TANZANIA YAJIPANGA KUTUMIA NISHATI YA NYUKLIA KUZALISHA UMEME

August 29, 2024

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha Mpango wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika (US-Africa Nuclear Energy Summit) unaoendelea Jijini Nairobi, Nchini Kenya.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika (US-Africa Nuclear Energy Summit) unaoendelea Jijini Nairobi, Nchini Kenya.

Dkt. Biteko atangaza msimamo katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia;

Asema mashapo 58,500 ya urani kutumika kama chanzo cha uzalishaji

Marekani kuendeleza ushirikiano na Afrika matumizi Nishati ya Nyuklia

Na Mwandishi wetu, Nairobi

Tanzania imeeleza mpango na utayari wake katika uendelezaji wa nishati ya nyuklia ikiwa ni moja ya vyanzo mbadala vya nishati safi ya umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha Mpango wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika (US-Africa Nuclear Energy Summit) unaoendelea Jijini Nairobi, Nchini Kenya.

Katika mkutano huo unaojumuisha viongozi katika Sekta ya Nishati, Watunga Sera na Wataalam kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, Dkt. Biteko amesema Tanzania iko tayari kuendeleza nishati ya nyuklia ikiwa ni moja ya vyanzo vitakavyoiwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika na ambayo inakidhi viwango vya kimataifa katika uhifadhi wa mazingira.

“Utayari wa Tanzania katika kuendeleza na kutumia nishati ya nyuklia unatiliwa mkazo katika Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sera ya Madini ya mwaka 2009, Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme na Mkakati wa Nishati Jadidifu ambapo nyaraka zote hizi zinatambua umuhimu wa nyuklia kukidhi mahitaji ya nishati nchini.” Ameeleza Dkt. Biteko

Amesema chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu zitakazowezesha matumizi ya nishati nyuklia kama moja ya vyanzo vya nishati safi ambapo hadi sasa Tanzania ina mashapo ya madini ya urani takriban tani 58,500 ambayo yanaweza kutumika kama chanzo cha uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Amefafanua kuwa, uwepo wa vyanzo mbadala wa vya umeme utawezesha nchi kuboresha mashirikiano yake ya kibiashara na nchi nyingine ndani na nje ya bara la Afrika na hivyo kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Mpango huu wa kuwa na umeme wa kutosha utawezesha hatua ya kuunganisha gridi za umeme miongoni mwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika na baadaye katika maeneo mengine ya Bara hili.” Amesema Dkt.Biteko

Ametumia mkutano huo kueleza nia ya Tanzania kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo nchi ya Marekani na Bara la Afrika ili kuendeleza nishati ya nyuklia hasa ikizingatiwa kuwa takriban watu milioni 600 barani Afrika na biashara ndogondogo zipatazo milioni 10 bado zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Amesema mahitaji ya umeme nchini Tanzania yanakua kwa asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka na ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, Tanzania imepanga kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Msaidizi Maalum wa Rais wa Marekani wa Masuala ya Uhifadhi wa Mazingira, Fedha na Uvumbuzi, Bw. Nana Ayensu amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwa nchi washiriki katika kufungua milango ya uendelezaji wa nishati ya nyuklia ambayo ni rafiki kwa matumizi ya binadamu na hifadhi ya mazingira na pia kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi husika.

Ameongeza kuwa nishati ya nyuklia itafanikisha ajenda za kimataifa za nishati safi zinazoendelea ikiwemo nishati safi ya kupikia inayopigiwa chapuo kimataifa huku kinara wake akiwa ni Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Akizungujmzia utayari wa nchi yake, amesema Marekani ipo tayari kushirikiana na nchi za Afrika ili kuendeleza matumizi ya nishati ya nyuklia ambayo inatoa uhakika wa upatikanaji nishati na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

WANAWAKE UWT KIBAHA MJI WAMPA HEKO RAIS SAMIA KWA KUCHAPA KAZI

August 29, 2024


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Umoja wa wanawake Wilaya ya Kibaha mjini (UWT) katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo imeamua kufanya kongamano kubwa la kumpongeza kwa dhati kutokana na kutenga fedha ambazo zimekwenda kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi.

Akizungumza katika kongamano hilo ambalo limehudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama na serikali pamoja na jumuiya zake Mwenyekiti wa UW T Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amebainisha kwamba lengo lubwa ni kumpongeza Rais kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akizifanya za kuwasaidia wananchi hususan kumtua mama ndoo kichwani.

"Sisi kama umoja wa wanawake UWT Kibaha mjini tumeungana kwa pamoja na kuandaa kongamano hili kwa lengo kubwa la kumpongeza Rais wetu Mama Samia kwani ameweza kufanya mambo makubwa katika nyanja mbali mbali ikiwemo kuboresha huduma ya afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, elimu sambamba na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ambayo imepelekea kumtua mama ndoo kichwani,"alisema Mgonja.

Mgonja alisema kwamba Rais Samia kwa kipindi chake cha miaka mitatu na nusu tangu alipoingia madarakani ameweza kuendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo katika Jimbo la Kibaha pamoja na Mkoa mzima wa Pwani ambayo baadhi yake imeanza kufanya kazi na kuwasaidia wananchi katika maeneo tofauti sambamba na kuongeza kasi ya kuleta uchumi.

Katika hatua nyingine hakusita kumshukuru kwa dhati Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka , Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mkurugenzi wa Kibaha mjini, Mlezi wa UWT Selina Koka,Mke wa mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mariam Ulega , pamoja na madiwani wote kwa kushirikiana bega kwa bega katika kuhakikisha kongamano hilo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Selina Koka ambaye pia mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini amesema kwamba amemshukuru Rais Samia kwa kuweza kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa vitendo katika Jimbo la Kibaha mjini ambayo imeweza kuleta chachu ya kuwasaidia wananchi katika nyanja tofauti tofauti.

Mama Koka amesema kwamba katika Jimbo la Kibaha mjini Rais Samia ameweza kuleta mageuzi makubwa katika nyanja mbali mbali kwenye kata zipatazo 14 ikiwemo sekta afya, katika kuboresha miundombinu ya zahanati, vituo vya afya, Hospitali, elimu, huduma ya maji safi na salama,nishati ya umeme pamoja na miundombinu ya barabara.

Naye mgeni rasmi katika Kongamano hilo Mariamu Ulega ambaye pia ni mke wa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga amewapongeza wanawake wa UWT kwa kuweza kuandaa kongamano hilo kwa lengo la kumpongeza Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwasaidia wananchi katika mambo mbali mbali ikiwemo kuwasogezea huduma za kijamii ikiwemo vituo vya afya, elimu, maji pamoja na mahitaji mengine.

Aliongeza kwamba wanawake wa UWT wameweza kufanya kitendo cha kiugwana kutokana na kutambua umuhimu na mchango mkubwa ambao ameufanya na Rais Samia katika kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo kwa kushirikiana bega kwa bega na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Umoja wa wanawake wa UWT Kibaha mjini katika kongamano hilo limeweza kugusia mambo muhimu ambayo yamefanywa na Rais ikiwemo utoaji wa vifaa vya Tehama,utoaji wa elimu bila malipo,kuboresha fursa za watoto wa kike katika elimu,stahiki za walimu,uboreshaji wa afya, huduma ya maji, pamoja na miundombinu ya barabara.













TOENI TAARIFA ZA BIDHAA ZISIZO RASMI – MAJALIWA

August 29, 2024

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watoe taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapokuta kuna bidhaa zisizo rasmi zimeagizwa kutoka nje, zinazalishwa au zinasambazwa nchini.

Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Agosti 29, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saasisha Mafue kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani ili kudhibiti tabia ya vijana kulewa sana nyakati za mchana hali ambayo inasababishwa na uingizaji holela wa pombe kali.

“Serikali inao utaratibu wa kutambua uzalishaji na uingizaji wa vileo nchini ambao unadhibitiwa kwa kutoa vibali vya biashara kwa wasambazaji. Vilevile inaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya ulevi kupitiliza ili kuwalinda vijana wetu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwahamasisha vijana wajiunge kwenye vikundi ili wafanye shughuli za ujasiriamali. Utaratibu huu umesaidia vijana wetu kupata kipato chao binafsi na familia zao.

Ili kudhibiti hali hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutoa elimu ili vijana wengi waingie kwenye shughuli za ujasiriamali na kuimarisha sheria za waagizaji, wauzaji na wasambazaji ili kuhakikisha kila kinachoingizwa nchini kinakidhi mahitaji ya afya ya Watanzania.

“Jamii itusaidie kutambua utengenezaji wa bidhaa usiokuwa rasmi ambao haujapata vibali rasmi kwani unachangia kutengeneza bidhaa zenye vileo vikali. Nitoe wito kwa taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya vijana ziendelee kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwafundisha maadili mema vijana wetu na kuwapa stadi za maisha.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa huduma za afya nchini zimeimarishwa sana na uwekezaji mkubwa umefanywa kiasi kwamba hatua za awali za utambuzi wa mama mjamzito zinaweza kubaini aina ya ulemavu kwa mtoto aliyenaye tumboni.

“Tafiti zetu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa hatua za awali zinaweza kubaini ulemavu na kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza ulemavu kwa zaidi ya asilimia 80. Kwa maana hiyo, uwekezaji uliofanywa kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, za mkoa, za kanda na Taifa si tu kuamua hospitali moja katika mkoa iwe inatoa huduma kwa walemavu bali kwenye vituo vyote ambavyo Serikali imeviboresha.”

Ametoa wito kwa akinamama wahudhurie kliniki mapema ili wapate elimu na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara hadi atapojifungua.

Alikuwa akijibu swali la Khadija Taya (Viti Maalum) ambaye alitaka kujua ni upi mkakati wa Serikali wa kuweka vituo katika kila mkoa ambavyo vitatoa huduma za kunyoosha viungo kwa watoto wanaozaliwa na ulemavu.

CPA MAKALA ATAKA UJENZI JENGO LA GHOROFA SITA HOSPITALI YA MBAGALA KUKAMILIKA KWA WAKATI, AKUMBUSHA MWAKANI WANA JAMBO

August 29, 2024

 Na Mwandishi Wetu


KATIBU wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo CPA Amoss Makala ametoa maelekezo kwa mkandarasi anayejenga jengo la ghorofa sita la Hospitali ya Mbagala mkoani Dar es Salaam kuhakikisha ifikapo Juni mwaka 2024 liwe limekamilika na kuanza kutoa huduma.

CPA Makala ametoa maelekezo hayo baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Mbagala ikiwa ni sehemu ya ratiba ya kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Mbagala ya Wilaya kwani hatua ambayo imefikia ni nzuri lakini niwakumbushe hakikisheni hadi Juni mwakani hospitali hii iwe imekamilika na ukizingatia mwakani tunajambo letu,hivyo lazima hospitali ikamilike mambo yawe mazuri,"amesema CPA Makala.

Amesema ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika utagharimu Sh.bilioni na kwamba Chama Cha Mapinduzi kinamshukuru Rais DK.Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa kuridhia na kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mbagara Rangi Tatu.

"Ujenzi wa hospitali hii wakati unaanza nikiwa Mkuu wa Dar es Salaam nilisimamia mchakato tangu ulipokuwa unaanza mpaka kumpata mkandarasi na sababu ni mahitaji makubwa ya huduma ya afya.Idadi ya watu Mbagala na Temeke ni kubwa."

"Nawapongeza Meya na madiwani kwa kuhakikisha dhamira ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuleta huduma karibu na wananchi.Mmmeamua kujenga ghorofa na tunafahamu changamoto ya ya maeneo hivyo tuliamua kujenga ghorofa.

"Baada ya kuona kuna changamoto ya elimu katika mkoa wa Dar es Salaam tulipata fedha lakini shida ilikuwa maeneo, hivyo nilitoa maelekezo nikiwa Mkuu wa Mkoa huu tuanze kujengaSekondari za ghorofa na hata katika hospitali hii ujenzi wake ni wa ghorofa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbagala Abdallah Chaurembo amesema wanamshuru Raia Dk.Samia Suluhu Hassan kutoa fedha Sh.bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi huku wao pia wakitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu amemshukuru CPA Makala kwa kufanya ziara katika majimbo ya 10 ya Mkoa huo na ziara yake imekuwa na mafanikio makubwa.






PSSSF YATOA HUDUMA KWENYE KIKAO KAZI CHA WENYEVITI WA BODI NA WAKUU WA TAASISI ZA UMMA AICC-ARUSHA

August 29, 2024

 ARUSHA.


MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umeweka kambi kwenye viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ili kutoa huduma kwa wajumbe wa Kikao Kazi cha Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma ambacho kimefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Agosti 28, 2024.

Kwa mujibu wa Meneja wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Bw. Venance Mwaijibe, amesema PSSSF imetehamisha huduma zake kutoka matumizi ya karatasi kwenda PSSSF Kidigitali, ambapo mwanachama atatumia Simu janja au Computer kupata huduma zote zinazohusiana na uanachama wake.

“Pamoja na kutoa huduma kwa wanachama, jambo kubwa tunalofanya hapa ni kuwaelimisha jinsi ya kutumia simu janja kupata huduma hizo ikiwemo, kupata taarifa za michango, taarifa za mafao, kuwasilisha madai mbalimbali, lakini na wastaafu nao wanaweza kujihakiki.” Amefafanua Bw. Mwaijibe.

Kikao hicho cha siku tatu, kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina kwa lengo la kuwaweka pamoja wakuu hao na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo maboresho yanayoendelea katika kuimarisha usimamizi, uendeshaji na utendaji wa Taasisi za umma sambamba na kubadilishana uzoefu.

Washiriki wanatoka katika Mashirika ya Umma 248 ambayo yanamilikiwa na serikali kwa silimia 100 na wengine wanatoka katika Mshirika 58 ambayo serikali inamiliki hisa hadi asilimia 50.

Kikao hicho kinagusa uchumi wa nchi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali unaozidi trilioni 76.

























RAIS SAMIA AMEWAJENGEA HESHIMA WANAWAKE KATIKA MAENDELEO NA KUSISITIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

August 29, 2024

 








Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
JUMUIYA ya Wanawake (UWT)Kibaha Mjini, Mkoani Pwani, imetoa wito kwa wanawake kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na kuboresha huduma za kijamii, huku ikisifu juhudi zake za kuleta mapinduzi kwenye sekta za usafirishaji, uwekezaji, nishati safi na uwezeshaji kwa wanawake.

Mbaraza kutoka UWT Mkoani Pwani, Mariam Ulega akiwa mgeni rasmi katika Kongamano la kumpongeza Rais Samia wilayani Kibaha alieleza ,Rais kawajengea heshima kubwa wanawake ,kwa kuwa miongoni mwa maRais nchini walioacha alama kwenye utendaji kazi wake.

Aliziomba Jumuiya ya wanawake,vijana na chama ziendelee kusema makubwa yaliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita ili jamii ifahamu.

Akielezea kuhusu Uwekezaji katika Miundombinu, anasema Rais ameweza kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo SGR ambao umeleta Mapinduzi kwenye sekta ya usafirishaji.

"Serikali pia imeendelea na ujenzi wa bwawa la umeme Stigo Rufiji ambalo litapunguza changamoto ya kukosa umeme wa uhakika na ukarabati wa barabara za wilaya na mkoa ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hususan kwa wakulima na wafanyabiashara"

Mariam alieleza mkoa umeendelea kuwa kitovu cha viwanda nchini Tanzania, na kusisitiza serikali imehimiza uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa hali itakayochangia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa mkoa.

Kadhalika Mariam Ulega aliwataka jamii kutumia nishati safi kwa kuachana na matumizi ya mkaa na kuni,na kuwataka wanawake,wanaume, wafanyabiashara, wakulima,vijana, shule ,vyuo, taasisi mbalimbali kuondokana na matumizi ya nishati chafu.

"Rais Samia Suluhu Hassan ni champion wa nishati safi, kwani amekuwa akisisitiza umuhimu wa kufikisha nishati safi kwa jamii , matumizi ya majiko sanifu ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa"

Mariam alifafanua kwamba, Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa na wawekezaji wa nje katika kukuza matumizi ya nishati safi, ambayo ni sehemu ya mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa taarifa ya Jumuiya, Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, Elina Mgonja alimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anazozifanya na kupeleka mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali wilayani Kibaha.

Vilevile katika kuonyesha shukrani kwa Rais Samia, Mgonja aliwataka wanawake na vijana kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao ili kumpa Rais Samia Suluhu Hassan kura za kutosha kuendelea kuleta maendeleo nchini.