Okwi (kulia) hachezi leo
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Wakati kikosi cha Mserbia Goran
Kopunovic cha Simba SC kinawakosa viungo Emmanuel Okwi na Said Hamis
Ndemla, wapinzani wao Mbeya City FC wanawakosa nahodha wao beki Hassan
Mwasapili katika mechi yao ya leo.
Simba SC na Mbeya City FC
zilizoambulia sare katika mechi zake za mwishoni mwa wiki, zitachuana
vikali katika mechi pekee ya kesho ya kiporo ya raundi ya 10 ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam saa 10 jioni.
Kocha Mkuu wa Mbeya City FC,
Juma Mwambusi, ameuambia mtandao huu jana mchana jijini hapa kwamba
kikosi chake kiko vizuri kuwavaa Simba SC kesho licha ya kuwa hatarini
kuwakosa nyota hao wawili.
Kwa mujibu wa ratiba ya VPL
msimu huu, mechi hiyo ilipaswa kuchezwa Januari 11 lakini ikapigwa
kalenda na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na ushiriki wa
Simba SC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar
ilikoibuka bingwa.
Mwambusi amesema: “Tumejiandaa
kwa mechi zote za msimu huu, kikubwa mashabiki wetu waje uwanjani kesho
kuona soka safi maana kikosi chetu sasa kiko vizuri.”
“Tuna wachezaji wengi ambao
tumekuja nao hapa Dar es Salaam, kuna uwezekano mkubwa wa kuwakosa
Mwasapili na Mwagane ambao leo wameshindwa kufanya mazoezi kutokana na
matatizo yanayowakabili lakini hilo haliwezi kutudhoofisha kwa sababu
tuna wachezaji zaidi ya 20,” amesema Mwambusi.
Kocha Bora wa VPL msimu
uliopita — Mwambusi, amesema Mwagane anasumbuliwa na malaria wakati
nahodha Mwasapili ana majeraha ya kifundo cha mguu.
Yeya anaikosa mechi ya leo
Mwagane ndiye mchezaji pekee wa
Mbeya City FC mwenye rekodi ya kufunga mabao matatu peke yake katika
mechi moja ‘hat-trick’ tangu timu hiyo ipande Ligi Kuu msimu uliopita.
Mkali huyo wa kupiga vichwa
vitamu kuliko washambuliaji wengine wote Tanzania, alifunga hat-trick
hiyo katika mechi yao ya mwisho ya mzunguko wea kwanza msimu uliopita
walitoka sare ya 3-3 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Azam, Dar es Salaam
Novemba 7, mwaja juzi.
Mwasapili ni beki tegemeo na
kiongozi katika kikosi cha Mwambusi, hivyo kukosekana kwake kesho huenda
kukaiathiri timu hiyo ya Jiji la Mbeya.
Simba SC ambayo Jumapili
ilishikwa kwa sare YA 1-1 dhidi ya vinara Azam FC, iko nafasi ya 10
katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13 na itaingia Uwanja wa Taifa
ikiwana kumbukumbu ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Mbeya City FC msimu
uliopita.
Mbeya City FC iko nafasi ya 12
ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi 10 sawa na Simba. Timu hiyo
inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, haijawahi kufungwa na
Simba tangu ipande Ligi Kuu msimu uliopita wakitoka sare katika mechi
zote mbili za VPL msimu uliopita.
Simba SC iliyoshinda mechi
mbili tu katika mechi 10 zilizopita za VPL ikitoka sare mara saba na
kupoteza mechi moja, itaingia Uwanja wa Taifa ikisaka ushindi wa pili
nyumbani msimu huu dhidi ya kikosi cha Mwambusi ambacho kimeshinda mechi
tatu tu kati ya 10 kikitoka sare mara tatu na kupoteza mechi nne.
Kiungo mshambuliaji wa Simba
SC, Mganda Emmanuel Okwi hatakuwamo katika kikosi hicho cha Msimbazi
kesho kutokana na maumivu ya shingo ambayo aliyapata katika mechi yao
iliyopita alipopigwa kiwiko na kupoteza fahamu na beki kisiki Mzanzibar
Aggrey Morris wa Azam FC.
Kiungo mwingine Ndemla ataikosa
mechi hiyo baada ya kupimwa na daktari wa Simba SC, Yassin Gembe na
kubainika kwamba atakaa nje ya uwanja kwa wiki mbili kuuguza majeraha ya
nyama za paja aliyoyapata katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi
2015 walilolitwaa baada ya kuifunga Mtibwa penalti 4-3 Uwanja wa Amaan,
Zanzibar Januari 13.
Licha ya maumivu hayo, Ndemla
aliendelea kupangwa katika kikosi cha Simba SC kilichoshinda 2-0 dhidi
ya Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wiki mbili
zilizopita, akapangwa pia katika kikosi cha Taifa Stars Maboresho
kilichotoka sare ya 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’
Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Alhamisi kabla ya kujitonesha katika mechi
iliyopita dhidi ya Azam FC Jumapili.