MICHUANO YA CHAMPIONSHIP KUONESHWA TV3 BILA CHENGA

September 13, 2023

  Na Khadija Seif, Michuzi TV


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limeingia makubaliano ya thamani ya shilingi Milioni 613 na Kampuni ya Startimes kuonesha mubashara michuano NBC Championship 2023 kwa mechi 170 kupitia TV3.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar, Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia amesema katika kipindi cha miaka 11 imekuwa mara ya pili kuingia makubaliano ya kuruhusu wadau kurusha matangazo ya mpira wa miguu (NBC Championship).

“Tutakuwa pamoja katika uongozi wangu sisi ni waungwana nathamini Tv3 kuja wakati Championship ikiwa katika kipindi kigumu, hivyo mtaendelea kuwa kipaumbele chetu kwa miaka ijayo baadae mambo yakiwa mazuri najua watu watakuja lakini sisi tutawapa kipaumbele Tv3,” amesema Karia 

“Tv3 itafika mbali na Championship itafika mbali pia mkataba huu ni wa miaka 3 wenye thamani ya Milioni 613 za kitanzania,” ameeleza Karia 

Karia amesema kuwa Ligi hiyo ni miongoni mwa ligi 5 kwa ubora Afrika hivyo inaenda kuwapa fursa watu wengi duniani kushuhudia vitu mbalimbali na ugumu wa ligi hiyo huku akiwatia moyo wadhamini hao (TV3) kuwa kwa sasa kuna miundombinu mizuri kwenye viwanja vilivyokidhi vigezo tayari kwa mechi hizo za NBC Championship.

Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Startimes, David Malisa amesema namna Tv3 ndani ya Kisimbuzi cha Startimes inakuwa kwa kasi na ndio Tv3 yenye miaka miwili tangu kuanzishwa kwake lakini tayari imeonesha michuano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha, Malisa ameongeza kuwa watatoa ushirikiano wa hali ya juu na mashabiki wa soka wategemee kuona picha angavu zenye ubora zaidi kama ilivyo dhamira ya Kampuni hiyo kuhakikisha mlaji anapata kilichobora siku zote.


Pia ameeleza kuwa mbali na mashabiki kupata fursa ya kushuhudia mubashara michuano hiyo pia watapata nafasi kila mkoa kutoa maoni ya namna ya mienendo ya ligi hiyo inavyokwenda na nini kifanyike ili kuwepo na maboresho mbalimbali. 

Kwa Upande wake, Msimamizi wa vipindi kutoka Tv3, Emmanuel Sikawa amesema ni hatua kubwa kufikia makubaliano hayo yenye tija na lengo la kukuza na kuinua mchezo wa soka la Tanzania. 

"Tumejipanga kutoa madhui ya Ligi hiyo ya NBC Championship 2023 kwa mechi zisizopungua 170 mubashara na tutegemee vilabu mbalimbali vinaenda kunufaika kupitia makubaliano haya,” amesema Sikawa.

Vile vile, Sikawa amewataka mashabiki wa michezo nchini kukaa tayari kwani wamejipanga vizuri kutoa maudhui ya kimichezo na hivi karibuni itawajia Tv3 Sport lengo ni kuweka Maudhui yote ya kimichezo kwa undani zaidi.

Aidha katika kuhakikisha ligi inakuwa bora Tv3 na StarTimes tumejipanga kweli kweli na Chaneli zote mbili za Tv3 na Tv3 Sports zitakuwa kwenye mfumo wa picha angavu,” amesema Malisa.

Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Wallace Karia, akiwa na wasimamizi wake wa Shirikisho hilo Msimamizi wa vipindi kutoka Tv3 Emmanuel Sikawa kushoto kwake Meneja Masoko wa Kampuni ya Startimes wakiwa picha mara baada ya kusaini mkataba  na baadae  kupokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 613 za kitanzania kuonyesha michuano ya Nbc Championship kwa mechi 170 mubashara tv3 kupitia Kisimbuzi cha Startimes ambapo Leo Septemba 13,2023 wamesaini mkataba huo wa miaka mitatu.

Rais wa Mpira wa Miguu nchini (TFF) Wallace Karia akizungumza na Wanahabari Leo Septemba 13,2023 mara baada ya kusaini mkataba wa makubaliano kati ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) pamoja na tv3 kuonyesha mubashara Ligi ya Nbc Championship kwa zaidi ya miaka mitatu mkataba wenye thamani ya shilingi Milioni 613 za kitanzania 
 Msimamizi wa vipindi kutoka Tv3 Emmanuel Sikawa akizungumza na Wanahabari, wadau wa Michezo pamoja na viongozi kutoka Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) akieleza zaidi kuwa tv3 imejipanga kutoa maudhui ya kimichezo na mashabiki wa michezo nchini watarajie ujio wa tv3 Sport lengo ni kukuza michezo nchini Tanzania 

SERIKALI YAWEKA MSISITIZO MAADILI MAKAO YA WATOTO

SERIKALI YAWEKA MSISITIZO MAADILI MAKAO YA WATOTO

September 13, 2023

 



 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na Watoto na wasimamizi wa Kituo cha Moyo wa Huruma kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Geita katika ziara yake mkoani Geita 

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa zawadi kwa Watoto wa Kituo cha Moyo wa Huruma kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Geita katika ziara yake mkoani Geita.

   


Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikagua mabweni katika Kituo cha Moyo wa Huruma kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Geita katika ziara yake mkoani Geita 

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika picha ya pamoja na Watoto mara baada ya kumaliza ziara yake mkoani Geita 
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
Na WMJJWM Geita
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis amekemea vikali baadhi ya wamiliki wa vituo na Makao ya Watoto wanaoendesha Taasisi hizo kinyume cha taratibu na maadili ya kitanzania.
Akiwa ziarani katika Makao ya Watoto Moyo wa Huruma Mjini wa Geita mapema amesema wamiliki hao wana dhima kubwa ya malezi kwa watoro hivyo, ni wajibu wao kuzingatia maadili.
Mhe. Mwanaidi amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wamiliki wa makao za watoto, bado kuna baadhi ya wamiliki wanaendesha Makao ya Watoto kwa kukiuka taratibu.
Amesema, baadhi ya Makao hayana Programu zinazosaidia kujenga maadili ya Watoto na hivyo kisababisha kuporomoka kwa maadili. 
Ameongeza kuwa Baadhi ya wamiliki wa Makao ya Watoto wanatafuta fedha kwa kuwapiga picha, kuchukua video na kusambaza matangazo kwenye mitandao kwa lengo la kujipatia fedha na misaada kutoka kwa wahisani.
“Jambo hili ni kosa na ni kinyume na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009. Baadhi ya Makao kuendeshwa bila kuwa na Kamati za Makao zenye jukumu kisheria la kusimamia maslahi ya watoto na kushauri kuhusu utolewaji huduma bora katika makao.” alisema Naibu Waziri Mwanaidi 
Aidha amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kuhakikisha wanatoa elimu kuhusu huduma ya malezi ya kambo na kuasili ili kutoa fursa kwa wananchi wanaokidhi vigezo waweze kupewa watoto hao kisheria 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita 
Mhe. Cornel Magembe amemuhakikishia Naibu Waziri Mwanaidi kusimamia uendeshaji wa Vituo na Makao ya Watoto katika Wilaya ya Geita ili yafuate taratibu na Sheria zilizopo na kuzingatia maadili ya kitanzania.
Akisoma risala ya Kituo cha Moyo wa Huruma Mkurugenzi wa Kituo hicho Sr. Maria Lauda Kulaya amesema Kituo hicho kinahudumia Watoto 159 ambapo Watoto wote wanapata huduma ya Malezi, elimu, Afya na stadi za kazi.
“Tunatoa shukrani kwa Serikali na wadau mbalimbali na wananchi kiujumla kwa kuendelea kusaidia watoto walioko katika Kituo hiki kwa Hali na mali, tunawaomba waendelee kuwa na moyo huo huo wa utoaji” alisema Sr. Maria
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Kikundi cha wajasirimali Safina na kuwaasa kuwa wabunifu katika utengenezaji wa bidhaa zao ili ziweze kupata soko hasa la kimataifa.

NEMC YAPOKEA MALALAMIKO ZAIDI YA 230 KUTOKANA NA KELELE ZILIZOZIDI KIWANGO

September 13, 2023

 

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12,2023 katika Ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam

******************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuwaonya wamiliki wa baa na kumbi za starehe kwa kuendelea na uchafuzi wa mazingira kutokana na kelele hivyo watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufungiwa biashara zao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12,2023 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, amesema uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele umeanza upya na tayari wamepokea malalamiko zaidi ya 230.

Amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la uchafuzi wa mazingira kwa kelele zilizopita viwango licha ya baraza hilo kutoa elimu kwa umma na wamiliki wa kumbi hizo na baa.

“Tuliokuwa tumewafungia walitii wakatimiza masharti tuliyowapa tukawafungulia lakini ndani ya mezi mitatu tumepata malalamiko zaidi ya 230 ya kelele kwa hiyo tunawaonya waachane na kelele kabla hatujaanza kuchukua hatua kali kama zilizopita,”Amesema

Aidha Dkt.Gwamaka amesema wote waliokuwa wamefungiwa walifunguliwa na kuendelea na biashara zao kama kawaida lakini katika siku za karibuni wamejisahau baada ya kuona utulivu na wameanza tena kupiga kelele hizo tena.

Pamoja na hayo amewakumbusha wamiliki hao kuwa sheria bado ipo na inafanyakazi na NEMC itaendelea kuwaelimisha kwamba kelele ni uchafuzi lakini wale watakaokaidi haitasita kuwachukulia hatua kama za hivi karibuni.

“Si kwamba NEMC inaona sifa kufunga biashara ya mtu, tunajua biashara hizo zimeajiri watu wengi sana na zinalipa kodi lakini kelele nazo zimekuwa zikisababisha athari kubwa kwa wananchi kwa hiyo fanya biashara yako bila kuathiri maisha ya mtu mwingine,” Amesema Dkt.Gwamaka
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12,2023 katika Ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12,2023 katika Ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE EMMANUEL MBATILO)
TRA PWANI YAPANIA KULETA MAGEUZI MAKUBWA KWA WALIPA KODI WAKE

TRA PWANI YAPANIA KULETA MAGEUZI MAKUBWA KWA WALIPA KODI WAKE

September 13, 2023

 

Na Victor Masangu,Pwani 

Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani katika kupambana na kudhibiti mianya ya ulipaji wa kodi imezindua  kampeni maalumu yenye lengo la kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu kutumia mashine za kielekroniki (EFD) pindi wanapouza bidhaa zao.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Masawa Masatu  wakati akizungumza na waandishi kuhusiana na  kampeni hiyo ambayo pia itaenda sambamba na kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanasai risiti pindi wanapofanya manunuzi kwani ni haki yao ya msingi.
Meneja Masawa alisema kwamba kampeni hiyo itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara waweze kutimiza wajibu wao katika suala zima la ulipaji wa kodi kwa hiari bila ya kukwepa lengo ikiwa ni kuisaidia serikali kukusanya mapato yake.
“Kikubwa nimewaita kwa ajili ya kampeni hii maalumu ambayo itajulikana kwa jina la Tuwajibike,’kodi yetu maendeleo yetu’ na kikubwa ni kutoa elimu katika Wilaya mbali mbali za Mkoa wa Pwani na kikubwa ni wafanyabiashara kulipa kodi ili kuisaidia serikali,”alisema Masawa.
Alifafanua kuwa wananchi wanapaswa kuhakikisha wanasai risiti zao halali pindi wanaponunua bidhaa zao na pia wafanyabiashara watoe risiti za kielectoniki pindi wanapouza bidhaa zao kwani kufanya hivyo kunasaidia serikali kupata mapato yake kihalali.
Aidha Meneja huyo alibainisha kuwa lengo kubwa ni kuweka mikakati madhubuti katika ukusanyaji wa kodi ambayo itaweza kusaidia katika mambo mbali mbali ikiwemo kutekeleza miradi ya maendeleo  kama vile ya elimu,afya,umeme,pamoja maeneo mengine.
Nao baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoani Pwani hawakusita kuzungumzia juu ya umuhimu wa kutumia mashine hizo za EFD huku wameipongeza TRA kwa hatua ya kwenda kuwatembea na kuwapa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa.
Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo la Loliondo alibainisha kuwa kutokana na elimu ambayo wamekuwa wakiipata kutoka kaa TRA Mkoa wa Pwani kumewasaidia wateja wao kusai risiti zao baada ya kumaliza kufanya manunuzi ya bidhaa zao.
Kampeni hiyo maalumu ambayo imepewa jina la Tuwajibike itafanyika kwa kipindi cha wiki moja katika Wilaya mbalu mbali za Mkoa wa Pwani ambapo italenha zaidi kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara juu ya kutoa risiti halali pamoja na kudai risiti.