UTALII WA MALIKALE WASHIKA KASI NCHINI, WAFARANSA WAFURIKA KILWA KISIWANI

February 12, 2024

 Na. Beatus Maganja 

Kwa miongo kadhaa kumekuwa na dhana ya kwamba wageni wengi wa nje hupendelea zaidi utalii wa kuona wanyamapori, lakini hivi karibuni dhana hiyo imeanza kubadilika kwa kasi ambapo Tanzania imeanza kupokea wageni makundi kwa makundi wakitembelea katika maeneo yetu ya Malikale hususan Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara.

Ni takrikani siku 9 sasa katika kipindi cha Mwezi Februari kuanzia tarehe 03 - 11, 2024, Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imeweza kushuhudia   Meli zilizosheheni makundi ya Watalii kutoka Mataifa mbalimbali zikipishana kutia nanga katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara na kufikisha idadi ya watalii wapatao 445 kwa safari nne (4) za kitalii zilizofanyika.

Kwa mara nyingine Februari 11, 2024 TAWA ilipokea kundi la nne (4) la watalii wapatao 114  kutoka Ufaransa ambao waliingia Kilwa kisiwani kwa ajili ya shughuli za utalii na kufanya idadi ya watalii wa nje waliotembelea hifadhi hiyo ndani ya siku 9 tu kuwa 445.

Hata hivyo, TAWA inategemea kuendelea kupata wageni wengi kutoka Kona mbalimbali za Dunia kuja kutembelea na Kutalii Katika Hifadhi hiyo kongwe yenye utajiri mkubwa wa kihistoria.

Kwanini Kilwa Kisiwani na Songo Mnara? Wahenga walisema ukitaka kuujua uhondo wa ngoma, uingie ucheze, hivyo TAWA inaendelea kuwakaribisha watalii wote wa ndani na nje kutembelea hifadhi hii kujionea  yaliyomo.









NIT YATOA MAFUNZO KWA WATOA HUDUMA WA MABASI YA MASAFA MAREFU 70 KWA KANDA YA KATI.

February 12, 2024

 Na JANETH RAPHAEL - MichuziTv Dodoma



Wahudumu wa Mabasi ya Masafa Marefu Nchini watakiwa kutumia Weledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao ili kupunguza malalamiko yaliyopo kutoka kwa wateja wao.

Rai hiyo imetolewa mapema leo Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh Rosemary Senyamule katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa Wahudumu wa Mabasi ya Masafa Marefu na Mijini yaliyofanyika Kikanda Jijini hapa Dodoma.

"Ni hakika,ikiwa kila Mmoja atatekeleza majukumu yake na kuyafanyia Kazi yote niliyotaja pamoja na mengineyo natumai kwamba malalamiko ya wateja wenu yatapungua. Ni muhimu kuzingatia yale mtakayojifunza ndani ya siku tano hapa,ili kuweza kufanikiwa ni lazima kila Mmoja wenu aweze kusoma na kufanya Kazi kwa Weledi wa hali ya juu".

"Hivyo nawaomba washiriki wa mafunzo haya kusoma kwa bidii mafunzo haya mtakayopata yakawaongezee tija katika vituo vyenu vya kazi. Ni Rai yangu kwenu kujituma katika mafunzo haya na kuwa wabunifu".

Aidha Mh Senyamule amesema kuwa kuwepo kwa mafunzo haya ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika mradi wa (EASTRIP.

"Ni dhahiri kuwa kuwepo kwa mafunzo haya ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, na Wizara ya Sayansi na Teknolojia waliowezesha kuwepo kwa mradi huu wa East Africa Skills For Transformation and Regional Intergration Project (EASTRIP)".

Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) Dkt Prosper S. Nyaki ameeleza kuwa Kozi hii ni ya muda mfupi itawajengea uwezo a umahiri katika kuzitambua Sheria za LATRA na kanuni zake.

"Kozi hii ni ya muda mfupi itawajengea uwezo na umahiri katika kuzitambua Sheria za LATRA na kanuni zake,utoaji wa huduma Bora kwa wateja,mbinu za utoaji wa huduma za kwanza,usalama wa abiria na Mali zao, utunzaji wa mizigo na utambuzi wa bidhaa hatarishi,kwa kuzingatia kanuni za Usafirishaji,namna Bora ya kushughulikia Malalamiko ya wateja,usafi na utunzaji wa mazingira,mahusiano na Mawasiliano,nidhamu na unadhifu wa mtoa huduma,pamoja na marifa ya utoaji na umuhimu wa tiketi Mtandao".

Katika salamu zake Kaimu Mkuu wa chuo Mipango ya Maendeleo Vijini Dkt Godrich Mnyone amesema kuwa Nchi yetu sasahivi inachangamoto ya watoa huduma wa jamii hivyo watakapo maliza mafunzo haya wao wakalete majibu.

"Nchi yetu sasahivi Ina shida ya watoa huduma wa jamii hivyo ninyi mtakapomaliza mafunzo haya muende mkalete badiliko".

Akitoa Shukurani kwa niaba ya Wana Mafunzo wenzake Lameck James Haule ameahidu Mara baada ya mafunzo haya watakwenda kuwa wabunifu na kutangaza mazuri ya Serikali.

"Mimi niseme kwa niaba ya wenzangu baada ya mafunzo haya tutakuwa wabunifu na kutangaza mambo mazuri ya Serikali hasa katika Sekta ya usafirishaji".

Mafunzo haya ni ya siku tano, lakini bado kutakuwa a mafunzo mengine kama haya kwa wahudumu wa Mabasi kwa nyakati tofauti katika Kanda zote hapa Nchini.


RAIS SAMIA AWEKA HISTORIA, AKUTANA NA PAPA FRANCIS VATICAN

RAIS SAMIA AWEKA HISTORIA, AKUTANA NA PAPA FRANCIS VATICAN

February 12, 2024

 



Rais Samia Suluhu Hassan Amekutana na Papa Francisko

Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu hususan katika sekta ya: elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa. Baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii ; masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu amani.



Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa kunako tarehe 19 Aprili 1968 na Askofu mkuu Pierluigi Sartorelli akateuliwa kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi tarehe 22 Desemba 1970.

Uhusiano huu kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Ali Abeid Aman Karume wa Tanzania mjini Vatican unasimikwa katika tunu msingi za: Amani, haki, mshikamano na uhuru, kwani haya ni mambo yanayopata asili yake kutoka katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni.

Ujumbe wa Tanzania na Baba Mtakatifu Francisko

Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linamiliki na kuendesha shule za awali 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 244, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu 5; taasisi za elimu ya 5 na vituo vya vyuo vikuu 2 ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, SAUT.

Vyuo vyote hivi vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi za afya ni 473, lengo likiwa ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Kuna uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki pamoja na dhamana ya Uinjilishaji wa kina inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Uinjilishaji nchini Tanzania.

Ili kutambua umuhimu huu, kuna haja kwanza kwa walimu, walezi na wanafunzi wenyewe kufahamu changamoto inayoletwa na Kanisa kwa wakati huu! Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya vijana: kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa, ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho nchini Tanzania.

Elimu bora inayotolewa na Kanisa inalenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na Kimataifa kwa kuwapatia: elimu, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Tanzania katika ujumla wake.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na Ujumbe wa Tanzania


Shule, vyuo, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vimekuwa ni vituo vya majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kurithisha imani, maadili na utu wema. Kutokana na dhamana hii, vijana wanapaswa kuwa kweli ni wadau wa uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili.


Jambo msingi kwa walimu, wazazi na walezi ni kutambua dhamana na utume wa shule za kikatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwajengea watoto na vijana msingi wa imani, maadili na utu wema.

Hapa ni mahali pa kujenga na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani, ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule za Kikristo waweze kuwa kweli ni wadau katika kuyatakatifuza malimwengu. Dunia inawahitaji vijana watakaotoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, shule na taasisi hizi ni vyombo makini vya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho!

Rais Samia akipokea zawadi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko


Imegota takribani miaka 17 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012. Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, tarehe 12 Februari 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baadaye, Rais Samia amebahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.

Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa. Baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania; masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita katika kudumisha amani ulimwenguni.

Rais Samia akimpatia zawadi Baba Mtakatifu Francisko

Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara hii ya kitaifa, alikuwa ameambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania. Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar pamoja na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezeshe watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria: ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu.

Aliwaombea upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele!

Watanzania wakiwa na Rais Samia Suluhu Hassana mjini Roma

Mtakatifu Paulo VI aliyezaliwa tarehe 26 Septemba 1897 na kufariki dunia tarehe 6 Agosti 1978. Alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 21 Juni 1963. Tarehe 19 Oktoba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Na tarehe 14 Oktoba 2018 akatangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Mtakatifu.

Ni kiongozi aliyetekeleza utume wake katika mazingira magumu ya Vita Baridi, akajitahidi kuwaganga na kuwafunga watu wa Mungu waliokuwa wamejeruhiwa, kwa haki na huruma ya Mungu. Imetimia miaka thelathini na nne tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Tanzania kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 5 Septemba 1990. Alibahatika kutembelea Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Songea, Tabora, Mwanza na Jimbo Katoliki la Moshi.


Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikuwa ni Papa wa 265 kuliongoza Kanisa Katoliki. Kumbukumbu yake ya kudumu itaendelea kubaki katika sakafu ya moyo wa Kanisa na binadamu wote katika ujumla wao. Kardinali Joseph Aloisius Ratzinger, alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 19 Aprili 2005, alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927 huko Markti nchini Ujerumani, Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, (1858) sanjari na Kumbukumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya Makardinali kuwapigia kura wenyeheri watatu waliokuwa wanatarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu alipoamua kwa hiyari yake mwenyewe, kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Akafariki dunia tarehe 31 Desemba 2022.
Rais Samia Suluhu Hassan

WAJASIRIAMALI ZANZIBAR WAMSHUKURU RAIS DK.MWINYI KWA KUFANIKISHA KUPATA MITUNGI YA ORYX 1000

February 12, 2024

 Na Mwandishi Wetu, Zanzibar


KAMPUNI ya gesi ya Orxy imetekeleza maombi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kupeleka mitungi ya gesi 2000 ambayo itagawiwa kwa wananchi wajasiriamali wanawake kwa lengo la kuwezesha kiuchumi sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza wakati wa Oryx ikibidhi mitungi 1000 kwa ajili ya wajasiriamali wa visiwani Unguja ,Zanzibar Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mudrik Ramadhan Soraga amesema anamshukuru na kumpongeza Rais Dk.Mwinyi kwa kutoa mapendekezo mahususi kwa kampuni ya Oryx gas kuhusu suala nzima la kuwapa nyezo safi na salama wajasriamali wanaofanya shughuli za mama upishi

“Naomba mfahamu Rais alielekeza hili jambo katika dhana nzima ya kuweka urahisi kwa mjasiriamali mwanamke anapofanya shughuli zake katika jiko basi oryx gasi wasaidie katika kutoa nishati safi

“Kwa hiyo tumpongeze Rais Dk.Mwinyi kwanza kwa kuja na mawazo hayo lakini kuthubutu kutoa maelekezo kwa Oryx na leo hii tunakutana hapa kutoa mitungi ya gesi ambapo leo tukabidhi mitungi 1000 kwa wajasiriamali wa Unguja na wiki chache zijazo itakabidhi mitungi mingine 1000 kwa wajasiriamali wa wa Pemba.”

Akieleza zaidi amesema wanawashukuru Oryx wamekuwa wadau muhimu katika sekta ya nishati ndani ya visiwa vya Zanzibar hususan katika kufanikisha ajenda ya kutumia nishati mbadala katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku katika majumba yao.

Ameongeza Oryx kwa kipindi cha muda mfupi wamekuwa na kampeni endelevu ya kuhakikisha matumizi ya gesi safi na salama yanapewa kipaumbele sambamba na kumuunga mkono Rais Dk.Mwinyi katika malengo yake ambayo amekusudia ya kuifanya Zanzibar kuwa ni sehemu inayotumia gesi katika shughuli zake zote za kiuchumi .

Aidha amesema Serikali ya Awamu ya Nane imekuwa na lengo la kuhakikisha inatoa fursa mbalimbali kwa wananchi wao kuweza kumudu maisha yao kupitia uwezeshaji au kutengeneza mazingira ambayo wenyewe wanaweza kujiajiri.

Amefafanua kupitia mpango wa uwezeshaji wanancho kiuchumi katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na mafanikio makubwa na kiasi cha Sh.bilioni 27 kimetolewa na Serikali kukopesha wananchi ambapo wajasiriamali wasiopungua 26000 wamepata mkopo.

“Kwa hiyo tunafarijika tunapoona wadau kama Orxy mnapojumuika kuunga mkono juhudi za Serikali kwnai bila ya mashirikiano hayo, kujitoa na kuthamini mchango wa serikali katika jambo hili hatuwezi tupambana na ukosefu wa ajira ambalo ndio adui mkubwa.”

Ameongeza ni vema juhudi hizo ambazo wanashirikiana na wadau wakiwemo Orxy lazima ziende na kubadilisha mtazamo wa namna tunavyofanya shughuli zao huku akisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia inakwenda kumpunguza changamoto mtoto wa kike ambaye amekuwa akitumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa.

“Tumeamuangalia mtoto wa kike na kuona tunamuewekea mazingira mazuri ili asilazimike kwenda mbali kutafuta kuni na mkaa .Akina baba tuondokane na ile dhana kwamba mtoto wa kike ndio analazimika na kutafuta kuni.Ni lazima tuhakikishe tunawalinda watoto wetu wa kike.”

Amesisitiza kuwa kutumia nishati safi ya gesi sasa kutamuwezesha mtoto wa kike kujikita katika masomo na kazi nyingine za shuleni badala ya kutumia muda mwingi kutafuta kuni huku akisisitiza kuwa umefika wakati kwa wananchi kutunza mazingira kwa kutokata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania LTD. Benoit Araman amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa kuwaalika Zanzibar ili kufikisha nishati safi ya kupikia huku akimpongeza kwa juhudi na kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha Zanzibar inakuwa sehemu kivutio kwa wawekezaji.

“Oryx ilianza kufanya biashara ya kupikia Zanzibar na Pemba mwaka 2016. Oryx Gas Zanzibar ilizinduliwa rasmi Desemba,2021. Hii ni ishara ya kwanza ya imani katika utawala wake. Tokea kipindi hicho Rais Mwiny ametupa msukumo mkubwa Oryx Gas kuendelea kuwekeza zaidi visiwani .

“Tumefanikiwa kuwa na mkataba wa ushirikiano kati ya Oryx Gas Zanzibar na Zanzibar Group TP ambao sasa hivi wamekua mdau wetu mwenye asilimia 30. Ushirikiano huu umefanikisha ujenzi wa terminal ya LPG ambayo itakua umekamilika kabla ya robo ya kwanza ya mwaka huu 2024.

“ Hili ni jukumu kuu ya Oryx Gas Zanzibar na TP kwa wananchi wa visiwa. Maono ya Rais Dk.Mwinyi pamoja na ujasiri wa Oryx Energies na mshirika wetu TP itaruhusu kufanya usambazaji wa LPG kuwa endelevu na nafuu zaidi kwa wakazi wa Zanzibar na Pemba. Pia itasaidia kuleta maendeleo bora sekta ya utalii.

Ameongeza Oryx inajivunia kuchangia katika maendeleo ya muda mrefu visiwani Zanzibar huku akitumia nafasi hiyo kueleza kupika kwa gesi kunasaidia kulinda mazingira na kutokomeza ukataji wa miti ili kutengeneza mkaa na kuni.

“Pia ina saidia kulinda afya ya wanawake ambao wanaathirika kwa moshi inayotokana na mkaa na kuni Wanawake wataweza kufanya shughuli nyingine nyingi wakipika kwa kutumia LPG maana watapika kwa haraka bila kuharibu ubora na ladha ya chakula.

“Tokea mwaka 2021, Oryx Gas imekua kampuni kinara na kiongozi katika kuimiza watu kupikia kwa nishati safi ya LPG. Tunajivunia kua wa kwanza kuleta nishati hii safi kwa wananchi wa Zanzibar na baada ya wiki kadha tunaeneza na Pemba pia.”

Hivyo amesisitiza wamekabidhi mitungi ya gesi 1000 kwa manufaa ya wananchi wa Unguja na hivi karibuni watakabidhi Pemba mtungi 1000.


Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga (katikati) akiwa pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma (wa kwanza kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar Juma Burhan Juma wakimkabidhi mtungi wa gesi ya kupikia ya oryx Madina Ali Makame ambaye ni mmoja wa wajasiriamali waliokabidhiwa mitungi 1000 katika hafla iliyofanyika jana katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga (katikati) akiwa pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma (wa kwanza kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar Juma Burhan Juma wakimkabidhi mtungi wa gesi ya kupikia ya oryx Ipsam Juma ambaye ni mmoja wa wajasiriamali waliokabidhiwa mitungi 1000 katika hafla iliyofanyika jana katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga (katikati) akiwa pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma (wa pili kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Idara ya Mauzo wa Kampuni ya Oryx Gas Shabani Fundi (wa kwanza kulia) wakimkabidhi mtungi wa gesi ya kupikia ya oryx mmoja wa wajasiriamali waliokabidhiwa mitungi 1000 katika hafla iliyofanyika jana katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.

Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Ajira na Uwekezaji Zanzibar Mariam Juma Sadalla akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.

Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar Juma Burhan Juma akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.


Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman akizungumza akizungumza jambo na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga


Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.


Baadhi ya wajasiriamali wakiwa katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga akiwa pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar Juma Burhan Juma wakiwa kwenye picha ya pamoja na wajasiriamali waliokabidhiwa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx Gas katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramdhan Soraga akiwa pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Benoite Araman na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar Juma Burhan Juma wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ya Oryx iliyofanyika leo Februari 12, 2024 katika viwanja vya Maisara Zanzibar.


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
NELSON MANDELA YAHAMASISHA WASICHANA KUPENDA SAYANSI.

NELSON MANDELA YAHAMASISHA WASICHANA KUPENDA SAYANSI.

February 12, 2024

  Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Neslon Mandela Prof. Suzana Augustino akichangia katika mdahalo wakati wa maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Jijini Arusha.


Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela inashiriki kikamilifu katika kuleta hamasa na chachu ya Wasichana na Wanawake kupenda na kujiunga na masomo ya Sayansi, Hisabati, Teknolojia, Uhandisi na Ubunifu katika kuongeza wataalam wa fani hizo nchini.



Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango,Fedha na Utawala wa Taasisi hiyo, Prof. Suzana Augustino wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wanawake na Watoto katika Sayansi iliyofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC jjini hapo.



"Katika kulitekeleza hili mbali na kutoa mafunzo ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu pia tunatoa hamasa kwa wanafunzi wa elimu ya Msingi na Sekondari ili wapenda masomo ya sayansi, Hisabati, Teknolojia, Uhandisi na Ubunifu kupitia klabu na vikundi vinavyofanya kazi na watafiti wetu" amesisitiza Prof. Suzana Augustino.



Ameongeza kuwa, taasisi imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na shule za msingi na sekondari kwa kutoa utaalamu kupitia wabunifu wake katika kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo kupitia nyanja mbalimbali.



“Kuna shule ambayo watoto wanajifunza mambo ya nishati mbadala ambapo taasisi yetu inatoa utaalamu lakini wao wanafanya kwa vitendo, kwa kufanya hivyo miaka mitano ijayo tutakuwa na watoto wanaopenda masomo ya sayansi na hivyo kuchangia katika adhma ya serikali ya kuongeza idadi na ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi” ameeleza Prof. Suzana Augustino.



Naye Mhadhiri kutoka Taasisi hiyo Prof. Neema Kassim ametoa wito kwa jamii kuwapa nafasi watoto ya kushiriki masomo ya vitendo ili kuweza kupenda wanachofanya kwa kuwashirikisha katika midahalo mbalimbali ili kuwa na uwezo wa kujiamini.



Maadhimisho ya siku ya wanawake na wasichana katika sayansi mwaka huu yameongonzwa na Kauli Mbiu “Wanawake na wasichana katika Uongozi wa Sayansi, Enzi Mpya ya Maendeleo Endelevu”.



Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiongea katika maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi tarehe 11 Februari,2024 Jijini Arusha.



Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Neslon Mandela Prof. Suzana Augustino akichangia katika mdahalo wakati wa maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Jijini Arusha.



Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Neema Kassim akichangia katika mdahalo katika maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Jijini Arusha.



Mhadhiri Mstaafu Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Verdiana Masanja akisoma risala wakati maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Jijini Arusha.

 Wanafunzi kutoka shule za Sekondari na Msingi jijini Arusha wakifuatilia matukio mbalimbali katika maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Jijini Arusha.



Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi za Elimu za juu wakati wa maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Jijini Arusha.

EPUKENI MATUMIZI YASIYO SAHIHI YA P2

February 12, 2024

 Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wananchi kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya kuzuia mimba maarufu kama P2 ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza pale dawa hizo zinapotumika bila utaratibu ikiwemo mvurugiko wa hedhi.


Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Dodoma  kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akijibu swali Namba 163 ambapo swali hilo limeulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Medard Ntara aliyeuliza Je, kuna mpango gani wa kuruhusu Sayana Press kama njia ya Uzazi wa Mpango badala ya kutumia P2 bila utaratibu.

Amesema P2 ni njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango ambayo hutumika kuzuia mimba kwa mwanamke aliyefanya tendo la kujamiiana bila kinga kwa mfano aliyebakwa au ametumia kondomu ikapasuka na anadhani anaweza kupata mimba asiyoitarajia wakati Sayana Press ni njia ya kuzuia kupata ujauzito kwa muda mrefu, hivyo matumizi ya kuzuia mimba kwa Sayana Press na P2 ni tofauti.

Hata hivyo Dkt. Mollel ameongeza kuwa Sayana Press imesajiliwa na TMDA na inapatikana kwenye vituo binafsi vya kutolea huduma za afya kwa wateja wanaohitaji.




PPRA YAWAPIGA 'MSASA' WATUMISHI WA MSD KUHUSU MFUMO MPYA WA UNUNUZI WA UMMA KWA NJIA YA MTANDAO (NeST)

February 12, 2024

 Zaidi ya Watumishi 100 wa Bohari ya Dawa (MSD) wanapatiwa mafunzo ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST). Mafunzo hayo yanayotolewa na Mamlaka ya udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) yanafanyika jijini Dar es Salaam kwa Siku Tano.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Mavere Tukai amesema watumishi wa MSD wanapaswa kushiriki na kujifunza kikamilifu mfumo huu ili kuhakikisha mfumo unatatua changamoto mbalimbali za kiutendaji na kuleta tija katika upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

“ MSD tumewekeza sehemu kubwa katika kuhakikisha mfumo huu unakuwa na tija katika manunuzi ya bidhaa za afya. Tuna timu ambayo inafanyakazi na timu ya kitaifa inayotengeneza mfumo huu ili kuhakikisha unawezesha kwa ufasaha majukumu ya MSD”. Amesema Tukai.

Naye mkufunzi kutoka Mamlaka ya udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Bw. Castor Claudius Komba - Meneja Mafunzo na Ushauri amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watumishi wa MSD wanakuwa na uelewa wa hali ya juu katika matumizi ya mfumo huo, kwani MSD ina majukumu nyeti ya kununua bidhaa za afya hivyo mfumo huu haupaswi kuwa kikwazo katika manunuzi ya bidhaa za afya nchini.

Pia Bw. Komba ameongeza kuwa anatarajia kuwa mfumo huo mpya utatatua changamoto zilizokuwepo wakati wa matumizi ya mfumo wa ununuzi wa Taneps.

Mafunzo haya ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST) yanatolewa kwa siku tano kwa watumishi wa MSD wanaotoka Makao Makuu na Kanda za MSD.





BILIONI 9 ZA CSR KUTOKA BARRICK NORTH MARA KUTUMIKA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO YA WANANCHI WILAYANI TARIME

February 12, 2024

 

Sehemu ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakiwa kwenye kikao chao kilichopitisha mpango wa CSR Barrick North Mara wa shilingi bilioni tisa.
Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, akiongea katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo juzi. Waliokaa ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto) na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Solomon Shati.

Maofisa kutoka halmashauri hiyo wakifuatilia matukio
Wawakilishi wa Barrick katika kikao hicho wakifuatilia mijadala ya madiwani

*

Katika kudhihirisha kuwa Uwekezaji katika sekta ya madini unazidi kunufaisha wananchi, mgodi wa Barrick North Mara uliopo Tarime mkoani Mara mwaka huu utatoa kiasi cha shilingi bilioni 9 za uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Fedha hizo ziliidhinishwa na kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Nyamwaga na kuhudhuriwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara na viongozi wengine wa Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles, alieleza kikao cha baraza hilo kuwa asilimia 60 ya fedha hizo za CSR kutoka Barrick North Mara, imeelekezwa kwenye vijiji 77 na asilimia 40 itapelekwa kwenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo.


“Kati ya asilimia 60 iliyoelekezwa kwenye vijiji 77, asilimia 30 imeelekezwa kwenye miradi ya kimkakati ya halmashauri na 30 imeenda kwenye vijiji husika,” amefafanua Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga.

Kiles pia alitoa wito kwa madiwani kuwatangazia wananchi miradi hii inayotekelezwa na fedha za uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka mgodi wa North Mara ili wafahamu umuhimu wa kuwepo mgodi huu katika eneo lao “Hakikisheni mnafanya mikutano ya hadhara ya wananchi kwenye kata zenu kwa ajili ya kuongelea miradi ya CSR ili wananchi waelewe faida ya kuwa na mgodi huu” alisisitiza.

Akizungumzia ufanisi wa miradi inayotekelezwa na fedha za CSR, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Vijijini, Solomon Shati, alisema ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya CSR katika wilaya hiyo umekuwa ukizidi kuwa bora mwaka hadi mwaka na kwa sehemu kubwa utajikita kwenye miradi ya kijamii ambayo ni vipaumbele vya wananchi wa maeneo husika, kama vilivyowasilishwa na wawakilishi wao [madiwani].

“Tunatekeleza mpango shirikishi, hatufanyi kama halmashauri - bila kupata mawazo ya wananchi na ninyi madiwani ambao ndio wawakilishi wao, na maelekezo ni kwamba mipango yote ijikite katika kutatua kero za wananchi na vipaumbele vyao,” alisema Shati.


Alisema Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na mgodi imezidi kuboresha utekelezaji wa miradi ya CSR, “ukichukua miradi ya mwaka 2019/2020 wakati CSR inaanza, ukailinganisha na miradi ya CSR kipindi hiki ni vitu viwili tofauti, na tumeendelea kushirikiana na wenzetu wa mgodi wa North Mara vizuri,” alisema Shati.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, alitoa ombi kwa madiwani hao kutangaza kwa wananchi miradi ya CSR katika kata zao, pamoja na kusaidia kukemea vitendo vya uvamizi mgodini vinavyofanywa na makundi ya watu wanaojulikana kama 'intruders'.

“Kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye jamii, na mnafahamu hata sasa kuna miradi ya bilioni 7.3 ambayo tunaikamilisha,” alisema Uhadi.

Uhadi alisema bado uvamizi wa mgodi ni tatizo na aliwaomba madiwani kuwaelimisha wananchi madhara ya vitendo hivi ambavyo vinaondoa utulivu katika uzalishaji na kusababisha hasara ikiwemo kuhatarisha maisha ya watu.

“Pia, tunawaomba mkatangaze kwenye kata zenu kwamba miradi hiyo inayotekelezwa chini ya CSR imetokana na fedha zilizotolewa na mgodi, maana kuna wananchi hawana taarifa kuwa mgodi unatoa fedha kwa jamii kwa ajili ya kuwaletea maendeleo sambamba na kuboresha maisha yao”, alisema Uhadi.

Mgodi huo ambao upo Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, na unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

EPUKENI MATUMIZI YASIYO SAHIHI YA P2

February 12, 2024

 Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wananchi kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya kuzuia mimba maarufu kama P2 ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza pale dawa hizo zinapotumika bila utaratibu ikiwemo mvurugiko wa hedhi.


Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Dodoma  kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akijibu swali Namba 163 ambapo swali hilo limeulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Medard Ntara aliyeuliza Je, kuna mpango gani wa kuruhusu Sayana Press kama njia ya Uzazi wa Mpango badala ya kutumia P2 bila utaratibu.

Amesema P2 ni njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango ambayo hutumika kuzuia mimba kwa mwanamke aliyefanya tendo la kujamiiana bila kinga kwa mfano aliyebakwa au ametumia kondomu ikapasuka na anadhani anaweza kupata mimba asiyoitarajia wakati Sayana Press ni njia ya kuzuia kupata ujauzito kwa muda mrefu, hivyo matumizi ya kuzuia mimba kwa Sayana Press na P2 ni tofauti.

Hata hivyo Dkt. Mollel ameongeza kuwa Sayana Press imesajiliwa na TMDA na inapatikana kwenye vituo binafsi vya kutolea huduma za afya kwa wateja wanaohitaji.