Maafisa Elimu msioenda na kasi yetu andikeni barua za kuacha kazi-RC-Tanga

July 08, 2013

Na Mwandishi Wetu,Korogwe.

MKUU wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa amewataka maafisa Elimu ya msingi na Sekondari ambao watashindwa kwenda na kasi ya uboreshaji wa elimu wasisite kuandika barua za kuomba kuacha kazi ili wenye uwezo wachukue nafasi zao.

Alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha kazi alichoitisha kujua
mikakati ya Halmashauri zilizopo mkoa wa Tanga iliyojiwekea kutekeleza malengo ya kupandisha ufaulu kutoka asilimia 45 hadi 75 katika mitihani ya kitaifa ya kidao cha nne na darasa la saba ya mwaka huu.

Alisema kila Halmashauri inatakiwa kuhakikisha imetekeleza kwa vitendo malengo ya kupandisha ufaulu wa watahiniwa wake watakaofanya mitihani ya kidato cha nne,sita  na darasa la saba wa mwaka 2013.

Alitoa agizo hilo baada ya kutoridhishwa na baadhi ya taarifa
zilizotolewa na maafisa elimu ya msingi na Sekondari katika kutekeleza mikakati ya kuhakikisha ufaulu unapanda katika mitihani ya mwaka huu.

“Baadhi ya taarifa mlizotoa hapa hazionyeshi kama mko makini katika kutekeleza malengo,lazima mfahamu kuwa mkoa wa Tanga sasa umeondokana na kufanya kazi kwa mazoea badala yake tubadilike na twende na kasi inayohitajika”alisema Gallawa.

Miongoni mwa taarifa zilizohimizwa kufanyiwa kazi kwa haraka ni pamoja na ile ya kuwazoesha wanafunzi kufanya mitihani kwa kutumia fomu zijulikanazo kwa jina la OMR zilizopitishwa na baraza la mitihani la Taifa na kusababisha idadi kubwa ya wanafunzi kufeli mitihani mwaka jana.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga,Benedikt Ole Kuyan aliwaagiza maafisa elimu wa Wilaya zote za mkoa wa Tanga kujifunza kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ambayo imekuwa ikiwafanyia mazoezi wanafunzi wake ya namna ya kujibu maswali kwa kutumia OMR.

                                MWISHO

Anthony John aibuka bingwa wa mbio za bagari,"Chilly Willy 7-7 Tanga Rally 2013 "

July 08, 2013


Na Oscar Assenga,Tanga.
DEREVA maarufu Anthony John jana alitwaa taji la bingwa wa mbio za magari za Chilly Willy 7-7 Tanga Rally 2013 baada ya kushinda mashindano ya ndani ya magari yaliyofanyika jijini hapa.

Anthony akiendesha gari aina ya Subaru aliweza kutumia muda wa dakika 2;21 kumaliza umbali wa kilomita 1.5 na hivyo kuongoza katika kundi la madereva wenye magari maalumu ya mashindano.

Mshindi wa pili katika kundi hilo la magari ya mashindano alikuwa
Twalin Khatib aliyetumia muda wa dakika 2;25 huku Ally Ahmed (Kiraka) akimaliza akiwa wa tatu baada ya kutumia muda wa dakika 2;28,wakati Jaml Nirmal alishika nafasi ya nne kwa kukimbia kwa dakika 2;32,Akida Saad likuwa wa tano kwa kukimbia kwa dakika 2;33.

Kwa upande wa magari ya kawaida "Standard Cars"aliyeongoza na
kukabidhiwa cheti na mgeni rasmi,Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Halima Dendego ni Ali Abbas Fazal aliyetumia dakika 2;21,Shani Faza mshindi wa pili akiwa amemaliza kwa muda wa dakika 2;22 na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Albail Sohanpal 2;25.

Mbio za Pikipiki mshindi alikuwa Ally Hamudi aliyetumia dakika 2;18 hadi kumaliza huku Lukman Hussein akiwa wa pili kwa kukimbia kwa dakika 2;21 na nafasi ya tatu imekwenda kwa Tarik Aziz aliyetumiadakika 2;28 na wa nne alikuwa Adis Khalid aliyekimbia kwa muda wa dakika 2;30.


Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi, Mwenyekiti wa chama cha mbio za magari  Mkoa wa Tanga ,Husein Noor (Makoroboi) alisema yamefanyika ikiwa ni kuunga mkono maadhimisho ya sabasaba na kuinua vipaji vya vijana katika mchezo wa magari.

   
             
 MWISHO.