YANGA YAANZA CHECHE ZAO,WAICHAPA MTIBWA SUGAR BAO 2-0

October 06, 2013

NA MAHMOUD ZUBEIRY,DAR ES SALAAM.

YANGA SC imepunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi kubaki tatu kufuatia ushindi wa mabao 2-0 jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga sasa inatimiza pointi 12 na kupanda hadi nafasi ya pili, wakati Simba SC inaendelea kuishi kileleni kwa pointi 15, baada ya timu zote kucheza mechi saba.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Isihaka Shirikisho, aliyesaidiwa na Mohamed Mkono na Kudra Omary wote wa Tanga, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao hayo 2-0.
La Kwanza; Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza Mrisho Ngassa baada ya kufunga bao la kwanza leo 

Pasi ndefu ya Athumani Iddi ‘Chuji’ ilimilikiwa vyema na Mrisho Khalfan Ngassa, akamzidi maarifa beki Salvatory Ntebe kabla ya kufumua shuti kumtungua kipa Hussein Sharrif ‘Casillas’ dakika ya sita.

Baada ya kufunga bao hilo, Ngassa aliwaelelekea mashabiki wa Simba SC na kuanza kuwatambia kwa ishara kwamba yeye anajua na anatumia akili.

Mrisho Ngassa tena alimtoka vyema beki wa pembeni wa Mtibwa, Paul Ngalema na kutia krosi maridadi iliyounganishwa nyavuni na Didier Kavumbangu dakika ya 24.
Kwa ujumla Yanga SC ilicheza vyema kipindi cha kwanza na kutawala mchezo na Mtibwa Sugar pamoja na kufanya mashambulizi kadhaa, lakini hawakuweza kuipenya ngome ya wana Jangwani.

Kocha Mecky Mexime wa Mtibwa alimtoa beki Salvatory Ntebe kipindi ha kwanza na kumuingiza Dickson Daud, ambaye hata hivyo mwanzoni mwa mchezo alionekana kufanya makosa mengi kabla ya kuimarika.

Kipindi cha pili, Mtibwa walirudi wakiwa imara zaidi na kuonyesha upinzani kwa Yanga, wakijitahidi kuwadhibiti vizuri washambuliaji wa timu hiyo na pia kushambulia.

Hata hivyo, uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga iliyoongozwa na mchezaji bora Tanzania, Kevin Yondan uliinyima Mtibwa japo bao la kufutia machozi. 

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk77, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan dk59, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk80.

Mtibwa Sugar; Hussein Sharif, Hassan Ramadhan, Paul Ngalema, Salvatory Ntebe/Dickson Daud dk33, Salim Abdallah, Shaaban Nditi, Ally Shomary, Awadh Juma, Mussa Mgosi/Juma Luizio dk66, Shaaban Kisiga na Vincent Barnabas/Masoud Mohamed dk37.

PRISON YAIPIGISHA KWATA MGAMBO SHOOTING.

October 06, 2013
NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
TIMU ya Maafande wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania Prison leo wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Maafande wenzao wa Jeshi la Kujenga Taifa Mgambo Shooting katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania bara iliyochezwa uwanja wa Mkwakwani.

Katika mchezo huo ambao ulianza kwa kasi na upinzani mkubwa kutokana na kukamiana kwa timu hizo ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzake ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya mashambulizi kwa timu zote iliyotokana na mabadiliko ya baadhi ya wachezaji wao.

Mabadiliko yalianzia kwa timu ya Mgambo Shooting ambapo walimtoa Martin Mlolela ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Mohamed Namkopwe huku Prison wakimtoa Julius Kwanga na kumuingiza Hamis Mahingo

Wakionekana kujipanga na kucheza kwa umakini mkubwa licha ya uwanja wa mkwakwani kuteleza kutokana na mvua ilionyesha nyakati za mchana kabla ya kuanza mchezo huo.

Tanzania Prison waliweza kufanya mashambulzi ya kushtukiza lango mwa Mgambo Shooting na kuwachukua dakika 17 ya kupindi cha pili kuweza kupata bao lao kupitia Julius Kwanga kwenye dakika ya 62 baada ya kutokea piga nikupige lango mwa Mgambo Shooting.

Baada ya kuingia bao hilo,Mgambo Shooting walijaribu kupambana ili kuweza kurudisha bao hilo bila mafanikio yoyote yale ambapo mpaka dakika 90 mwamuzi wa mchezo huo anapuliza kipenga ubao ukasomeka 1-0.

Kwa matokeo hayo Tanzania Prison watakuwa wamejikusanyia pointi 7 katika msimamo wa Ligi kuu Tanzania bara huku wakijiandaa na mechi yao inayofuata na Simba kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

PAMBANO LA RUVU, SIMBA LAINGIZA MIL 75/-

October 06, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Ruvu Shooting na Simba lililochezwa jana (Oktoba 5 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 75,692,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 43 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 walikuwa 13,395.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 17,983,902.31 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 11,546,237.29.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 9,144,357.11, tiketi sh. 3,183,382, gharama za mechi sh. 5,486,614.26, Kamati ya Ligi sh. 5,486,614.26, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,743,307.13, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 1,066,841.66 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,066,841.66.