Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzina Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akimhoji Mhandisi Magesa Mwita wa
TANROADS, Mbeya kuhusu taarifa anayoitoa kwake ya maendeleo ya ujenzi wa
jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya wakati wa
ziara yake uwanjani hapo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzina Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya
la abiria la uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya wakati wa ziara yake
uwanjani hapo
Muonekano wa jengo jipya la
abiria ambalo halijamalizika ujenzi wake la uwanja wa ndege wa Songwe,
Mbeya kama lilivyokutwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye
(hayupo pichani) wakati wa ziara yake uwanjani hapo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akipita kwenye eneo la uwanja wa
ndege wa Mbeya ambao wananchi wamepimiwa viwanja 75 vya makazi kimakosa
ambapo Serikali inaurejesha kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania,
mmiliki halali wa eneo hilo ili uendelezwe. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa
Wilaya ya Mbeya Bwana William Paul Ntinika
…………………………………………………………………………
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi
Atashasta Nditiye ameielekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA) kumfikisha mahakamani mkandarasi anayejenga jengo jipya la abiria
la uwanja wa ndege wa Songwe lenye uwezo wa kuchukua abiria 1,500,000
kwa mwaka.
Mhandisi Nditiye ametoa maelekezo
hayo kwa TAA wakati wa ziara yake uwanjani hapo ya kukagua maendeleo ya
ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja huo. “Naielekeza TAA kuchukua
hatua za kisheria kwa kampuni hii ya DB Shapriya na kumpeleka
mahakamani mkandarasi huyu kwa kuwa mkataba wa miezi minane umechukua
miaka mitano na Serikali imeshamlipa fedha zote tangu mwaka 2015”,
amefafanua Mhandisi Nditiye.
Amesisitiza kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli haiko tayari kumvumilia mkandarasi
yeyote anayetumia vibaya pesa ya Serikali ya wananchi walipa kodi, hivyo
mkandarasi huyu ataitema fedha hii.
Mhandisi Nditiye ameongeza kuwa
Serikali itamshitaki mkandarasi huyu kwenye Bodi ya Usajili wa
Wakandarasi na Serikali haiko tayari kuendelea kufanya kazi na
wakandarasi wa namna hii. Aidha, amewahakikishia wananchi watanzania
kuwa jengo hilo litakamilika na Serikali itatafuta mkandarasi mwingine.
Mhandisi Nditiye ameitaka TAA
kuanzia tarehe 31 Januari mwaka huu ambapo ilipewa maelekezo na Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ianze kuikata
fidia ya uchelewashaji wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo mkandarasi huyo.
Naye Mhandisi Mshauri wa
kampuni ya kiuhandisi ya UNETEC kutoka Dubai Mhandisi Silanda Dustan
amesema kuwa mkandarasi hajafikia kiwango kinachotakiwa cha kujenga
jengo hilo la abiria ambapo wananchi wanakosa huduma na Serikali inakosa
mapato.
Serikali iliingia mkataba wa kazi
ya kujenga jengo jipya la abiria la uwanja huo na mkandarasi DB
Shapriya wa Tanzania wa gharama ya shilingi bilioni kumi na moja.
Mkataba huo ulisainiwa mwezi Februari mwaka 2013 na kazi ya kujenga
jengo hilo jipya la abiria ilitarajiwa kukamilika ndani ya miezi minane
hadi mwezi Oktoba mwaka 2013.
Akiwa uwanjani hapo, Mhandisi
Nditiye ametembelea uwanja huo ili kukagua na kujiridhisha kuhusu suala
la ukosefu wa taa za kuongoza ndege ambapo jambo hilo limezungumzwa
kwenye vikao baina ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu. Amebaini kuwa uwanja huo hauna
taa na hauwezi kufanya kazi saa 24 ambapo lengo la Serikali ni kuufanya
uwanja huo kuwa wa kimataifa na kwa sasa unahudumia abiria wa nchi za
jirani za Malawi, Zambia na RDC Congo.
Meneja wa Uwanja wa ndege wa
Songwe, Mbeya Bwana Hamisi Amiri amesema kuwa tayari mkandarasi wa
kampuni ya GECI Ispanola amepatikana kwa ajili ya kuweka taa za kuongoza
ndege kwa gharama ya shilingi bilioni 4.7 ambapo inajumuisha taa za
barabara ya kuruka na kutua ndege na taa za barabara. Ameongeza kuwa
uwanja wa ndege wa Songwe una uwezo sawa na uwanja wa ndege wa Mwalimu
Julius Nyerere wa Dar es Salaam wa kutua ndege kubwa ambapo kiwanja kina
ukubwa wa eneo la hekari 1,800 na barabara ya kutua na kuruka ndege
yenye urefu wa mita 3333 na upana wa mita 45.
Katika hatua nyingine Mhandisi
Nditiye ametembelea uwanja wa ndege wa Mbeya wenye ukubwa wa hekari 179
uliovamiwa na wananchi ambapo maafisa ardhi wasio waaminifu wamepima
viwanja 75 vya makazi na kuwapatia wananchi, na amelaani kitendo hicho
na Serikali itawachukulia hatua maafisa waliohusika. Pia amewaelekeza
TAA kuwekeza kwenye uwanja huo kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa
kuwa Serikali imefuta hati za viwanja hivyo na itaipatia TAA hati miliki
ya eneo lake. Pia, amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Amos Makalla
kwa kufuatilia eneo hilo na kuzuia wananchi kuliendeleza.
Naye Katibu Tawala Msaidizi wa
Miundombinu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Jeremia Minja amefafanua kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya Bwana Amosi Makalla amesimamisha zoezi la wananchi
kumiliki viwanja vya makazi na ameielekeza TAA kujipanga kuendeleza eneo
hilo.
Meneja wa uwanja wa ndege wa
Songwe, Mbeya Bwana Hamisi Amiri amesema kuwa TAA itapima eneo hilo
haraka mara baada ya kupata hati miliki kutoka kwa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.