TA VETERAN SC YAANZA TAMBO

July 22, 2013

(Kikosi cha timu ya TA Veteran SC Kutoka kushoto ni David Stanlaus,Mohamed Kirua(Kazungu),Edgar Mdime,Daud Kabingwa,Iddy Bilal,Kilango Salum,Peter Kwingwa,Acheni Maulid na Dastan Charles)

Na Oscar Assenga,Tanga.
TIMU ya Maveteran ya TA Veteran SC ambayo inaundwa na wachezaji kutoka sekta mbalimbali mkoani hapa imeanza mazoezi yake mwishoni mwa wiki kwenye uwanja wa shule ya Msingi Bombo ikijiandaa na bonanza la maveteran.


Akizungumza na blog hii,Katibu wa timu hiyo,Edgar Mdime amesema uanzishwaji wa timu hiyo ni kuleta changamoto ya kisoka mkoani Tanga pamoja na kutoa burudani kwa wapenda soka mkoani hapa hasa ukizingatia maveteran wanapokutana hubadilishana mawazo na kukumbushana enzi zao.


(Mshambuliaji wa timu ya TA Veteran SC Edgar Mdime akiwa mazoezini mwishoni mwa wiki)

Mdime alisema wanatarajiwa kufanya ziara ya kimichezo katika wilaya zote za mkoani wa Tanga kucheza mechi za kirafiki na maveteran za wilaya hizo lengo likiwa kutoa burudani kuonyesha soka la kisasa.

Kikosi cha timu hiyo kinaundwa na David Stanlaus, Mohamed Kirua(Kizungu),Edgar Mdime, Daud Kubingwa,Iddy Bilal,Kilango Salum,Peter Kwingwa, Acheni Maulid na Dastan Charles .

Mwisho.

TANESCO TANGA YAPATA HASARA YA MILIONI 200 NDANI YA KIPINDI CHA MIAKA MIWILI ULIOTOKA NA WIZI WA MIUNDO MBINU.

July 22, 2013

(Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tanga,Johnson Mwigune akiwa ofisni mwake leo mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari)

Na Oscar Assenga, Tanga.
SHIRIKA la Umeme Mkoa wa Tanga (TANESCO)limepata hasara ya shilioni milioni 200 ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na wizi wa miundombinu yake ikiwemo wezi wa nyaya na mafuta ya transfoma unaofanyika katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo ofisini kwake ,Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tanga,Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tanga,Johson Mwigune alisema wizi huo unafanyika hasa katika wilaya tatu ambazo ni sugu kwa matukio ya aina hiyo ambazo ni Muheza,Korogwe na Lushoto.

Mwigune alisema wizi huo unaliletea athari kubwa shirika hilo ikiwemo kulikosesha mapato wakati umeme huo ukipotea bure bila ya kutumika na kuwasababishia watumiaji wa nishati hiyo usumbufu mkubwa na uharibifu wa mali zao.

Meneja huyo alisema kwa upande wao wamejipanga vilivyo ili kuweza kuhakikisha wanakabiliana na wezi wa miundo mbinu hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na ushirikishwaji wa wanakijiji katika maeneo husika ili kulitokomeza suala hilo.

Aidha alisema katika siku za hivi karibuni kumetoka wizi wa nyaya za umeme za shirika hilo ambao ulifanyika eneo la Kerenge Makaburini wilayani Korogwe ambapo walifanya jitihada za kuwasaka na baadae kufanikiwa kuwakamata na kuwahukumu na kufanikiwa kumuhukumu Twaha Dege miaka 18 katika kesi iliyosikilizwa kwenye mahakama ya wilaya ya Korogwe.

Aliongeza kuwa tukio lengine ambalo limetokea ni watu kujiunganishia huduma ya umeme bila kufuata taratibu ambapo walilifuatilia na kufanikiwa kuwakamata watu wawili mmoja akiwa ni mfanyakazi mwengine akiwa sio mfanyakazi ambapo hukumu yao ilitoka kwa kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka minne ambapo aliyekuwa mfanyakazi wao alifariki dunia.

Hata hivyo,Mwigune alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na shirika hilo kwenye kulinda miundombinu yake kwa kutoa taarifa hasa pale ambapo watabaini kuwepo kwa vitendo vya wizi ,uharibifu vinafanyika kwenye maeneo yao.

Mwisho.

Vijana tushikamane.

July 22, 2013
(MWENYEKITI wa Jumuiya wa Umoja wa Vijana wilaya ya Tanga,Salim Perembo akizungumza mwishoni mwa wiki katika kikao cha Baraza la Vijana wilaya hiyo kulia kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga (CCM)Kassim Mbuguni na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Halima Dendego)

Na Oscar Assenga, Tanga.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga, Kassim Mbuguni amewataka vijana kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kukulinda na kukitumikia chama hicho pamoja na kujenga mshikamano miongoni mwao.
 
Mbuguni alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha baraza la Jumuiya ya Vijana Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga (UVCCM) kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa chama hicho uliopo barabara 20 jijini Tanga.
 
Alisema ili kuweza kuhakikisha chama hicho kinazirudisha kata tisa zilizochukuliwa na vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao lazima umoja huo unapaswa kuwa macho kujua kinachotakiwa kwenye kata zao ili kuyafanyia kazi kwani chama hicho kipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote.
 
“Jumuiya ya umoja wa vijana lazima wawe macho ndani ya chama kwa kutoa taarifa na kinachotokea ndani ya chama lengo likiwa kuzifanyia kazi na kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye maeneo yao “Alisema Mbuguni.
 
Katika kikao hicho Jumuiya hiyo kilipitisha majina ya wajumbe wa kamati ya mipango, uchumi na fedha itakayokuwa na kazi ya kuhakikisha wanabuni miradi ambayo itaiwezesha jumuiya hiyo kuwa na vitega uchumi vyao wenyewe ili iweze kusimama imara lakini pia itawasaidia kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
 
Majina ya wajumbe ambao wataunda kamati hiyo yalipitishwa na kikao cha baraza la Vijana wilaya ya Tanga ni Mwenyekiti,Ameet Ranjit,Katibu Akida Machai, ambao watakuwa wakishirikiana na wajumbe Mbaruku Asilia,Khalid ,Yazidu Msika,Abdul Ahmed Kassim Kassim,huku wajumbe wengine wakina mama wakitarajiwa kuongeza kwenye kamati hiyo.
 
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Tanga, Salim Perembo aliwataka vijana kuendeleza mshikamao na umoja ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye umoja huo lengo likiwa kukiimarisha chama hicho huku akiwataka vijana kutokubali kutumiwa kama ngazi.
 
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 60 kutoka kata za Chongoleani, Tangasisi, Kiomoni, Usagara, Maweni, Duga,Msambweni,Majengo,Mzingani,Marungu,Chumbageni,Kirare,Ngamiani kusini,Nguvumali,Central ,Mzizima,Pongwe na Ngamiani .
 
Mwisho.

TAIFA STARS KWENDA KAMPALA J5

July 22, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaondoka Mwanza keshokutwa kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la CHAN itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kuanzia saa 10 kamili jioni.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza chini ya Kocha Kim Poulsen tangu Julai 14 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Timu hiyo itaondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir, na inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 10.15 jioni.

Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen kesho (Julai 23 mwaka huu) atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya kikosi chake. Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye hoteli ya La Kairo jijini Mwanza.

LIGI KUU YA VODACOM 2013/2014 KUANZA AGOSTI 24

July 22, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote 14 kuwa viwanjani katika miji saba tofauti.

Hata hivyo, kabla ya ligi hiyo kuanza kutakuwa na mechi ya kufungua msimu (Ngao ya Jamii- Community Shield) kati ya bingwa mtetezi Yanga na Makamu bingwa Azam itakayochezwa Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi za Agosti 14 mwaka huu zitakuwa kati ya Yanga na Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mtibwa Sugar na Azam (Uwanja wa Manungu, Morogoro), na JKT Oljoro na Coastal Union (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).

Nyingine ni Mgambo Shooting na JKT Ruvu (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers na Simba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Kagera Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Ruvu Shooting na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani).

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 3 mwaka huu wakati wa pili utamailizika Aprili 27 mwakani. (Ratiba ya mzunguko wa kwanza na wa pili imeambatanishwa- attached).