MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AWAFAGILIA BAKIZA NA BAKITA KWA KUENEZA KISWAHILI DUNIANI
MAKAMU wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman akikagua vitabu pamoja na kazi za sanaa za ufundi nje ya ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman akihutubia katika Kongamano la Kimataifa la Saba la BAKIZA katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil- Kikwajuni , Unguja
KATIBU Mtendaji wa BAKIZA, Dk. Mwanahija Ali Juma
WAZIRI wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mh. Tabia Maulid Mwita
****
NA. ELISANTE KINDULU, UNGUJA
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mh. Othman Masoud Othman ameyapongeza mabaraza ya kiswahili kwa kueneza vema kiswahili ndani na nje ya nchi.
Mh. Othman alitoa pongezi hizo alipokuwa akifunga kongamano la Saba la kimataifa la baraza la kiswahili Zanzibar (BAKIZA) lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, mwanzoni mwa wiki hii Kikwajuni- Unguja.
"Napenda nitumie fursa hii kuzipongeza BAKIZA na BAKITA kwa kueneza kiswahili kitaifa na kimataifa ikiwa pamoja na kufundisha lugha hiyo kwa wageni ndani na nje ya nchi".
Amesema kiswahili kimekuwa na watumiaji wengi duniani ambapo takribani watu milioni 200 wanaitumia lugha hiyo, hivyo amewaasa wataalamu wa lugha hiyo kuendelea kuitumia katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuandika vitabu na kuvisambaza.
Aidha Makamu huyo wa Kwanza wa Rais amewataka watumiaji wa lugha hiyo ikiwa pamoja na wanazuoni kuendelea kujifunza zaidi utaalamu katika lugha hiyo ili kuepuka mapungufu katika kuandika na kuzungumza.
" Hata kisu kikali lazima kinolewe. Mimi niliwahi kuwa mwalimu wa kiswahili kabla ya kuingia katika tasinia ya sheria. Lakini hadi leo bado mwanafunzi wa Kiswahili. Hivyo sote kwa pamoja licha ya kukieneza kiswahili lakini bado tunahitajika kujifunza zaidi.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Tabia Maulid Mwita alitoa wito kuwa vijana wanaotumika katika sanaa za maonyesho kwenye dhifa mbalimbali waendelezwe ili
kusasisha vipaji vyao.
Mapema akitoa taarifa za baraza hilo, Katibu Mtendaji wa BAKIZA Dk. Mwanahija Ali Juma alisema kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Sweden, India, Korea kusini, Uganda, Kenya, Komoro, Tanzania bara na Tanzania Visiwani.
Jumla ya maazimo 11 yaliwasishwa na washiriki wa kongamano ikiwemo wanaotafsiri tamthilia mbalimbali watafsiri kwa uhalisia wake ili kuepuka upotoshaji katika matumizi ya lugha.
WAZIRI MWIGULU AZINDUA OFISI ZA TADB KANDA YA KASKAZINI
-Kuhudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Fedha, Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba leo amezindua Ofisi ya Kanda ya Kaskazini ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha na mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima na wafugaji wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Nchemba aliishukuru TADB kwa kazi nzuri inayoendelea kufanya katika kuinua sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini, pamoja na sekta ya fedha kwa ujumla.
“Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta hii, imeendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira, kuchukua hatua za kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu, pamoja na kubainisha fursa za masoko za mazao hayo zilizoko ndani na nje ya nchi yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa ofisi hiyo ya Kanda ya Kaskazini ya TADB itakwenda kuimarisha huduma za kifedha kwenye Mikoa ya Kaskazini na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji, kufungua fursa na kuendeleza zaidi ukuaji wa biashara katika mnyororo wa thamani katika mikoa yote minne ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. Mikoa hiyo inasifika kwa kuzalisha mazao muhimu kwa uchumi wa nchi, kama vile kahawa, mahindi, ngano, na sekta zingine kama utengenezaji wa mbolea, ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa, ufugaji wa samaki na kuku wa nyama na mayai, kilimo cha maua, mboga mboga na matunda .
“Naihakikishia Bodi na Menejimenti ya TADB kuhusu utekelezaji wa agizo nililotoa wakati wa Bunge la Bajeti, ambapo nilitangaza kwamba Serikali itaiongezea Benki ya TADB na TIB jumla ya mtaji wa Shilingi Bilioni 235.9 kwa lengo la kupanua wigo wa mikopo kwa sekta binafsi kwa ajili ya miradi ya kukuza sekta za uzalishaji na kuongeza thamani.
Pia serikali itatekeleza programu ya kuwezesha mtaji usiopungua Shilingi Trilioni 1 kwa miaka mitano hadi kumi kwa benki kama TADB ili ziweze kufanya shughuli ya utoaji wa mikopo kwa ufanisi zaidi, na wakulima wazidi kupata mitaji ya kujiendeleza,” Waziri alisema.
Aliwasisitizia Wananchi wa mikoa hiyo kuchangamkia fursa ya uwepo wa Ofisi hiyo ya Kanda kupata uelewa zaidi wa utaratibu wa kupata mikopo, kufanya matumizi sahihi ya mikopo na kulipa kwa wakati, na pia kuishauri Menejimenti ya Benki na watumishi wake kuweka masharti nafuu ya mikopo, kuwatembelea wanufaika katika miradi yao na kutoa elimu ili kusimamia kikamilifu mikopo husika kwa wakulima, wavuvi na wafugaji.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw Frank Nyabundege alielezea kuwa ufunguzi wa ofisi hiyo ni mwendelezo wa mafanikio ya benki ya TADB kutimiza malengo yake kutoa mikopo ya masharti nafuu, kwa viwango vya riba za chini na kutoa muda mrefu zaidi wa marejesho kwa wakulima wadogo, wa-kati na wakubwa katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya kilimo, ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Hadi kufikia Novemba mwaka huu mizania yetu ya mikopo imeendelea kukukua na kufikia kiasi cha Shilingi Bilioni 600.7 mwezi Novemba, 2023. Ofisi hii ya Kanda ya Kaskazini inaenda kupunguza adha kwa kufikisha huduma za benki karibu zaidi na wateja wake waliokuwa wanahudumiwa na ofisi ya Dodoma, ambapo hadi kufikia Novemba 2023, TADB imekwisha wezesha wakulima na wafugaji wa kanda ya Kaskazini kwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 18.3 kwa Mkoa wa Tanga, Shilingi bilioni 7.9 Mkoa wa Arusha, Shilingi bilioni 3.2 Mkoa wa Kilimanjaro na Shilingi bilioni 3.1 kwa mkoa wa Manyara.
Mikopo hii imewezesha upatikanaji wa pembejeo na viwatilifu, mbegu bora za mifugo, ukuzaji viumbe hai kwenye maji na uvuvi.”
Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchochea maendeleo ya nchi kupitia kilimo na kuiongezea TADB mtaji wake kufika Shilingi Bilioni 268, pamoja na juhudi nyingine za kuongeza mitaji na mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.Tunathamini juhudi mbalimbali za serikali kuhakikisha benki yetu inafanya kazi kwa mafanikio ya malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
TADB sasa ina ofisi saba mbazo ni Kanda ya Ziwa yenye ofisi Mwanza - na kuhudumia mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga, Geita na Simiyu; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye ofisi Mbeya - na kuhudumia mikoa ya Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa.
Kanda ya Mashariki yenye ofisi Dar es salaam na kuhudumia mikoa ya Pwani na Morogoro; Kanda ya Magharibi yenye ofisi Tabora na kuhudumia mikoa ya Katavi na Kigoma; Kanda ya Kati yenye ofisi Dodoma na kuhudumia mkoa wa Singida; Kanda ya Kusini yenye ofisi Mtwara na kuhudumia mikoa ya Lindi na Ruvuma; na sasa Kanda ya Kaskazini yenye ofisi Arusha na kuhudumia Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
“Aidha, tumeshapata ofisi ndogo Zanzibar tukiwa tunasubiri vibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufungua ofisi kubwa na ya kisasa Zanzibar,” Bw Nyabundege alielezea.
Serikali iliamua kuanzisha Benki ya TADB mwaka 2015 kwa malengo makubwa mawili; Ambayo ni: kuchangia utoshelevu na usalama wa chakula nchini; pamoja na kuchagiza mapinduzi ya kilimo toka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara.
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa ofisi za kanda ya Kaskazini za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) jijini Arusha Arusha. Ofisi hiyo ya kanda itahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba (wa kwanza kulia) akizundua rasmi ofisi ya kanda ya Kaskazini ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) itakayohudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. Wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni mmbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo akifuatiwa na mwenyekiti wa bodi ya TADB Ishmael Kasekwa.
Mwenyekiti wa bodi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Ishmael Kasekwa (kati kati) Akimtambulisha mkurugenzi mtendaji wa Benki hiyo Frank Nyabundege (kulia) kwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto) muda mfupi kabla ya uzinduzi wa ofisi za kanda ya Kaskazini za benki hiyo uliofanyika jijini Arusha
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba (kati kati) akisalimiana na wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi tawi la benki hiyo kanda ya Kaskazini jijini Arusha. Ofishi hiyo ya kanda itahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na kufurahia jambo na Meneja Masoko na mwasiliano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Amani Nkurlu (kulia) muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi tawi la benki hiyo kanda ya Kaskazini jijini Arusha. Ofisi hiyo ya kanda itahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
RAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AWASILI NCHINI AKITOKEA NCHINI QATAR ALISHIRIKI JUKWAA LA DOHA (DOHA FORUM)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla,Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Mhe Mahmoud Muhammed Mussa, alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar akitokea Nchini Qatar,baada ya kumalizika kwa Jukwaa la Doha (Doha Forum) lililofanyika Jijini Doha, alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakisalimiana na Wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar akitokea Nchini Qatar,baada ya kumalizika kwa Jukwaa la Doha (Doha Forum) lililofanyika Jijini Doha, alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.(Picha na Ikulu)
PROFESA NDALICHAKO AIPONGEZA GGML
CCM YATOA SALAMU KWA VIONGOZI VIJANA WANAWAKE KUTOKA NCHI 16 ZA AFRIKA
MKURUGENZI WA PANGANI AJITAFAKARI KWA KUSHINDWA KUSIMAMIA MIRADI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Isaya Mbenje na watendaji walio chini yake kujitafakari juu ya mwenendo wa utendaji kazi wao kutokana na kushindwa kusimamia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.
Mhe Ndejembi ametoa kauli hiyo leo alipotembelea miradi ya elimu ya msingi na sekondari inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa mwaka mpya wa masomo 2024
Katika ziara yake, Mhe Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Pangani Halisi iliyogharimu kiasi cha Sh. Bilioni Moja, Shule ya Sekondari Masiaka inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP inayogharimu Sh. Milioni 585 na Shule ya Msingi Bushiri iliyogharimu Sh. Milioni 440 ikijengwa kupitia mradi wa BOOST.
Amesema Shule ya Pangani Halisi ilipaswa iwe imeshakamilika lakini mpaka sasa ujenzi huo haujakamilika huku halmashauri ikiwa imeishiwa fedha ikilinganishwa Shule ya Masiaka ambayo imepata sh. Milioni 580 majengo yake yapo kwenye hatua kubwa na inaendelea na ujenzi.
“Ofisi ya Rais-TAMISEMI chini ya Waziri Mhe Omary Mchengerwa hatutomchekea yeyote anayechezea fedha za umma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na wasaidizi wako mjitafakari kwa sababu hawamsaidii kazi Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika ngazi ya huku chini kuna tatizo la usimamizi wa miradi na kutojali fedha zinazoletwa kutekeleza miradi hii. Sasa kwa TAMISEMI hii hatuwezi kuja tukakuta usimamizi mbovu wa miradi tukashindwa kuchukua hatua,”amesema.