WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA TURIANI WATAKIWA KUFUATA SHERIA.

August 26, 2024

 



Na. Ramadhani Kissimba, WF, Morogoro

Watoa huduma ndogo za fedha katika tarafa ya Turiani Mkoani Morogoro wametakiwa kutoa huduma hizo kwa wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na serikali.

Akizungumza katika mfufulizo wa program ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fedha, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtibwa kaika tarafa ya Turiani, Wilayani Mvomero, Bi. Rudhaa Antony alisema baadhi ya Taasisi zilizopo katika tarafa hiyo zimekuwa zikitoa huduma bila ya kuzingatia taratibu zilizowekwa kwa kutoa huduma hizo kwenye magari badala ya kuwa na ofisi rasmi ya kutolea huduma hizo.

‘’Kwa kupitia elimu hii namuomba mwenyekiti wa wafanyabiashara aliyepo hapa, Taasisi za kutoa huduma ndogo za fedha zote zielezwe kuzingatia utozaji wa riba iliyowekwa na Benki Kuu, na pia kuacha kutoa huduma kwenye magari na kudai marejesho saa tisa usiku kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume cha sheria’’ alisema Bi. Rudhaa.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kutokana na elimu iliyotolewa itawasaidia wananchi wa tarafa ya Turiani hasa wakina mama kuachana na tabia ya kukopa kwenye Taasisi ambazo zimekuwa kero kwa wananchi jambo ambalo linachangia kuzorotesha Uchumi wa eneo hilo kutokana na wananchi kukimbia makazi yao kwa kushindwa kumudu kulipa madeni yanaoyotokana na riba kubwa inayotozwa na baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha.

Aidha, Bi. Rudhaa aliwata Wananchi kuzifichua Taasisi zote zinazotoa huduma za fedha kwa kukiuka misingi ya leseni ya utoaji huduma hiyo hasa wale wanaotoa mikopo kandamizi (mikopo kausha damu) kwa wateja wake pamoja na kuwafanyia vitendo vya uzalilishaji ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.

Kwa upande wake, Mratibu wa huduma ndogo za fedha Wilaya ya Mvomero Bw. Clement Maganga alisema kuwa kwa sasa wananchi wameshaelewa mikopo inayokubalika kwa serikali inayotolewa na taasisi za fedha zilizosajiliwa ni ile isiyotoza riba zaidi ya asilimia 3.5 kwa mwezi na atakayezidisha kiwango hicho atakuwa amefanya kosa.

Bw. Maganga alisisitiza kuwa wananchi kuendelea kuimarisha na kusajili vikundi vyao vya huduma ndogo za fedha kwa sababu kuwepo kwa vikundi hivyo vitapunguza wimbi la wananchi wanaokimbilia katika mikopo ya kausha damu.

Aidha kwa upande wake, afisa usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba alisema kuwa Taasisi zote zitakazo bainika kukiuka misingi ya utoaji mikopo kama ilivyoelekezwa na Benki Kuu ya Tanzania zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutiwa leseni huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Wilaya pindi wanaposhuhudia ukiukwaji wa misingi ya leseni kwa watoa huduma za fedha.

Bw. Mushumba aliongeza kuwa ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Mvomero amewataka wananchi kuyaelewa masharti ya mikopo kabla ya kuchukua mikopo hiyo na kuzitaka taasisi zinazotoa huduma za fedha kuainisha na kuweka wazi masharti na taratibu za kupata mikopo katika taasisi zao.

Katika program ya utoaji elimu ya mauala ya fedha, Serikali inakusudia hadi kufikia mwaka 2025 takribani asilimia 80 ya wananchi wawe wamepata uelewa wa masuala ya fedha na kupelekea kundi kubwa kufaidika na huduma hizo na hivyo kuongeza fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza pato la Taifa.Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtibwa, katika tarafa ya Turiani , Wilayani Mvomero Bi. Rudhaa Antony akizungumza katika program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.
Mkazi wa Mtibwa,Wilaya ya Mvomero Bi. Latifa Japhari akichangia mada iliyotolewa na wataalamu wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na washirika wa sekta ya nchini katika program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.
Mratibu wa huduma ndogo za fedha Wilaya ya Mvomero, Bw. Bw. Clement Maganga akizungumza wananchi wa kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani Wilayani Mvomero waliohudhuria program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiashara Wilaya ya Mvomero, Bw. Juma Kibacho akichangia jambo katika program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.Afisa usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba akizungumza wananchi wa kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani Wilayani Mvomero waliohudhuria program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha – Morogoro)

TUME YAVIASA VYAMA VYA SIASA KUTOINGILIA MCHAKATO WA UBORESHAJI WA DAFTARI

August 26, 2024

 

Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila.
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila. 
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila. 
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani akizungumza wakati akiwasisha mada ya maandalizi ya uboreshaji kwa wadau wa uchaguzi Mkoa wa Mara. 
Mkurugenzi wa Daftari na TEHAMA wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Stanslaus Mwita akiwasilisha mada ya mifumo wakati wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara.
Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akiteta jambo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima Ramadhani wakati wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara.


Wadau wakishiriki katika majadiliano. 

Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akiongoza majadiliano. 

Wadau wa uchaguzi wakiwa katika majadiliano.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima Ramadhani akijibu hoja mbalimbali wakati wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara.
***************
Na. Waandishi wetu, Mara
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeviasa vyama vya siasa kutoingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika vituo vya kuandikishia wapiga kura.
 
Wito huo umetolewa leo tarehe 25 Agosti, 2024 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika mkoani Mara.
 
Mhe. Jaji Mwambegele amesema mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji vituoni kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya uchaguzi.
 
Amehimiza viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria ya uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya tume, na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi la uboreshaji wa Daftari.
 
Pia amevitaka vyama vya siasa kutumia sheria zilizopo kuwasilisha changamoto zinazojitokeza kwa tume, ambapo ameongeza kuwa INEC itazingatia Katiba, sheria ya uchaguzi, na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi la uboreshaji.
 
Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhan Kailima amsema Tume inategemea vyama vyenye usajili kamili kutumia fursa za kisheria zilizotolewa kwao kuhakikisha zoezi la uboreshaji linafanikiwa na kuongeza kuwa endapo kutajitokeza changamoto zozote wakati wa zoezi, Vyama vitumie taratibu zilizoainishwa kwenye sheria kuwasilisha changamoto hizo.
 
“Viongozi wa vyama hawapaswi kuingilia utekelezaji wa majukumu ya watendaji wa vituo wakati wote wa uandikishaji wa wapiga kura vituoni kama kuomba orodha au idadi ya walioandikishwa au kuboresha au kuhamisha taarifa zao,”
 
Ameeleza kuwa, Tume inaowajibu wa kuwapatia vyama vya siasa taarifa hizo mara baada ya zoezi kukamilika.
 
Mkutano kama huo umefanyika pia mkoani Simiyu na Manyara ambapo akifungua mkutano mjini Bariadi, mkoani Simiyu, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk S. Mbarouk, amewataka wadau kuwaelimisha wananchi kujiandikisha mara moja tu ili kuepuka uvunjaji wa sheria.
Naye Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari, ambaye alifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Manyara, amewahimiza watu wenye ulemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito, na akina mama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni kujitokeza kwa wingi kwa kuwa watapewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni.
 
Mikutano hiyo ni maandalizi ya mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao utajumuisha mkoa wa Mara, Simiyu na  baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu ambapo uboreshaji utaanza tarehe 04 Septemba, 2024 hadi 10 Septemba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
-- Mroki Mroki Online Reporter/Blogger Mob: +255 755 373999 Email: mrokim@gmail.com. Blog: https://mrokim.blogspot.com/ DODOMA, TANZANIA

Vyuo Vikuu Vyote vya Afya na Sayansi Shirikishi Nchini Vyatakiwa Kutumia Mtaala Mmoja Wa Elimu

August 26, 2024

 


Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Peter Msofwe akizungumza wakati wa ufunguzi wa  kongamano la mradi wa kufundisha wataalamu wa Afya (THET), ambapo mbali na mambo mengine wamejadili  kuanzishwa kwa Academy ambayo itatumika kuboresha mafunzo ya walimu wa vyuo vikuu katika sekta ya afya, kutengenezwa na kuanza kutumika kwa mitaala linganifu kwenye vyuo vikuu vya afya nchini na kutengenezwa kwa mfumo wa kuunganisha wahitimu wa afya nchini. Kongamano hilo imefanyika leo Agosti 26,2024 MUHAS Jijini Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Prof.  Apollinary Kamuhabwa akizungumza wakati wa kongamano la wa THET leo Agosti 26,2024 jijini Dar es Salaam.
Prof. Blanding Mbaga kutoka kutoka  Kilimanjaro Christian Medical University College,  akizungumza wakati wa kongamano hilo.
Mratibu wa mradi wa mapitio wa namna ya kufundisha wataalamu wa afya  (THET) Profesa Gideon Kusigabo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo lililofanyika leo Agosti 26,2024 katika chuo cha MUHAS Jijini Dar Es Salaam.

Na Karama Kenyunko Michuzi TV
SERIKALI imevielekeza vyuo vyote vya Afya na Sayansi Shirikishi nchini kutumia mtaala mmoja ili kuwa na watoa huduma wenye ujuzi na ubora unaolingana baada ya mtaala wa awali kuonekana kutotosheleza mahitaji.

Hayo yamesemwa leo Agosti 26,2024 jijini  Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msofwe wakati wa kongamano lililoandaliwa na Mradi wa THET.

Mradi huo wa mapitio wa namna ya kufundisha wataalamu wa afya (THET)  ulishirikisha vyuo vikuu vya Afya na Sayansi  Shirikishi vya Muhimbili (MUHAS), KCMC, Chuo cha Katoliki CUHAS, San Francisco na Chuo Kikuu cha Duke.

Ameeleza kuwa wadau walipendekeza kutumika kwa mbinu za kibunifu kwa ajili ya kuhakikisha elimu ya juu kwa upande wa vyuo vya Afya vinakuwa na ubora ili kuondoa mashaka kwa wagonjwa pindi wanapohudumiwa.

"Tuna Sera ya Elimu ya mwaka 2023 imebadilisha mitaala kwa ngazi zote kuanzia shule ya msingi hivyo nasisitiza vyuo vya Afya viwe na mtaala mmoja," alisema Profesa Msofwe.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Apollinary Kamuhabwa amesema kuwa mradi huo uliangalia namna wanavyowatahini madaktari wa binadamu na wauguzi.

Alisema kuwa mtaala huo utainua ubora na mafunzo ya elimu ya juu nchini kwa madaktari na wauguzi watakuwa na uelewa wa pamoja.

"Teknolojia imebadilika magonjwa yamekuwa mengi na watu wengi hupitia kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kwenda kuonana na daktari hivyo ni lazima wataalamu wa afya wajiandae na mabadiliko haya," amesema Profesa Kamuhabwa.

Naye, Mratibu wa THET Profesa Gideon Kusigabo amesema kuwa mtaala wa awali waliokuwa wanautumia haukuwa vizuri kwani walimu walikuwa wanashindwa jinsi ya kuandaa mafunzo kwa vitendo.

Pia amesema wanalenga kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa ajili ya kutekeleza mtaala na kuongeza uwezo wa walimu wawe bora katika masuala ya afya.

"Tunalenga kuendeleza tafiti ndani ya ufundishji ili tuwe na walimu bora kwani walimu wengi wanaingia kufundisha lakini hawana viwango bora na athari zake ni kutoweza kutahini wauguzi na madaktari wazuri na kutoweza kufundisha vizuri," amesisitiza.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kwamba watoa huduma za afya hususan wahitimu wa udaktari na uuguzi kutokuwa na ubora unaotakiwa.

TIRA YAPAZA SAUTI BIMA ZA VYOMBO VYA MOTO KWENYE WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI

August 26, 2024

 



Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki katika ufunguzi rasmi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 2024 ambayo inaadhimishwa kitaifa mkoani Dodoma katika Viwanja vya Jamhuri. 

Maadhimisho haya yamezinduliwa rasmi leo Agosti 26, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango ambaye pia alitembelea banda la TIRA.

Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware amemueleza Mhe. Dkt. Mpango alipotembelea banda la TIRA kuwa Mamlaka inahakikisha kuwa watoahuduma za bima ya vyombo vya moto wanawafikia watanzania kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha huduma na bidhaa za bima zinawafikia walengwa na zinatumiwa ipasavyo kwa maendeleo endelevu na kuleta ustahimilivu wa soko na sekta ya bima kwa ujumla. 

Aidha, Dkt. Saqware ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watanzania kutumia vyombo vya moto vilivyokatiwa bima kwa ajili ya usalama wao. 

Kupitia kaulimbiu ya mwaka huu ambayo ni “Endesha Salama, Ufike Salama” inayolenga kuhamasisha na kuchochea kila mmoja kuchukua tahadhari awapo kwenye chombo cha moto, Mamlaka pia imeendelea kutoa elimu ya bima na kuwahamasisha watanzania kuhusu masuala mbalimbali ya bima ikipaza sauti kupitia maadhimisho haya juu ya umuhimu wa bima ya vyombo vya moto na fidia wanazopata watumiaji wa bima hiyo.




RAIS DKT. SAMIA KUFUNGUA RASMI KIKAO KAZI CHA MSAJILI WA HAZINA NA WAKUU WA TAASISI AGOSTI 28, 2024 JIJINI ARUSHA

August 26, 2024

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua rasmi kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali (CEO FORUM 2024), kitakachofanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2024, kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC Jijini Arusha.

Mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina una lengo la kuwaweka pamoja wakuu hao na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo maboresho yanayoendelea katika kuimarisha usimamizi, uendeshaji na utendaji wa Taasisi za umma sambamba na kubadilishana uzoefu.

Akizungumza na waandishi wa Habari Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda amesema kuwa kikao hicho kitafunguliwa rasmi Agosti 28, 2024, siku moja baada ya watendaji hao kuanza kukutana, nakwamba kinatarajiwa kufungwa rasmi Agosti 30 huu.

Aidha Mhe. Makonda, ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka kutumia ugeni huo kuweza kujinufaisha kupitia fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji.

Kikao kazi hicho ni cha pili baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza Mwezi Agosti 2023, ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma kuwekeza Nje ya Tanzania' ('Public and Statutory Corporations Business Strategies Beyond Tanzania')

Kaulimbiu hii inalenga kuhimiza Taasisi na mashirika ya umma kuangalia fursa za kuwekeza au kupanua wigo wa Biashara nje ya Tanzania.

Aidha, Kaulimbiu hiyo inaunga mkono kauli ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Kikao Kazi cha mwaka jana 2023.

Katika Kikao hicho, Mhe. Rais alielekeza kuangalia uwezekano wa Mashirika kwenda kufanya Biashara au kupelekea huduma zake nje ya Tanzania.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia Taasisi na Mashirika ya Umma 304 Idadi hiyo inajumuisha Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chini ya asilimia 51.

Taasisi na Mashirika hayo yamekuwa na mchango muhimu katika kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali zikiwemo sekta za fedha, elimu, afya, hifadhi ya jamii, viwanda, biashara na kilimo.

Taasisi hizo pia zinachangia katika kukuza Pato la Taifa, kuchangia mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali, kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kukuza ajira, kurahisisha upatikanaji wa huduma na bidhaa, pamoja na kuhakikisha kuwa huduma na bidhaa zinazotolewa zinakuwa na ubora na bei stahiki.

FURSA YA UFADHILI WA MASOMO CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA

August 26, 2024

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza Mradi wa miaka mitano wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia na unatekelezwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania huku ukisimamiwa vyema na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.