TAFIRI NA OMAN KUFANYA UTAFITI WA SAMAKI BAHARI YA HINDI

May 13, 2022




Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye mazungumzo ya awali na uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA), ukiwa umeambatana na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi katika ofisi za Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutia saini hati ya makubaliano ya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. (12.05.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini hati ya makubaliano ya utafiti katika Sekta ya Uvuvi kwa Ukanda wa Bahari ya Hindi baina ya Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ana matumaini na uhakika kazi itafanyika vizuri na kuleta matokeo ambayo nchi ina matarajio makubwa katika kukuza Sekta ya Uvuvi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama wa pili kutoka wa kulia) na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania (aliyesimama wa tatu kutoka kushoto) Dkt. Salim Al-Harbi, wakishuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano baina ya Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) katika ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi, wakibadilishana nyaraka mara baada ya utiaji saini hati ya makubaliano baina ya OIA na TAFIRI kwa ajili ya kufanya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari wa Hindi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi na watafiti kutoka Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, mara baada ya hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi baina ya TAFIRI na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA). (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Na. Edward Kondela

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetia saini hati ya makubaliano na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) ili kufanya utafiti utakaosaidia kutathimini kiwango cha samaki kinachoweza kupatikana kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi hivyo kusaidia ongezeko la wawekezaji katika Sekta ya Uvuvi.

Utiliaji saini wa makubaliano hayo yamefanyika leo (12.05.2022) jijini Dar es salaam baina ya Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei na Mkurugenzi Mtendaji wa OIA katika Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi, ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki mara baada ya kushuhudia makubaliano hayo amesema yana lengo la kutathimini kiwango cha samaki kinachoweza kupatikana katika eneo la bahari na itakuwa ni mara ya kwanza kufanyika hapa nchini.

Waziri Ndaki amefafanua kuwa kazi ya kutathimini kiwango cha samaki kilichopo katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ina gharama kubwa na kwamba inahitaji fedha nyingi na rasilimali zingine ili kuweza kufanya kazi yenye matokeo mazuri.

“Tuna matumaini na uhakika kazi itafanyika vizuri na kuleta matokeo ambayo sisi kama nchi tuna matarajio makubwa sana.” Amesema Mhe. Ndaki.

Waziri Ndaki ameongeza kuwa bado sekta ya uvuvi inachangia pato dogo kwa taifa hivyo utafiti huo utasaidia nchi kuwa na mipango ya uhakika juu ya uvunaji wa rasilimali za uvuvi na kushawishi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei akafafanua juu ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kubainisha kuwa utafiti huo utafanyika kwa kushirikisha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI) ili kutimiza malengo ya sekta ya uvuvi Tanzania Bara na Visiwani.

Dkt. Kimirei amesema makubaliano hayo yatawezesha muda wowote kuwasili kwa meli ya kufanya utafiti ili kuiwezesha nchi kupata takwimu ya aina, wingi na mtawanyiko wa samaki katika ukanda wa bahari ili nchi iweze kupata taarifa sahihi ya uwepo wa samaki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi amesema utafiti huo utasaidia kuongeza thamani ya biashara katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kwa Tanzania na kwamba wanatarajia huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano baina ya Tanzania na Oman katika shughuli mbalimbali zinazohusu Sekta ya Uvuvi.

Zoezi la utiaji saini wa hati ya makubalino baina ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) kwa ajili ya kufanya utafiti wa samaki katika ukanda wa Bahari ya Hindi limeshuhudiwa pia na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi.

Mwisho.

UJERUMANI NA TANZANIA KULINDA HIFADHI ZA BAHARI YA HINDI

May 13, 2022

 

Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei, Mratibu wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Dkt Nichrous Mlalila na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) Bw. John Komakoma wakiwa kwenye mazungumzo na Mratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania Bw. Ralf Senzel na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann waliofika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo namna ya kukazia ushirikiano baina ya Tanzania na Ujerumani, kupitia mradi wa uhifadhi wa bainuai za Bahari ya Hindi na Maeneo Tengefu ya Ukanda wa Pwani, utakaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani. (Picha na Edward Kondela – Afisa habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akisoma moja ya nyaraka za mradi wa uhifadhi wa bainuai za Bahari ya Hindi na Maeneo Tengefu ya Ukanda wa Pwani, utakaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kuanzia Mwezi Agosti Mwaka huu katika kipindi cha miaka minne kwa thamani ya Euro Milioni 2.17 sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 5.2, mradi utakaotekelezwa Kaskazini mwa Tanzania katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga na Kwale Mkoani Kenya, mara baada ya kutembelewa na ujumbe kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, ambapo Dkt. Tamatamah amesema mradi huo una faida kubwa katika kuhifadhi bainuai na kutoa elimu kwa jamii inayokaa katika maeneo hayo. (Picha na Edward Kondela – Afisa habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei akichangia hoja wakati wa mazungumzo baina ya ujumbe wa Tanzania kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini pamoja na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) juu ya mradi wa uhifadhi wa bainuai za Bahari ya Hindi na Maeneo Tengefu ya Ukanda wa Pwani, utakaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kuanzia Mwezi Agosti mwaka huu. Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam. (Picha na Edward Kondela – Afisa habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Kutoka kushoto ni Mratibu wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Dkt. Nichrous Mlalila na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) Bw. John Komakoma wakimsikiliza Mratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania Bw. Ralf Senzel na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann waliofika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam kuzungumzia mradi wa uhifadhi wa bainuai za Bahari ya Hindi na Maeneo Tengefu ya Ukanda wa Pwani, utakaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani katika kipindi cha miaka minne. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia), Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann (kulia kwake) na Mratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania Bw. Ralf Senzel (kushoto kwake), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei (wa pili kutoka kushoto), Kaimu Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) (wa kwanza kushoto) na Mratibu wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Dkt. Nichrous Mlalila (wa kwanza kulia), mara baada ya kuhitimisha mazungumzo ya kukazia ushirikiano baina ya Tanzania na Ujerumani hususan katika Sekta ya Uvuvi yaliyofanyika katika ofisi ndogo za wizara zilizopo jijini Dar es Salaam. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)



Na. Edward Kondela



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amekutana na ujumbe kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na kufanya mazungumzo ya kukazia ushirikiano baina ya Tanzania na Ujerumani, kwenye uhifadhi wa bainuai za Bahari ya Hindi na Maeneo Tengefu ya Ukanda wa Pwani.

Akizungumza leo (13.05.2022) mara baada ya kukutana na ujumbe huo katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam, Dkt. Tamatamah amesema katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kutakuwa na miradi mingi ambapo kwa kuanzia Mwezi Agosti Mwaka huu 2022, mradi utafanyika Kaskazini mwa Tanzania katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga na Kwale Mkoani Kenya.

Katibu mkuu huyo mara baada ya kukutana na ujumbe huo ambao ni Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann na Mratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania Bw. Ralf Senzel, amesema Tanzania itapata Euro Milioni 2.17 sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 5.2 kwenye mradi huo katika kipindi cha miaka minne.

“Huu mradi una faida unalenga kuhifadhi bainuai, utatoa elimu kwa jamii inayokaa katika maeneo hayo na tunategemea mradi utafanya rasilimali kuwa endelevu kwa muda mrefu na utaongeza kipato kwa wananchi, kwa kuwa wataelimishwa njia mbadala za maisha na kuhifadhi Maeneo Tengefu.” Amesema Dkt. Tamatamah.

Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann amesema ana furaha kwamba ushirikiano baina ya Ujerumani na Tanzania katika maeneo ya bainuani na Maeneo Tengefu utakuwa na nguvu katika kuhakikisha Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi unatunzwa pamoja na kuhakikisha rasilimali zilizopo katika Maeneo Tengefu zinaendelezwa, huku Mratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania Bw. Ralf Senzel, amesema mradi huo utajenga uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo baina ya Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann pamoja na Mratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania Bw. Ralf Senzel, yamehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) Bw. John Komakoma ambapo mradi huo utatekelezwa na Mratibu wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Dkt .Nichrous Mlalila.

Mwisho.