MHANDISI JOYCE KISAMO WA WIZARA YA NISHATI ATWAA TUZO YA KIMATAIFA YA LUCE 2024

May 16, 2024

 

Mhandisi. Joyce Kisamo akiwa mwenyefuraha baada ya kukabidhiwa TUZO ya LUCE ya mwanamke aliyefanya vizuri katika nishati, mazingira na sekta endelevu (Legacy Women Category).
 
🔴Ni  Tuzo ya kutambua mchango wa mwanamke aliyefanya vizuri katika nishati, mazingira na sekta endelevu
Ni tu
 
Na. Mwandishi wetu
Mtanzania Mha. Joyce Kisamo kutoka Wizara ya Nishati amekua muafrika wa pili kutwaa tuzo ya LUCE ya mwanamke aliyefanya vizuri katika nishati, mazingira na sekta endelevu.
 
Mnigeria Onyinye Anene-Nzelu ambaye ni Mkuu wa Gridi Ndogo katika Ufikiaji wa Nishati nchini Nigeria, aliwahi kunyakua Tuzo katika kundi la wanawake chipukizi 2023.
 
Joyce, ambaye ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati alibuka mshindi wa shindano hilo la Tuzo za LUCE katika kundi la Mwanamke mwenye uzoefu na aliyeacha alama na kuwashinda wanawake wengine 15 kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya na Asia.
 
Zaidi ya kura 2,000 zilipigwa duniani kote na kura 600 zilitosha kumpa ushindi Mha. Joyce ambaye alikuwa mwafrika pekee na katika kinyang’anyiro hicho ameibuka mshindi kwa kuacha alama nyingi katika utendaji wake wa kazi (Legacy Women Category).
 
Kwa ushindi huo Joyce ametambulika kimataifa kuwa Mwanamke mwenye uzoefu, aliyefanyakazi na kuacha alama zenye manufaa kiuchumi, kimazingira na kijamii katika Sekta Endelevu hususani Nishati Safi na Endelevu.
 
Makabidhiano ya tuzo hiyo yamefanyika leo tarehe 16 Mei,2024 huko Florence nchini Italy kisha mshindi atahudhuria Mkutano wa masuala ya Nishati Safi na Endelevu. (Flagship Conference) kuanzia tarehe 23 hadi 25 Mei, 2024 katika European University Institute.
 
Tuzo za LUCE, zimefanyika kwa mara ya pili na linaandaliwa na mpango wa Lights on Women kwa ushirikiano na Landwärme na Edison, linalenga kutambua na kusherehekea mchango mkubwa wa wanawake.
 
Lengo la kuanzisha mashindano hayo ni kutetea majukumu muhimu ya wanawake kuelekea matumizi bora ya nishati endelevu.




Makonda aipongeza Benki ya CRDB msaada wa Pikipiki kwa Jeshi la Polisi kuimarisha Usalama kwa Watalii Jijini arusha

May 16, 2024

 

Arusha 16 Mei 2024 - Serikali imeipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa msaada wa pikipiki kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha ili kuimarisha doria zitakazoongeza usalama kwa watalii wanaokuja nchini. Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alipopokea pikipiki hizo zenye thamani ya Shilingi Milioni 50 kwenye hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Hoteli ya Gran Melia ya jijini humo.

Makonda amesema sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika uchumi na maendeleo ya wananchi nchini kwani ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni, ikiwa ya pili kwa kuchangia kwenye Pato la Taifa, na ya tatu kwa kutoa ajira.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa msaada huu wa pikipiki 20 ambao Benki ya CRDB imeutoa kwa Jeshi letu la Polisi. Pikipiki hizi zitasaidia askari wetu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na hivyo kuimarisha usalama kwa watalii na kuufanya mkoa wetu kuwa kivutio kikubwa cha wageni,” amesema Makonda huku akipongeza pia mpango wa Benki hiyo kuwawezesha wananchi kujenga nyumba za malazi maarufu kama ‘BNB’ kupitia programu ya IMBEJU inayotekelezwa na taasisi yake ya CRDB Bank Foundation.

Mwaka 2020, sekta ya utalii ilichangia asilimia 10.6 kwenye pato la taifa ila kiasi hichi kilishuka hadi asilimia 5.7 mwaka 2021 kutokana na athari za UVIKO-19 hivyo kuilazimu Serikali kuchukua hatua za makusudi kuifufua kwa kufuata taratibu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufanya matangazo kimataifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe kurekodi filamu ya ‘The Royal Tour.’
Mwaka 2023, idadi ya watalii waliofika Tanzania iliongezeka kwa asilimia 24.3 hadi kufikia 1,808,205 kulinganisha na watalii 1,454,920 mwaka 2022. Mapato ya utalii ya Tanzania yalifikia rekodi ya juu ya Dola za Marekani 3,368.7 milioni ikilinganishwa na Dola za Marekani 2,527.8 milioni mwaka 2022. Kutokana na kuimarika kwa sekta hiyo, Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limekadiria kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 sekta ya utalii itachangia 19.5% ya Pato la Taifa.

Ili kuhakikisha usalama wa watalii wanaokuja nchini, Serikali ilianzisha kitengo maalum cha utalii na diplomasia kwa ajili ya kuwahudumia watalii na wanadiplomasia wanaofika nchini kutalii ama kuwekeza kwa haraka. Kwa kuwa jiji la Arusha ndio kitovu cha utalii nchini, kituo hicho kimejengwa huko na askari wake walipewa mafunzo ya ziada ndani na nje ya nchi. 
Akikabidhi pikipiki hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kila mmoja anafahamu umuhimu wa amani, utulivu na usalama katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo Benki hiyo imetoa kipaumbele katika eneo hilo kupitia Sera yake ya Uwekezaji katika Jamii.

“Pamoja na kuwepo hali ya amani na utulivu nchini, bado baadhi ya matukio ya uhalifu hujitokeza kama vile vile uporaji wanaofanyiwa raia hata watalii wanaokuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini. Ili Jeshi la Polisi litekeleze majukumu yake kwa ufanisi linahitaji vitendea kazi vya kutosha,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi huyo amesema pikipiki hizo zitakwenda kuwasaidia askari kuwadhibiti wahalifu wanaowapora watalii na wananchi wengine hivyo kuharibu sifa njema za jiji hilo la kitalii. Mwaka jana Benki ya CRDB ilikabidhi pikipiki 15 kwa ajili ya kituo hicho kwa aliyekuwa Waziri wa Utalii wa kipindi hicho, Mohammed Mchengerwa.


Benki ya CRDB yawakaribisha Wanahisa kwenye Mkutano Mkuu wa 29

May 16, 2024

 

 
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (katikati), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wapili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (watatu kushoto), Katibu wa Kampuni Benki ya CRDB, John Rugambo (watatu kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (wakawanza kushoto, Mkurugenzi wa Manunuzi Benki ya CRDB, Pendason Philemon (Wakwanza kulia), na Meneja wa Kanda ya Kaskazini Benki ya CRDB, Cosmas Sadat wakionyesha Taarifa ya Mwaka 2022 ya Benki ya CRDB wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuwakaribisha wanahisa wa benki hiyo katika Mkutano Mkuu wa 29 utakaofanyika siku ya jumamosi ya tarehe 18 Mei 2024.
 
 ======     ========     =======

Arusha 16 Mei 2024 - Benki ya CRDB inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa siku ya Jumamosi tarehe Mei 18 kuanzia saa 2 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Taarifa hiyo imetolewa leo katika mkutano na waandishi wa habari uuliofanyika hoteli ya Gran Melia ambapo Benki ya CRDB pia ilizindua Ripoti yake ya Mwaka na Ripoti ya Uendelevu kwa mwaka 2023.

Mkutano huo unafanyika kufuatana na Sheria ya Makampuni namba 212 ya mwaka 2002, ambapo kila mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo unaowapa Wanahisa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha au kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki.
Akizungumzia katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay amesema mkutano huo utafanyika kwa njia mseto “Hybrid Meeting” ili kutoa fursa kwa wanahisa wengi zaidi kushiriki kwa njia ya kidijitali.
 
Dkt. Laay alisema kupitia mtandaoni Wanahisa wataweza kujiunga kuanzia saa 2:00 asubuhi kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App, ambapo imewekwa sehemu ya ya kujisajili kushiriki Mkutano Mkuu. 

“Tumeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa,” alisema Dkt. Laay huku akiwahakikishia kuwa Benki hiyo vizuri katika kuhakikisha wanashiriki bila chanagamoto yoyote.
Ajenda mbalimbali zitajadiliwa katika Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ni pamoja na uchaguzi wa wajumbe huru wa bodi, kuteua wakaguzi wa hesabu, na kujadili na kupokea Taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi, na Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa, pamoja na gawio kwa mwaka 2023 ambapo pendekezo la gawio la Sh 50 kwa hisa litawasilishwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, alisema pendekeo hilo la ongezeko la gawio kwa hisa linatokana na Benki ya CRDB kuendelea kupata matokeo mazuri sokoni ambapo mwaka wa fedha ulioisha ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi 423 bilioni ukilinganisha na Shilingi 351 bilioni  mwaka 2022.
Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utatanguliwa na semina maalum kwa wanahisa na umma yenye kauli mbiu ya “Ustawi wa Pamoja” itakayofanyika siku ya Ijumaa tarehe 17/05/2024 kuanzia saa 3 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). 

Dkt. Laay amesema Semina hiyo ambayo pia itaambatana na maonyesho ya wanufaika wa programu ya IMBEJU itafunguliwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema katika mkutano mkuu wa 29 wanahisa wa benki hiyo watapata nafasi ya kujadili juu ya mwaka mmoja wa utekelezaji mkakati mpya wa biashara wa muda wa kati wa miaka mitano wa 2023 – 2027. 
 
Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha wanahisa wa Benki ya CRDB kujitokeza kwa wingi kwani ushiriki wao utaiwezesha Bodi na Menejiment kupata maoni yao ya namna bora ya kuboresha utendaji wetu.
Akielezea kauli mbiu ya Mkutano wa mwaka huu wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ya “Ustawi wa Pamoja”, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Prof. Neema Mori amesema inaelezea namna ambavyo benki hiyo imedhamiria si tu kutengeneza faida bali pia kuongeza thamani ya uwekezaji wa wanahisa, kuchangia maendeleo ya wateja, na jamii kwa ujumla.