TARURA YAENDELEA KUIFUNGUA KILOSA KIUCHUMI

September 21, 2023

 


#Ujenzi wa madaraja kwenye mito kuwaepushia vifo wananchi

****
Imeelezwa kwamba ndani ya kipindi kifupi kumekuwa na maendeleo katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi katika maeneo ya vijijini na mijini hii inatokana na kazi kubwa ilivyofanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunganisha barabara za mijini na vijijini ikiwemo maeneo ya masoko pamoja na maeneo ya uzalishaji.


Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo wakati akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofanya na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Kilosa.


Mhe. Londo amesema kuwa kazi kubwa imefanyika Mikumi na kwa mafanikio makubwa ujenzi wa daraja la Ruhembe lenye urefu wa mita arobaini kukamilika kwake litasaidia kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa eneo hili waliyokuwa nayo kwa muda mrefu wakiwemo wajawazito na wagonjwa waliokuwa wakienda kupata huduma mbalimbali ng’ambo ya mto huo.


“Daraja hili ni muhimu sana kwa maisha ya wakazi wa Bonde la Ruhembe, kata za Kidodi na Ruaha kwa sababu linaenda kuwapunguzia umbali kutoka kilomita 32 walizokuwa wakizunguka hapo awali mpaka kilomita 2 kutoka barabara kubwa kwenda kijijini, pia eneo hili ni mabondeni hivyo wakati wa mvua barabara zilikua hazipitiki kabisa na kusababisha akiba ndogo ya mkulima kutumika sana kwa ajili ya usafirishaji wa pembejeo za kilimo na kukamilika kwa daraja hili linaenda kupiga vita adui umaskini”,amesisitiza Mhe. Londo.


Kwa upande wa barabara Mbunge huyo amesema barabara ya kilomita tano kutoka Kidodi kwenda Kidunda imekamilika ambapo kijiji hicho cha Kidunda hakikuwahi kupata barabara tangia uhuru”Milima ya Kidunda ndio ilikua ikilisha eneo kubwa la mkoa hivyo sasa hivi uzalishaji umeongezeka kwani sasa mazao yote yanasafirishwa kwa usafiri mbalimbali na hivyo tunaweza kuona miundombinu hiyo inavyoleta maendeleo na uwekezaji unaongezeka”.
Aidha, amesema barabara ya kilomita 42 kutoka Ulaya kwenda Kisanga upande wa Kilosa ambayo ilikua haipitiki takribani miaka 20 na sasa inaenda kukamilika na kuunganika kwa barabara hiyo inaenda kumpunguzia mwananchi umbali wa zaidi ya kilomita 75 ambapo alikua akitumia saa tatu na hivyo kukamilika kwa barabara hiyo mwananchi ataenda kutumia nusu saa kufika pia kukosekana na barabara hiyo ilisababisha vifo vingi kwani watu wengi walikua wanachelewa kupata huduma muhimu hususani huduma za afya.


Amesema sasa hivi jimbo la Mikumi linaenda kuunganishwa na ndio fahari kwa wananchi kwani Serikali ya Awamu ya Sita inaenda kutatua kero kwa wananchi”Kila mmoja anaguswa na hii miradi ya TARURA kwani inashiriki kikamilifu kwa kuhakikisha miundombinu wanayojenga inawagusa kila mwananchi na hivyo kuinua uchumi kwa kuongeza tija katika uzalishaji”.


Hata hivyo amewataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara isiharibike ili kuifanya Serikali kuweza kupeleka maendeleo sehemu nyingine kwakuwa wajibu wa mwananchi ni kulinda miundombinu na kuifanya serikali kutumia fedha zake kwa maendeleo mengine.


Naye, Diwani wa Kata ya Ulaya Mhe. Ally Kibati ameishukuru TARURA kwa usimamizi mzuri wa kukamilisha barabara na ujenzi wa Box karavati la Ulaya-Kisanga ambapo kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakipata changamoto nyingi hususani za kusafirisha mazao yao lakini hivi sasa barabara imefunguka na hivyo kuwapunguzia gharama za usafirishaji.


Wakati huo huo Mkazi wa Kata ya Ulaya Steven Mahanga ameipongeza Serikali kwa kuwaletea mradi wa ujenzi wa Box karavati la ulaya-kisanga kwa sababu awali kulikuwa kunatokea mauaji mengi kutokana na kukatika kwa barabara na hivyo kama raia wapo tayari kuilinda miundombinu hiyo ili kupata maendeleo zaidi katika kata yao.

NEMC YATOA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA ZEBAKI KWENYE MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA

September 21, 2023

 


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea na utoaji wa elimu ya Matumizi sahihi ya Kemikali ya Zebaki bila kuathiri afya na mazingira katika Maonesho ya Sita ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Mkoani Geita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho hayo wakati wa semina Mkurugenzi wa Tathimini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (NEMC) Bi. Lilian Lukambuzi amesema wanashiriki katika maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ambao hasa wamekuwa wakitumia Zebaki katika kuchenjua madini ya dhahabu.

"Hii imetokana na Mradi ambao tunausimamia unaolenga kuhifadhi mazingira na kudhibiti matumizi ya Zebaki, lengo letu waweze kuelewa na kuona shughuli ambazo wanazifanya katika uchenjuaji wa madini kwa kutumia zebaki zinawezaje kuathiri afya na mazingira". Amesema

Aidha, amesema elimu hiyo itawafanya waelewe ni namna gani wanaweza kutumia teknolojia mbadala ili waweze kuepuka madhara ya kiafya na mazingira katika matumizi ya Zebaki.

Kwa upande wake Mchimbaji mdogo wa dhahabu Mkoani Geita Bw. Alex Bawaziri ameipongeza NEMC kwa kuhakikisha inawapa elimu ya kutosha wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika matumizi ya zebaki kwenye uchenjuaji, hivyo watatumia elimu hiyo kuhakikisha wanajiepusha na matumizi yasiyosahihi ya Zebaki.

Nae mchimbaji mdogo wa dhahabu kutoka Mkoani Mwanza, Bi. Salome Kusekwa amesema mafunzo hayo yamewaelimisha hasa katika kujikinga na zebaki katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu, hivyo atatumia elimu ambayo ameipata kwenda kuwaelimisha wachimbaji wenzake ambao wamekuwa hawana elimu ya matumizi sahihi ya zebaki.

Huduma za uzazi wa mpango zaimarika Simiyu, mwanaume aridhia kufunga kizazi

September 21, 2023

 

Mwanaume mmoja katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ameridhia kufunga mirija ya uzazi kama njia ya kudumu ya uzazi wa mpango, kwa lengo la kuwa na watoto wachache anaomudu kuwahudumia.

Mwanaume huyo, John Sayi (47) mkazi wa Kijiji cha Sulu Kata ya Mbalagani amesema tayari ana watoto sita hivyo ameridhia kwa hiari uamuzi huo baada ya kupata elimu ya umuhimu uzazi wa mpango kupitia vyombo vya habari.

“Nilipata msukumo kutoka kwa baba mzazi ambaye alikuwa na wanawake wanne lakini hakutana kuwa na watoto wengi kwani alizaa watoto sita tu. Wake zake watatu kila mmoja alizaa mtoto mmoja akiwemo mama yangu na mwingine alizaa watoto watatu” amesema Sayi.

Amesema alipata nafasi ya kuongea na baba yake ambaye ametangulia mbele za haki aliyemweleza kwamba alikuwa akitumia njia ya asili ya uzazi wa mpango hivyo na yeye ikamuingia akilini kuwa na watoto wachache.

Mwaka 1998 Sayi alioa mke wa kwanza na kuzaa naye watoto wawili kabla ya kutengana mwaka 2002 ambapo kwa sasa anaishi na mke wa pili aliyemuoa mwaka 2,000 na kujaaliwa kupata watoto wanne hadi alipofunga mirija mwaka huu 2023.

“Wasukuma tuna tabia ya kuzaa watoto wengi, mwanaume ukimwambia mwanamke aache kuzaa anafikiri akifanya hivyo utaendelea kuzaa na wanawake wengine hivyo nilipomwambia mke wangu nataka kufunga uzazi aliamini nimedhamiria kutoendelea kuzaa” amesema Sayi na kuongeza na kukubaliana nami;

“Kwenye tendo la ndoa najisikia vizuri maana kwa sasa nachelewa kumaliza tofauti na hapo awali, wengi hatupendi kumaliza mapema hivyo wanaume wenzangu wasiwe na hofu kwamba ukifunga mirija ya uzazi utapata madhara” ameeleza Sayi.

Inaelezwa watu wengi wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango za muda mfupi na muda mrefu ambazo ni pamoja na vidonge, vipandikizi, vitanzi na kondomu tofauti na ilivyo kwa njia ya kudumu ambayo ni kufunga mirija ya uzazi kama alivyofanya Sayi.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH, Mratibu wa afya ya uzazi na mpango mkoa wa Simiyu, Mary Makunja amesema wanawake wanaoongoza kwa kutumia uzazi wa mpango ikilinganishwa na wanaume.

“Kabla ya mradi huduma za uzazi wa mpango zilikuwa asilimia 36 mwaka 2022 lakini kwa sasa (2023) ni asilimia 45 huku idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya/ hospitali ikifikia asilimia zaidi ya 90” amesema Makunja.

Amebainisha kuwa mwitikio wa kutumia njia za uzazi wa mpango za muda mfupi na mrefu ni mkubwa ikilinganishwa na njia ya kudumu; akisema “kwa mwaka idadi ya wanawake wanaoridhia kufunga mirija ya uzazi inafikia 100 huku wanaume wakiwa kati ya mmoja hadi watatu”.

Makunja ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa jamii ya wakazi wa Simiyu kutumia uzazi wa mpango hatua itakayowasaidia kuwalea vyema watoto wao tofauti na ilivyo sasa ambapo mwanamke anaweza kuwa na nzao kati ya saba hadi kumi jambo ambalo ni hatari kiafya.

“Jamii ya watu wa huku asilimia kubwa ni wakulima hivyo wanaona ni fahari kuoa mwanamke zaidi ya mmoja na kuzaa watoto wengi wakiamini watawasaidia kwenye shughuli za uzalishaji mali hivyo tunaendelea kuwaelimisha” amesema Makunja.

Kutokana na umuhimu wa uzazi wa mpango katika kukabiliana na vifo vya uzazi kwa wanawake na watoto, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali likiwemo shirika la JHPIEGO linalotekeleza mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuelimisha jamii, kuwajengea uwezo wataoa huduma za afya pamoja na kuboresha huduma katika vituo vya afya na hospitali ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mmoja wa wanaume mkoani Simiyu, John Sayi (47) aliyeridhia kutumia njia ya uzazi wa mpango ya kudumu akizungumza na wanahabari waliomtembelea wilayani Maswa kwa ajili ya kufanya naye mahojiano.
Mratibu wa afya ya uzazi na mpango mkoa wa Simiyu, Mary Makunja akizungumzia hali ya utoaji huduma za uzazi wa mpango.

GST YABAINISHA UWEPO WA MGODI WA URANI UTACHOCHEA UTALII WA MADINI NAMTUMBO

September 21, 2023


*GST yashiriki Kongamano la Wadau kuhusu Fursa za Uwekezaji Namtumbo* 

Wilaya ya Namtumbo imetajwa kuwa na fursa kubwa ya uwepo wa Utalii wa Madini baada ya kugundulika kuwa na kiasi kikubwa cha madini ya Urani ambapo ndiyo utakuwa na mgodi wa kwanza wa uzalishaji wa Madini hayo kwa Afrika Mashariki na miongoni mwa nchi chache zitakazo kuwa na mgodi wa urani duniani.

Hayo ameyabainisha Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Maswi Solomon wakati akimuwakilisha Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoa mada kwenye Kongamano la Wadau kuhusu Fursa za Uwekezaji Wilaya ya Namtumbo lililofanyika katika ukumbi wa St. Agness-Namtumbo uliopo Wilayani humo.

"Mgodi wa kuzalisha Urani wa Mkuju ndiyo utakuwa mgodi wa kwanza Afrika Mashariki kuzalisha Urani, hivyo tunaona ni fursa kwetu katika kuchochea Utalii wa Madini kwa watu kuja kujionea ni namna gani kama nchi tumeweza kuendesha mgoni wa Urani unaoweza kutoa mionzi yenye madhara kama tahadhari isipozingatiwa, hivyo Wilaya ya Namtumbo inaenda kuwa kitovu cha Utalii wa Madini na mtapokea wageni wengi kuja kujifunza uzalishaji wa madini hayo kama ambavyo na sisi tumekuwa tukienda kujifunza kwenye migodi ya nchi kama Namibia," amesema Maswi.

Maswi amesema GST  inajukumu kubwa la kukusanya taarifa za madini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji na kuishauri Serekali lakini pia, ina jukumu la kutoa elimu ya majanga ya asili ya Jiolojia ikiwemo matetemeko ya ardhi na madhara ya Jiolojia kama milipuko ya volkano na miamba inayoweza kuwa na sumu au mionzi.

Pia, Maswi amesema Namtumbo imebahatika kuwa na madini ya Urani ambayo yanatumika kutengeneza nishati safi isiyo na hewa ya ukaa na amewatoa wasiwasi wakazi wa Namtumbo kuwa, uchimbaji wa madini ya Urani hauwezi kuathiri mazingira kama taratibu za kitaalamu zitazingatiwa katika uchimbaji na uchakataji wake ambapo ametoa mfano kwa nchi za Namibia, Niger, Afrika Kusini na Gaboni ambapo uzalishaji wake unaendelea lakini hakuna madhara yoyote yaliyotokea hivyo Tanzania haita kuwa nchi ya kwanza kuwa na mgodi wa Urani kwa Afrika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngollo Malenya amefarijika kuona Wilaya ya Namtumbo kuwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo urani, dhahabu, chuma, Ulanga na Vito mbalimbali ambapo Kampuni ya Mantra imejenga mgodi mdogo wa majaribio kwa ajili ya kuanza kuyavuna madini hayo.

"Kama tungepata Wawekezaji wengi, Wilaya ya Namtumbo tungekuwa mbali kimaendekeo hivyo, kupitia Kongamano hili naomba tushirikiane ili tuone ni kwa namna gani tutaweza kuinua Sekta ya Madini katika Wilaya yetu," amesema Malenya.

Kongamano hilo lililokutanisha zaidi ya washiriki 400 limebebwa na Kauli Mbiu isemayo "Mapinduzi ya Kilimo, Biashara Utalii Hifadhi ya Mwalimu Nyerere na Utalii wa Madini".

HAFLA YA BALOZI GASTON KUKABIDHIWA OFISI YA NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

September 21, 2023

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akishuhudia makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Everisto Longopa (kulia) ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ya vitendea kazi Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mpya, Balozi Prof. Kennedy Gaston. Hafla hiyo fupi iliyofanyika katika Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Septemba 20,  2023.Hafla hiyo pia ilihusisha kumuaga Dkt Longopa. 
Balozi Prof. Gaston akikabidhiwa na Jaji Dkt. Longopa nyaraka mbalimbali  za kufanyia kazi.


Jaji Dkt. Longopa (kushoto) akimkabidhi rasmi ofisi Balozi Prof. Gaston.
Balozi Prof. Gaston akisaini kwenye kitabu baada ya kukabidhiwa ofisi.
Jaji Dkt. Longopa akizungumza wakati wa hafla hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Balozi Prof. Gaston.
Balozi Prof. Gaston akitoa neno la shukrani baada ya kukabidhiwa ofisi na Jaji Dkt. Longopa na kuomba ushirikiano na watumishi wa ofisi hiyo.
Katibu Sheria Mkuu wa ofisi hiyo, Esther Cheyo akitoa neno la kumkaribisha Balozi Prof. Gaston.
Mwandishi Mkuu wa Sheria wa ofisi hiyo, Onorius Njole akitoa neno la kumkaribisha Balozi Prof. Gaston kwa niaba ya watumishi wa ofisi hiyo na kuahidi kwamba watumishi wako tayari kutoa ushirikiano kwake.
Baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo wakiwa nje tayari kumlaki  Balozi Prof. Gaston.
Balozi Prof. Gaston akikabidhiwa shada la maua alipowasili  katika ofisi hiyo.
Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Huduma za Ushauri wa ofisi hiyo, Dkt. Gift Kweka akitoa neno la kumkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mhe. Jaji Dkt. Feleshi kuzungumza wakati wa makabidhiano hayo.
Baadhi ya viongozi wa ofisi hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza wakati wa makabidhiano hayo na kuwataka watumishi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Balozi Prof. Gaston.


 Mwanasheria Mkuu wa Seikali (AG), Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (katikati) akiwa na Balozi Prof. Gaston (kulia) pamoja na Jaji Dkt. Longopa.

IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA

0754264203


NCAA KUFUNGUA MALANGO MAPYA MAWILI YA KUINGIA HIFADHI YA NGORONGORO.

NCAA KUFUNGUA MALANGO MAPYA MAWILI YA KUINGIA HIFADHI YA NGORONGORO.

September 21, 2023

 

Na Kassim Nyaki, NCAA.

Katika uboreshaji wa huduma kwa watalii wanaongia ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inatarajia kufungua malango mawili mapya katika eneo la Engaruka na Eyasi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Kamishna wa NCAA (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii) Elibariki Bajuta wakati wa ziara ya Viongozi Chama cha waongoza utalii Tanzania (TTGA) waliotembelea hifadhi ya Ngorongoro.

Bajuta ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuboresha huduma kwa wageni wanaongia ndani ya hifadhi, kuongeza mtawanyiko kwenye vivutio vya utalii na kupunguza msongamano wa wageni katika geti la Loduare na barabara kuu ya Loduare, Seneto hadi Golini ambapo ni mpakani mwa hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti.


Naibu Kamishna Bajuta amebainisha maeneo yatakayojengwa malango hayo kuwa ni eneo la Eyasi ambapo ujenzi wa lango umekamilika na kazi zinazoendelea ni kusimika mifumo ya malipo na mtandao wa intaneti sambamba na uboreshaji wa barabara ya kutoka Eyasi kupitia mlima Endulen, Ndutu hadi uelekeo wa Serengeti ili wageni wanaokuwa eneo la ziwa Eyasi kwa shughuli za utalii wa kiutamaduni (Cultural Tourism) wasilazimike kurudi Karatu na kuingilia geti la Loduare kwenda Ngorongoro.

Lango la pili litajengwa mpakani mwa eneo la Engaruka na Empakaai kreta na ujenzi huo utaenda sambamba na kufungua barabara itakayoanzia Engaruka kuelekea kreta za Empakaai, Olmoti kreta, mlima Lolmalasin hadi kreta ya Ngorongoro.

“Ujenzi huu unalenga kupanua wigo wa huduma kwa wageni ili watawanyike kwenye vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi, geti la mpakani mwa Empakaai na Engaruka litakapokamilika wageni wanaoenda kutalii eneo la ziwa Natron hawatalazimika kurudi mto Wambu hadi Karatu ili waingie hifadhi ya Ngorongoro” ameongeza Bajuta.

Amebainisha kuwa ujenzi wa malango hayo utaanza katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 na kukamilika mwaka ujao wa fedha 2024/2025.

Sambamba na ujenzi wa malango hayo Serikali kupitia NCAA iliweka mkandarasi wa kukarabati barabara kutoka eneo la View Point hadi Nayobi yenye urefu wa kilomita 78 ambayo tayari imeshakamilika na kusaidia ongezeko la watalii kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko mashariki mwa hifadhi Ngorongoro ambavyo ni, Empakaai Kreta, Olmoti Kreta, Mlima Lolmalasin na maeneo ya nyanda za juu kaskazini.

Aidha katika kuongeza mtawanyiko wa watalii ndani ya Hifadhi, NCAA inaendelea na ujenzi wa barabara mpya ya kiwango cha changarawe kutoka Enduleni hadi Ndutu yenye urefu wa kilomita 45, hadi sasa kilomita 20 zimekamilika na kilomita 25 zilizobaki mkandarasi anaendeleo na ujenzi.

Barabara hii inayopita eneo la Ndutu ambalo ni maarufu kwa mazalia ya Wanyama wanaohama (Nyumbu) itakapokamilika, wageni watapata fursa ya kupitia Endulen, Ndutu hadi mpakani mwa hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti bila kupita barabara kuu ya Loduare, Seneto, Golini, Serengeti.