PSSSF TAYARI IMEWALIPA WANACHAMA 750 WALIOKUMBWA KWENYE SAKATA LA VYETI FEKI

December 02, 2022

 NA MWANDISHI WETU, ARUSHA.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) tayari umewalipa wanachama 750 waliokumbwa na sakata la vyeti “feki”, baada ya kuwasilisha madai yao na nyaraka stahiki.

Akizungumza wakati wa kikao kazi na wanachama wapatao 60 wa klabu ya waandishi wa habari jiji la Arusha kwenye ukumbi wa Kituo Cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) leo Ijumaa Desemba 2, 2022, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe amesema, zoezi la kuwalipa lilianza Novemba 1, 2022 na ni endelevu.

“Zoezi linaendelea vizuri, Wanachama waliopo katika orodha ya serikali na PSSSF  ni 9,771 ambao wanadai malipo ya takribani shilingi bilioni 22.22.” Alifafanua. 

Akizungumzia madhumuni ya kikao hicho na wanachama wa klabu hiyo ya waandishi wa habari jijini Arusha wapatao 60,  Bw. Mlowe alisema “lengo ni kutoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko pamoja na kuendeleza uhusiano mzuri ukiopo kati ya Mfuko na wanahabari wa Arusha”.

Mambo mengine aliyozungumzia Bw. Mlowe ni pamoja na Malipo ya Mafao na Pensheni, Uwekezaji, Thamani ya Mfuko pamoja na mafanikio ambayo PSSSF imeyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF, PPF,LAPF na GEPF.

“ Kila mwezi PSSSF inaingiza kwenye mzunguko zaidi ya shilingi bilioni 180 ikijumuisha malipo ya pensheni ya mwezi zaidi ya shilingi bilioni 60 zinazolipwa kwa wastaafu 158,000 pamoja na Mafao mengine zaidi ya shilingi bilioni 120,” alibainisha.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanachama wa klabu hiyo, Katibu wa klabu hiyo, Bw. Seif alisema wanashukuru kwa fursa hii na wameweza kufahamu kwa undani juu ya PSSSF na utekelezaji wa majukumu yake na sasa wanaweza kutoa taarifa sahihi na muhimu kwa wadau wa PSSSF.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe(kulia), akizungumza kwenye kikao hicho, kushoto ni Kaimu Meneja wa Klabu ya Waandishi wa Habari Kanda ya Kaskazini, Bw. Baraka Kitundu.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe(kulia), akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.
Bi. Hilda Kileo, akizungumza kwenye kikao hicho.
Bw.Allan Kileo akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.


. KHALFAN S. 0716745281

AFRIKA YAKUTANA KUJADILI HATMA YA PUNDA

December 02, 2022
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) na baadhi ya Viongozi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) wakifurahia jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam.
Mkurugenzi wa Mtandao wa kutetea haki za wanyama kutoka Kenya Bw. Josphat Ngonyo akiwaeleza Waziri wa Mifugo na Uzalishaji wa wanyama kutoka Chad Dkt. Abderahim Awat (kushoto) na  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) namna wanyama aina ya Punda wanavyotumika nchini kwake  muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam. Wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Vuongozi na watendaji kutoka zaidi ya mataifa 20 wanachama wa Umoja wa Afrika na watendaji kutoka Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) na Shirika linaloshughulikia haki za wanyama kazi (Brooke East Africa) wakati wa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameziongoza nchi zaidi ya 20 wanachama wa Umoja wa  Afrika ambazo zimekutana leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam kwa ajili ya kujadili hata ya wanyama aina ya punda wanaodaiwa kuwa kwenye hatari ya kutoweka.

Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Ulega amewataka wataalam kutoka katika nchi hizo kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo ya kitafiti na kisayansi kuhusu njia zinazoweza kutumika kuwaokoa wanyama hao na kuziwasilisha ili zijumuishwe  katika sera na kanuni  kwa ajili ya utekelezaji.

“Kama tulivyofanikiwa katika kupiga vita biashara nyingine ambazo zilikuwa zikitupelekea kwenye kupoteza wanyama wetu basi mtafakari kama wataalam na kuja na tafiti za kisayansi zitakazotushawishi sisi watunga sera ili tuweke mkazo wa kupiga marufuku kama tulivyoweka kwa upande wa biashara ya meno ya Tembo” Amesisitiza Mhe. Ulega

Aidha Mhe Ulega amependekeza wanyama aina ya punda kujumuishwa kwenye kundi la viumbe waliopo hatarini kutoweka ili kuongeza nguvu ya jitihada zinazofanywa kwa ajili ya kuokoa hatma yao ambapo amesema kuwa hatua hiyo itafufua jitihada za kuongeza idadi ya wanyama hao.

“Lakini pia wakati mkijadili mnapaswa kujua kuwa pamoja na umuhimu wake kule vijijini wananchi wanashawishiwa kuuza punda wao kwa sababu ya umasikini hivyo wakati tunafikiria namna ya kudhibiti hali hii ya utowekaji wa Punda tufikirie namna ya kuwaelimisha na kuangalia njia mbadala kwa wanakijiji hao ili wasiwauze”Ameongeza Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa msisitizo mkubwa wa Tanzania katika mkutano huo ni kuueleza ulimwengu kuhusu hatua walizochukua katika kudhibiti hali ya kutoweka kwa punda ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uuzwaji na uchinjwaji wa wanyama hao.

“Lakini jambo jingine tumeiambia dunia kuwa sisi kupitia mfumo wetu wa Sera tumeamua kulinda wanyama hawa kupitia eneo la ustawi wa wanyama lililopo kwenye mabadiliko ya sera ya Mifugo ya mwaka huu ambayo yanaendelea kufanyika” Amesema Nzunda.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) Dkt. Nick Nwankpa amesema kuwa katika nchi zote za Afrika wanyama aina ya Punda wamekuwa na msaada mkubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kusaidia katika shughuli zote za kiuchumi.

“Lakini pamoja na msaada huo, Punda wamekuwa wakichukuliwa kama wanyama kazi tu ambao wamesahaulika hata kwenye sera na kanuni mbalimbali zinazolinda haki za wanyama na kadri idadi kubwa ya watu inavyoongezeka ndipo idadi ya punda inavyopungua” Amesema Dkt. Nwakpa.

Akielezea sababu za kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania Mwenyekiti wa Shirika linaloshughulikia haki za wanyama kazi (Brooke East Africa) Bw. Erick Kimani amesema kuwa hatua hiyo imetokana nchi hiyo kuwa ya kwanza kupiga marufuku biashara ya Punda ambapo amezitaka nchi nyingine za Afrika kuchukua hatua hiyo ili kuondoa hatari ya kutoweka kwa wanyama hao.

Mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar-es-salaam umelenga kujadili kwa kina umuhimu wa wanyama aina ya punda kiuchumi na kijamii na unatarajia kuwa na maazimio yatakayosaidia kuwaondoa wanyama hao kwenye hatari ya kutoweka.

 

WAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WADAU WA MKONGE

WAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WADAU WA MKONGE

December 02, 2022

 



Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Tatu wa Wadau wa Mkonge utakaofanyika Desemba 4, mwaka huu jijini Tanga.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona katika taarifa iliyotolewa kwa umma na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa bodi hiyo Esther Mbusi, mkutano huo utawakutanisha viongozi mbalimbali wa kitaifa na Wadau wa Sekta ya Mkonge nchini.

“Napenda kuwakaribisha wakazi wa Tanga na maeneo jirani kuhudhuria kwenye Mkutano huo mkubwa wa Wadau wa Sekta ya Mkonge unaofanyika kwa mujibu wa Sheria ya Na. 2 ya Sekta ya Mkonge ya Mwaka 1997.  
 
“Katika mkutano huo tunatarajia Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, lakini viongozi wengine watakaokuwepo kwenye ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde ambaye atamwakilisha Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, viongozi wote wa Mkoa, Waheshimiwa Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa jirani hususani ile inayolima Mkonge.
 
“Kama mnavyofahamu, Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele na ameshika bendera ya kuhamasisha Kilimo cha Mkonge, tulianza naye tangu mwaka 2019 hadi mwaka 2021 amekuwa akija Tanga kuhimiza watu waingie kwenye Kilimo cha Mkonge kwa sababu anafahamu faida za Mkonge zao ambalo linaweza kubadilisha maisha ya Watanzania kwa muda mfupi sana, zao la kudumu la uhakika na biashara ya Mkonge ni nzuri,” amesema Kambona kwenye taarifa hiyo. 

Kambona amesema mkutano huo pia ni fursa kwa Wanatanga kibiashara kwani kutakuwa na wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao watahudhuria mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Mkonge nchini.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi Desemba 2, na Kikao cha Kamati Ndogo ya Maendeleo ya Zao la Mkonge inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima na Mwenyekiti Mwenza, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella utakaofanyika Desemba 3, wilayani Korogwe jijini Tanga. Kauli mbiu ya mkutano huo ni; ‘Mkonge ni biashara, wekeza sasa.’