MZEE KINESI AMECHAFUA HALI YA HEWA SIMBA SC, YETU MACHO HUKO MSIMBAZI

November 19, 2013

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam

MGOGORO mwingine unakuja Simba SC, katika wakati ambao klabu inahitaji kujipanga ili kurejesha makali yake yaliyopotea kwa mwaka wa pili sasa.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, walikutana jana usiku katika kikao bila ya Mwenyekiti wao, Alhaj Ismail Aden Rage na kuchukua maamuzi mazito.

Maamuzi hayo ni; kwanza kumsimamisha Mwenyekiti wao, Rage kwa madai hawana imani naye na pili kuwasimamisha makocha wa timu hiyo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ na Msaidizi wake, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’, kwa madai hawaridhishwi na uwezo wao.
Mzee umechafua hali ya hewa; Joseph Itang'are Kinesi kushoto akiwa na Geoffrey Nyange 'Kaburu' kulia jana Uwanja wa Karume, saa chache kabla ya kwenda kufanya kikao cha kumng'oa Rage

Baada ya hayo, Kamati pungufu ya Utendaji, bila ya Mwenyekiti aliyechaguliwa na wanachama kuongoza klabu, ikaamua kumfanya Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ kuwa kocha Msaidizi wa kocha mpya, atakayetangazwa Desemba 1.

Matola ambaye kwa sasa ni kocha wa Simba B, ataanza kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi wakati kocha mpya wa kigeni akisubiriwa.

Aidha, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ ambaye alichaguliwa kama Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, akajibebesha jukumu la kukaimu nafasi ya Rage, wakati tayari anakaimu nafasi ya Makamu Mwenyekiti, iliyoachwa wazi na Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyejiuzulu mapema mwaka huu.

Kikao kilifanyika jana Jumatatu, wakati Jumapili Rage alifanya zoezi la kusajili wachezaji wawili wapya, kiungo Awadh Juma na mshambuliaji Ally Badru, wote kutoka Zanzibar.

Kinesi alipoulizwa na Waandishi wa Habari kuhusu Rage kutokuwepo kwenye kikao cha jana, akajibu amesafiri, lakini swali linakuja kwa nini kikao kisifanyike akiwepo na kama kuna tuhuma akazijibu?

Lakini pia, Kinesi hakuweza kuwaambia Waandishi wa Habari sababu ya kumsimamisha Rage, zaidi ya kusema tu hawana imani naye.

Mamia ya wanachama walionyesha imani kwa Rage na wakamchgua kwa kura nyingi kuwa Mwenyekiti wao, iweje leo watu wanne au watano wachukue maamuzi mazito dhidi yake?

Wazi hapa Kinesi na wenzake waliokutana kwenye kikao cha jana waneleta mgogoro ambao utazidi kuiyumbisha Simba SC na kuifanya pia izidi kuboronga katika Ligi Kuu.       

Simba SC ina tatizo la uongozi na hilo limeonekana wazi katika kipindi chote cha utawala wa Rage kuwapo madarakani, lakini kitendo cha baadhi ya Wajumbe kufikia maamuzi mazito jana ni ukaribisho wa tatizo lingine kubwa ndani ya klabu.

Rejea mapema mwaka huu wakati baadhi ya wanachama walipofanya Mkutano na kutangaza kuung’oa uongozi mzima wa Rage, baadaye likatokea kundi kubwa la wanachama kumpokea Uwanja wa Ndege kwa maandamano ya kishujaa akitokea India na kutibiwa na kusistiza huyo ndiye Mwenyekiti wao.

Na hali kama hii ndiyo inatarajiwa kujirudia sasa ila katika makali zaidi, kwa sababu safari hii si wanachama waliofanya maamuzi, bali viongozi wenzake Rage. Yetu macho na masikio huko Msimbazi.   

*UFOO SARO ASHIRIKI IBADA MAALUM YA KUSHUKURU MUNGU KWA KUMPONYA NA UMAUTI KWA TUKIO LILILOMKUTA

November 19, 2013


Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro (wa pili kulia) akisoma somo kwenye biblia  wakati wa ibada maalumu ya shukrani kwenye Kanisa la (KKKT ) Usharika wa Kibamba nje kidogo ya Jiji la Dare Salaam jana. Picha na Sanjito Msafiri.  
MTANGAZAJI wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi, amefanya ibada na kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumponya.”
 
Ni mara ya kwanza Saro kuzungumza tukio hilo tangu aliporuhusiwa kutoka Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu, MOI ya Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.
Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, Jimbo la Magharibi, Ufoo huku akitokwa na machozi na wakati mwingine kushindwa kuzungumza alisema: “Ni miujiza tu ya Mungu yeye kunifanya mimi kuwa hai leo.” 
Mtangazaji huyo ambaye alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili, aliwashukuru watu wote waliomtia moyo, kumsaidia kipindi chote alichokuwa mgonjwa.
  
“Sina cha kuwalipa, ninawashukuru sana kwa wema wenu, pia kwa kuniombea. Mungu ni mkubwa na amenipigania, naendelea vizuri kwa sasa,” alisema na kuongeza:
  
“Mungu alinisimamia na nyinyi pia mliniombea, hakika sina budi kushukuru kwa kila jambo. Nitasoma zaburi ya 146 katika Biblia Takatifu ili kumshukuru Mungu kwa kunisaidia.”
  
Ufoo alisema kuwa ameamua kumshukuru Mungu kwa sababu siyo watu wote wanaopata matatizo kama yake wanapona.
  
Mchungaji aliyeongoza misa hiyo iliyoanza saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana, Joseph Maseghe alisema Mungu hakupanga Ufoo afariki dunia kwa kupigwa risasi.
  
“Mungu bado anakuhitaji, hakupanga ndiyo maana upo nasi leo. Hautakiwi kulia huu ni mwanzo wa maisha yako mengine, usilie unachotakiwa ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema.
  
Misa hiyo ilihudhuliwa na watu mbalimbali wakiwamo wafanyakazi wa ITV pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kihwelu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche.
  
Baada ya kumalizika kwa misa hiyo, ndugu na marafiki wa karibu wa Ufoo walialikwa na mtangazaji huyo katika hafla fupi ya chakula cha mchana.
  
Akizungumza wakati akiwakaribisha wageni katika chakula cha mchana, alisema: “Nimepata pigo kubwa katika maisha yangu, familia yetu sasa haina baba wala mama, kweli namshukuru Mungu na nawaombea kwa Mungu wote walioniombea na kunitakia mema, sijui nimpe nini Mungu, sijui kwa kweli. Chanzo:- MWANANCHI.

MWALALA:TUMEPANIA KUCHEZA LIGI DARAJA LA KWANZA

November 19, 2013

Muheza.
KOCHA Mkuu wa timu ya Halmashauri ya Muheza inayoshiriki Ligi ya mkoa wa Tanga,Benard Mwalala amesema timu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika michuano hiyo ni ishara tosha wanakaribia kutimiza malengo yao ya kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Mwalala alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Tanga Raha mara baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi hiyo kati yao na Lushoto Stars ambapo walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-0,mchezo uliochezwa katika uwanja wa soka Jitegemee wilayani hapa.

Bao la kwanza la Halamshauri lilipatikana katika dakika ya 20 kupitia Chalengwa Sultani ambaye alitumia uzembe wa mabeki wa timu pinzani kupachika wavuni bao hilo kabla ya Abasi Athumani kupachika bao la pili dakika ya 25.

Mpaka timu zote zikienda mapumziko,Halmashauri FC waliweza kutoka kifua mbele kwenye mchezo huo na kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo iliwachukua dakika 16 ya kupindi hicho Halmashauri kupata bao la tatu ambalo lilifungwa na Abasi Athumani ambaye aliifungia timu hiyo na bao la nne kaatika dakika ya 70.

Karamu ya mwisho ya mabao kwa timu hiyo iliweza kuhitimishwa na Ramadhani Msumi aliyemalizia krosi maridadi iliyopigwa na Abasi Athumani na kukwamisha wavuni bao hilo .

Mwalala alisema malengo yake makubwa na timu hiyo ni kuhakikisha wanapambana vilivyo ili kuweza kupata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa wa mikoa na hatimaye ligi daraja la kwanza na ligi kuu soka Tanzania ili kurudisha hamasa ya soka iliyokuwepo wilayani hapa.

WANANCHI kOROGWE WAUKATAA MRADI WA UMWAGILIAJI

November 19, 2013

Korogwe
WANANCHI wa Kijiji cha Mswaha Darajani Kata ya Mswaha wilayani Korogwe mkoani Tanga wamekataa kuupokea mradi wa umwagiliaji wa kijiji hicho kwa madai ya kujengwa chini ya kiwango.
 
Hatua ya wananchi hao waliiweka bayana katika mkutano wa kijiji hicho  ambao ulifanyika Novemba 7 mwaka huu katika mradi huo uligharimu zaidi ya milioni 42 kuanzia hatua za awali mpaka mwisho.
 
Kilichopelekea mradi huo kukataliwa na wananchi hao mbele ya diwani wa Kata hiyo,Aweso Omari ambaye aliambatana na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo Paulo Mzava kilitokana na ukuta wa kukingia maji uliojengwa kumepasuka na hivyo kushindwa kutumika licha ya kugharimu fedha hizo.
 
Akizungumza katika mkutano hao mmoja ya wananchi hao ,Juma Mussa alisema wanamuomba mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwapelekea wataalamu ili waangalie jinsi mradi huo ulivyohujumiwa ikiwemo kuchukuliwa hatua wahusika.
 
   “Ninaamini endapo Mkurugenzi wa Halamshauri atakuja kuangalia mradi huo yatapatikana mafanikio ikiwemo kulipatia ufumbuzi suala la mradi huo “Alisema Mussa.
 
Mussa alifika mbali zaidi kwa kumuomba mkuu wa wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo kutembelea eneo hilo ili ajionee jinsi mradi huo ulivyoharibika na kushindwa kufanya kazi huku wananchi wakiendelea kuteseka.
 
Akizungumzia mradi huo,Diwani Aweso alisema mradi huo ulitengewa sh.milioni 35kwa ajili ya utengenezaji huo wa mradi ambao ulipagwa kutumika kwenye shughuli za umwagiliaji kwenye mbuga ya mswaha darajani.
 
  “Baada ya kuchelewa kwa mradi huo nililazimika kumtafuta diwani wa kata hiyo Aweso ambapo alinijibu kuwa mradi huo utapasuka muda wowote ule kutokana na kujengwa chini ya kiwango“Alisema Aweso wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili.
 
Aweso alisema mkandarasi aliyepewa kujenga mradi huo alijenga chini ya kiwango hali ambayo ilipelekea kushindwa kufanya kazi ipasavyo badala yake kupasuka na kuendelea kuwapa tabu wananchi wa maeneo hayo.

JAMHURI FC YAONGOZA KWA KUTAFUTA MAKOCHA

November 19, 2013

 Na Masanja Mabula - Pemba .

Wakongwe wa soka Kisiwani Pemba Timu ya Jamhuri ya Pemba imebainika kuwa ni moja ya vilabu vinavyongoza kuwafuta kazi makocha wake ambapo kwa kipindi cha miaka mitano klabu hiyo imewahi kufundishwa na makocha watano .

Utaratibu huo wa kuwafukuza makocha wanaoifundisha klabu hiyo , huenda ikawa ndiyo sababu ya kuifanya ishindwe kufanya vyema kwenye ligi kuu ya soka Visiwani Zanzibar kwani wachezaji wameshindwa kushika mbinu na kocha ambao wamekuwa hawadumu na kikosi .

Timu hiyo ambayo ni ya  kwanza kuwahi  kuchukua ubingwa wa ligi Kuu wa Zanzibar kwa timu za kutoka Kisiwani Pemba , msimu uliopita ilifundishwa na Kocha Salum Bausi ambaye muda mfupi alibwaga manyanga kwa kile alichodai kupingana na uopngozi wa klabu hiyo .

Bausi ambaye kwa sasa ni kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar , aliicha timu ya Jamhuri baada ya kubaini uswahiba uliopo kati yake na timu ya Mafunzo ya Mjini Unguja .

Kocha mwengine aliyewahi kuifundisha na kuipa mafanikio ni Renatus Shija ambaye aliwezesha kushika nafasi ya pili ya ligi kuu ya Zanzibar na kuishiriki ligi ya Shirikisho Barani Afrika ambapo walitolewa katika hatua ya kwanza na timu ya Hwange kutoka Zimabwe .

Shija ambaye alikuwa nakubaklika na wachezaji pamoja na mashabiki wa timu kutokana na mbinu zake , alitimuliwa na nafasi yake ikashinkwa na Sebastian Mkoma ambaye naye hakuchukua duru na kubwaga manyanga .

Baada ya kocha Sebastian kuiacha timu hiyo ilikuwa chini ya Kocha msaidizi Mohammed Mzee  , na msimu huu timu hiyo iliongezea nguvu kwa kumwajiri kocha Said Mohammed ambaye naye amaipa kisog hivi karibuni kutoka na sintofahamu kati yake na  Viongozi .

Kwa sasa timu hiyo yenye mashabiki wengi Kisiwani Zanzibar inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi kuu ya Zanzibar baada ya kushuka uwanjani mara 11 huku ikiambulia alama tatu baada ya kutoka sare michezo mitatu pekee .