayo inafanyakazi ya kuwafuata waganga wa tiba asili na kutoa elimu ya athari ya TB, maambukizi yake na namna ya kujikinga na kuwaondoa wagonjwa hao na kuwapeleka hospitalini kupata tiba.

Hata hivyo alisema mafanikio yaliyotokana na kampeni hiyo kuwa ni ongezeko la wagonjwa kutoka asilimia 30 ya mwaka 2015 hadi kufikia 66 ya mwaka 2017/018 ambapo ni wagonjwa 443 waligundulika kuugua kati ya 613 waliyopima.

Alieleza kuwa mwaka 2016 waliopima ni wananchi 600 huku waliogundulika kuugua ni 437 ambapo 2017 waliyopima 715 waliyogundulika 463 jambo ambalo linaonekana kuwepo kwa ongezeko la maambukizi hayo.

Katika mafunzo hayo ambayo yalifungulia na mganga mkuu wa Wilaya hiyo, Dr Mathias Abuya iliwashirikisha wadau wa afya wakiwemo watumishi wa halmashauri, viongozi wa dini,wanasiasa na watu maarufu katika jamii,zilitolewa mada kuhusu magonjwa ya kifuakikuu,saratani ya mlango wa kizazi na tezidume. Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku tatu, Dr Abuya aliwataka washiriki hao kuwa chanzo cha ukombozi kwa jamii kwa kutumia elimu watakayoipata kuhamasisha familia upimaji wa afya.

TANZANIA KUNADI VIVUTIO VYA UTALII DUNIANI KUPITIA TAMASHA LA URITHI WA UTAMADUNI WA MABARA NCHINI UFARANSA

April 19, 2018


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ Jijini Dar es Saalam jana.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 za bara la Afrika zitakazoshiriki katika tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ linalotarajiwa kufanyika nchini Ufaransa katika mji wa ‘Cherbourg’ mwezi Julai mwaka huu.

Tanzania inashiriki tamasha hilo la kihistoria kwa mara ya kwanza ambapo itapata fursa ya kutangaza utamaduni wake na vivutio vya utalii vya mambo ya kale hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha hilo Jijini Dar es Saalam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, alisema tamasha hilo litatoa fursa pana kwa nchi kutangaza vivutio vyake ikiwemo vile vya Zamadamu.

“Kimsingi tamasha hilo linatarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania kutangaza vivutio vyake na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini, kila nchi itapewa banda lake la kuonyesha vivutio vyake , Tanzania naamini inakuwa na vivutio vingi vyenye kupendeza watalii kama vile Zinjathropus, Ngoma za makabila mbalimbali pamoja na nyimbo.

“Baada ya tamasha hilo, kutakuwa na ongezeko kubwa la watalii nchini na ninaamini hata zile nchi ambazo hazina rekodi nzuri ya kuja Tanzania kwa wingi zilizopo Bara la Asia zitaanza kuja,’’. alisema Kigwangwala.

Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kuhusisha takriban nchi zote za bara la Afrika, zaidi limelenga kutangaza tamaduni na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika mataifa yote yatakayoshiriki huku likitajwa kuwa tamasha bora na kubwa la utalii pengine kuliko matamasha mengine yote kutokana na kila nchi kujitokeza kuonyesha vivutio vinavyopatikana katika mataifa yao.


“Tanzania tunavyo vivutio mbalimbali tunavyotarajia kwenda kuvionyesha katika tamasha hilo, ukiacha vivutio vya mambo kale, tuna bonde la Olduvai Gorge na mengineyo, tunayoamini kuwa kupitia tamasha hilo tutaweza kuyatangaza na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini” alisema Dkt. Kigwangalla.

Hata hivyo alisema baada ya kukamilika kwa tamasha hilo, Septemba mwaka huu hapa nchini kutakuwa na tamasha la ‘Urithi wa Mtanzania’ linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza na litakuwa likifanyika kila mwaka kuadhimisha urithi wa Mtanzania.

Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha mwezi mzima, pia litatoa fursa kwa kila wilaya kutangaza vivutio vyake, huku akizitaka kila wilaya kujiandaa na tamasha hilo, litakalotoa fursa pia kwa mikoa na wilaya hizo kukuza utalii wa maeneo yao.

Waziri Kigwangalla akisalimiana na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asngya Bangu akiongoza zoezi la utambulisho.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ Jijini Dar es Saalam jana.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax mabula akizungumza katika mkutano huo.

Picha ya pamoja ya Waziri Kigwangalla na washiriki wa mkutano huo.

Waziri Kigwangalla akifurahia jambo na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.

ELIMU KWA WAKULIMA WA PAMBA KATIKA MIKOA YA KANDA YA ZIWA YAPAMBA MOTO ILI KUCHOCHEA TANZANIA YA VIWANDA

April 19, 2018
Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeendelea kutoa elimu kwa wakulima pamoja na kuhakiki mizani itakayotumika kununulia zao la Pamba ikiwa ni maandalizi ya msimu wa ununuzi wa Pamba kwa mwaka huu (2018). Zoezi hili la utoaji elimu na uhakiki wa mizani itakayotumika kununulia Pamba linaendelea katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Mara pamoja na Kagera kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Vipimo Makao Makuu.

Dhumuni kuu la utoaji elimu kwa wakulima wa zao la Pamba Kanda ya Ziwa ni kuwawezesha wakulima kutambua mizani iliyosahihi (inayoruhusiwa kwa biashara) na ile iliyochezewa (isiyoruhusiwa kwa biashara) ili waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa vipimo wanapokuwa hawapo katika vituo vya kuuzia Pamba yao na pia ni kuwawezesha wakulima kupata faida ya thamani kamili ya jasho lao.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Mwanza, Hemed Kipengere akitoa elimu kwa wakulima wa Pamba Wilayani Magu kuhusiana na mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kupima Pamba kwenye mizani ili Wakulima waweze kupata faida ya jasho lao la kulima Pamba.

Akizungumza na Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano Bi. Irene John, alisema katika maandalizi ya msimu mpya wa ununuzi wa Pamba Mwanza wanategemea kutoa elimu kwa Wilaya tano (5), Simiyu Wilaya tano (5), Shinyanga Wilaya tatu (3), Geita wilaya sita (6), Tabora Wilaya tatu (3) , Kagera Wilaya mbili (2) pamoja na Mara Wilaya tano (5). Hivyo, kwa mwaka huu jumla ya Wilaya 28 zimelima Pamba na zote zitapatiwa elimu inayohusu matumizi ya vipimo sahihi na faida zinazopatikana kwa mkulima kwa kuuza mazao yake kupitia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo.

Mwaka huu tofauti kidogo na mwaka jana maana Serikali imefufua Vyama vya Ushirika ambapo ununuzi wote wa Pamba utafanywa na Vyama vya Msingi ambayo vinasimamiwa na wakulima wenyewe badala ya kuuza Pamba yao kupitia Mawakala kama ilivyokuwa imezoeleka miaka ya nyuma. Mkulima wa Pamba atanufaika zaidi kwa kuuza mazao yake kupitia vyama vya msingi sababu mazao yote yatakayopatikana kutoka kwenye Pamba yaani mbegu pamoja na nyuzi mkulima atahusika kupata faida ya uuzaji wa mazao hayo tofauti na mwanzo faida kama hii ilikuwa haipatikani kwake isipokuwa kwa mfanyabiashara tu.


Afisa wa Wakala wa Vipimo mkoani Mara wakionesha mizani sahihi na ile isiyo sahihi ili wakulima waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa wanapokuwa hawapo.

Pia kuuza Pamba kupitia vyama vya msingi itapunguza ulaghai kwenye mizani sababu wasimamizi na watumiaji wa Mizani watakuwa ni wakulima wenyewe wa Pamba wala siyo mawakala.
Irene alisema Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara ikiwa ni pamoja na kuweka sticker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa na kukutwa kikiwa sahihi ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.

Bi. Irene ameongezea kuwa Wakala wa Vipimo itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza na wakawaida wakati wowote baada ya msimu wa ununuzi wa Pamba kuanza ili panapokuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uonevu katika mizani yaweze kutatuliwa kwa haraka.
Bi. Irene John aliwasihi wakulima wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga kwenye Pamba kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja ili kuleta biashara ya haki.

Lengo kuu la Wakala wa Vipimo ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha na siyo kupunjwa na wafanyabiashara wajanjawajanja. Irene alisisitiza kuwa kwa wale watakaobainika kuchezea mizani kwa ajili ya kuwaibia wakulima adhabu imeboreshwa kuanzia mwaka juzi ( Nov. 2016) hivyo, faini itaanzia laki moja badala ya elfu kumi kama ilivyokuwa imezoeleka kufikia hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa. Kesi ikifikishwa mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Irene alisema Tanzania ya viwanda itafanikiwa endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumizi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao, ufungashaji hadi utumiaji wa mazao yenyewe. Wakala wa Vipimo ina imani kuwa matumzi ya vipimo sahihi yakizingatiwa viwanda vingi vitaweza kupata malighafi za kutosha sababu mkulima na mfanyabiashara kila mtu atakuwa na imani na mwenzake kupitia matumizi ya vipimo sahihi. Msema kweli na mleta haki katika biashara ni kipimo sahihi kilichohakikiwa na Wakala wa Vipimo wala siyo vinginevyo.

Wakala wa Vipimo itaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara ili wajue thamani ya kuuza kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na kumsaidia mkulima kupata fedha kulingana na thamani ya mazao yake, kufanya biashara ya haki na kuepusha migogoro/migongano, kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla pamoja na kukuza mauzo ya Pamba ya Tanzania katika soko la Dunia. Irene alisema kuwa Wakala wa Vipimo imepewa jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika au vinavyotarajiwa kutumika Kisheria kwenye maeneo ya biashara hapa nchini, hivyo Wakala inaowajibu wa kumlinda mkulima wa Pamba katika uuzaji wa Pamba yake kwa kutumia vipimo sahihi.

Wakulima wa Pamba wilayani Magu Mkoani Mwanza wakiwasikiliza maafisa wa Wakala wa Vipimo namna ya kutambua mizani sahihi na ile isiyo sahihi.

Bi. Irene alisema "elimu kwa pande zote mbili (Mkulima na Mfanyabiashara/Vyama vya Msingi) ni muhimu lakini zaidi kwa mkulima kwani, mbali ya kutumia muda wake mwingi katika kuandaa shamba, kulima, kupalilia na hata kuvuna bado ameoneka kuwa mnyonge kwenye mazao yake ndiyo maana kwa sasa tunazunguka Kanda ya Ziwa Mikoa inayolima Pamba kwa wanunuzi ( vyama vya msingi) na wakulima kwa ajili ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mizani kabla ya uuzaji wa zao la Pamba kuanza.

Bi. Irene alisema kuanzia hatua ya awali ya kuandaa shamba hadi kuvuna mkulima anahitaji matumizi sahihi ya vipimo lakini wakati wa kuuza mazao, umakini wa matumizi sahihi ya vipimo unahitajika sana, ambapo kipimo kikiwa sahihi na kikatumiwa kwa usahihi, kitatoa matokeo sahihi kumwezesha muuzaji (mkulima) kupata fedha sawa na thamani ya bidhaa aliyouza.

Hivyo, nia na lengo la utoaji wa elimu pamoja na uhakiki mizani ni kuwasaidia wakulima kabla ya msimu wa Pamba kuanza wapate elimu ya kutosha hatimaye mkulima aweze kupata fedha kulingana na thamani ya bidhaa atakayoizalisha na kuwasilisha sokoni. Mkulima naye anao wajibu wa kumpatia Afisa Vipimo ushirikiano kwa kumsaidia kumpa taarifa zote atakazo zihitaji, kupeleka mazao yake kwenye chama cha ushirika au kituo kitakachokuwa kimeteuliwa na kukubalika na bodi ya Pamba pamoja na kuhakikisha anauza Pamba yake kwa kutumia mizani sahihi iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo.

MADAKTARI BINGWA WABAINI WAGONJWA ZAIDI YA 460 WA MOYO SONGWE

April 19, 2018

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo George Lyego Longopa Kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete akichukua maelezo ya mgonjwa wa moyo katika hospitali ya Vwawa-Mbozi.
Afisa Muuguzi Kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Flora Kasembe akimpima shiniko la damu mwandishi wa habari Manuel Kaminyoge katika hospitali ya Vwawa-Mbozi
Baadhi ya wagonjwa wakisoma kipeperushi kinachoeleza masuala ya lishe wakati wakisubiri kupata huduma ya madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya Vwawa-Mbozi.
Wagonjwa 467 wenye matatizo ya moyo wamebainishwa na kupatiwa huduma ya ushauri na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa waliotoa huduma kwenye kambi maalumu ya siku 4 katika hospitali ya Vwawa-Mbozi Mkoani Songwe.

Timu ya Madaktari Bingwa na wauguzi 5 wameeleza kuwa wagonjwa 18 kati ya hao waliowahudumia wamepewa rufaa ya kufika hospitali za Rufaa kwa ajili ya matibabu Zaidi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo George Lyego Longopa Kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete amesema wameanza matibabu siku ya Jumanne na kila Daktari amekuwa akiona zaidi ya wagonjwa 60 kutokana na hamasa ya wagonjwa waliojitokeza kupata matibabu ya magonjwa ya moyo.

“Tumeona wagonjwa wengi na tumeamini kuwa Songwe tatizo la Magonjwa ya moyo bado ni kubwa, wagonjwa wengi wamekutwa na matatizo ya shinikizo la damu, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri pamoja na matatizo ya mishipa ya damu kuziba”, amesema Dkt Longopa.

Afisa Muuguzi Kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Flora Kasembe ameeleza kuwa mtindo wa maisha ya wananchi wa Songwe unaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa ya moyo hasa kutokana na uwepo vyakula vingi lakini wananchi hawali mlo kamili.

Kasembe amefafanua kuwa, “tumekuwa tukitoa elimu ya kuzingatia mlo kamili ili hivi vyakula vingi vilivyopo huku visaidie kuimarisha afya na sio waishie kuuza tu bila wao kutumia, pia wananchi wajenge mazoea ya kufanya mazoezi na endapo watabainika na matatizo na wakaanzishiwa dawa wazitumie kwa usahihi waiache”.

Baadhi ya wagonjwa waliohudhuria kupata matibabu ya moyo wameishukuru serikali kwa kusogeza huduma karibu na utaratibu huo ufanyike mara kwa mara ili wananchi wengi wapate huduma ya madaktari bingwa.

Brigita Haule ambaye amepata matibabu ya moyo ameeleza kunufaika na huduma hiyo kwani hakuwa akifahamu kama ana tatizo la moyo mpaka alipofika katika huduma hiyo.

“Wengi tunajiamini ni wazima kwakuwa hatusikii kuumwa sana ila tunatembea na magonjwa mbalimbali ambayo tunakuja kuyafahamu yakiwa katika hali mbaya, mimi pia sikufahamu kama nina tatizo hivyo nawashauri wote tuwe na utaratibu wa kupima afya zetu”, amefafanua Bi Haule.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Kheri Kagya amesema utaratibu wa kuwaalika madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete uliangaliwa na uongozi wa Mkoa baada ya kubaini kuwa kuna wagonjwa 210 wa moyo. Dkt Kagya ameongeza kuwa wagonjwa waliojitokeza wamekuwa wengi kuliko matarajio ya awali huku akieleza kuwa hayo ni mafanikio kwakuwa wameweza kuwabaini wagonjwa ambao hawakutambulika hapo awali.
MAJALIWA AKUTANA NA VIONGOZI WA CHAMA CHA WANUNUZI WA PAMBA NCHINI NA WAKUU WA MIKOA INAYOLIMA PAMBA

MAJALIWA AKUTANA NA VIONGOZI WA CHAMA CHA WANUNUZI WA PAMBA NCHINI NA WAKUU WA MIKOA INAYOLIMA PAMBA

April 19, 2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Chama Wanunuzi wa Zao la Pamba Tanzania pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Morogoro, Manyara, Mwanza, Singida, Simiyu, Shinyanga na Tabora, Ofisini kwa Waziri Mkuu, bungeni mjini Dodoma, Aprili 19, 2018.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
TCAA YAAGIZWA KUSIMAMIA USAFIRI WA ANGA

TCAA YAAGIZWA KUSIMAMIA USAFIRI WA ANGA

April 19, 2018

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari wakati akitoa maelezo ya awali kabla ya ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la Mamlaka hiyo, mjini Dodoma.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la Mamlaka hiyo, lililofanyika mjini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari nyaraka mbalimbali mara baada ya kulifungua mjini Dodoma.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) lililofanyika mjini Dodoma.

……………

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kusimamia usafiri wa anga kwa kuzingatia taratibu na kanuni za usafiri huo ili kuweka uwiano wa haki kwa waendeshaji na abiria wanaotumia usafiri huo.

Ametoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati akizindua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo na kuwapongeza kwa kuamua kuweka mikakati ya kununua rada nne kwa kutumia fedha za ndani.

“Lazima msimamie kanuni na taratibu zilizopo, wajibu wenu ni kutoa haki kwa watumiaji na abiria kwa usawa, hatutaki kusikia mnakandamiza watumiaji wa usafiri na mkisimamia vizuri eneo hili mtafanya idadi ya watumiaji kuongezeka na makampuni kuendelea kuwekeza zaidi kwenye usafiri” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amesema yeyote anaevunja taratibu zilizowekwa kwenye usafiri wa anga Mamlaka hiyo ichukue hatua stahiki kulingana na taratibu zilizopo ili usafiri huo uweze kuwa na nidhamu.

“Kila Kampuni mkiiachia ifanye inavyotaka hatutafika popote na malalamiko kwenye usafiri wa anga yataendelea kuwepo, hivyo naomba msimamie makampuni haya kwa ukaribu mkubwa,’ amesisitiza Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa ili mamlaka ifikie lengo na kufanikiwa lazima Menejimenti ishirikishe watumishi kwa karibu ili kutimiza malengo iliyojiwekea.

Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa TCAA kuwawezesha watumishi wake kitaaluma na kimaslahi ili kuongeza tija katika kazi na kufikia malengo ya utendaji Kitaifa na Kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw, Hamza Johari, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa TCAA imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia vyanzo vya ndani ili kuvutia makampuni ya ndege ya ndani na nje ya nchi.

“Nikuhakikishie kuwa tumejipanga kutekeleza miradi mingi zaidi kwenye usafiri wa ndani ili kuchochea kasi ya usafiri huo lakini pia kutimiza amza ya kuboresha usafiri huo, ”amesema Johari.

Ameongeza kuwa kwa sasa mamlaka iko kwenye hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa kufunga vifaa maalum vya kuwezesha ndege kwa usalama katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Zanzibar ambapo mradi huo ukikamilika utaimarisha huduma za kuongozea ndege katika kiwanja hicho.
RAIS WA TFF WALLACE KARIA AIPONGEZA YOUNG AFRICANS KUTINGA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO BARANI AFRICA

RAIS WA TFF WALLACE KARIA AIPONGEZA YOUNG AFRICANS KUTINGA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO BARANI AFRICA

April 19, 2018

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Ndugu Wallace Karia ameipongeza klabu ya Young Africans kwa kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Africa.
 
Young Africans imefanikiwa kuingia kwenye hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 baada ya kushinda mchezo wao wa kwanza kwa mabao 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 na timu ya Welaitta Dicha ya Ethiopia.

Rais wa TFF Ndugu Karia kwa niaba ya TFF ameipongeza klabu ya Young Africans kwa hatua hiyo kubwa iliyofikia ambayo inaakisi mpira wa Tanzania kiujumla.

“Mafanikio ya klabu ya Young Africans ni mafanikio ya Tanzania kiujumla na TFF ambao ni wasimamizi wa Mpira nchini tunajivunia mafanikio hayo ya Young Africans ambao tumekuwa tunashirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania”amesema Karia.

Amesema anaamini watafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye hatua hiyo ya makundi.

NDITIYE: SHULE ZA SEKONDARI KIBONDO ZAONGOZA UFAULU KITAIFA

April 19, 2018
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (Mb) wakati akipokea mbio za mwenge wa Uhuru ulipowasili Wilaya ya Kibondo kwenye jimbo lake la Muhambwe ukitokea Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma. Amesema kuwa Wilaya ya Kibondo imeongoza kwa ufaulu wa shule za sekondari kwa miaka miwili mfululizo ya masomo mwaka 2016 na 2017 ambapo kidato cha pili wameshika nafasi ya nane kitaifa na kidato cha nne wameshika nafasi ya tisa kitaifa na kuzibwaga sekondari nyingine zilizopo kwenye jumla ya Wilaya 187 nchini.

Nditiye amefafanua kuwa shule hizo zimezawadiwa kiasi cha shilingi milioni 680 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mpango wa Elimu kwa Matokeo (E4P) ambao umeleta chachu, ari na ushindani kwenye kiwango cha ufaulu kwenye shule mbalimbali nchini. Amefafanua kuwa fedha hizo zimetumika kugharamia upatikanaji wa miundombinu mbalimbali kwenye shule ya sekondari ya Malagarasi na ya Wasichana ya Kibondo.

Ameongeza kuwa ushindi huo umeleta chachu na mwamko zaidi kwa wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na wadau wa elimu kwenye Wilaya hiyo ambapo wamejipanga kuchangia ujenzi wa miundombinu mbali mbali kwenye shule za Wilaya hiyo ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi ambapo imeendana na kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu isemayo, “Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Wekeza Sasa kwenye Elimu kwa Maendeleo ya Taifa”.

Mhandisi Nditiye amesema kuwa Wilaya ya Kibondo inaunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muunano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure nchini kote kwa shule za msingi na sekondari ambapo wazazi hawalipi ada yeyote hivyo inawawezesha kushirikiana kuendeleza miundombinu ya shule na mahitaji ya huduma nyingine ili wanafunzi waweze kujisomea na hivyo kuongeza ufaulu wao.

Naye kiongozi wa kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu Bwana Charles Kabeho amewataka wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanamuunga mkono Mhe. Rais wa nchini yetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata sare za shule, vitabu vya masomo mbali mbali na miundombinu mingine ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa manufaa ya wanafunzi na walimu.

Amefafanua kuwa azma ya Dkt. Magufuli ni kuwa na nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ambapo haya yote hayawezekani pasipo kuwa na taifa lenye rasilimali watu yenye elimu, ujuzi na maarifa ya kuendesha na kusimamia viwanda vyetu.

Bwana Kabeho amemshukuru na kumpongeza Mhandisi Nditiye kwa kutambua umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa na kujumuika na wananchi wa jimbo lake la Muhambwe lililopo kwenye Wilaya ya Kibondo. “Mheshimiwa Nditiye, natambua majukumu uliyonayo katika kipindi hiki cha Bunge la bajeti ambalo linaendelea mkoani Dodoma lakini umejali na kuja kujumuika nasi katika kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye Wilaya hii,” amesema Kabeho.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zimepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Mheshimiwa Loyce Bura kwenye kijiji cha Mkubwa mpakani mwa Wilaya ya Kibondo ukitokea kwenye Wilaya ya Kakonko. Mwenge umetembezwa kwenye Wilaya ya Kibondo na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya shilingi 1,512,000,000 ikiwemo kituo cha Afya cha Mabamba, kiwanda cha kusindika na kuzalisha unga wa muhogo, ofisi ya ushauri wa kibiashara, hoteli na kugawa asiimia kumi ya mapato ya Halmashauri hiyo kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na walemavu kiasi cha shilingi milioni 58.

Mwenge umekabidhiwa kwenye Wilaya ya Kasulu ili kuendelea na mbio zake na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo nchini ambapo makabidhiano hayo yamefanyika kwenye kijiji cha Mvugwe mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kasulu.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (Mb) akipokea Mwenge wa Uhuru baada ya kuwasili kwenye jimbo lake la Muhambwe Wilayani Kibondo mkoani Kigoma.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akishiriki uzinduzi wa Kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa uliofanyiwa na kiongozi wa kitaifa wa mbio hizo Bwana Charles Kabeho (wa tatu kushoto) kwenye kata ya Mabamba wilayani Kibondo, Kigoma

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Mheshimiwa Loyce Bura (kulia) akipokea mbio za Mwenge wa Uhuru wa Taifa kwenye kijiji cha Mkubwa kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kakonko

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akigawa chandarua kwa wanawake wenye watoto baada ya uzinduzi wa kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma wakati wa mbio za Mwenge wa uhuru za kitaifa

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, Mbunge wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma akipiga ngoma kuburudisha wapiga kura wake wakati wa kupokea mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa uliowasili kwenye Wilaya hiyo
Shule za sekondari za Wilaya ya Kibondo zaongoza kwa ufaulu wa elimu katika ngazi ya kitaifa kwa miaka miwili mfululizo na kushika nafasi kati ya shule kumi bora za kitaifa na kuzishinda wilaya nyingine zote nchini
DK.SHEIN AKUTANA NA MAKAMU WA SHIRIKA LA NDEGE LA MISRI EGYPTAIR LEO

DK.SHEIN AKUTANA NA MAKAMU WA SHIRIKA LA NDEGE LA MISRI EGYPTAIR LEO

April 19, 2018

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Makamo wa Rais wa Shirika la Ndege la Misri EGYPTAIR Bw.Mohamed Alabbady alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na Ujumbe aliofuatana nao Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na Makamo wa Rais wa Shirika la Ndege la Misri EGYPTAIR Bw.Mohamed Alabbady (katikati) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na Ujumbe aliofuatana nao
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na Makamo wa Rais wa Shirika la Ndege la Misri EGYPTAIR Bw.Mohamed Alabbady alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na Ujumbe aliofuatana nao (hawapo pichani),
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akibadilishana mawazo na Makamo wa Rais wa Shirika la Ndege la Misri EGYPTAIR Bw.Mohamed Alabbady (kushoto) mara baada ya mazungumzo yao yalifanyifika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na Ujumbe aliofuatana nao (wa pili kulia) Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor na Kaimu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ofisi ya Zanzibar Bw.Mohamed Haji Hamza(wa pili kulia),

Picha na IkulU

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AKUTANA NA MKURUGENZI MTENDAJI MBADALA BENKI YA DUNIA, KANDA YA AFRIKA

April 19, 2018

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wakwanza kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe (hayumo pichani) kuhusu mpango kazi wa kuboresha uwekezaji Tanzania. Kushoto kwake ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga na Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila.

Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe (kulia) akimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayumo pichani) wakati wa majadiliano ya namna ya kuendeleza miradi ya maendeleo nchini Tanzania, kushoto kwake ni Mshauri wa Mkurugenzi huyo Bw, Zarau Kibwe.
Picha ya pamoja ya wajumbe walioshiriki majadiliano ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe kuhusu uboreshaji wa sekta binafsi, miradi ya maendeleo, ukuaji wa uchumi pamoja na sekta ya ukuaji wa viwanda. Wanaopeana mikono kulia Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)kushoto Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe. Kutoka kulia ni Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Charles Kichere, wa pili kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga na wa pili kushoto ni Mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, kanda ya Afrika Bw, Zarau Kibwe.

Na. WFM- Washngton DC

Mikutano ya Bodi ya Magavana ya Shirika la Fedha la Kimataifa na kundi la Benki ya Dunia kwa mwaka 2018 imeanza rasmi mjini Washington D.C. Katika mikutano hiyo kutakuwa na Magavana, Mawaziri wa Fedha, Sekta Binafsi pamoja na Wanataaluma mbalimbali kuweza kujadili hali ya uchumi wa dunia pamoja na kupunguza umasikini.

Katika mikutano hiyo Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe, kuhusu maendeleo ya hali ya uchumi wa Tanzania huku akisisitiza kwamba ni wakati mzuri sasa wa kusemea hali ya uchumi wetu kwa nguvu zote.

Akiendelea kutoa ufafanuzi Dkt Mpango alieleza hatua ambazo Serikali imezifanya ili kuweka mazingira mazuri katika sekta binafsi, na kwamba Serikali imeandaa mpango kazi wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika Taifa la Tanzania.

Pia Waziri Mpango alielezea miradi mikubwa ambayo nchi imeanza kuitekeleza, ikiwamo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa na Ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha Umeme wa Megawati 2100 la ‘Steigler's Gorge’ katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji.

Kupitia miradi hiyo ambayo Serikali imepanga kuifanikisha kwa wakati Dkt. Mpango alimuomba Bw. Bvumbe kuendelea kuzungumza na uongozi wa Benki ya Dunia ili uweze kutusaidia katika kuwezesha uwekeza katika miradi hiyo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe alisema kuwa anaipongeza Tanzania kwa jitihada inazozionesha hasa katika kupambana na rushwa na ametutia moyo tuendelee na juhudi zetu za kuimarisha uchumi wetu hususani katika sekta ya kilimo na pia amefurahishwa na hatua mbalimbali zinazofanya kwa ajili ya kuendeleza sekta ya viwanda.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha na Mipango

Washington D.C
MATUKIO KATIKA PICHA BUNGENI MJINI DODOMA LEO APRIL 19,2018

MATUKIO KATIKA PICHA BUNGENI MJINI DODOMA LEO APRIL 19,2018

April 19, 2018

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akisisitiza kuhusu umuhimu wa wananchi wanaoishi mabondeni kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka maafa yanayotokana na mvua, wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni Mjini Dodoma, leo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kulipa fidia kwa wananchi pale maeneo yao yanapotwaliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania ( JWTZ) kwa matumizi ya shughuli za Jeshi hilo, Bungeni Mjini Dodoma leo
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akitoa mikakati ya Wizara hiyo kuliwezesha Jeshi hilo kuzalisha kwa wingi hivyo kujitosheleza na kupunguza utegemezi kutoka Serikalini.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwasilisha Bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo leo Bungeni Mjini Dodoma.
Waziri wa Maji na umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akisisitiza jambo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo Bungeni Mjini Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akisisitiza jambo mapema leo Bungeni Mjini Dodoma mara baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Sehemu ya wageni waliofika Bungeni wakifuatilia kipindi cha maswali na majibu mapema leo Bungeni Mjini Dodoma.

(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO
WAGONJWA 19,371 WATIBIWA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE KUTOKA JANUARI HADI MACHI 2018

WAGONJWA 19,371 WATIBIWA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE KUTOKA JANUARI HADI MACHI 2018

April 19, 2018


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha miezi mitatu ya Januari hadi Machi 2018 imeona jumla ya wagonjwa 19,371 wenye matatizo mbalimbali ya moyo kati ya hao wagonjwa wa nje ni 18,481 na waliolazwa ni 890.

Wagonjwa 105 walifanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kati ya hao watu wazima 53 na watoto 52. Kati ya wagonjwa 105 waliofanyiwa upasuaji 66 walifanyiwa na madaktari wetu bingwa wa magonjwa ya moyo watoto wakiwa ni 35 na watu wazima 31.

Upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab ulifanyika kwa wagonjwa 231 kati ya hao watoto ni 20 na wakubwa 211. Kati ya wagonjwa 231 waliotibiwa wagonjwa watu wazima 211 walifanyiwa upasuaji na madaktari wetu wa ndani.

Kwa kipindi cha miezi mitatu tumekuwa na jumla ya kambi za matibabu nane (8) ambapo tulifanya matibabu kwa kushirikiana na washirika wetu kutoka nchi za Ujerumani, Israel, Australia , Marekani, India na Falme za Kiarabu. Katika kambi hizo jumla ya wagonjwa 39 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua kati ya hao watoto 17 na watu wazima 22. Wagonjwa 72 walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kati ya hao watoto 20 na watu wazima 52.

Tumefanya upasuaji wa kuunganisha mishipa ya damu (AVF- Arterio Venous Fistula) kwa ajili ya kusafishia damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo (Hemodialysis) 36.

Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri hivyo basi tunawaomba wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na kama wanamatatizo wataweza kupata tiba kwa wakati.

Wazazi na walezi tunawaomba wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha Hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo. Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo.

Aidha kwa upande wa gharama za matibabu Taasisi yetu imeyagawa katika makundi manne (4) tuna wagonjwa wanaotibiwa kwa bima mbalimbali ambazo tumeingia makataba nazo. Wagonjwa wanaolipia gharama zote wenyewe, wagonjwa wanaochangia kidogo huku gharama zingine zikilipwa na Serikali. Kundi la mwisho ni wagonjwa ambao hawalipii kabisa gharama za matibabu ikiwa watakidhi vigezo vyote vya kutokulipa.

Huduma zetu za matibabu ya moyo zinatolewa kwa watanzania wote wa Bara na Visiwani. Ifahamike kwamba fedha za matibabu zinazolipwa na wagonjwa zinatumika kununua vifaa tiba vya moyo kama mlango wa moyo (Valve), betri ya moyo (Pacemaker) na vinginevyo.

Kutokana na matibabu ya moyo kuwa ya gharama kubwa tunaendelea kuwasisitiza wananchi wajiunge na mifuko ya bima za afya ambayo itawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapohitaji kutibiwa. Pia itasaidia Hospitali yetu kuendelea kujiendesha yenyewe kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine.

HUDUMA ZA MAJI ZAIMARIKA, TEKNOLOJIA KUONDOA MATUMIZI YA MKAA

April 19, 2018

Upatikanaji wa maji mijini na vijijini umeimarika kutoka chini ya 50% ya awali kutokana na umakini katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji safi nchini. Aidha, ili kukabiliana na mazingira Serikali imeanza mchakato wa kutumia mifumo ya kisayansi ili kuondoa matumizi ya mkaa majumbani.

Hatua hizo zimebainishwa na Mhe. Isack Kamwelwe, Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Mhe. Januari Makamba, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira) walipokuwa wakieleza utekelezaji wa hoja za CAG katika sekta zao.

Akizungumzia hoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji nchini, Waziri Kamwelwe amesisitiza kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, ufuatiliaji na kuzibwa mianya ya ubadhirifu vimeleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini.

“Sisi kwa upande wetu CAG anatuonesha njia ili tufanye vizuri zaidi. Hadi kufikia Desemba, 2017, upatikanaji wa maji mijini umepanda hadi kufikia asilimia 78. Kwa upande wa vijijini, hadi kufikia Machi 2018, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imejenga vituo vya kuchotea maji 123,888 vyenye uwezo wa kuhudumia takribani watu milioni 30 sawa na asilimia 68.8,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri Makamba amesema hoja za CAG zimewasaidia kuongeza mikakati hasa ya kutumia sayansi na teknolojia kupata mbadala wa matumizi ya mkaa ili kuokoa misitu na kutunza mazingira. Amesema tayari Ofisi yake na wadau wanafanya majaribio ya baadhi ya teknolojia hizo.

Kuhusu changamoto za kupambana na taka za kielektroniki, amekiri kuwa Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea inakumbana na changamoto ya kupokea vifaa vingi vilivyotumika kama kompyuta, simu na chaja ambavyo huharabika haraka na kutupwa kama taka za kielectroniki.

“Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kutoa vibali kwa makampuni 16 yenye utaalamu kwa ajili ya kukusanya, kusafirisha na kurejeresha (recycling) taka za kielektroniki,” alisema.

Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.


Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akijibu hoja mbalimbali zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Wizara yake mapema mjini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari ( hawapo pichani).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akijibu hoja mbalimnbali zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Ofisi hiyo mapema mjini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisisitiza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utaratibu wa Mawaziri wote kukutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Wizara zao mapema mjini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akifurahia jambo na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso mapema mjini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliowashirikisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba. (Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma)