ADC KUTOA MIFUKO 100 YA SARUJI KUCHANGIA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI

January 21, 2024

Na Mwandishi Wetu,HANDENI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Alliance Demokratic Change ADC) Doyo Hassani Doyo ameshiriki katika mkutano wa kuchagua viongozi wa tawi la Kibaya wilayani Handeni Mkoani Tanga huku akiwahaidi wananchi chama hicho kitashirikiana nao katika suala la maendeleo

Doyo aliyasema hayo wakati kabla ya kuanza uchaguzi huoi ambao pia amewahaidi wananchi kuwa wao kama chama watatoa Mifuko 100 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari kibaya endapo mchakato huo ukiwa sawa .

Alisema kwamba wataanza kutoa mifuko 40 kwanza kisha wakati ujenzi ukiendelea  watamalizia  mifuko 60  iliyobakia lengo likiwa ni kuhakikisha kua sula la maendeleo linafanyika katika eneo hilo .

Hatua hiyo ya ADC kutoa mifuko hiyo ya Saruji ni baada ya wananchi wa eneo hilo kutoa kero juu ya watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda shule ya Mzeri na wakatti wa mvua hishindwa kwenye shule kutokana na uchafu wa barabara 

Kutokana na uwepo wa changamoto hiyo wananchi hao waliomba kujengwe shule ya Sekondari maeneo ya karibu ambapo Katibu huyo kupitia chama chao wakahaidi  kuchangia mifuko 100 ya cement kwaajii ya kusapoti mambo ya kijamii.


KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ELIMU YARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA COSTECH

January 21, 2024


NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na matumaini yao kuona fedha wanazopatiwa zinafanya kazi iliyokusudiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20,2024 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mussa Sima amesema kuwa wametembelea tume hiyo na kujiridhisha kwa juhudi wanazozifanya hasa kwenye masuala ya utafiti ambazo zimekuwa zikiibuliwa na wataalamu nchini.

"Tumeona kazi nzuri sana inafanyika kwa ajili ya utafiti na utafiti huu si wa Elimu tu unagusa maeneo yote, tumeona hata kwenye kilimo wameshirikiana na Taasisi ya chuo Kikuu Cha Kilimo Sokoine (SUA) kwenye maabara yao wameandaa vipimo vya kupima afya ya udongo". Amesema Mhe. Sima

Aidha amesema kuwa katika sekta ya Elimu kuna mabadiliko makubwa kupitia mtaala mpya ambao utaleta mapinduzi makubwa wakati ambao serikali inaandaa sera na sheria ambazo zitasaidia kuondokana na changamoto za kukosa walimu wa masomo ya sayansi,uhandisi na hisabati ili kuongeza umahiri kwa wanafunzi waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amesema kuwa wataendelea kufanya jitihada zao kufadhili kupitia pesa wanazopatiwa ili kufanya Tafiti ambazo zitarudisha matokeo chanya kwa jamii ambapo pia watatumia matokeo wanayo yapata kuisaidiaa serikali.

Aidha Dkt. Nungu ameeleza kuwa wanafanya tafiti ya matumizi ya Teknolojia ya Akili bandia ambapo wanatarajia kupata matokeo baada ya miaka miwili kwa ajili ya matumizi halisia ya kila siku.

"Tunategemea baada ya miaka miwili kupata matokeo ya akili bandia (Artificial intelligence) sio tu kwa masuala ya mtandaoni lakini kwa maisha halisia, kama nchi tunafadhili tafiti katika maeneo hayo". Ameeleza.

Pamoja na hayo Dkt. Nungu amewaalika vijana kuleta kazi zao bunifu kuzionesha ili waweze kuinuka kiuchumi na kukidhi mahitaji yao kwa lengo la kuongeza ajira na kuokoa kupeleka nje fedha za kigeni.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu akimpokea Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mussa Sima mara baada ya kamati hiyo kuwasili katika ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mussa Sima akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kamati hiyo kutembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo pamoja na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kamati hiyo kutembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayehusika na Elimu, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo pamoja na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kamati hiyo kutembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam



Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakichangia jambo kwenye kikao na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kamati hiyo kutembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mussa Sima akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayehusika na Elimu, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu wakiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo mara baada ya kutembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mussa Sima akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayehusika na Elimu, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu wakiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kamati hiyo kutembelea ofisi za (COSTECH) leo 20, 2024 Jijini Dar es Salaam.


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

DKT. NCHIMBI: KUKIMBILIA MAANDAMANO NI UOGA WA HOJA, KUKWEPA MAZUNGUMZO

January 21, 2024


-Asema CCM itaongeza kasi kusimamia Serikali kwa weledi, bila kiburi, wala kuwatukana watendaji

-Asisitiza Watanzania wanatambua CCM ndiyo Chama kiongozi, hakuna haja ya kutukana kusimamia Ilani ya Uchaguzi

-Awataka wanasiasa kutambua watapimwa kwa hoja, sio maandamano

Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Dkt. Emmanuel John Nchimbi amewataka viongozi wa CCM kuongozea kasi ya kutimiza wajibu wa Kikatiba na kikanuni wa kuisimamia Serikali na watendaji wake wanapotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa weledi na heshima, bila kiburi wala kuwatukana.

Ndugu Nchimbi amesema kuwa katika kuisimamia Serikali inapotekeleza wajibu wake kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, wanaCCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuelezea mafanikio na kazi kubwa inayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Ndugu Nchimbi pia amesisitiza jinsi ambavyo milango ya CCM, ikiwa ni pamoja na kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama, iko wazi kwa ajili ya kushirikiana na vyama vingine vya siasa na kuzungumza masuala mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya taifa, huku akisema kuwa wanasiasa wanaohamasisha maandamano badala ya kujenga hoja katika majadiliano, ni waoga na wanakwepa mijadala.

Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi ameyasema Jumamosi, Januari 20, 2024 wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi mbalimbali wa Jiji la Dar Es Salaam, wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa CCM waliojitokeza kwa wingi Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar Es Salaam, kumlaki wakati wa mapokezi ya kumpongeza kwa kuteuliwa kushika dhamana hiyo ya Mtendaji Mkuu wa CCM.

“Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutimiza ahadi zake na kuisimamia serikali. Ninawaahidi, kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama, tutaendelea kukiimarisha chama lakini pia kuhakikisha hatumuangushi Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Chama kwa imani yake aliyotupatia. Chama chetu kitaendelea kupata ushindi kwa sababu tumefanya kazi kubwa na zinazoeleweka.

“Tuendelee kufanya kazi usiku na mchana, kazi ya kutafuta ushindi wa chama chetu. Tufanye kazi kwa juhudi na umakini zaidi katika maeneo yaliyobakia. Wakati huo huo Chama chetu kisikwepe wajibu wa Kikatiba na Kikanuni kuisimamia Serikali, kwa weledi bila kutukana. Tuongoze kwa weledi, ili watendaji wa Serikali wafanye kazi vizuri na wajue kuwa tunawapenda na kuwaheshimu. Isipokuwa tu wote tuongeze kasi ya kuwatumikia wananchi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi,” amesema Ndugu Nchimbi.

Akisisitiza kuhusu umuhimu wa Watanzania kudumisha utaifa wao na kuenzi tunu za amani na utulivu kuwa ndiyo msingi wa maendeleo na alama kubwa ya Tanzania duniani, Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi amsema kuwa milango ya CCM na hususan kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, iko wazi wakati wowote utakapohitajika ushirikiano baina ya vyama vya siasa, kwa maslahi ya taifa.

“Tunavyo vyama vya siasa nchini, tuendelee kushirikiana navyo. Milango ya ofisi yangu iko wazi. Wote tuna nia moja. Tutaendelea kushirikiana nao. Lakini kushirikiana nao haimaanishi kupunguza kasi ya kutafuta ushindi, kuongeza wabunge bungeni na madiwani, Serikali za Mitaa na ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Rais mwakani.

“Vyama vya siasa, wanasiasa na wadau wote wa maendeleo dhamira ya mazungumzo ni muhimu ikaakisi kote. Kukimbia na kukwepa mazungumzo sio ujasiri. Huo ni uoga. Hoja hujengwa kwa mdomo sio kwa miguu. Tunataka tuwapime kwa hoja zao, sio kwa miguu yao kuandamana. Vyama vya siasa vijitofautishe na mashindano ya urembo ambako hupimwa kwa jinsi wanavyotembea. Tutumie ubongo kufikiria, sio miguu,” amesema Ndugu Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi pia alitumia hadhara hiyo pia kuwapatia pole wakazi wa Dar Es Salaam kutokana na athari za mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia siku ya mapokezi hayo, akimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Ndugu Albert Chalamila kuhakikisha serikali mkoani humo inachukua juhudi za makusudi kuwasaidia wananchi kutokana na athari kubwa zilizosababishwa na mvua hiyo.

Amesisitiza kuwa katika utendaji kazi wake, daima amekuwa mtu anayependa vitendo zaidi, kuliko maneno, kwa sababu tija inayokusudiwa na kutumainiwa na wananchi, kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote, itapatikana kupitia vitendo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar Es Salaam Ndugu Abbas Mtevu amesema chama kinatarajia kushinda kwa kishindo mitaa yote 574 ya mkoa wa huo.

Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Ndugu Albert Chalamila amesema wanatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, hivyo viongozi wanapoanza kampeni hawatapata tabu kujieleza kwa wananchi, kwa sababu kazi zinajieleza zenyewe, huku pia akiahidi kuwa hata miundombinu iliyoathirika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku, itafanyiwa kazi ndani ya saa 24 kurejesha hali vizuri.












SIASA