UKAGUZI WA AFCON UMEENDA VYEMA – YAKUBU

August 05, 2023

 


Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw Saidi Yakubu amesema timu ya Wakaguzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kwa maandalizi ya AFCON 2027 imemaliza ukaguzi wao vyema katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kupitia kapeni ya EA Pamoja Bid.

 

 

Akiongea katika Kipindi cha Jambo kinachorushwa ya Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) Agosti 5, 2023 jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Bw Yakubu amesema timu hiyo imemaliza kazi yao vizuri hapa ambapo ukaguzi wao ulianzia nchini Kenya, Uganda na Tanzania na kuhitimisha kazi yao kikao cha majumuisho kilichofanyika Zanzibar.

 

 

Maeneo mengine waliyokagua ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, HospitaIi ya Taifa Muhimbili, Uwanja wa Amaan Zanzibar, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Hospitali ya Mnazi Moja, Uwanja wa uwanja wa Mao Tse Tung Zanzibar pamoja na hoteli zitakazotumiwa wakati wa mashindano hayo kulingana na viwango vya CAF.

 

 

“Baada ya ziara yao hiyo Kenya, Uganda na Tanzania, walifanya mkutano wa majumuisho, Hatupo vibaya, tupo vizuri. Kinachotazamwa na wakaguzi ni pamoja na utayari wa Serikali namna ilivyojipanga katika kuhakikisha tukio hili tumelipokea, ukweli ni kwamba ziara yote hii ilikuwa inaongozwa Katibu Mkuu tayari inaonesha kwamba Serikali ipo tayari” amesema Katibu Mkuu Bw Yakubu.

 

 

 

Vigezo zingine ambavyo wakaguzi hao wa AFCON waliangalia ni mtiririko wa matukio kuelekea AFCON, kwa maana ya miundombinu ni lazima yote ikamilike kabla ya tarehe 31 Desemba 2025, Tanzania inajenga kiwanja kipya cha Arusha ambapo walioneshwa michoro, nyaraka zote muhimu na mapango wa mtiririko wa fedha utakavyokuwa katika kukamilisha ujenzi wa uwanja huo.  

TUME YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO WA MBARALI NA KATA SITA

August 05, 2023

 

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima akizungumza leo Agosti 5,2023 wakati akitoa taarifa uwepo wa Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Mbarali Mkoani Mbeya na Kata sita za Tanzania bara. Taarifa hiyo ameitoa jijini Dodoma baada ya kikao cha Tume kilichokutana leo .  
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mh. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele (katikati) akiongoza kikao cha Tume kilichokutana leo Agosti 5,2023 jijini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk na Kulia Katibu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima. 
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiendelea na kikao chao hii leo Agosti 5,2023  jijini Dodoma.
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiendelea na kikao chao hii leo Agosti 5,2023  jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mh. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele (wanne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichokutana leo jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine walipitisha tarehe ya uchaguzi mdogo katika jimbo la mbarali na Kata sita za Tanzania bara. 
**********
Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023.

Akisoma taarifa kwa umma jijini Dodoma leo tarehe 05 Agosti, 2023, baada ya kikao cha Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima amesema wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.
 
Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi mdogo kuwa ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” amesema Bw. Kailima.

Aliongeza kuwa, Tume imetoa taarifa hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiitaarifu Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya.  Nafasi hiyo wazi inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Francis Mtega.  Spika ametoa taarifa hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

 “Tume imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye Dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara. Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,” alisema Bw. Kailima.

Aliongeza, “Tume kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Mbarali na Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara”.

SPIKA WA BUNGE DKT. TULIA ACKSON ATEMBELEA BANDA LA WCF NANENANE MBEYA

August 05, 2023


 

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MBEYA

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), ametembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF) kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Tanzania kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya leo Agosti 4, 2023.

Mhe. Dkt. Ackson ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, alipata fursa ya kupewa elimu ya Fidia kwa Wafanyakazi iliyokuwa ikitolewa na Afisa Mfawidhi WCF, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta.

Alijulishwa kuwa WCF inatoa fidia endapo mfanyakazi ataumia au kuugua kutokana na kazi na endapo atafariki basi wategemezi wake watalipwa fidia.

Pia alielezwa kuwa Mfuko uliundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263 marejeo ya mwaka 2015] na inahusu waajiri na waajiriwa wote kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara.

Aidha Mhe, Spika alielezwa kuwa Mfuko unatoa jumla ya Mafao saba ambayo ni pamoja na Huduma ya matibabu, Malipo ya ulemavu wa muda, Malipo ya ulemavu wa kudumu, Malipo kwa anayemhudumia mgonjwa, Huduma za utengemao, Msaada wa mazishi na Malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.

Maonesho ya mwaka huu ambayo yalifunguliwa rasmi Agosti Mosi, 2023 na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, yamewaleta pamoja washiriki kutoka nchi zinazofikia 30, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera na yamebeba kaulimbiu isemayo “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mfumo Endelevu wa Chakula”

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), akionyesha furaha baada ya kupata elimu ya fidia alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Tanzania kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 4, 2023.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), akisikiliza kwa makini kuhusu elimu ya fidia kwa wafanyakazi iliyokuwa ikitoelwa na Afisa Mfawidhi WCF, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), akisikiliza kwa makini kuhusu elimu ya fidia kwa wafanyakazi. 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), katikati, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa WCF.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), katikati, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa WCF.

 

MSTAAFU PSSSF AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUWALIPA MAFAO NA PENSHENI KWA WAKATI

August 05, 2023

 

 

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MBEYA

MSTAAFU wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutoka wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Bi. Monica Kamoza, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali Wastaafu na Wazee kwa kuwalipa pensheni na mafao kwa wakati.

Bi. Kamoza ametoa shukrani hizo Jumamosi Agosti 5, 2023 wakati akikabidhi zawadi ya boga kubwa kwa watumishi wa PSSSF kufuatia kile alichoeleza ni kufurahishwa na huduma nzuri anazopata kutoka PSSSF

“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa upendo wake, anatujali sisi Wastaafu na Wazee, haya yote tunayofurahia ya kupata huduma bora yanatokana na uongozi wake mzuri.” Alisema

Bi Kamoza ambaye alikuwa mfanyakazi katika hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kyela akiwa kama mtaalamu wa afya ya macho, alistaafu Desemba 26, 2021 na kilichompeleka kwenye banda la PSSSF ni kupata huduma zinazohusiana na taarifa zake za ustaafu.

“Nimefurahishwa na huduma safi na za haraka nilizopewa kwenye banda la PSSSF, kilichonileta hapa ni kupata taarifa yangu ya malipo ya mkupuo ili nijue kama kulikuwa na mapunjo au la, nimepewa taarifa na ufafanuzi wa kina na hakukuwa na mapunjo yoyote.” Alifafanua Bi. Kamoza.

Mstaafu huyo alisema, ukiacha huduma aliyopewa kwenye banda hilo, jambo lingine lililomfurahisha hata wakati anastaafu alipata malipo yake ya mkupuo ndani ya mwezi mmoja na hata malipo ya pensheni ya kila mwezi hayajawahi kuchelewa.

“Mwezi uliopita (Julai) nimepokea malipo yangu ya pensheni tarehe 21, mwezi wa sita tarehe 24, kwa kweli nawapongeza sana kwa huduma zenu bora na nzuri.” Alipongeza.

Akizungumza baada ya kupokea zawadi hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wa Mfuko wanaotoa huduma kwenye banda la PSSSF, Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, alimshukuru Bi. Kamoza kwa zawadi hiyo kwa wafanyakazi wa PSSSF.

“Zawadi hii ina maana kubwa sana kwetu, inaonyesha kutambua ubora wa huduma tunazotoa kwa wanachama na wastaafu wa Mfuko na tunachoahidi ni kuendelea kutoa huduma bora na za viwango.” Alisema.

Huduma zinazotoelwa kwenye banda la PSSSF ni kama zile zinazotolewa kwenye ofisi za Mfuko huo zilizoenea kote nchini.

Mwanachama wa PSSSF anapofika ataweza kupata taarifa za uanachama wake, taarifa za michango, taarifa za mafao, taarifa za uwekezaji, mstaafu ataweza kujihakiki na kupata elimu ya hifadhi ya jamii kwa ujumla.

Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, akipokea zawadi ya boga kubwa kutoka kwa Mstaafu Bi. Monica Kamoza
Mfanyakazi wa PSSSF, Bi. Zainab Mjungu (kushoto) akimkabidhi mstaafu wa PSSSF, Bi. Monica Kazola, taarifa ya malipo ya mkupuo alipofika kwenye banda la PSSSF kupata huduma.
Mstaafu wa PSSSF, Bw. Jimmy Nyamoga, akijihakiki kwenye banda la PSSF Agosti 5, 2023. Kushoto ni Bi.Zinab Mjungu.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas (kushoto) akimsikiliza Afisa Uhusiano Mkuu PSSSF, Bw. Abdul Njaidi, alipotembelea banda la Mfuko huo Agosti 5, 2023.
Afisa Matekelezo Mwandamizi PSSSF, Bi. Winfrida Siriaki Jory (kushoto) akimsikilzia mwanachama wa Mfuko huo, akiyefika kupata elimu kuhusu uanachama wake.
Afisa wa PSSSF, Bi. Saluna Aziz Ally (kulia) akimuelekeza mwanachama wa Mfuko huo jinsi ya kutumia huduma za Mfuko kupitia PSSSF Kiganjani.