UWEPO WA MASHINE YA CT -SCAN KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA –BOMBO UMESAIDIA KUPUNGUZA RUFAA ZA WAGONJWA 900

February 09, 2024


Na Mwandishi Wetu,TANGA

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imejipambanua kwenye uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo katika huduma za afya ambapo kuna maboresho makubwa yamefanyika na hivyo kuwezesha huduma kuendelea kuimarika kwenye maeneo.

Si tu katika Hospitali za Taifa  na Kanda lakini pia Hospitali za Rufaa na wilaya ni miongoni mwa ambazo zimenufaika kupitia uwekezaji huo na hivyo kupunguza changamoto ambazo walikuwa wakikutana nazo wananchi awali kufuata baadhi ya huduma nyengine nje ya mikoa yao.

Miongoni mwa uwekezaji huo ni uwepo wa mashine za CT-Scan ambazo ni muhimu kwa kufanya uchunguzi kwa kutumia mionzi ambazo zinatumika kupima vipimo mbalimbali vya kichwa ,ubongo,kifua,tumbo pamoja na mshipa wa damu.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji huo ambapo kwa kiasi kikubwa umekuwa chachu na hivyo kuondoa changamoto ambazo walikuwa wanakumbana nazo wananchi hususani wa hali ya chini walikuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu.

Athumani Toba ni Mteknolojia wa Mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga  anasema uwekezaji huo uliofanywa na Serikali umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaondolea wananchi adha kubwa waliokuwa wakikutana nayo kulazimika kusafiri nje ya mkoa huo kwa ajili ya kwenda kupata huduma hiyo.

Anasema kwamba uwepo wa CT Scan ambacho ni kifaa muhimu katika kufanya uchunguzi kwa wagonjwa wakiwemo waliopata ajali za barabarani,wagonjwa walipata Shinikizo la damu, vipimo vya kifua ,kuangalia changamoto zilizopo kwenye vifua ikiwemo kufanya uchunguzi na kugundua magonjwa mbalimbali kwenye tumbo uvimbe,kansa na kugundua kansa kwenye utumbo na ubongo.

Toba anasema kitengo hicho kinamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba na hivyo kusaidia kupunguza rufaa  kwa wagonjwa kwenda kupata huduma hizo nje ya mkoa wa Tanga pamoja na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Frank Shega kwa kusimamia huduma hiyo ya CT Scan ambayo imewaondolea wananchi usumbufu wa kuifuata umbali mrefu.

 Akielezea huduma hiyo ilivyoanza anasema ilianza mwezi February mwaka 2023 na mpaka sasa wamekwisha kutoa huduma kwa wagonjwa 900 ambao wangeweza kupewa rufaa kwenye hospitali mbalimbali za nje ya Tanga na hivyo uwepo wake umesaidia kupunguza gharama kwa wateja na usumbufu kwao.

 “Kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa hili kwani wagonjwa hao wangelezimika kupatiwa rufaa kwenda nje ya mkoa wa Tanga kupata huduma hizo hivyo tunapenda kuishukuru Serikali kwa uwekezaji huo ambao umesaidia kuondoa kero kwa wananchi wa mkoa wa tanga

Hata hivyo anasema kwa sasa katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Bombo kupitia kitengo cha Mionzi,Idara ya Radiolojia inatoa huduma ya X-ray na Utrasound ambapo huduma za X-ray zinatolewa kuanzia za kawaida na zile maalumu hivyo hivyo kwa Utrou sound zinatolewa kuanzia zile za kawaida na maalumu na wanafanya ultrasound za wajawazito na magonjwa mbalimbali ya wakina mama na wanaume ikiwemo tezi dume.

 

SERIKALI YATIMIZA AHADI YA KUPELEKEA UMEME WA UHAKIKA LINDI NA MTWARA

February 09, 2024


--Mtambo wa Megawati 20 wawasili mkoani Mtwara
--Wabunge wapongeza

MTWARA

Serikali imeendelea kutekeleza ahadi ya kupeleka umeme wa uhakika katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameongoza mapokezi ya mtambo wa megawati 20 utakaozalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia.

Mtambo huo aina ya TM16 wenye mfano wa injini ya ndege ya Boeing 747 utafungwa katika Kijiji cha Hiari, Wilaya ya Mtwara Vijijini ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa changamoto ya upatikanaji umeme kwenye mikoa hiyo inatatuliwa.

Akipokea mtambo huo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, amesema kuwa mtambo huo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme kwenye Mkoa wa Lindi na Mtwara.

“ Mhe. Rais alitoa maelekezo kwa Wizara ya Nishati, kufanya kila jitihada ili changamoto ya umeme kwenye mikoa hiyo itatuliwe kwa haraka, tunashukuru leo tumeweza kutimiza ahadi hiyo kwani mtambo huu ni miongoni mwa mitambo ya kisasa kabisa ya umeme iliyowahi kuletwa nchini ambayo inatoa uhakika wa kuzalisha umeme kwa kipindi kirefu.” Amesema Mha.Mramba

Aidha, Mhandisi Mramba ameongeza kuwa, maelekezo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuhusu kuepeleka umeme wa gridi kwenye mikoa hiyo yameshaanza kutekelezwa ambapo kabla ya mwezi wa sita mwakani umeme wa Gridi ya Taifa utakuwa umefika kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ya kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo inayozalisha gesi kwa wingi wananufaika na uwepo wa nishati hiyo, amesema tayari wameanza kuboreshewa huduma mbalimbali ikiwemo kuwajengea kituo cha Polisi, ununuzi wa boti ya kisasa kwa ajili ya usafiri wa wananchi eneo la Songosongo mkoani Lindi na ujenzi wa kituo cha afya eneo la Madimba mkoani Mtwara..

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed alisema kuwa, wananchi wa Mtwara wamepokea kwa furaha mtambo huo ambao utafungua fursa za uwekezaji kwa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika kwani takriban asilimia 80 ya matumizi ya umeme mkoani humo yanatumika kwenye sekta ya biashara.

“ Tunamshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. Samia kwa kutimiza ahadi yake na na mapenzi ya dhati aliyoyaonyesha kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara na kufanya mikoa hii kupata umeme wa uhakika ambao utainua sekta ya uchumi kwa ujumla.” Amesema Kanali Ahmed

kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda ameishukuru Serikali kupitia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko kwa kusikiliza kilio cha wabunge wa mikoa juu ya changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuipongeza Wizara ya Nishati kwa hatua kubwa inazochukua kuhakikisha sekta ya umeme inaimarika.







MSAJILI WA HAZINA ZANZIBAR AWASHIKA MKONO WAATHIRIKA WA MAAFA HANANG’

February 09, 2024

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea mfano wa Hundi ya kiasi cha Shilingi Milioni 54.3 kutoka kwa Msajili wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Waheed Mohammad Ibrahim Sanya, kwa ajili ya waathirika wa Maafa ya Hanang’, Ofisini kwake Bungeni Dodoma Tarehe 9 Februari 2024.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea mfano wa Hundi ya kiasi cha Shilingi Milioni 54.3 kutoka kwa Msajili wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Waheed Mohammad Ibrahim Sanya, kwa ajili ya waathirika wa Maafa ya Hanang’, Ofisini kwake Bungeni Dodoma Tarehe 9 Februari 2024.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)




NA; MWANDISHI WETU – DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amepokea mchango wa Msajili wa Hazina Kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar uliyowasilishwa kwake Februari 9, 2024 wa kiasi cha Shiliingi za Kitanzania Milioni Hamsini na Nne nukta Tatu (54.3 Milioni) kwa ajili ya waathirika ya Maafa ya maporomoko ya tope, miti na mawe yaliyotokea tarehe 3 Disemba, 2023 mkoani Manyara.

Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma tarehe 9 Februari, 2024 Waziri Mhagama ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuguswa kwa kiasi kikubwa na maafa yaliyotokea Hanang’ ambayo yamesababisha watu kupoteza maisha na mali zao na kuongeza kusema kuwa, baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kutangaza hali ya hatari kabla ya kutokea kwa maafa hayo, Kamati za Maafa za Mikoa zilikuwa zimeshajipanga kwa kutoa elimu na tahadhari.

Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa Serikali inatekeleza ahadi yake ya kuwajengea nyumba waathirika wa maafa hayo na maandalizi ya awali yameshaanza kutekelezwa.

Aidha, Waziri Mhagama ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa msimu huu wa mvua za el nino zinazoendelea na kuongeza kusema kuwa msimu wa mvua za masika unakuja hivyo kila mmoja aendelee kuchukua tahadhari.

“Mmefanya jambo kubwa kuungana nasi kwa kuwashika mkono waathirika wa maafa ya Hanang’ kipekee ninawashukuru sana kwa moyo huu na mmeonesha faida za Muungano wetu na mashirikiano tuliyonayo katika hali zote, iwe furaha au majonzi kama haya, ninaahidi kuendelea kutoa ushirikiano nanyi,” alisisitiza Mhe Mgahama.

Kwa Upande wake Msajili wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Waheed Mohammad Ibrahim Sanya alisema, Ofisi yake iliguswa na maafa yaliyotokea Hanang’ na kuona kuna kila sababu ya kuungana kwa kuwashika mkono waathirika hao kwa kutoa mkono wa Pole.
=MWISHO=

RPC MANYARA AKERWA NA VITENDO VYA UKATILI, KUINGIA MTAANI KUTOA ELIMU

February 09, 2024

 Na John Walter -Manyara


Ukatili wa kijinsia unasalia kuwa kitendo cha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu duniani kote.

Nchini Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa raia wa kwanza kuonesha wazi kukerwa na wanaofanya vitendo hivyo viovu na kuagiza vyombo vinavyohusika kusimamia kikamilifu kuvitokomeza.

Ukifika mkoani Manyara ukatili unazungumzwa kila uchwao lakini bado wapo wasiosikia hali ambayo imemlazimu Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Manyara George Katabazi kulazimika kuingia mtaani na kwenye vijiji kuzungumza na wananchi akisisitiza kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na vitendo vingine vya uhalifu kwa kutoa taarifa kabla tukio halijatokea.

Mkoa wa Manyara ni Miongoni mwa mikoa inayotajwa kuongoza kwa matukio ya ukatili vikiwemo vipigo, ubakaji na mauaji.

Februari 6 mwaka huu majira ya asubuhi katika kijiji cha Magugu, Binti (19) mwenye ulemavu wa kutokusikia na kuongea, alibakwa na mtu mmoja anayedaiwa aliwahi kuhukumiwa jela miaka 30 mwaka 2022 kwa Kosa la kumbaka Binti huyo huyo na baadaye kuachiliwa huru baada ya kukata rufaa.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Magugu wilayani Babati, Katabazi amesema vitendo vya Ukatili haswa ubakaji vinavyofanyika katika kata ya Magugu na maeneo mengine ya mkoa wa Manyara sio vya kunyamaziwa kwa kuwa vinaharibu taswira ya mkoa.

Jeshi hilo limeahidi kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa huyo ili kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria kujibu tuhuma zinazomkabili.

KIWANDA CHA SUKARI CHA MKULAZI YAINGIZA SHEHENA ZA SUKARI MTAANI

February 09, 2024

 Na Mwandishi wetu


Kiwanda kipya cha Sukari cha Mkulazi Kilichopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kimeingiza rasmi sheheza za bidhaa ya sukari kwa matumizi ya majumbani kwa mara ya kwanza tangu kuanza uzalishaji wenye lengo la kupunguza makali ya bei za sukari yanayowakabili wananchi katika Maeneo mbalimbali hapa Nchini.

Afisa mwandamizi wa masoko na mauzo kutoka Kampuni hodhi ya Mkulazi Bi,Milkasia Joseph Mnkeni amebainisha hayo wakati wa zoezi la upakiaji wa Sukari ya ujazo wa kilogram 25 ambayo imeanza kuingizwa rasmi sokoni kwa mkoa wa Morogoro.

Milkasia alisema Sukari hiyo imekidhi viwango vya ubora wa hali juu baada ya bidhaa hiyo kupitishwa katika vipimo vyote kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo imelengwa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kiungo katika aina mbalimbali za mapishi yanayotajwa Kwenda kuwafurahisha watumiaji wa sukari hiyo sokoni.

“Tumeanza zoezi la kuuza Sukari, na kuanza kupakia kwenye magari ya wateja ambayo yamefika kiwandani kwetu leo, Kwasasa tayari tumeshaainisha wateja wetu, Tunawakaribisha Watanzania wote ambao ni wafanyabiashara kufanya kazi na sisi, Kuingiza Sukari yenye ubora wa hali ya juu wa hali ya juu sokoni, Kwaajili ya Kuisadia Nchi yetu na kupunguza nakisi ya Sukari.” Alisema Bi Milkasia Joseph.

Naye Afisa uhusiano wa Kampuni hodhi ya Mkulazi Bi, Clementina Patrick alisema wamejipanga vyema kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia Watanzania wote kwa bei elekezi za Serikali ili kuwapunguzia watumiaji wa bidhaa hiyo machungu kutokana na mfumuko wa bei uliosababishwa na uhaba wa sukari mtaani.

“Kama mnavyoona leo ndio siku ya Kwanza tunaingiza bidhaa yetu ya sukari sokoni, Kwasasa tumeanza na sukari ya majumbani (Brown Sugar) na tunatarajia hapo baadae kuzalisha pia na sukari za viwandani, Sukari yetu tumeiuza kwa bei elekezi kwa Wafanyabiashara, Pia tunatarajia itawafikia Watanzania kwa bei elekezi ya Serikali ili kuwapunguzia Wananchi makali.” Alisema Bi Clementina Patrick.

Kwaupande wake Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi Mhandisi Aaron Mwaigaga alisema kiwanda hicho kinaendelea na zoezi la uchakataji wa sukari ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo mtaani unaosababishwa na mvua zinazondelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.

Mhandisi Mwigaga alisema Mkulazi imejidhatiti kuendelea kupeleka sukari sokoni licha ya changamoto za Mvua zinazoendelea lakini pale hali ya hewa inapotulia watajitahidi kuendelea na zoezi la uchakataji wa Sukari ili kupunguza nakisi ya sukari kwa wananchi kama ambavyo malengo ya Serikali yalivyo katika kupunguza makali ya bei kwa jamii.

Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ni Kiwanda Kipya kikimilikiwa kwa ubia wa hisa asilimia 96% kutoka kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na hisa asilimia 4% zikimilikiwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza (SHIMA) huku kikianza Uzalishaji wa majaribi ya sukari yake mwezi Disemba 2023.





DKT. TULIA AKIFUNGUA MKUTANO WA KIBUNGE MAREKANI

February 09, 2024

 Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson, akifungua Mkutano wa Kibunge wa Umoja wa Mabunge Duniani katika Umoja wa Mataifa (2024 Parliamentary Hearing at the United Nations) leo tarehe 8 Februari, 2024. 

Mkutano huu unaofanyika katika Ukumbi wa Kamisheni ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani, unaohudhuriwa na Mabunge ya nchi 180 Duniani na mwaka huu unaangazia mada kuu ya “Amani na Usalama wa Kesho: Nia nzuri ya kuleta matokeo ya pamoja.”PICHA NA OFISI YA BUNGE.



SERIKALI YAIAGIZA MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO (EGA), KUDHIBITI MATAPELI WA MTANDAONI

February 09, 2024



Na Seif Mangwangi,Arusha

SERIKALI imeutaka uongozi wa Mamlaka ya Serikali mtandao kushirikiana na mamlaka zingine za ulinzi na usalama kutafuta suluhu ya kudhibiti matapeli wanaotumia mtandao kuibia watu jambo ambalo limekuwa likigombanisha Serikali na wananchi inayowatumikia.

Wito huo umetolewa leo Februari 8, 2024 na Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa kikao kazi cha nne cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) uliokuwa ukifanyika jijini hapa.

Naibu Waziri Kikwete amesema matapeli wamekuwa kero kubwa kwa nchi na mbaya zaidi wamekuwa wakiwatapeli watu masikini ambao Uchumi wao ni mdogo kwa kutumia matangazo ya uongo huku wakiwadai fedha.

“Binafsi nilishawahi kutapeliwa na bwana mmoja ambaye alinipigia simu akidai kuwa tunafahamiana na alikuwa na tatizo, na mimi bila kujua nilimtumia fedha lakini baadae ndio nikaja kugundua nimetapeliwa, amesema na kuongeza:

“Hawa jamaa wanatumia akili nyingi sana, wanaweza ku edit matangazo mbalimbali na kuwatumia watu, unakuta mtu ni maskini na ana uhitaji wa huduma hiyo kama ni kazi au masomo na mwisho akitakiwa kutuma fedha atatuma na hapo anakuwa kisha tapeliwa, hii sasa ni mbaya sana, niwatake tu watendaji wa eGA, muangalie namna ya kufanya kuthibiti hili tatizo.”amesema.

Amesema Serikali itahakikisha maombi mbalimbali yaliyowasilishwa na mamlaka hiyo itayatekeleza kwa wakati ili kurahisisha utendaji kazi wa mamlaka hiyo hususani kuharakisha taasisi zote za Serikali zinaunganishwa Pamoja.

Aidha amewataka wakuu wa Taasisi za Serikali kuhakikisha wataalam wa Tehama katika taasisi zao wanaendelezwa kitaaluma ili kuendana na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia ambayo imekuwa ikikua kila siku.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema katika kikao hicho wameweza kubainisha changamoto mbalimbali ikiwemo udurufu wa taarifa za Serikali lakini wameshaweka mikakati ya kukomesha hali hiyo.

Ndomba amesema zaidi ya wadau 3,000 wameweza kushiriki katika kikao hicho ikiwa ni ongezeko la zaidi ya wadau 2000 waliokuwa wakitarajiwa kushiriki hapo awali jambo ambalo limeleta mafanikio makubwa kwa mamlaka hiyo na kurahisisha utendaji wake wa kazi.

Washiriki katika Kikao hicho walitoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma wakiwemo; Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA, Maafisa TEHAMA Pamoja na watumiaji wengine wa TEHAMA katika taasisi hizo kwa lengo la kujadili na kutoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao katika taasisi za umma.




HIFADHI YA TAIFA BURIGI -CHATO TAYARI KUPOKEA WATALII

February 09, 2024

 Na Pamela Mollel,Chato

 Hifadhi ya Taifa ya Burigi -Chato, Sasa ipo tayari kupokea malfu ya watalii baada ya Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) kukamilika miundombinu ya barabara na mawasiliano ambayo awali ilikuwa ni shida.

Hifadhi hii iliyonzishwa mwaka 2019 ,kiasi cha sh bilioni 3.3 tayari zimetumika kuimarisha miundombinu yake ili watalii wa ndani na nje waweze kutembelea .

Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi Ismaili Omari akizungumza na waandishi wa habari za Utalii na Uhifadhi waliotembela hifadhi hiyo, alisema wanaalika watalii kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea hifadhi hiyo.

" Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA ) limefanya maboresho makubwa ya Miundombinu na kazi inaendelea lakini pia Kampuni ya simu ya TTCL imeweka mnara wa Mawasiliano hifadhini" amesema.

Mhifadhi Omar alisema barabara zenye urefu wa kilomita 97.5 pamoja na madaraja na vivuko yamejengwa lakini pia sasa umekamilika ujenzi wa kambi za Utalii na makazi ya bei nafuu ya watalii ndani ya hifadhi .

"Lakini pia tunahifadhi mazingira na uoto wa asili na Sasa wanyamapori wameongezeka na wanaonekana kirahisi"amesem

Afisa utalii hifadhi ya Burigi- Chato ,Aldo Mduge amesema upekee wa hifadhi hiyo ni uwepo wa ndege aina ya Domo kiatu (African Shoebill) maziwa yanayo zunguka hifadhi wanyama wengi na ndege aina 400.

Mduge amesema hivi Sasa kuingia katika hifadhi hiyo ni rahisi kwa usafiri wa barabara,Anga na kupitia Maji .

"Awali kulikuwa na changamoto lakini Sasa hifadhi inafikika maeneo yote na tuna vivutio vingi ikiwepo wanyama wa kubwa kama Tembo,Simba,Chui,Nyati,Twiga na wengine "amesema

Akizungumzia makazi wa ndani ya hifadhi, Kaimu mkuu idara ya utalii hifadhi hiyo, Emmanuel Nyundo hiyo alisema uwekezaji walio ufanya ikiwemo kujenga kambi ya wageni ya kudumu huku akiwakaribisha wageni kuwekeza katika hifadhi hiyo kwani kuna maeneo mazuri.

"Kuna maeneo ya ujenzi wa kambi za Utalii,mahoteli na vivutio vingine vya Utalii"amesema

Hifadhi hii ina kilomita za mraba 4707 katika wilaya za Biharamulo,Chato,Karagwe ,Ngara na Muleba ipo katika mikoa ya Kagera na Geita.



HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAPOKEA MAGARI YA KUBEBEA WAGONJWA

February 09, 2024

 



Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha sekta ya afya kwa kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma ili kusaidia wagonjwa wa kanda ya kati kufika kwa wakati Hospitalini.

Akizungumza baada ya hafla ya kupokea magari hayo, Mbunge wa Dodoma mjini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema magari hayo yataondoa changamoto ya wagonjwa wanapopata rufaa.

"Naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha sekta ya afya na kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kupata Huduma bora za afya”,amemshukuru Mhe. Mavunde.

Ameongeza kuwa magari ya kubebea wagonjwa ni muhimu sana kwa BMH kwani Hospitali hii imekuwa kimbilio sio tu kwa wakazi wa Dodoma na kanda ya kati bali kwa watanzania kwa ujumla.

"Tutasimamia magari haya yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kubeba wagonjwa ," amesisitiza Mhe. Senyamule

Nitajitahidi kwa nafasi yangu kuhakikisha tunaongeza gari lingine la wagonjwa kwa kuwa hospital hii inahudumia watu wengi zaidi ya hospital nyingi za hapa Dodoma hivyo ni muhimu kuboresha eneo hili”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amesema magari hayo yatasaidia sana katika kusafirisha wagonjwa wa rufaa kutoka Hospitalini hapo na hivyo kutumia fursa hiyo kuishukuru sana serikali kwa magari hayo ya kisasa na yenye vifaa muhimu vya matibabu ambayo yatarahisisha utoaji huduma kwa wagonjwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya sekta ya Afya mkoani Dodoma na kuutaka uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuyatunza magari hayo na kuhakikisha yanafanya kazi iliyokusudiwa.





RAIS SAMIA AMPOKEA MGENI WAKE RAIS WA POLAND ANDRZEJ DUDA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

February 09, 2024

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mgeni wake Rais wa Poland Mhe. Andrzej Duda mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Poland Mhe. Andrzej Duda mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024
.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama pamoja na mgeni wake Rais wa Poland Mhe. Andrzej Duda wakati wa Wimbo wa Taifa ukiimbwa katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.

Rais wa Poland Mhe. Andrzej Duda akikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Poland Andrzej Duda, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.

Rais wa Poland Andrzej Duda akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni wake Rais wa Poland Andrzej Duda, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Poland Mhe. Andrzej Duda wakati wakielekea kwenye mazungumzo Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari, 2024.

KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU DKT JIM YONAZI AONGOZA KIKAO MAALUMU UENDELEZAJI WA MAKAO MAKUU DODOMA

February 09, 2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameongoza Kikao maalum kilichohusu uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma, Kikao kimefanyika katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Dodoma, Tarehe 9 Februari, 2024.