MSD YAGAWA VYANDARUA KWA WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI

February 17, 2023

 






Na Oscar Assenga,Tanga

Mkoa wa Tanga umezindua zoezi la ugawaji vyandarua kwa wanafunzi wa shule ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba kwa shule 1083.


Zoezi la ugawaji vyandarua hivyo limeratibiwa na serikali kupitia Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI lengo ni kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya malaria kinapungua hadi kufikia asilimia (0)ifikapo mwaka 2030

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyandarua hivyo kwa Wanafunzi,Mkuu wa mkoa wa Tanga Omar Mgumba amesema jumla ya vyandarua 529,641 vitagawiwa kwa wanafunzi katika shule zote 1083 za Msingi katika mkoa.

"Usambazaji wa vyandarua hivi mashuleni utatekelezwa kwa siku 45 na utaendelea katika Halmashauri za Korogwe,Muheza,Mkinga,Pangani,Handeni,Kilindi,Lushoto na Bumbuli"alisema RC Mgumba

Pia RC Mgumba amewataka vingozi wa serikali,dini na jamii kwa ujumla kusimamia matumizi ya vyandarua kwa usahihi vitakavyogawiwa kwa wanafunzi wa shule za msingi,na jamii ielimishwe juu ya matumizi sahihi ya vyandarua.

Naye Meneja wa MSD Mkoa wa Tanga,Sitti Abdulrahaman ameitaja mikoa itakayofaidika na vyandarua hivyo kuwa ni Iringa,Dodoma,Tanga,Manyara pamoja na Kilimanjaro.

"Lengo ni kupunguza maambukizi ya Malaria kutoka asilimia 7.5 kwa mwaka 2017 hadi kufikia kiwango cha chini cha asilimi 3.5 ifikapo mwaka 2025,na kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030"alisema Meneja wa MSD Sitti.

"Bohari ya Dawa MSD ina majukumu manne ambayo ni uzalishaji,ununuzi,utunzaji na usambazaji wa bidhaa Afya,kwenda kwenye vituo vya afya ya Umma na vile vya binafsi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya,na imepewa jukumu la kusambaza vyandarua 529,641 vyenye thamani ya Shilingi Billioni 2.9 kwenye shule zote za msingi 1083 katika mkoa wa Tanga"
 alisema Meneja wa MSD Sitti.

Mwisho.

TASAC-ELIMU YA USALAMA USAFIRI MAJINI YAPUNGUZA AJALI GEITA

February 17, 2023





Na Mwandishi Wetu,Geita

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kutoa elimu ya Usalama wa vyombo, abiria pamoja na mali zao wanapotumia usafiri majini.

Akizungumza wakati akitoa elimu ya namna ya kujiokoa abiria pamoja na wavuvi katika mwalo wa Chato beach uliyopo wilayani Chato Mkoani Geita,Afisa Mfawidhi Tasac Mkoa wa Geita  Bw. Rashid Katonga mesema mkakati uliowekwa na TASAC ni kuondokana na vifo ambavyo vimekuwa si vya lazima huku akisema atakaye kaidi kuvaa jaketi okozi “life jacket” sheria itachukua mkondo wake.

Aidha aliongeza kuwa TASAC wamesema vifo vingi ambavyo vimekuwa vikitokea majini vimekuwa vikisababishwa na ulevi kupindukia pamoja na watumiaji wa vyombo vya maji kutovaa life Jacket katika safari ambazo zimekuwa zikifanywa kila siku.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato Bw. Deusideth Katwale ameiomba TAKUKURU kuhakikisha wanakomesha vitendo vya rushwa katika mialo hiyo kwani pia imekuwa kichocheo cha ajali nyingi ndani ya ziwa.

TASAC inaendelea kuzunguka maeneo mbalimbali ya Mikoa pamoja na wilaya zake kwa lengo la kutoa elimu kwa abiria pamoja na wavuvi namna ya kujiokoa wawapo katika safari zao za kila siku.