TUPO TAYARI KUIKABILI ZIMBABWE- NOOIJ
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema
wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi ya
Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja
Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo anawafahamu
wachezaji wengi.
Amesema wachezaji wanaounda kikosi
chake ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya mechi
hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi
iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Nooij amesema ujio wa washambuliaji
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.
Samata na Ulimwengu watawasili
nchini Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines
wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi ya Ligi
ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.
Wachezaji waliopo kambini kwa sasa
ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin Yondani,
Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Himid Mao, Mwinyi
Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Simon Msuva,
Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin
Friday.
Wakati huo huo, timu ya Zimbabwe
(Mighty Warriors) inawasili kesho alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ndege ya
Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 27. Kesho saa 4 asubuhi (Mei 17
mwaka huu) Kocha wa timu hiyo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari katika
ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo
zinaanza kuuzwa kesho (Mei 17 mwaka huu) kwenye vituo vya Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, OilCom Ubungo,
Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala. Viingilio ni
sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 tu.
…MDAU AAHIDI WACHEZAJI MIL 5/-
Mdau mmoja wa mpira wa miguu ambaye
hataki jina lake litajwe ameahidi kutoa sh. milioni tano kwa wachezaji wa Taifa
Stars iwapo wataifunga Zimbabwe katika mechi ya Jumapili.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linamshukuru mdau huyo, na linatoa mwito kwa wadau wengine
wajitokeze kutoa motisha kwa Taifa Stars.
Bonasi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) kwa wachezaji wa Taifa Stars itatolewa kwa mujibu wa taratibu
zilizopo.
TFF YAOMBOLEZA VIFO VYA WASHABIKI DR CONGO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi mwenzake wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- FECOFA, Omar Constant kutokana na vifo vya
washabiki.
Washabiki 12 walipoteza maisha
uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya nchi hiyo kati ya TP Mazembe na AS Vita
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tata Raphael, jijini Kinshasa.
“Tumeguswa na msiba huo mzito, tunatoa
salamu za rambirambi kwako (Rais wa FECOFA), familia za marehemu pamoja na
wadau wote wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,” imesema
sehemu ya barua hiyo ya Rais Malinzi.
KOZI ZA UKOCHA LESENI A, B KUFANYIKA JUNI
Kocha a ukocha wa mpira wa miguu
kwa ajili ya leseni A na B zinazotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) zitafanyika jijini Dar es
Salaam kuanzia Juni 2 mwaka huu.
Ada
kwa kozi zote ni sh. 300,000 ambapo wale watakaofanya ya A (equivalent) itaanza
Julai 21-26 mwaka huu. Washiriki wa kozi hiyo ni wale wenye leseni B za ukocha
za CAF.
Kwa
wale watakaoshiriki kozi ya leseni B ambao ni wale wenye leseni C watakuwa na
vipindi viwili. Kipindi cha kwanza ni kuanzia Juni 2-15 mwaka huu wakati cha
pili kinaanza Juni 23 mwaka huu na kumalizika Juni 28 mwaka huu.
Wakufunzi
wanaotambuliwa na CAF watakaoendesha kozi hiyo ni Sunday Kayuni na Salum Madadi
kutoka Tanzania, na washiriki watajigharamia kwa kila kitu. Baadaye CAF
watatuma Mkufunzi mwingine kwa ajili ya mitihani.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)