FA CHADAI KUWA CARROL AJITOA TIMU YA TAIFA KUTOKANA NA MAJERUHI.

May 22, 2013
CHAMA cha Soka nchini Uingereza {FA} kimedai kuwa mshambuliaji wa kimataifa wa nchi hiyo, Andy Carroll amejitoa katika timu ya taifa kutokana nakuwa majeruhi. Carroll mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kisigino baada ya kocha wa timu ya taifa Roy Hodgson kumuita katika kikosi chake ambacho kitacheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki kati ya Ireland Mei 29 na Brazil Juni 2 katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Mshambuliaji huyo wa Liverpool amekuwa akicheza kwa mkopo katika klabu ya West Ham United msimu uliopita huku vyombo vya habari nchini Uingereza vikiripoti kuwa klabu hiyo imekubali kumchukua moja kwa moja kwa ada ya paundi milioni 15. Carroll anaungana na nahodha wa Liverpool Steven Gerrard na kiungo wa Arsenal Jack Wilshere kukosa mechi hizo za kujipima nguvu kabla ya mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Moldova na Ukraine Septemba mwaka huu.

MURRAY AJITOA MICHUANO YA WAZI UFARANSA:

May 22, 2013
MCHEZAJI nyota maarufu wa tenisi kutoka Uingereza Andy Murray amejitoa katika michuano ya wazi ya Ufaransa kutokana na maumivu ya mgongo yaliyopelekea kushindwa kuendelea kucheza katika michuano ya wazi ya Italia. Murray ambaye anashika namba mbili katika orodha za ubora Duniani kwa upande wa wanaume amejitoa katika michuano hiyo baada ya kushauriwa na madaktari wake na anatarajia kurejea tena uwanjani katika michuano ya Wimbledon katikati ya mwezi ujao. Nyota huyo ambaye ni bingwa wa michuano ya wazi ya Marekani amesema umekuwa ni uamuzi mgumu kufanya kwani huwa anapenda kucheza jijini Paris lakini imekuwa nje ya uwezo wake kwasababu ya ushauri wa kiafya aliopewa. Murray aliwaomba radhi waandaaji wa michuano hiyo na kuwashukuru mashabiki wake kwa kumtumia ujumbe wa kumuunga mkono na sasa kazi kubwa aliyokuwa nayo ni kuhakikisha anapona na kurejea haraka uwanjani.

KOCHA WA LIVERPOOL RODGERS HANA MPANGO WA KUMUUZA SUAREZ.

May 22, 2013

BOSI wa  majogoo wa jiji la londo Liverpool Brendan Rodgers amesema hana mpango wa kumuuza mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Luis Suarez. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay alikosa mechi nne za Liverpool mwishoni mwa msimu huu baada ya kufungiwa mechi 10 kwa kumng’ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic lakini alimaliza katika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu nchini Uingereza akiwa na mabao 23. Liverpool haijafuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya toka mwaka 2009 lakini pamoja na vilabu vikubwa kummezea mate Suarez, kocha huyo ana imani kwamba ataweza kumbakisha mchezaji huyo kwa msimu ujao. Rodgers amesema kwasasa wanajipanga kutengeneza kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao na Suarez ni sehemu ya kikosi hicho ingawa amekiri kwamba zipo baadhi ya klabu kubwa zinazomtaka.

KAGAME CUP KUCHEZWA SUDAN JUNI 18-JULAI 21 NCHINI:

May 22, 2013
MASHINDANO ya 39 ya kusaka Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati CECAFA KAGAME CUP 2013 yatachezwa huko Sudan kuanzia Juni 18 hadi Julai 2 na Mabingwa Watetezi Yanga wamepangwa Kundi C na wataanza kwa kucheza na Express ya Uganda hapo Juni 20 Mjini Al Fasher, Mji Mkuu wa Darfur ya Kaskazini.

Jana huko Mjini Khartoum, Sudan ndio ilifanyika Droo ya Timu 13 kupangwa Makundi matatu na Droo hiyo ilisimamiwa na Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kagame Cup, Raoul Gisanura, wa kutoka Rwanda.
KUNDI A:
Merrickh El Fasher (Sudan), Simba (TZ), Al Mann (Somalia), APR (Rwanda).
KUNDI B:
Hilal Kadougli (Sudan), Ahli Shandi (Sudan), Al Nasr (S.Sudan), Tusker (Kenya), Super Falcon (Zanzibar).
KUNDI C:
Yanga (Tanzania), Express FC (Uganda), Vital O (Burundi), AS Port (Djibouti)
Mashindano haya yatachezwa kwa Wiki mbili katika Miji ya Kaskazini ya Sudan, Al Fasher na Kadugli, South Kordufan State, na Yanga, ambao ni Mabingwa Watetezi, wanawania kutwaa Ubingwa huu kwa mara ya 3 mfululizo.
Zanzibar wanawakilishwa na Super Falcon ambao walitwaa Ubingwa wa Zanzibar Msimu wa 2011/12 lakini hivi sasa, huko Visiwani, wameshashushwa Daraja.
Super Falcon wataanza kucheza Juni 18 na Tusker ys Kenya huko Kadugli, South Kordufan State, Sudan.
Mashindano haya yanadhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, na zawadi ni Dola 60,000.

MWAMUZI WA AFRIKA KUSINI KUICHEZESHA STARS MOROCCO.

May 22, 2013
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
 limemteua mwamuzi kutoka Afrika Kusini kuchezesha
 mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kati 
ya Tanzania (Taifa Stars) na wenyeji Morocco (Lions of 
the Atlas).

Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech, Morocco kwenye Uwanja wa Grand kuanzia saa 3 kamili usiku kwa saa za Morocco. Mwamuzi atakayechezesha mechi hiyo ni Fraser Daniel Bennett.

Bennett atasaidiwa na Thusi Zakhele Siwela pia wa Afrika Kusini, wakati mwamuzi msaidizi namba mbili atakuwa ni Marwa Range kutoka Kenya. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni Lwandile Mfiki wa Afrika Kusini.

Kamishna wa mechi hiyo ni Robert Mangollo-M’voulou wa Gabon wakati mtathimini wa waamuzi (referee assessor) ni Charles Masembe kutoka Uganda.

Taifa Stars ambayo iko chini ya Kocha Kim Poulsen, na ikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini katika hoteli ya Tansoma ikiendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo ambapo kabla itajipima na Sudan (Nile Crocodiles) Juni 2 mwaka huu jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Ratiba ya mazoezi kwa timu hiyo ni kama ifuatavyo;

Mei 22                 Saa 10 jioni                             Uwanja wa Karume
Mei 23                 Saa 1 asubuhi na Saa 10 jioni   Uwanja wa Karume
Mei 23                 Saa 10 jioni                             Uwanja wa Karume


Mei 25                 Saa 1 asubuhi na Saa 10 jioni     Uwanja wa Karume

Mei 26                 Saa 3 asubuhi                            Uwanja wa Karume