Kama ni mfuatiliaji mzuri wa vipindi vipya vya redio
nchini Tanzania, basi lazima utakuwa umekutana na Shujaaz Radio Show inayoendeshwa na kijana
anayejiita DJ Tee. Kitu kimoja tofauti sana ambacho kijana huyu anakifanya
kwenye shoo yake ni kuelimisha vijana wengine, kuwapa meseji mbali mbali
kuhusiana na mapenzi, mahusiano, na fursa mbali mbali, kwa njia rahisi
sana ya burudani.
Wiki iliyopita katika harakati zangu za kutafuta vitu
vipya, nilijikuta nikisikiliza TBC FM kwa muda mrefu na pasipo kutegemea,
nilijikuta nikiisikia Shujaaz Radio Show. Nilidhani nimebadilisha
frequency, lakini nilikuja kuhakikishiwa baadae na shabiki mmoja wa DJ Tee ambaye nimekuwa nikimuona akiizungumzia sana shoo hii
kwenye akaunti yake ya Twitter.
Nilijikuta nikijiuliza – Hivi kuna shoo gani nyingine
nchini Tanzania ambayo inarushwa na redio stesheni nne tofauti tofauti?
Jibu sahihi ni HAKUNA! Ukiangalia alipotokea kijana huyu tangu nilipoanza
kufuatilia stori yake kwenye kijarida cha SHUJAAZ, nimeona ni jinsi gani amefanikiwa
sana kwa kufikia watu wengi ndani ya muda mfupi sana.
Kwa ufahamu wangu nikikurudisha nyuma kidogo, SHUJAAZ ilizinduliwa nchini Tanzania mwezi Februari mwaka jana
2015 (mwaka mmoja uliopita), na redio shoo za SHUJAAZ tulianza kuzisikia mwezi Novemba
mwaka jana 2015 kupitia East Africa Radio. Mwaka huu 2016
ulipoanza (Januari) tuliweza kusikia redio stesheni nyingine mbili zikirusha
shoo hii kali ya vijana, Chuchu FM ya Zanzibar na Kings FM kwa mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Habari zilizopo ni kwamba hivi sasa shoo hii pia inasikika
kupitia TBC FM kila Jumamosi saa kumi na moja jioni. Hii inafanya shoo
hii kusikika kupitia vituo 4 vya redio nchini Tanzania. Kilichonivutia
zaidi ni utofauti wa maudhui kwa shoo za kila kituo kwa kuwa kama utapata
nafasi ya kuzisikiliza zote, utagundua kuwa kila stesheni ina kitu chake
tofauti kabisa kupitia Shujaaz Radio Show.
Vijana wengi wamekiri waziwazi kuwa SHUJAAZ kwa ujumla imewasaidia kwa kiasi
kikubwa kubadilisha mitazamo na fikra zao kuelekea mafanikio kwa staili
rahisi na yenye kuburudisha.
Kijarida cha SHUJAAZ hutoka kila Jumamosi ya mwisho
wa mwezi na husambazwa na gazeti la Mwanaspoti na wauzaji maalum wa Coca Cola nchi nzima. Vipindi vya redio
vya SHUJAAZ
husikika kupitia East Africa Radio kila Jumamosi saa TISA kamili alasiri, Chuchu FM kila Jumamosi saa KUMI jioni, TBC FM kila Jumamosi saa KUMI NA MOJA jioni na Kings FM kila Jumamosi saa KUMI NA MBILI jioni.
Pia, DJ Tee anapatikana kwenye mitandao ya kijamii
kwa jina @djtee255