NSSF YALIPA MAFAO YA BILIONI 56.688/- KWA MIEZI SITA

February 15, 2024

 *Wastaafu wote hulipwa pensheni zao tarehe 23 ya kila mwezi


*Matumizi ya mifumo ya TEHAMA yazidi kuimarika, hasa Mfumo wa Waajiri(Employer Portal)

Na MWANDISHI WETU

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umelipa shilingi bilioni 56.689 kama mafao ya wastaafu katika kipindi cha miezi sita iliyoanzia mwezi Julai mpaka Disemba 2023.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omari Mziya alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake Makao Makuu ya NSSF, Jengo la Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, alisema Mfuko umeandaa mpango mahususi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wanachama na tayari mpango huo unaendelea kutekelezwa kwenye ofisi mbalimbali za NSSF kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Bw. Mziya alisema NSSF inawathamini wanachama wake, hivyo inawaomba waajiri wote wa sekta binafsi kutimiza wajibu wao kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi ili kuwaondolea usumbufu watakapostaafu waweze kulipwa mafao yao kwa wakati.

Alisema Mfuko unaendelea kulipa pensheni kwa wastaafu, ambapo katika kipindi cha mwezi Januari 2024, imelipa shilingi bilioni 9.93.

“NSSF tunajivunia kuwa na wastaafu ambao tunawalipa kwa wakati kila inapofika tarehe 25 ya kila mwezi, dhamira na lengo letu ni kuona wafanyakazi wote katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wanaingia katika malipo ya pensheni ili kupunguza umasikini utokanao na uzee au kukosa kipato,” alisema Bw. Mziya.

Alisema Mfuko upo katika zoezi la uhakiki wastaafu ambalo lilianza tarehe 1 Februari na litaendelea mpaka tarehe 30 Aprili, 2024, ambapo alitoa wito kwa wastaafu na wategemezi kutumia kipindi hiki kufanya uhakiki kwenye ofisi zote za NSSF zilizopo Tanzania Bara na waliopo Zanzibar wafike katika ofisi za ZSSF.

Bw. Mziya alisema uandikishwaji wanachama umerahisishwa ambapo Mfuko hutumia mifumo ya TEHAMA kuandikisha wanachama na kupitia mifumo hiyo mwajiri anaweza kumuandikisha mwanachama kupitia mfumo wa Employer Portal.

“Natoa rai kwa waajiri ambao hawajaingia kwenye mfumo huu wa Employer Portal wajiunge kwa sababu ni mfumo wenye faida nyingi sana ikiwemo ya kurahisisha uandikishaji wanachama,” alisisitiza.

Bw. Mziya alisema ukusanyaji wa michango ni jukumu muhimu la NSSF na kazi hiyo inaifanywa kwa ushirikiano kutoka kwa waajiri kwa sababu michango ni makato ya mshahara ya watumishi ambayo yanasimamiwa na waajiri wenyewe.

Alitoa wito kwa waajiri wote wa sekta binafsi kuhakikisha wanawaandikisha wafanyakazi wao katika Mfuko na kuwasilisha michango yao kila mwezi.

Naye, Mzee Nicholas Kingazi, mkazi wa Tabata alisema anafurahishwa na huduma zinazotolewa na NSSF hasa kwa wazee wastaafu ambapo wasiojiweza wamekuwa wakifuatwa majumbani kwa ajili ya kuhakikiwa taarifa zao.

“Nimefarijika sana kwa sababu kitendo mlichokifanya NSSF cha kufuata wazee wasiojiweza kuwahakiki majumbani kwao,” alisema Mzee Kingazi.

Alitoa shukran zake kwa uongozi wa NSSF na wafanyakazi kwa ujumla kutokana na kujali wanachama wao wakiwemo wazee wastaafu, huku akishukuru kwa namna ambavyo Mfuko umekuwa ukiwalipa wastaafu wake kila ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi.


BoT YAWEKA MAZINGIRA BORA KUZIWEZESHA BENKI ZA KIJAMII KUKUA

February 15, 2024

 Na. Peter Haule, WF, Dodoma


Serikali imeeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kimfumo ili kuziwezesha benki za biashara na za kijamii (Community Banks) kukua na kushamiri, ikiwemo Benki ya MUCOBA.


Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuzisaidia Benki za kijamii kama MUCOBA BANK iliyopo mkoani Iringa ili kukuza uchumi wa wananchi wa hali ya chini.


Mhe. Chande alisema kuwa Hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kutafuta mwekezaji mpya wa MUCOBA, ambaye ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), kurekebisha kanuni za usajili wa wakala wa benki kwa kuondoa kigezo cha uzoefu wa miezi 18.


Alizitaja hatua nyingine kuwa ni kuanzisha mfuko maalum wa shilingi trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wakulima kwa riba ya asilimia tatu kwa mwaka, kutoa unafuu wa kiasi cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu (SMR) kwa benki zinazotoa mikopo kwa sekta ya kilimo.

Mhe. Chande alisema BoT imepunguza kiwango cha riba kinachotolewa katika akaunti za wateja wa watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi (MNOs) kuwa sawa na riba za amana za sekta ya benki na kudhibiti uwiano wa gharama za uendeshaji wa benki na pato la benki usizidi asilimia 55 na mikopo chechefu isizidi asilimia tano ya mikopo yote.

Akijibu swali la nyongeza kuhusu Benki hiyo kusumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuchukua fedha zaidi ya milioni 600 kwenye Benki hiyo kupitia Benki ya NMB kwa kisingizio cha Kodi, Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema kuwa Fedha hazikuchukuliwa kwa kisingizio cha Kodi bali ilikuwa ni kodi halali.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania imeridhia kukutana na Benki hiyo ili kuona namna bora ya kuwasaidia ili benki iweze kujiendesha na kutoa huduma, hivyo amemuomba Mbunge wa Iringa Mjini kuwataarifu viongozi wa Benki hiyo kuonana na uongozi wa juu wa Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, ili kutatua changamoto hiyo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, alietaka kufafanuliwa hatua za kuisaidia Benki ya MUCOBA ambapo inadaiwa kusumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuzisaidia Benki za Jamii (Community Banks) kama MUCOBA BANK iliyopo mkoani Iringa ili kukuza uchumi wa wananchi wa hali ya chini.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)