TANROADS WATAKIWA KUPAMBANA NA UGONJWA WA BARABARA KUHARIBIKA KABLA YA MUDA WAKE.

February 14, 2024

 Na Janeth Raphael - MichuziTv - DODOMA.



Waziri Mwenye Dhamana katika Wizara ya Ujenzi, Mh Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutafuta ufumbuzi kuhusu suala la kuharibika kwa barabara kabla ya muda uliopangwa ili kuokoa fedha za Serikali zitakazotumika kurekebisha miundombinu hiyo.

Ameyatoa maagizo hayo jijini Dodoma leo Februari 14, 2024 katika kikao cha 19 cha Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS na kuwasisitiza kusimamia miradi kwa weledi na uzalendo ili kusaidia miradi kukamilika kwa viwango na kwa wakati.

“Suala la kuharibika kwa barabara kabla ya wakati ‘pre-mature failure’ ni tatizo, hakikisheni mnapambana nalo, chukueni hatua za kisheria kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi chini ya kiwango”.

Aidha, Waziri Bashungwa ameagiza tena TANROADS kutumia kikamilifu mtambo wa Ukaguzi wa Barabara (Road Scanner) wakati wa kufanya ukaguzi wa miradi ya barabara na madaraja na hata kutumia vifaa vingine vitakavyoweza kuwasaidia kubaini ubora wa mradi mapema kabla ya kukabidhiwa.

Ameielekeza TANROADS kuimarisha na kukijengea uwezo Kitengo chake cha Usimamizi wa miradi (TECU), ili kusimamia miradi kwa weledi na ufanisi.

Kadhalika, Bashungwa ameitaka TANROADS kusimamia sheria ya uzito wa magari barabarani na kutoa faini au adhabu nyingine kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwaelekeza Maafisa wanaofanya kazi kwenye mizani kutii na kufuata sheria kama inavyoelekeza ili kuzilinda barabara nchini.

“Hakuna kiongozi wala mtumishi ambaye yupo juu ya sheria, hata mimi siwezi kumsaidia yeyote anayekiuka sheria hii, atakayekiuka achukuliwe hatua na sio kunipigia simu".

Sambamba na hayo amesisitiza umuhimu wa Wakala huo kuwajengea uwezo Wataalam wake ikiwemo katika eneo la usimamizi wa miradi na mikataba ili kuleta tija kwa TANROADS na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, amemhakikishia Waziri Bashungwa kutekeleza maagizo aliyowapa na kuendelea kufanya kazi kwa ari na bidi katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija kwa Wakala huo.

Naye, Mweyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyingine (TAMICO), Eng. Nchama Wambura, amesema wataendelea kushrikiana na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa utekelezaji sahihi na ubora kwa miradi wanayoendelea kutekeleza nchini.

Ni siku mbili za Mkutano wa 19 wa Baraza lawafanyakazi wa TANROADS ambao imefanyika hapa Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 100 kutoka Mikoa yote Nchini.




HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAANZA KAMBI YA UPASUAJI WA MOYO

February 14, 2024

 Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma imeanza kambi ya upasuaji wa moyo kwa watu wazima.


Daktari Bingwa wa Moyo wa BMH, Dkt Kelvin Masava, amesema leo kuwa kambi hii ya pamoja ya wiki moja kati ya wataalam wa BMH na wenzao kutoka Uholanzi itahusisha vipimo na matibabu kwa njia ya upasuaji wa kufungua kifua.

"Mpaka sasa, tuna wagonjwa 450 ambao watafanyiwa uchunguzi, watakaokutwa na matatizo watapatiwa matibabu," amesema Daktari huyo Bingwa wa Moyo na kufikia sasa wamewafanyia uchunguzi wagonjwa 146 na wagonjwa wawili wamenufaika na huduma ya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo kwa mishipa iliyoziba bila kuusimamisha moyo "Off-pump Coronary Artery Bypass surgery"

Dkt Masava ametoa wito kwa watu wazima wenye matatizo ya moyo katika Kanda ya Kati na mikoa ya jirani waitumie kambi hii ya matibabu katika BMH kwa ajili ya kupata suluhisho.

Dkt Masava ameongeza kuwa lengo la kambi hii ya pamoja na wenzao wa Uholanzi ni kutoa huduma pamoja na kubadilishana uzoefu.


TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO NA MAONESHO YA 11 YA PETROLI AFRIKA MASHARIKI

February 14, 2024


Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeipitisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Machi 2025.

Mbali na hayo mkutano huo umepitisha bajeti ya kiasi cha Dola za Marekani 1,842,467 kwa ajili ya maandalizi ya kongamano na maonesho hayo.

Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya, na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.

Katika hatua nyingine mkutano huo umetoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya na watu wake.

Aidha, katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye pia ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar umependekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji.

Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara ameeleza kuwa Jumuiya itaweza kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na biashara endapo, pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikana wa nishati ya uhakika na salama.

“Sekta ya Nishati ina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya. Hivyo umuhimu wa upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama na gharama nafuu ni jambo la lazima na sio la hiyari kwani ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji na kufanya bidhaa na huduma zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la ndani na kimataifa”. Alieleza Waziri Kaduara

Vilevile Mhe. Kaduara alitumia fursa ya mkutano huo kutoa mwaliko kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuja nchini, kushuhudia na kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Maji wa Bwawa la Julius Nyerere, unaotarajia kuzalisha Megawatts 2115 utakaofanyika tarehe 25 Februari 2024.

Mkutano huo wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika kwa siku tatu kuanzia 12-14 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, ulitanguliwa na Mkutano wa Wataalam na Makatibu Wakuu.

Viongozi wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC wakisaini (walioketi) taarifa ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 14 Februari 2024. Waliosimama ni Watendaji mbalimbali kutoka nchi wanachama wakishuhudia zoezi hilo.

Viongozi wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC wakisaini (walioketi) taarifa ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 14 Februari 2024. Waliosimama ni Watendaji mbalimbali kutoka nchi wanachama wakishuhudia zoezi hilo.

Viongozi na Watendaji wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumazika kwa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 14 Februari 2024, jijini Arusha.

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AZINDUA UTAFITI WA GHARAMA ZA UTAPIAMLO NCHINI

February 14, 2024
Naibu Waziri Ofisi Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la utafiti wa Gharama za utapiamlo nchini zoezi lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Ngome Jijini Dodoma.Tarehe 14 Februari 2024.

Mwakilishi Mkazi  Nchini wa Shirika la Mpango wa  Chakula Duniani (WFP) Bi, Sara Gibson  akitoa neno la utangulizi katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la utafiti wa Gharama za utapiamlo nchini zoezi lizoezi lilofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Ngome Jijini Dodoma. Tarehe 14 Februari, 2024.

Matukio katika picha Wajumbe mbalimbali walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la utafiti wa Gharama za utapiamlo nchini zoezi lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Ngome Jijini Dodoma. Tarehe 14 Februari, 2024




NA MWANDISHI WETU; DODOMA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amezindua Rasmi zoezi la utafiti wa gharama za Utapiamlo nchini, ikiwa ni sehemu ya  utekelezaji wa maazimio ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kupitia mpango ujulikanao kama “The Cost of Hunger Study in Africa – COHA” ambapo Mheshimiwa DKt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia ufanyike ikiwa ni  nia yake ya dhati ya kuondoa utapiamlo nchini.

Uzinduzi huo Uliofanyika katika Ofisi wa Waziri Mkuu Jijini Dodoma Tarehe 14 Februari, 2024. Naibu Waziri Nderiananga Alisema, Lengo la utafiti ni kubainisha makadirio ya gharama zinazosababishwa na matatizo ya lishe duni yani utapiamlo kijamii na kiuchumi na hususan katika nyanja za sekta ya afya, elimu na nguvu kazi. 

Aliongezea kuwa Tanzania itakuwa nchi ya 22 Barani Afrika kufanya utafiti kama huo pindi utakapokamilika na  kwa mwaka 2024, takribani nchi 6 (ikiwemo Tanzania) zimeonesha utayari wa kufanya utafiti huo ili kuwezesha nchi kupanga malengo ya kupunguza upotevu wa pato ghafi itokanayo na utapiamlo na kuwekeza katika maeneo ya maendeleo.

Aidha, Naibu Waziri Nderiananga  amewashukuru wataalamu wa Chakula na Lishe kwa kuishauri vyema Serikali juu ya umuhimu wa utafiti katika nchini.


“Tunapokwenda kuandaa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, niwashukuru wadau wetu wakiwemo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ambao tayari wameshatoa fedha ambazo zitasaidia sana katika hatua muhimu za utafiti huu”. Alisisita

Kwa upande wake Mwakilishi  kutoka UNICEF Bw. John George ametoa pongezi kwa Serikali kwa kujiunga na Mpango wa COHA na kutambua nafasi ya mtoto ambaye ndiye mlengwa mkubwa katika mpango huo na kwa tafiti zilizotoa takwimu za utapiamlo nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mwakilishi Mkazi Nchini, wa Progamu ya Chakula Duniani (WFP) Bi Sarah Gibson Alisema Tafiti hizo zitasaidia kukabiliana na madhara yatokanayo na Utapiamlo nchini kama vile ukuaji kwa mtoto na huweza kuleta athari katika elimu ya mtoto na Maendeleo ya Taifa kwa Ujumla.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw.Salihina Ameir alisema kwa Upande wa Zanzibar, Ofisi hiyo ina nafasi kubwa katika Uratibu wa masuala ya Kiuchumi kisiasa na Kijamii ikiwa ni Pamoja na masula ya Tafiti za Lishe.

Zoezi hili la suala zima la uzinduzi wa gharama za zoezi la Tafiti za Utapiamlo nchini, linafadhiliwa na Programu ya Chakula Duniani (WFP) pamoja na  wadau wengine wa maendeleo nchini kama vile USAID, FAO, Irish Embassy, Hellen Keller International – HKI na UNICEF
February 14, 2024

 

Dar es Salaam. Tarehe 09 Februari 2024: Baada ya wateja wanne wa Benki ya CRDB kupelekwa nchini Ivory Coast kutizama mechi za ufunguzi za Michuano ya Mataifa Huru Barani Afrika (Afcon), wateja wengine watatu wamepata nafasi ya kwenda kuangalia fainali za michuano hiyo.

Waliobahatika awamu hii ni Bakari Mikidadi kutoka jijini Dodoma pamoja na Veronica Mshometa na Dickson Kabaka wote wa wawili wa jijini Dar es Salaam.

Katika droo hiyo, washindi walipatikana baada ya droo kadhaa zilizochezeshwa wiki iliyopita ambazo ama wateja hawakupokea simu au walipokea lakini hawakukidhi vigezo hasa kile cha kuwa na pasi ya kusafiria iliyo hai.

Akiwaaga washindi hao katika hafla fupi iliyofanyika kwenye studio za Redio ya Wasafi, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kadi wa Benki ya CRDB, Farid Seif amesema washindi wa awamu hii wamepatikana kwenye kampeni ya Tisha na Tembocard Tukakiwashe Afcon iliyozinduliwa Novemba 2023 ambayo sasa imehitimishwa baada ya kudumu kwa miezi mitatu ikiwahamasisha Watanzania kutumia kadi zao kufanya malipo ya matumizi wanayoifanya kila siku.
“Kigezo kikubwa cha kushinda zawadi zetu zilizojumuisha samani za ndani, vifaa vya kielektroniki pamoja na safari ya kwenda Ivory Coast kutizama michuano ya Afcon ilikuwa kutumia kadi yako ya Tembocard.

Washindi hawa watatu tunaowaaga leo wamekuwa vinara wa kufanya hivyo kwa mwezi Januari. Tunafurahi kuwaaga wateja wetu hawa wanapoelekea Abidjan kuungana na mashabiki wengine wa soka kutoka kila pembe ya Afrika na dunia kwa ujumla,” amesema Seif.
Licha ya wateja hao wanaoenda Ivory Coast, mteja mwingine, Charles Onesmo Lyimo wa jijini hapa amejishindia samani za ndani pamoja na vifaa vya kielekitroniki hivyo kuungana na Fatima Mwatime Nundu kutoka jijini Tanga alinyakua samani za ndani zinazojumuisha seti ya sofa na meza zenye thamani ya shilingi milioni 8 kwenye droo ya kwanza iliyochezeshwa Desemba 2023 pamoja na Marion Albert Casari aliyeshinda seti ya vifaa vya kielektroniki inayojumuisha runinga, friji na ‘sound bar’ kwenye droo ya pili.

Katika kampeni hiyo ya matumizi ya kadi, Benki ya CRDB ilikuwa inashirikiana na kampuni ya kimataifa ya Visa hivyo washindi waliopatikana watalipiwa kila kitu katika safari yao hiyo  kuanzia malazi, nauli mpaka kiingilio cha uwanjani pamoja na mizunguko yote watakayoifanya nchini Ivory Coast.

“Dunia inaondoka kwenye mfumo wa kulipa kwa fedha taslimu. Benki ya CRDB inachukua kila hatua muhimu kushawishi matumizi ya mifumo mbadala ya kufanya miamala kwa kuwahamasisha wateja wake kulipa kwa kutumia kadi. Ukiwa na Tembocard, unao uhakika wa kununua bidhaa au kulipia huduma mahali popote duniani.
Huna haja tena ya kuhangaika kubadili shilingi ulizonazo au kutembea na fedha taslimu kwani hilo tumeshalifanya ndani ya kadi yako. Tunawakaribisha Watanzania ambao hawajajiunga na huduma zao kuja kupata uzoefu wa aina yake wanapotaka kufanya miamala iwe ndani ya nchi au nje ya mipaka ya Tanzania,” amesisitiza Seif.

Katika awamu ya kwanza, Benki ya CRDB iliwapeleka nchini ivory Coast kushuhudia mechi za ufunguzi wateja wake wanne akiwamo Mbunge wa Morogoro Kusini, Mheshimiwa Hamisi Shaban Taletale pamoja na Evelyne Gasper Rwebugisa na Josephine William Marealle pamoja na Dickson Christian Kabaka wa jijini Dar es Salaam.
Seif amesema zawadi kubwa ya kampeni hii ilikuwa safari ya kwenda nchini Ivory Coast ikilenga kutimiza malengo mawili kwa wateja wao. Kwanza ikiwa ni kuwapa nafasi ya kuungana na mashabiki wenzao wa mpira wa miguu kwani mchezo huo unapendwa zaidi nchini na Afcon ndio michuano mikubwa kwa Bara la Afrika. Pili, amesema ni kuwapa nafasi ya kutanua jiografia kwa kulifahamu zaidi bara lao.

“Nimefurahi kupata fursa hii kati ya wateja wengi wa Benki ya CRDB ambapo katika safari hii mbali na kufika Ivory Coast tutapata nafasi ya kupita na  kukaa Dubai kwa muda kabla ya kuunganisha ndege ya kwenda Ivory Coast. Huu mzunguko nimeupenda, unatoa nafasi ya kushuhudia na kujifunza mengi,” amesema Veronika Mshometa, mmoja wa washindi hao.









RAIS SAMIA AZUNGUMZA KATIKA JUKWAA LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA NORWAY JIJINI OSLO

February 14, 2024

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Biashara lililowahusisha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Tanzania na Norway Jijini Oslo tarehe 13 Februari, 2024.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akichangia jambo katika Mkutano wa Jukwaa la Biashara lililowahusisha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Tanzania na Norway Jijini Oslo tarehe 13 Februari, 2024.
Viongozi, Wawekezaji na Wafanyabiashara mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa Jukwaa la Biashara lililowahusisha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Tanzania na Norway Jijini Oslo tarehe 13 Februari, 2024.