UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO BADO IPO JUU TANGA.

November 18, 2013
Na Oscar Assenga, Tanga.
IMEELEZWA kuwa hali ya uhalifu katika mkoa wa Tanga hasa kwenye makosa yanayohusu ukatili wa kijinsia na watoto inaonyesha bado upo juu huku jitihada kubwa zaidi zikihitajika kuweza kukabiliana nayo ili kuweza kutokomeza vitendo hivyo .

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Constatine Massawe aliyasema hayo wakati akizungumza hali ya ukatili wa kijinsia na watoto mkoa wa Tanga kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Januari hadi Octoba mwaka huu na kueleza takwimu zinaonyesha kuwapo kwa makosa hayo ambayo yanaathiri sana afya ya mwili na akili kwa mwanadamu kitendo ambacho ni ukiukwaji
mkubwa wa haki za binadamu.

Massawe alisema takwimu hizo zinaonyesha katika kipindi hicho jumla ya kesi 308 za ubakaji zilirekodiwa katika vituo vya polisi mkoa wa Tanga ambapo kati ya hizo 148 bado zipo chini ya upelelezi ,100 zinaendelea mahakamani,13 zilipata ushindi kwa washtakiwa kupatiwa adhabu mahakamani wakati kesi nyengine 5 zilishindwa mahakamani na 42 zilifungwa katika vituo vya polisi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa ushahidi wa kuweza kupeleka kesi hizo kwa mwanasheria waserikali kwa hatua zaidi za  kisheria.

Aidha alisema ndani ya miezi kumi iliyopita jumla ya makosa ya kulawiti 46 yalirekodiwa katika vituo vya polisi mkoa wa Tanga ambapo kesi 18 zipo chini ya upelelezi ,kesi 16 zipo mahakamani,kesi 01
ilipata ushindi mahakamani kwa washtakiwa kupatiwa adhabu wakati moja ilishindwa mahakamani na kesi 10 zilifungwa katika vituo vya polisi kwa sababu mbalimbali.

Kamanda Massawe aliongeza kuwa katika makosa ya kutupa watoto yalirekodiwa 04 ambapo kesi zote nne zilifungwa kwa sababu mbalimbali
pamoja na kueleza katika kipindi hicho makosa ya wizi wa watoto yalirekodiwa matatu kwenye vituo vya polisi ambapo kesi 02 zinaendelea mahakamani wakati kesi 01 ilifungwa.

Akizungumzia mauaji yaliyotokana na wivu wa mapenzi/ugoni na mauaji majumbani kwa kipindi hicho yalikuwa ni matukio 16 na kutoa wito kwa
jamii kuacha kufanya vitendo vya ukatili wa  kijinsia kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria .

ZIMBABWE KUTUA MCHANA KUIKABILI STARS

November 18, 2013

ZIMBABWE KUTUA MCHANA KUIKABILI STARS
Kikosi cha Zimbabwe kinawasili leo mchana (Novemba 18 mwaka huu) kuikabili Taifa Stars katika mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date itakayofanyika kesho (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo ukiwa na watu 30 utatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya Kenya Airways yenye mruko namba KQ 484 kupitia Nairobi.

Kocha wa timu hiyo Ian Gorowa atazungumza na waandishi wa habari mara baada ya timu hiyo kutua JNIA. Kiongozi wa msafara wa timu ya Zimbabwe ni John Phiri.

Wachezaji wanaounda kikosi hicho ni makipa; Frankson Busire, Maxwell Nyamupangedengu na Tapiwa Kapini. Mabeki ni Carrington Nyadombo, Felix Chindungwe, Innocent Mapuranga, Nkosana Siwela, Ocean Mushure na Patson Jaure.

Viungo ni Isaac Masami, Kundakwashe Mahachi, Milton Neube, Misheck Mburayi, Obey Mwenehari na Silas Dylan Songani. Washambuliaji ni Gerald Ndlovu, Lot Chiungwa, Nqobizitha Masuku, Simba Sithole na Themba Ndlovu.

Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Uganda wakati Kamishna atakuwa Leslie Liunda wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.

Viingilio ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B, sh. 15,000 kwa VIP C wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000.

Tiketi zinauzwa kwenye magari maalumu katika vituo vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Dar Live Mbagala, OilCom Ubungo, Uwanja wa Uhuru, na kituo cha mafuta Buguruni.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF