RC ANTHONY MTAKA AKABIDHI MAGARI 13 SEKTA YA AFYA KWA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI MKOANI NJOMBE

February 17, 2024


Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka leo Februari 16, 2024 amekabidhi magari 13 kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Njombe, zoezi hilo limefanyika katika uwanja wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe zilizopo kata ya Mji Mwema Mtaa wa Lunyanywi.

Magari hayo yamekabidhiwa kwa lengo la Kwenda kutoa huduma kwa wananchi kwenye maeneo hayo ikiwa ni Pamoja na gali za kubebea wagonjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Madereva katika hafla ya makabidhiano ya magari hayo Mhe. Mtaka amevitaka vituo ambavyo vimekabidhiwa magari hayo waende wakayatumie kwa shughuli zilizokusudiwa.

“Nakabidhi Magari haya 13 kwaajili ya kwenda kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Njombe, hivyo yatumieni Magari haya kwa malengo kusudiwa ili wananchi wapate huduma bora za matibabu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia Magari haya ili tuwahudumie wananchi, na ninamshukuru Rais wetu kwa kuendelea kutupatia vitendea kazi mbalimbali kwenye sekta mbalimbali kwenye mkoa wetu ikiwa ni Pamoja na Idara ya Afya.”
amesema Mhe. Anthony Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Njombe.




PINDA AWATAKA WATANZANIA KUENZI MEMA YA LOWASSA

February 17, 2024

 Na Pamela Mollel,Arusha 

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda amewataka watanzania kuendelea kuyakumbuka na kuyaenzi mambo mema aliyoyafanya hayati Edward Lowassa wakati wa uhai wake na kuona namna gani ya kuendelea kuyasimamia yale mema ambayo alikuwa anataka yatekelezwe.

Mhe.Pinda ameyasema hayo wakati akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa waziri mstaafu hayati Edward Lowassa iliyofanyika nyumbani kwake katika  kijiji cha ngarash Monduli ambapo amesema hayati Edward Lowassa alikuwa ni kiongozi shupavu na mzalendo wa nchi yake.

Awali akitoa salamu za pole katika msiba huo Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Kimataifa Cha AICC Laurence Mafuru amesema kuwa watamuenzi hayati Edward Lowassa kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kukuza uchumi na utalii wa mikutano ambayo ndiyo azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu ya kuifanya Tanzania kama kitovu cha utalii.

Kwa upande wake Jenista Mhagama Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na masuala ya sera,bunge na uratibu amesema hayati Edward Lowassa ameacha alama wakati akiwa mtumishi na mtendaji ndani ya serikali kwani matunda na alama aliyoicha inaigusa nchi.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuenzi na kutambua mambo mema aliyoyafanya ambapo inaungana na kila mmoja kujifunza kutokana na mifano mema aliyoifanya na kuitenda wakati wa uhai wake.

Naye Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha (IAA)Prof.Eliamani Sedoyeka   anasema atamkumbuka Hayati Edward Ngoyai Lowassa kwa mchango wake mkubwa kwenye sekta ya elimu ambapo aliweza kuanzisha na kusimamia shule za kata kwa nchi nzima

"Kabla ya kujenga shule za kata hapa nchini kulikuwa na shule elfu moja tu,baada ya kujenga tulifanikiwa kupata shule 3500-4000,kwa nchi nzima ukichanganya na shule za binafsi unapata shule 5000"alisema Sedoyeka 

Aliongeza kuwa sasahiv tunawasomi wengi waliopitia shule za kata na wanafanya vizuri,yote hayo ni juhudi za Lowassa.




DKT. MOLLEL ATOA SALAMU ZA POLE, MSIBANI KWA HAYATI EDWARD LOWASA

February 17, 2024


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Lowasa Kijijini Ngarash Wilayani Monduli leo Februari 16, 2024.
Sekta ya Afya itaendelea kumuenzi Hayati Edward Lowasa kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika maendeleo ya Sekta ya Afya kwa kushiriki kikamilifu kwenye uhuishaji wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007, ambayo inatoa dira katika upatikanaji wa huduma za matibabu nchini.

Hayati Lowasa aliongoza katika uandaaji wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi ambao ulituongoza katika kuibua miradi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya hadi ngazi ya msingi ya jamii na sasa tunashuhudia matunda ya kuwa na Vituo hivyo hadi ngazi ya Jamii (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya)

"Natoa pole kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Watanzania wote kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowasa. Kifo chake kimetugusa wengi, tutaendelea kummuenzi kwa mema yote aliyotufanyia lakini kikubwa zaidi kuziishi falfasa zake za utumishi uliobora katika kuwatumikia Wananchi" amesema Dkt. Mollel.
Buriani Hayati Edward Lowasa.