AZAM FC YALISAKA KOMBE LA MAPINDUZI KWA MARA YA TATU, KUTUA ZANZIBAR JANUARI 1 KAMILI GADO!!

December 29, 2013
Imewekwa Saa 12:01mchana leo Desemba 29.
MABINGWA watetezi wa kombe la Mapinduzi, klabu ya Azam FC imetamba kwenda kutetea taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano inayoanza kutimua vumbi januari mosi mwakani.

Jafari Idd Maganga, Afisa habari wa klabu hiyo amesema panapo majaaliwa timu hiyo inatarajia kung`oa nanga jijini Dar e salaam januari 1 mwaka huu kuelekea visiwani Zanzibar tayari kuanza harakati za kutafuta kombe hilo.

“Michuano hii ni muhimu sana kwetu. Kocha mkuu Mcameroon, Joseph Marius Omog atakuwa na nafasi nyingine ya kupima kikosi chake na kuelewa wapi kuna matatizo ili kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara na michuano ya kimataifa”. Alisema Jafar.
Jafar aliongeza kuwa tangu timu ipate kocha mpya, wachezaji wamekuwa wakipambana kutafuta nafasi   katika  kikosi cha kwanza.

“Mapinduzi Cup itawajenga wachezaji wetu. Kila mchezaji anataka kuonekana mbele ya kocha, ushindani umeongezeka zaidi, bila shaka baada ya kumalizika kwa michuano hii muhimu, Kocha Omog atakuwa amepata kikosi chake”.

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI TFF LEO

December 29, 2013
Release No. 216
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 29, 2013

KLABU ZATAKIWA KUREKEBISHA KASORO USAJILI MDOGO
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.

Baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.

Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.

Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.