TUTATOA KADI KWA MPENZI MMOJA MMOJA NA SIO KIKUNDI CHA WAPENZI-AURORA.

April 22, 2014
NA OSCAR ASSENGA, TANGA.
MWENYEKITI wa Klabu wa Coastal Union ya Tanga,Hemed Aurora amesema baada ya kumalizika Ligi kuu ya Vodacom watatangaza muda wa kutoa za uanachama wa klabu hiyo kwa mtu yoyote anayetaka kuwa mwanachama lakini sio kikundi kutokana na katiba yao inavyosema.

Kauli hiyo inatokana na malalamiko yaliyotolewa na  wapenzi cha timu hiyo iliyoyatoa kwenye kikao chao na waandishi wa habari jana kuelezea masikitiko yao ya kuzungushwa kupewa kadi za uanachama bila sababu za msingi kwa kipindi cha miezi miwili.

Akizungumza kwenye mkutano huo, wapenzi hao ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa Hotel ya Splended na kuhudhuriwa na wapenzi hao ambao wanajiita Coastal Asili ,Kiongozi wa wapenzi hao,Abdullatif Omari Famau alisema wanakaribu miezi miwili wamekuwa wakifuatilia suala la kadi bila kumkuta katibu wa klabu hiyo,Kassim El Siagi.

Katika maelezo yake,Famau alieleza kuwa Kutokana na hali hiyo wakaamua kumfuata katibu huyo nyumbani kwake kwa sababu kuna watu ambao walikwenda nyumbani kwake na kufanikiwa kupewa kadi hizo nao wakaona watumie njia hizo kwa sababu katibu anakaa na vitu vya klabu.

Alisema baada ya kutokea hali hiyo waliamua kumpigia simu Katibu huyo ambaye aliwajibu kuwa kadi za uanachama za klabu hiyo simesitishwa kutolewa kwa sababu klabu hiyo inataka kuingiliwa na watu ambao ni wavamizi ambao wanataka kuiharibu timu hiyo hivyo wao hawatakubali

Baada ya kutokea hali hiyo waliamua kuunda kundi hilo ambalo wamelipa jina la wapenzi wa Coastal Union ambao lengo lao ni kutaka kupatiwa kadi na waliamua kwenda nyumbani kwake na kumkuta mkewe na kumuachia maagizo ambapo baadae katibu aliwapigia ujumbe kwenye simu akiwaambia wasipeleke magenge nyumbani kwake kwa sababu hapendi mambo ya klabu yafike nyumbani kwake.

Kutokana na hali hiyo waliamua kuandika barua yenye nakala tatu ambazo zilipelekwa  Chama cha soka Mkoa wa Tanga TRFA,Chama cha soka wilaya ya Tanga TDFA na kwa katibu wa Coastal Union lengo la barua hiyo ilikuwa ni kumuomba katibu huyo kuwa muwazi ni lini fomu za uanachama zitakuwa tayari lakini mpaka leo hawajapata majibu

Hivyo hali hiyo iliwapelekea wanachama hao kujiunga pamoja na kuchora mabango na kupita nayo kwenye mechi yao na Kagera Sugar ambayo yalikuwa yana ujumbe tofauti tofauti ambapo baadhi yao yalikiwa yakisomeka “Uongozi wa Coastal Union umefeli” Kadi za uanachama  wa Coastal Union ni haki yetu na Mwenyekiti fanya kazi na wajumbe na sio wapambe.

Alisema wao watakwenda klabu Jumatano kuangalia kama suala la ujazaji wa fomu hizo zitakuwa likifanyika kama waliyoelezwa na Mwenyekiti huyo lakini akasema kuna baadhi ya watu waliokwenda kwa uongozi huo na kutoa pesa na kupewa kadi bila kujadiliwa .

Binafasi wakati tunafuatilia jambo hilo la kadi walichukua katiba ya Coastal Union na kuingalia wakaelewa sifa za mwanachama na wengi wao wakawa na sifa hizo lakini bado katibu huyo akawa mzito kutoa kadi hizo.

Alisema endapo watashindwa kupatiwa fomu za uanachama watawashtaki kwa shirikisho la soka nchini TFF kwa kuanzia ngazi za chini kwa sababu wao walifuata utaratibu mzuri ili kuweza kupata kadi hizo za uanachama.

Aurora alisema wao waliwaambia wapenzi hao wasubiri mpaka ligi itakapomalizika ndio wapewa fomu za uanachama kwa mtu mmoja mmoja na sio kwa kundi ambao watapewa kadi za uanachama na kujaza baadae wajadiliwe kwa mujibu wa katiba yao na hawana matatizo na mtu yoyote

Alisema lakini kitendo ambacho kimefanywa na wapenzi hao kwenye mechi hiyo kuigawa timu hiyo na kuwadhalilisha uongozi kimewaumiza sana kwani ishara hiyo inaonyesha kuna mpasuko jambo ambalo sio la kweli.

Alisema hivi sasa hawawezi kulumbana na wapenzi badala yake wanafanya matayarisho kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu simu ujao ikiwemo mikakati mingine ya kuipa maendeleo timu hiyo na sio vyenginevyo.

Akizungumzia suala la mabango,Meneja wa timu hiyo,Akida Machai alisema yenye anafikiri suala hilo limetokana na uongozi wa klabu hiyo kurekebisha makosa yaliyopo kwenye timu hiyo ikiwemo kuacha kuvaa jezi za kampuni ya sound ambazo walikuwa wakizivaa zamani bila faida yoyote ndani ya miaka miwili na nusu.

Machai amesema malumbano hayo yote yanayokana na wao kubadilika na kuacha kuvaa jezi hizo na badala yake hivi sasa wamepata mdhamini mpya wa kiwanda cha Pembe ambaye wanamtumia hivyo hata jezi zao zimeandikwa jina la Pembe.

  “Wadhamini wetu waliopita walikuwa wababaishaji kutokana na hawakuwa na manufaa yoyote kwetu hivyo sasa tumebadilika ndio chanzo cha kuleta hali hiyo ndani ya timu hiyo “Alisema Machai.

Kwa upande wake,Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa timu hiyo,aliupongeza uongozi huo kwa manufaa makubwa ambayo wameyaleta kwenye timu hiyo ambayo hapo awali hayakuwepo lakini anashangazwa na kitendo cha mashabiki wanaotaka kuivuruga.

MWENYEKITI WA UVCCM ARUSHA-HAONI UMUHIMU WA SERIKALI TATU

April 22, 2014
NA OSCAR ASSENGA ,KOROGWE.
MWENYEKITI wa Jumuiya wa Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha,Robinson Meitinyiku amesema haoni umuhimu wa kuwepo serikali tatu badala yake watanzania washikamane kuhakikisha zinapatikana serikali mbili ili waweze kudumisha muungano uliochwa na waasisi wa Taifa hili hayati Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.

Meitinyiku aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Hale Mkoani Tanga baada ya kumalizika mbio za pikipiki za uzalendo zilizofanywa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana Taifa  ambazo zinakwimbizwa nchi nzima zikiwa na lengo la kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar


Alisema  serikali tatu itakuwa na madhara makubwa ikiwemo kuwaongezea watanzania gharama za uendeshwaji wake,kuigawa nchi yetu pamoja na kuudhofisha muungano ambao ndio nguzo kuu iliyowachwa na viongozi waliowahi kuliongoza Taifa hili.

Meitinyiku ambaye pia ni Mratibu wa mbio za Pikipiki Kanda ya Kaskazini alisema watanzania walitegemea uchaguzi uliofanywa kwa Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph  Warioba na Rais wa Jakaya Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba ungeleta tija na mafanikio kwa sababu ya nyadhifa ambazo aliwahi kuzishika kwa Taifa hili badala yake anataka kuwaangamiza watanzania kwa kutaka serikali tatu.

    “Tuna mshangaa sana Jaji Warioba kama alitaka serikali tatu basi angesema tokea kipindi kile akiwa waziri mkuu na sio wakati huu“Alisema Meitinyiku akisisitiza serikali tatu ni sawa na kuwaletea matatizo watanzania.

Aliongeza gharama za serikali ya tatu zitapatikana wapi kutokana na kutokuwa na vyanzo vya kuingizia mapato hivyo kutaka fedha ambazo zingeweza kutumika kwenye matumizi hayo ni bora zingetumika kuongeza maendeleo ya nchi.

     “Tutasema kweli fitna kwetu mwiko….nawaambieni tukiomuonea haya Warioba wakati huu atatuangamiza watanzania lazima tuwe na umoja ili kuweza kupinga serikali tatu kwa nguvu zote “Alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha alisema hakuwahi kuona nchi ikiitwa Tanganyika kama Warioba anasema hilo linawezekana basi yenye na familia yake waende wakaishi ziwa Tanganyika ili aweze kutimiza malengo yake na sio watanzania.

Hata hivyo alisema watanzania wanamshukuru Mwenyekiti wa tume ya Katiba kwa aliyowafanya lakini kwa suala la serikali tatu hawatakuwa tayari kumuungano mkono hata kidogo.

Alisema tukiongeza serikali  ni dhahiri kuwa kutakuwa na kizazi kijacho ambacho hawataweza kusoma hivyo lazima tumuenzi mwalimu Nyerere kwa kuendelea kudumisha serikali mbili ambazo zitaleta maendeleo.

Alieleza kuwa wakati umefika sasa kumtetea Rais Kikwete kwa rasimu aliyoianzisha kwa nia njema aliyokuwa nayo ya kuwapatia watanzania katiba mpya lazimi viongozi walioteuliwa kuisimamia wanataka kumuyumbisha.

     “Jaji Warioba amestaafu alipopewa kazi hiyo alionekana anaweza kuifanya lakini kumbe anataka kuharibia hivyo anaangaliwe kiumakini ili asije akalitia taifa kwenye janga kutokana na misimamo yake ya kutaka kuudhofisha serikali mbili “Alisema Mwenyekiti huyo.

Awali akizungumza,Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga,Abdi Makange alisema jumuiya hiyo popote pale watasimama imara kupigia debe serikali mbili kwa sababu wanaotaka tatu ni waroho wa madaraka.

Makange alisema viongozi wanaotaka serikali tatu wanataka kulisababishia taifa hili machafuko na hiyo itakuwa ni dhahiri kuwagawa watanzania ambao wanaendelea kuienzi tunu ya amani walioachiwa na waasisi wetu.

    “Serikali ya tatu ardhi yake itapatikana wapi ?mapato yake yatapatikanaje tusikubali kabisa kwani wanaotaka hivyo hawana nia njema nasi bali watatusababishia machafuko .

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa aliipongeza Jumuiya ya Umoija wa Vijana Chama cha Mapinduzi kwa kuamua kuendesha mbio hizo za uzalendo.

MKOA WA TANGA KUONGEZA UPATIKANAJI WA HUDUMA YA MAJI SAFI

April 22, 2014
NA OSCAR ASSENGA,TANGA. 
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu,Chiku Gallawa amesema mkoa huo umepanga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 65 vijijini na mijini 75 ifikapo mwaka 2015 katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.

Gallawa alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema upatikanaji wa maji kwa mkoa hadi kufikia octoba 2013 vijijini ilikuwa ni asilimia 46,Tanga Jiji ilikuwa ni asilimia 91,Korogwe mji asilimia 65 na miji midogo iliyobaki ilikuwa ni asilimia 39.

Akizungumzia mpango wa kutekeleza matokeo makubwa sasa mkoa wamepanga kujenga miradi ya maji kwenye vijiji 100 hadi kufikia Juni 2014,kujenga vituo (vitalu)2,831 vya maji kwenye vijiji hivyo 100 hadi kufikia kipindi hicho.

Alisema pamoja na hayo wamepanga kuunda vyombo vya watumiaji maji COWSOs(Community Owned Water Supply and Sanitation Organisations)815 hadi kufikia mwezi Juni 20 ambapo mpango huo unatekelezwa kwenye vijiji 10 kwa kila halmashauri.

Alivitaja vijiji ambavyo vilivyopewa kipaumbele na miradi hiyo ,kwenye halmashauri  kumi ambapo Handeni ni Pozo,Misima, Kibaya,Kwamsangazi, Msilwa,Kwaluwala,Msanje, Gole, Kilimilang’ombe, Malezi, Kwandungwa na Manga ambapo vijiji ambavyo miradi hiyo imekamilika ni Misima(bwawa 1 limejengwa na Tanzania Japan Food Aid Counterpart wakati Mkata mradi huo pia umekamilika.

Aliongeza vijiji vyengine kwenye halmashauri hiyo kuwa ni Hoza,Komkonga ,Kwanyange,Mkata na Komnara ambayo vilinufaika na mradi huo ambao utapunguza adha ya huduma hiyo kwao.

Alisema halmashauri nyengine ni Kilindi ambapo vijiji hivyo ni Mafisa,Mgera,Muungano, Kilindi,Mswaki, Balang’a,Jungu,Negero,Kimbe,Chamtui,Kwediboma,Mafuleta,Kikunde,Saunyi na Kwekivu wakati kwa halmahauri ya Korogwe mji, ni Kwamsisi,Kwakombo,Kwamndolwa,Kwameta, Mahenge,Kwasemangube, Lwengera,Relini,Mgombezi,Mgambo na Msambiazi.

Kwenye halmashauri ya Korogwe vijijini ni Mwenga,Mlembule,Hale, Mnyuzi,Vugiri,Kwamkole, Changalikwa,Mashewa,Makumba na Kwashemshi ambayo tayari miradi iliyofanyika kwenye vijiji vya foroforo vilula nane,walei vituo kumi na nane na lewa vituo vipatavyo kumi na tano.

Aidha alizitaja halmashauri nyengine ambazo zinanufaika na mradi huo ni Muheza ambapo vijiji vya Kibanda,Nkuba,Kwemkohi,Kisiwani,Ubembe,Misongeni,Mikwamba,Kigogo Mawe,Kivindo,Kilongo na Mlingano huku miradi iliyokamilika mpaka mwezi desemba ilikuwa ni vijiji vya Misongeni,Mikwamba na Kigongo-Mawe.

Aliongeza kuwa katika halmashauri ya Jiji la Tanga vijiji ambayo vinatarajiwa kunufaika na mradi huo kuwa ni Mwarongo,Kirare,Mapojoni,Marungu,Geza,Mpirani,Chongoleani,Ndaoya,Kibafuta na Mleni wakati kwenye halmashauri ya Mkinga vijiji vya Mapatano,Daluni Kibaoni,Bamba Mwarongo,Doda, Kichalikani,Kilulu Duga,Palungu Kasera,Mwakijembe,Mbuta na Bwagamacho.

Aliita halmashauri ya wilaya ya Lushoto kuwa ni Irente,Mlola-Lwandai,Ngulu,Mlalo-Mwangoi,Shume,Gologolo,Madala na Kivingo wakati Irente na Mwangoi-Mlalo miradi hiyo imeshakamilika.

Hata hiyo alisema kwenye halmashauri ya wilaya ya Pangani miradi hiyo inatekelezwa kwenye vijiji vya Mwera,Kigurusimba,Mzambarauni,Mikocheni,Kimang’a,Madanga,Kwekibuyu,Bweni,Masaika na Stahabu huku halmashauri ya Bumbuli miradi hiyo ikiendeshwa  Bumbuli, Kweminyasa, Mgwashi, Kwalei, Kwadoe,Kwekitui na Soni wakati miradi iliyokamilika tayari ni Bumbuli na Kweminyasa.

Mwisho.
WAZIRI MKUU PINDA JANA AMEONGOZA WATANZANIA KUAGA MWILI WA DC CHANG'A , ATAKAYE ZIKWA LEO MJINI IRINGA

WAZIRI MKUU PINDA JANA AMEONGOZA WATANZANIA KUAGA MWILI WA DC CHANG'A , ATAKAYE ZIKWA LEO MJINI IRINGA

April 22, 2014

 
                       DC Moshi Chang'a enzi  za uhai  wake
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza viongozi kadhaa na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Bw. Moshi Chang’a ambaye alifariki dunia Aprili 20, 2014 kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
 
Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu Chang’a kwa wakazi wa mji wa Dar es Salaam ilifanyika leo mchana (Jumanne, Aprili 22, 2014) nyumbani kwake Mbagala, Kibonde Maji, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwili wake utasafirishwa leo jioni kwenda Kihesa, mkoani Iringa kwa mazishi.
 
Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu Pinda alisema amemfahamu Bw. Chang’a kwa muda mrefu kwa sababu sehemu kubwa ya utumishi wake ameifanya akiwa Serikalini.
 
“Ninyi mlimfahamu Bw. Chang’a kivingine lakini mimi nilimfahamu kwa namna ya tofauti kutokana na jinsi alivyokuwa msaada mkubwa kwa Serikali kila tulipokuwa tukipata shida ama migogoro ya kiuongozi.”
 
“Kama TAMISEMI, tumemtumia sana kusawazisha mambo kwa sababu Mungu alimjalia kipaji cha pekee ambacho ni ucheshi... hata jambo lingekuwa gumu vipi, huyu Bwana alijua kufikisha ujumbe bila kumuudhi mhusika kutokana na maneno yake,” alisema Waziri Mkuu.
 
Alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi kwa wafiwa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko safarini kikazi.
 
Vilevile, aliwataka wanafamilia ambao wamebaki bila mama wala baba, wawe na umoja na mshikamano na kuahidi kuwa Serikali itawasaidia watoto wa marehemu wakamilishe malengo ya elimu yao kama ambavyo baba yao alikuwa amepanga.
 
Marehemu Chang’a anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumatato, Aprili 23, 2014) huko Kihesa, Manispaa ya Iringa ambapo Serikali itawasilishwa na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia. Marehemu ameacha watoto watano, wa kike watatu na wa kiume wawili.
 
(mwisho)
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM
JUMANNE, APRILI 22, 2014

RAIS KIKWETE AZINDUA OFISI YA TRA KARATU

April 22, 2014
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi4IAWTCwhIDDB4wZHzPIevz-NrelIHe_L_VtfACpG6OT5YDxKd_IcZN-9gRbrbEVGjbJ8oStCjCRQdfiNpnI22dDSwO-dsaas4P3BxDbF2kMAxoLiigadGpgMnmHuVXrXaj1TCAvMxdOHC/s1600/D92A6757.jpgRais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunu kitambaa katika jiwe la msingi kuashiria kufungua rasmi ofisi ya Mamlaka ya mapato Wilaya ya Karatu leo mjini Karatu.picha na Freddy Marohttps://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj2GK2YCDT-cNdeWm0D65lf3H9F_AuUp3LusTvIRj46UuUHnd-SorsG7SL-LiGkVMnvUm6wXiqgmOOCVdM3tRJExkKUWg7xemxk2NeHXCE3xu24sKSzHNr_3d9ikWg-CKlh8uQLAiUHrXrA/s1600/D92A6774.jpgRais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Mbumge wa Karatu mchungaji Israeli Nase(Watatu kushoto),Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe(Wapili kushoto),Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo(kushoto) na Mkurugenzi wa Utumishi na utawala wa TRA aliyemwakilisha Kamishna mkuua wa TRA Bwana Abubakari Kunenge(wapili kulia) na kulia ni mwakilishi wa ofisi ya TRA Mkoa Bi.Caroline Ntinku.

*RAIS WA ZANZIBAR, DKT. SHEIN APOKEA TAARIFA YA SITTA JANA AMPAKUHUSU MWENENDO WA BUNGE MAALUM LA KATIBA

April 22, 2014

 Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Samuel Sitta akimpatia taarifa juu ya mwenendo wa Bunge Maalum la katiba na ulipofikia, Rais Wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, alipomtembelea nyumbani Ikulu ya Migombani Zanzibar. Mhe Sitta alikuwa Visiwani Zanzibar kwa lengo la kuonana na Mhe. Shein kumpatia taarifa kamili ya shughuli za Bunge Maalum la Katiba. 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Samuel Sitta jana amefanya ziara ya kikazi Visiwani Zanzibar na kutana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, kumpatia taarifa juu ya mwenendo wa Bunge Maalum la katiba na hatua lilipofikia. Mhe. Sitta amekutana na  Dkt. Shein katika Ikulu Ndogo Ya Migombani, Zanzibar ambapo aliweza kumpatia picha halisi ya maendeleo ya Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba unaoendelea Mjini Dodoma, Rais wa Zanzibra.
Akizungumzia mchakato wa Utungaji Kanuni, Mhe. Sitta amemwambia Dkt. Shein jinsi hatua hiyo ilivyokuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na jinsi Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo Mhe. Pandu Ameri Kificho alivyoweza kufanikisha zoezi hilo kwa kuunda kamati ya watu 20 kuongoza utungaji wa Kanuni hizo ikiongozwa na Mheshimiwa Profesa Costa Ricky Mahalu, ambapo alisema matarajio utungaji wa Kanuni ulikadiriwa kukamilika ndani ya muda wa siku tatu, hata hivyo, kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe na haja ya kuwa na Kanuni makini kwa ajili ya kuendesha Bunge, muda huo haukutosha na badala yake Bunge lilichukuwa wiki tatu kukamilisha kazi ya kutunga Kanuni hizo.
Mhe. Sitta alisema baadhi ya mambo yaliyojitokeza na kuchukua muda mwingi wa mjadala wakati wa Kutunga kanuni ni suala la mfumo wa upigaji kura kwenye vifungu vya Rasimu na Rasimu yenyewe.
“Wajumbe walijadiliana na kutofautiana kwa hoja kuhusu mfumo upi wa upigaji kura utumike kati ya ule wa kura ya wazi na wa kura ya siri. Katika hatua hiyo, wajumbe walikubaliana kupitisha Azimio la Kanuni huku suala la mfumo wa upigaji kura likiachwa katika hatua ya maridhiano ambapo Azimio la upitishwaji wa Kanuni za Bunge Maalum lilifanyika tarehe 11/3/2014” Alisema Mhe. Sitta
Kuhusu kuundwa kwa Kamati za Bunge Maalum, Mhe. Sitta amemweleza Dkt. Shein kuwa  kazi yake ya kwanza kama Mwenyekiti baada ya kuapishwa ilikuwa ni kufanya uteuzi wa wajumbe kwenye kamati kumi na mbili kwa ajili ya kupitia sura za rasimu na kuwasilisha ripoti, ambapo Kwa wastani kila kamati ina wajumbe wasiopungua hamsini na wawili (52) ukiacha Kamati Maalum za uandishi na ile ya Kanuni, ambapo pia ipo Kamati ya Maridhiano.
“Nilipata fursa pia ya kuteuwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ambayo inaundwa na wenyeviti wa kamati za Bunge Maalum., ikiwa ni pamoja na wajumbe wengine watano kwa mujibu wa Kanuni ambao wanaingia katika kamati ya uongozi, ambapo hivi sasa Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wapo 21”. Alisema Sitta.
Akifafanua kuhusu kazi za Kamati, Mhe. Sitta alisema Kamati kumi na mbili za Bunge Maalum, zilipewa jukumu la kupitia sura mbili mbili za rasimu ya Katiba yenye sura 17 na kuwasilisha ripoti zake Bungeni ili zijadiliwe. Kwa kuanzia, Kamati ya Uongozi, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kupanga ratiba ya shughuli za Bunge Maalum, iliagiza kamati zianze kupitia sura ya kwanza na sura ya sita kwa kuwa sura hizo ndiyo roho ya Rasimu ya Katiba, ambapo Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum, kamati zimeruhusiwa kujumuisha katika taarifa zao maoni yaliyoafikiwa na wajumbe walio wengi pamoja na maoni ya wajumbe walio wachache.
Akielezea kuhusu sura hizo, Mhe. Sitta alimweleza Dkt. Shein kuwa wakati wa kupitia sura ya 1 na sura ya 6 kwenye kamati, baadhi ya kamati zilifikia maamuzi na kupitisha ibara za sura hizo kwa kura za theluthi mbili za wajumbe kutoka upande wa Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka upande wa Zanzibar na baadhi ya kamati hazikupata idadi hiyo.
Hata hivyo, kwa kuwa kamati hazifanyi maamuzi ya mwisho ya kupitisha sura hizo, zilitakiwa kuwasilisha ripoti zao kwenye Bunge kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye maamuzi yafanyike. Kamati zote ziliwasilisha taarifa zao na mjadala wa sura hizo mbili ulianza tarehe 8/4/2014 na unaendelea hadi sasa.
Pamoja na hayo yote, Sitta alimweleza Shein kuwa mjadala wa Ripoti za Kamati ulitakiwa ufanyike kwa muda wa siku tatu. Hata hivyo, kutokana na maombi ya wajumbe wengi waliotaka kuchangia (433) na kutokana na umuhimu wa sura zilizowasilishwa kwenye ripoti za kamati, Kamati ya Uongozi iliamua kutoa fursa pana ya mjadala, kwa kuongeza muda wa siku zaidi, ili wajumbe wengi wapate fursa ya kuchangia, ambapo wajumbe wengi walitoa michango yao na mijadala ilikuwa mikali li cha ya kuwa baadhi ya wajumbe walitumia lugha kali na hata nyingine zisizofaa na Kutokana na hisia kali zilizotawala ilikuwa vigumu kudhibiti kikamilifu hali hiyo ukumbini.
Kuhusu Madai ya Kundi la UKAWA kususia Bunge Maalum, Mhe. Sitta alisema wakati Bunge likiendelea na mjadala tarehe 16/4/2014, kundi la “UKAWA” linaloundwa na baadhi ya wabunge na wawakilishi kutoka CUF, CHADEMA na NCCR – Mageuzi liliamuwa kutoka Bungeni kwa madai mbali mbali na kuamua kususia Bunge.
“Pamoja na kutoka nje siku hiyo, wajumbe hawa hawakutoa taarifa zozote katika Ofisi yangu kama ususaji huo ni kwa muda tu au ndiyo basi hawataendelea tena na mchakato huo”. Alisema Mhe. Sitta.
Sitta anasema Juhudi za kukutana na viongozi wa “UKAWA” hazijafanikiwa kwa kuwa viongozi wa kundi hilo wameendelea kukataa kuonana na nae, licha ya kuwa jitihada zinaendelea kuwasiliana na kundi hilo kujua msingi wa madai yao ili yaweze kushughulikiwa kwa taratibu za kibunge.
“Moja ya jambo linalodaiwa kusababisha wajumbe hao kutoka ni madai ya kauli za kibaguzi zinazodaiwa kutolewa nje ya Bunge na mjumbe mmoja ambaye pia ni kiongozi wa Serikali. Kutokana madai hayo kuwa mazito, Nilitumia busara ya kumtafuta mjumbe huyo ili aje atoe ufafanuzi wa madai hayo Bungeni, na mjumbe huyo alifanya hivyo. Madai mengine ni kauli za matusi na ubaguzi walizodai ziliwalenga wao”.  Alisema Sitta
Madhumuni ya ziara ya Mhe. Sitta kukutana na Rais wa Zanzibar ilikuwa ni kumpatia taarifa kuhusu mwenendo wa Bunge Maalum ulivyoanza na hadi hatua hii ulipofikia

BALOZI IDDI AZINDUA VYOO VYA SHULE YA KIJITOUPELE NA MABOMBA

April 22, 2014


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akivizindua rasmi vyoo vya Skuli ya Kijitoupele A, B na Sekondari pamoja na Mabomba,Tangi la Maji vilivyojengwa na ufadhili ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Watoto (UNECEF).
 Sehemu ya Mabomba hayo ya maji yakiwa yamezungukwa na wanafunzi wakati wa sherehe ya kuzinduliwa rasmi ambayo imejengwa kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi wa Skuli ya Kijitoupele A,B na Sekondari.
 Moja kati ya madarasa ya skuli ya msingi ya Kijitoupele yanaonekana kuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi wasiopunguwa idadi ya 240.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Kijitoupele Nd. Manafi Said Mwinyi mara baada ya hafla ya kuzinduliwa kwa vyoo vya skuli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza mwakilishi wa UNICEF hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini kwa uamuzi wa shirika lake kusaidia ufadhili wa ujenzi wa vyoo vya skuli ya Kijitoupele iliyopo Wilaya ya Magharibi. Nyuma ya Bibi Francesca ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee Abdulla. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
*********************************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba misingi ya ufundishaji wanafunzi Maskulini itaendelea kukosekana iwapo idadi kubwa ya Wanafunzi  itapindukia kiwango kilichowekwa Kitaifa au Kimataifa.
Alisema idadi ya kawaida ya wanafunzi ndani ya darasa moja inahitajika kuwa    watoto wasiozidi arubaini wakiwa na vikalio pamoja na vifaa vyote wanavyohitajika kuwa navyo wanafunzi hao darasani.
Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kukabidhiwa na kuvizindua rasmi vyoo 18 vya Skuli za Kijitoupele  za Msingi A na B  pamoja na ile ya Sekondari hafla iliyofanyika katika Skuli  hiyo na kuhudhuriwa na Wanafunzi, Walimu pamoja na Wazazi wa Wanafunzi wa Skuli hizo.
Balozi seif alisema msongamano wa watoto wengi Darasani mbali ya kwenda kinyume na mfumo, taratibu na maadili ya ufundishaji ndani ya darasa lakini pia unabebesha mzigo mkubwa walimu  kuweza kuhudumia wanafunzi hao kwa wakati mmoja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Kijitoupele kwa uamuzi wao wa kukubali Wanafunzi wao kuhamishwa kwenda kupata taaluma skuli nyengine  ili kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi ndani ya Skuli hizo.
“ Walimu wetu wamekuwa wakiendelea kupata mzigo mkubwa  kuwasomesha watoto wetu kutokana na wingi wa idadi yao darasani. Inasikitisha sana kuona Darasa moja la Skuli hii lina wastani wa wanafunzi 240 jambo ambalo pia ni hatari kwa afya ya wanafunzi wenyewe “. Alifafanua Balozi Seif.
Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuangalia maeneo mengine ya wazi ndani ya Wilaya ya Magharibi ili kutoa fursa ya ujenzi wa Skuli nyengine Mpya  zitakazosaidia kukidhi mahitaji ya wanafunzi  wa maeneo hayo.
Balozi Seif aliwasihi Wanafunzi hao kuendelea kuvitunza vyema vyoo hivyo ili vidumu kwa muda mrefu pamoja na kuwakumbusha kupenda masomo yao  kwa lengo la kushika nafasi za Uongozi na Taaluma kwa Taifa hili hapo baadaye.
“ Nawajibu wa kuwapongeza Walimu na Kamati ya Wazazi wa Skuli hii kwa juhudi zao za usimamizi mzuri wa wanafunzi wao na kupelekea kutoa wanafunzi wengi wanaofaulu vizuri kuingia katika skuli mbali mbali za Michepuo hapa Nchini “.
Akisoma Risala kwa niaba ya Wanafunzi, Walimu na Wazazi wa Skuli hizo Mwalimu Hidaya Haji Mkema alilipongeza Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa { UNICEF } kwa msaada wa vyoo hivyo ambavyo lilikuwa na uwezo wa kuvijenga Skuli nyengine.
Mwalimu Hidaya alisema Skuli za Kijitoupele bado zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi changamoto ambayo iko katika hatua ya kutafutiwa ufumbuzi wake  ifikapo mwaka 2015.
Alisema uandikishaji wa wanafunzi wapya katika skuli hizo za Kijitoupele A na B umefikia idadi ya watoto 800 kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa kupindukia mfumo na utaratibu uliowekwa wa sera ya Elimu.
Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto { UNICEF } Mwakilishi wa Shirika hilo hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini alisema watoto wana haki ya msingi ya kupata elimu inayoambatana na usafi wa mazingira.
Bibi Francesca alisema utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika suala la huduma za usafi wa mazingira  maskulini umethibitisha hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 300 kwa mwaka.
Mwakilishi huyo wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa hapa  Zanzibar alieleza kwamba Taasisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  tayari wameshatengeneza muongozo  wa ujenzi wa vyoo katika maskuli mbali mbali unguja na Pemba.
Alisema muongozo huo una lengo la kuwajengea mazingira rafiki wanafunzi na  tayari umeshazinufaisha skuli nane za Pemba naTano kwa Unguja wakati awamu ijayo itahusisha skuli nyengine Sita hapa Zanzibar.
Naye kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar { WEMA } Bibi Mwanaid Saleh alisema mradi huo uliohusisha Skuli 13 Unguja na Pemba kwa  ufadhili wa Unicef  umegharimu Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tatu na Ishirini na Tano { 325,000,000/- }.
Katibu Mkuu  Mwanaidi alizitaja Skuli zilizofaidika na mradi huo kuwa ni pamoja na Makombeni, Vitongoji, Wingwi,Kwale,Pujini, Mabatini na Konde kwa Pemba na Kijitoupele, Nyerere Msingi,Tunguu, Bububu na  Mtopepo kwa Unguja.
Akimkaribisha Balozi Seif katika hafla hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna  alisema Madarasa 40 yanahitajika kujengwa ndani ya Wilaya ya Magharibi ili  kukidhi mahitaji yaliyopo ndani ya Wilaya hiyo.
Waziri Shamhuna alifafanua kwamba upo mradi maalum wa ujenzi wa Skuli kumi za Sekondari  katika Wilaya zote za  Zanzibar  mradi ambao utatoa upendeleo wa kwanza kwa wilaya ya Magharibi ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi katika Skuli za Wilaya hiyo.

HUU NDIO UKWELI JUU YA JOKATE KUPIGA PICHA ZA UTUPU

April 22, 2014
Jokate Mwegelo amekanusha vikali kuhusiana na picha za utupu zilizozagaa mitandaoni hivi karibuni kuwa si zake.

Akizungumzia ishu hiyo, Jokate ambaye pia ni mwigizaji alisema kuna mitandao imeanzisha uvumi huo kwa kuweka picha ya mtu mwingine na kudai ni yeye.


Mitandao ya kijamii inakera sana. Kila mtu anaandika habari itakayowafanya watu wafungue ‘blogi’ yake, siwezi kupiga picha ya utupu,” alisema Jokate
MJADALA: NANI ANAFAA KUWA KOCHA AJAYE WA MAN UNITED KATI YA HAWA

MJADALA: NANI ANAFAA KUWA KOCHA AJAYE WA MAN UNITED KATI YA HAWA

April 22, 2014


Who could replace David Moyes? Baada ya David Moyes kufukuzwa kazi katika klabu ya Manchester United habari kubwa inayosubiriwa kwa hamu ni kocha gani atakekuja Old Trafford msimu ujao kuziba nafasi iliyoachwa wazi na David Moyes.
Majina mengi yanatajwa lakini majina ya kocha wa Uholanzi anayemaliza muda baada ya fainali za kombe la dunia Louis Van Gaal, Ryan Giggs, Jurgen Klopp, Laurent Blanc, Diego Simeone, Robert Martinez na Carlos Quieroz.
JE KATI YA HAWA UNADHANI NI  NANI ANASTAHILI KURITHI MIKOBA YA MOYES
  • Louis van Gaal
  • Jurgen Klopp
  • Ryan Giggs
  • Laurent Blanc
  • Diego Simeone
  • Roberto Martinez
  • Carlos Quieroz

WACHEZAJI WA AIRTEL RISING STARS KUTOKA SIERRA LEONE WAWASILI DAR

April 22, 2014


 Meneja Uhusiano Airtel Tanzania Jackson Mmbando akiongea kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius mara ya kupokea timu ya Airtel Rising Stars kutoka Sierra Leone ambao watahudhuria kliniki ya soka ya kimataifa ya Manchester United itayoanza Jumatano, 23-27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
 Mchezaji Fatmata Mansaray wa timu ya Airtel Rising Stars chini ya miaka  17 kutoka Sierra Leone, akiongea na waandishi wa habari baada ya kufika Dar es Salaam kuhudhuria kliniki ya soka ya kimataifa ya Manchester United itayoanza Jumatano, 23-27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
 Mchezaji Fatmata Mansaray wa timu ya Airtel Rising Stars chini ya miaka  17 kutoka Sierra Leone, akiongea na waandishi wa habari baada ya kufika Dar es Salaam kuhudhuria kliniki ya soka ya kimataifa ya Manchester United itayoanza Jumatano, 23-27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Wachezaji wa Airel Rising Stars kutoka Sierra Leone wakiwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhudhuria kliniki ya soka ya kimataifa ya Manchester United itayoanza Jumatano, 23-27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AFUNGUA KONGAMANO LA 28 LA MWAKA LA WANASAYANSI LA TAASISI YA TAIFA YA UTAFITI WA TIBA (NIMR)

April 22, 2014


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifungua pazia kuashiria kuzindua rasmi Kongamano la 28 la Mwaka la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR),  lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi hiyo ya (NIMR). Kutoka (kushoto) ni Mkurugenzi wa NIMR, Dkt. Mwele Malecela, Naibu Waziri wa Afya, Kabwe Steven na Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Samwel Masele.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata utepe kuashiri kuzindua Mpango wa Mkakati wa Nne wa Utafiti Bora wa Afya, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 28 la Mwaka la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR),  lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi hiyo ya (NIMR). Kushoto ni Mkurugenzi wa NIMR, Dkt. Mwele Malecela (katikati) ni Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Samwel Masele.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya Mwanasayansi Bora wa mwaka wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti NIMRI, Steven Magesa, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 28 la Mwaka la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR). Lililofanyika jijini Dar es Salaam, leo Aprili 22, 2014. Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Samwel Masele.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya Mwanasayansi Bora wa mwaka wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti NIMRI, Prof. Wenceslaus Kilama, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 28 la Mwaka la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR). Lililofanyika jijini Dar es Salaam, leo Aprili 22, 2014. Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Samwel Masele. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na wanasayansi waliopata tuzo bora za mwaka za wanasayansi wa mwaka wa NIMR, baada ya kukabidhiwa.
 Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati akizindua rasmi Kongamano la 28 la Mwaka la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR). Kongamano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, limeandaliwa na Taasisi hiyo ya (NIMR).
 Makamu wa Rais Dkt. Bilal, akiwa na baadhi ya viongozi wa Kongamano hilo.
 Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo.
 Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo.
 Wasanii wa THT, wakitoa burudani wakati wa ufunguzi huo.
ya pamoja na washiriki wa Kongamano hilo.