SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL

October 04, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAM.
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka huu)  kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

KUTIMUA VUMBI VIWANJA KUMI

October 04, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea wikiendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana katika viwanja kumi tofauti.

Jumamosi kutakuwa na mechi kati ya Green Warriors na Friends Rangers (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa Majimaji, Songea) na Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi, Mafinga).

Polisi Dodoma na Stand United (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Toto Africans na JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mwadui na Polisi Mara (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi Tabora na Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi kati ya African Lyon na Transit Camp (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa Squad dhidi ya Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam).

WASHABIKI WENYE SILAHA MARUFUKU VIWANJANI

October 04, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.

Jeshi la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zinakataza silaha viwanjani.

Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba. Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.

Hivyo, kwa washabiki wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala yake tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.

Pia tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.

SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE

October 04, 2013
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.

Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.

Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine inazopata hapo.

Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.

“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia wachezaji wetu,” amesema.

Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe

UAMUZI KAMATI YA MAADILI KUFANYIWA MAPITIO

October 04, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Shirikisho liko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar es salaam.

Hivi sasa, wagombea wanasubiri vyombo vya juu vya uamuzi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kabla ya kuanza kampeni na hatimaye uchaguzi.

Hata hivyo, baada ya Kamati ya Maadili kufanya uamuzi dhidi ya kesi nane zilizowasilishwa mbele yake, Sekretarieti imeona kuwepo kwa ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kuna baadhi ya mambo yanaonekana kuwa na ugumu katika kuyatekeleza.

Sekretarieti si chombo chenya mamlaka ya kutafsiri uamuzi wa vyombo huru vya Shirikisho, kazi yake kubwa ni kupokea uamuzi na kuutekeleza, hivyo kwa kuwa kuna ukakasi huo imeamua kuwasilisha uamuzi huo kwenye Kamati ya Rufani ya Maadili kwa ajili ya kuufanyia mapitio (revision) na pia kutoa mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi huo kwenye Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kuendelea na mchakato.

Sekretarieti imefanya hivyo kwa lengo la kusaidia wagombea ambao wengi wanaonekana kuwa njia panda baada ya kupokea uamuzi wa Kamati ya Maadili na kuiuliza Sekretarieti kuwa inakuwaje Kamati ya Maadili iwaone hawana hatia, lakini hapo hapo ikubaliane na uamuzi wa kuwaengua, jambo ambalo kwa kweli limetufanya tukose majibu sahihi na hivyo kuamua kuomba revision na mwongozo.

Pia mwongozo utakaotolewa na Kamati ya Rufani ya Maadili utasaidia kuweka mwelekeo mzuri wa masuala ya Maadili katika siku zijazo.

Miongoni mwa mambo yanayoonekana kuwa na ukakasi ni kuwaona watu wote ambao kesi zao ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana hatia, lakini hapo hapo kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa kuwaengua baadhi yao kwa sababu za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara mbili kwa kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi.

Ili haki itendeke na ionekane inatendeka, Sekretarieti imeona ni vizuri masuala hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na kutolewa mwongozo ili kuondoa ukakasi uliojitokeza miongoni mwa wagombea, Shirikisho na wadau na hivyo kujenga hisia kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya baadhi ya wagombea.

Uamuzi huu haumaaniishi kuwa Sekretarieti inapingana na uamuzi wa Kamati ya Maadili, bali ni utaratibu wa Sekretarieti kuomba ufafanuzi au mwongozo kutoka vyombo husika pindi inapotokea ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi wa vyombo vya uamuzi vya Shirikisho.

Sekretarieti imeshamwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Maadili ili aitishe kikao kwa manajiri ya kufanya mapitio na kutoa mwongozo ambao utasaidia Shirikisho kuendelea na uchaguzi bila ya ukakasi.

TUPO IMARA KUPAMBANA NA AZAM FC-MORROCO

October 04, 2013
NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
KOCHA MKUU wa Timu ya Coastal Union ya Tanga,Hemed Morroco amesema kikosi cha timu kipo tayari kuwavaa wapinzani wao Azam Fc katika mchezo wa Ligi kuu Tanzania bara ambao utachezwa kesho kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.

Morroco alitoa kauli hiyo leo wakati wa mazoezi ya asubuhi ambapo timu hiyo inajifua katika uwanja wa soka Disuza ikiwa na wachezaji wake wote lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mpambano huo utakaochezwa saa kumi kamili za jioni Jumamosi hii.

Akizungumza hali za wachezaji,Morroco alisema wapo imara na wanaendelea kufanya maandalizi yao ya mwisho kabla ya kuwakabili wanarambaramba hao ambapo alisema wamepania kuibuka na ubingwa kwenye mchezo huo.

Morroco alisema wachezaji wake wote wanaendelea vizuri na mazoezi na wapo imara kuweza kuwakabili wapinzani wao hao isipokuwa mchezaji wao Abdi Banda ambaye anasumbuliwa na majeraha madogo madogo lakini akaongeza kuwa upo uwezekano mkubwa wa kucheza mechi hiyo.

Morroco aliongeza kuwa watahakikisha kuwa wanacheza kufa na kupona ili kuweza kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa.


Kwa upande wake,Msimamizi wa kituo cha Tanga,Khalid Abdallah alitaja viingilio kwenye mechi hiyo kuwa ni 7000 na 5000 mzunguko ili kuweza kuwapa fursa wadau wa soka kuhudhuria mchezo huo.

HALL MECHI YETU NA COASTAL UNION KESHO ITAKUWA NGUMU.

October 04, 2013
NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
KOCHA Mkuu wa timu ya Azam FC "Wanarambaramba"Stewart Hall amesema mechi yao ya Ligi kuu Vodacom Tanzania bara dhidi yao na Coastal Union itakayochezwa Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani itakuwa ngumu kutokana na Coastal Union kuwa na sapoti kubwa ya mashabiki hasa inapokuwa ikicheza nyumbani.

Hall alitoa kauli hiyo wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini hapa na kuelezea maandalizi kwaupande wao yanaendelea vema licha ya kuwa na wachezaji wenye majeraha madogo madogo ambao huenda wakacheza mechi hiyo.

Aliongeza kuwa licha ya kuwa na sapoti lakini ni timu nzuri hivyo
watahakikisha wanafanya kazi ya zaida ili kuweza kupata ushindi kwenye mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa.

   "Tunajua Coastal Union inasapoti kubwa sana ya mashabiki hasa
wanapokuwa wakicheza nyumbani hivyo sisi tunahitaji kujiandaa vya kutosha ili kuweza kupata ushindi kwa kucheza kwa umakini
mkubwa"Alisema Hall.

Hall alisema mchezaji kwenye majeraha ambaye huenda akaukosa mchezo huo ni mlinda mlango wao Aishi Manula ambaye pia amewasili mkoani hapa akiwa na wenzake.

Azam Fc imetua juzi jijini Tanga ikiwa na wachezaji wake wote na
imekuwa ikifanya mazoezi katika uwanja wa Mkwakwani ambapo mashabiki nawapenzi wa soka mkoani hapa wamekuwa wakijitokeza kushuhudia mazoezi hayo.

Wakati Azam Fc ikifanya mazoezi Mkwakwani wapinzani wao Coastal Union wao wanaendelea na mazoezi yao katika uwanja wa soka Disuza ikiwana wachezaji wake wote kamili kuweza kuwakabili wanaramaramba hao.

Katika mechi hiyo viingilio vinatarajiwa kuwa sh.7000 na 5000 mzunguko ili kuweza kuiwapa fursa wadau wa soka mkoani hapa kuweza kupata nafasi ya kuitazama mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa

HALMASHAURI YA SIHA MKOANI KILIMANJARO INAKABILIWA NA UPUNGUFU WA WATUMISHI 379

October 04, 2013
NA OMARY MLEKWA.
WAJUMBE wa Baraza la Madiwani Wilayani Siha mkoani Kilimanjaro limeiomba serikali  kutoa kibali kwa halmashauri nchini  kuajiri watumishi ili  kukabiliana na uhaba wa watumishi katika halmashauri zote kwa madhumuni ya kuleta maendeleo zaidi.
 
Ombili hilo limetolewa  katika  kikao cha baraza maalumu la Madiwani wilayani Siha cha kupokea taarifa ya hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012  ambapo wameiomba serikali kuwapatia kibali cha kuajiri watumishi  ili kuboresha huduma kwa wananchi
 
Halmashauri hiyo  inakabiliwa  na upungufu wa watumishi 379 wa idara mbalimbali hali inayochangia zaidi   kuzorotesha maendeleo ya halmashauri hiyo.
 
Wakizungumza katika baraza hilo wajumbe hao walisea baadhi ya hoja zilizotolewa na mkaguzi wa serikali zimechangia na upungufu wa watumishi idara mbalimbali kutokana na watumishi kuzidiwa na kazi wanazofanya isiyoendana  kasi ya ongezeko la wananchi pamoja na miradi inayotekelezwa katika wilaya ya hiyo
 
Akichangia hoja hiyo, Makamu Mwenyekiti  wa Halmashauri hiyo Dancan Urasa alisema kutokana na upungufu walionao katika kitengo cha ukaguzi wa ndani kumesababisha kuwepo kwa hoja ambazo zingeweza kutatuliwa na wakaguzi hao kwa kushirikiana na wataalamu wengine
 
Alisema kitengo hicho kwa sasa kinawatumishi wawili tu hali ambayo inakuwa shida kukaguzi shughulizote zinazotekelezwa  ndani Wilaya na kuiomba wizara husika kuwapatia kibali cha kuajiri angalau mtumishi mwingine mmoja ili kuimarisha kitengo hicho
 
Urassa alisema ikiwa halmashauri zitapewa mamlaka ya kuajiri watumishi zitaweza kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuwa watumishi watakaoajiriwa watachukuliwa wakiwa wanatambua mazingira wanayokwenda kufanyia kazi kwenye halmashauri husika .
 
Awali akiwakilisha hoja za mkaguzi  hesabu za  serikali  kwa niaba ya mkaguzi mkazi ofisi ya Taifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali mkoani Kilimanjaro,Fredi Mapunda alisema wilaya hiyo katika ukaguzi ilipata hoja 38  ambapo hoja nane zilifungwa kutokana na kudhirishwa  na majibu yaliyotolewa na wataalamu
 
Mapunda alisema halmashauri hiyo ihakikishe kuwa inafuatilia maoni ya mkaguzi ambapo mkaguzi aliwashauri kukumbushia ofisi ya Rais  menejment na utumishi wa Umma na Wizara ya fedha kuruhusu kupata kibali cha kuajiri
 
Akijibu hoja hizi mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Siha, Rashidi Kitambulio alisema walishaandika barua kwa katibu mkuu Menejment ya utumishi wa umma na kupatiwa watumishi wa 70 wa idara ya elimu  na 19 wa idara ya afya  na halmashauri imeshatuma barua ya ajira mbala kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo
 
Alibainisha kuwa athari zinazotokana na upungufu huu wa watumishi ni utoaji wa huduma usioridhisha, pamoja na watumishi kukosa ari ya kufanya kazi kwa kuwa mtumishi mmoja kwa wastani anafanya kazi ya watu wawili hadi watatu jambo ambalo huchangia ucheleweshaji wa shughuli nyingi za kimaendeleo ndani ya halmashauri hii.
 
Hata hivyo wajumbe hao walishauri serikali  baadhi ya kada ya ajira zake zifanywe na halmashauri  ili kuweza kuwapata watumishi hao ikiwemo ajira za watendaji wa kata na kijiji  badala ya ajira hizo kutolewa na Menejmenti ya Utumishi wa Umma pekee