Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amkabidhi rasmi Ofisi Rais John Pombe Magufuli

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amkabidhi rasmi Ofisi Rais John Pombe Magufuli

November 12, 2015

10
Rais Mstaafu awamu ya nne Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi nyaraka kama ishara ya kukabidhi rasmi ofisi kwa Rais Mpya awamu ya tano Dkt.JohnPombe Magufuli wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika ikulu jijini Dar es Salaam leo.
20
30
Rais Dkt.John Pombe Magufuli, Rais Mstaafu awamu ya NNe Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais Mh.Samia Hassani Suluhu na katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue muda mfupi baada ya Rais Mstaafu Kikwete kumkabidhi rasmi ofisi Rais Dkt.John Pombe Magufuli ikulu jijini Dar es Salaam leo.
(Picha na Freddy Maro)

MOHAMED TSHABALALA MCHEZAJI BORA WA MWEZI OCKTOBA SIMBA SPORT CLUB

November 12, 2015

Katika kuongeza morali na kuwazawadia wachezaji wanaofanya vizuri, Klabu ya Simba ilianzisha Tunzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kuanzia mwezi wa Septemba 2015.
Mshindi wa mwezi wa Oktoba, 2015 ni Mohamed Hussen Tshabalala ambapo alipigiwa kura nyingi na mashabiki na wapenzi wa Simba na soka la Tanzania kwa ujumla kupitia simu za mkononi ambao pia wamejiunga na huduma ya Simba News.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam Rais wa Simba Evans Aveva alisema “Uongozi, wanachama na wapenzi wa Simba wanathamini mno mchango wa wachezaji katika kuifanya timu yetu ifanye vizuri, hivyo tumeona ni jambo la busara kuwa klabu ya kwanza Nchini Tanzania kuwa na tunzo za mchezaji wake bora. Tunaamini kuwa Tunzo ya Mchezaji bora wa mwezi wa Simba itaongeza ari na kujituma kwa wachezaji wetu. Sisi tukiwa kama viongozi ni kazi yetu ya msingi kuhakikisha kuwa wachezaji wetu hasa wale wanaojituma zaidi wanatambuliwa na kuenziwa’’.
Akizungumza jinsi tunzo ya mchezaji bora itakavyoendeshwa, Mkurugenzi Mkuu wa EAG Group ambao ni washauri na watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba, Imani Kajula alisema “Wanachama na wapenzi wa Simba na wapenda michezo ndio watakao kuwa wanachagua mchezaji bora wa mwezi kwa kutuma jina la mchezaji wanayempendekeza kwenda kwenye namba 15460, Ni wale tu ambao wamejiunga na Simba News kupitia mtandao wa Voda na Tigo wataweza kupiga kura kuchagua mchezaji bora wa mwezi wa Simba’’
Simba News ni huduma iliyoanzishwa na Simba ili kuwapa wapenzi wa Simba habari mbalimbali za Simba popote pale walipo ikiwemo matokeo, majina ya wachezaji wanaocheza mechi, usajili na habari nyingine za klabu ya Simba. Kujiunga na Simba News tuma neno Simba kwenda namba 15460 ni maalum kwa Tigo na Vodacom.
Serikali YAombwa kulinda usalama wa Tembo

Serikali YAombwa kulinda usalama wa Tembo

November 12, 2015

images 
Na Mwandishi wetu – Maelezo
……………………………..
 Serikali imeshauriwa  kuiomba China kutekeleza ahadi yake ya kufunga masoko yote ya meno ya Tembo  ili kuweza kulinda usalama wa muda mrefu wa wanyama  hao kwani nchi hiyo  ni mtumiaji mkubwa wa meno hayo na kwa  kufunga biashara hiyo kutapelekea  kuanguka kwa haraka kwa biashara katika sehemu nyingine ulimwenguni.
Ombi hilo limetolewa leo na Taasisi  inayopinga uwindaji haramu wa tembo wakati wakisoma barua yao ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam.
Akisoma barua hiyo Shubert Mwarabu ambaye ni mratibu wa kampeni ya okoa Tembo wa Tanzania alianza kumpongeza Mhe. Rais kwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano na kuisihi Serikali  kutumia urafiki wa kihistoria kati yake  na China kufunga masoko ya meno ya Tembo yaliyopo nchini China.
Alisema takribani asilimia 90 ya meno ya Tembo toka Tanzania yanauzwa China, ambapo biashara halali ya meno ya Tembo inatumika kama mwavuli wa biashara haramu ya meno ya Tembo ambacho ndio chanzo kikuu cha tatizo la ujangili wa Tembo.
“Tunakuandikia barua leo kukuomba kuchukua hatua juu ya suala la kupungua kwa kasi idadi ya Tembo nchini kutokana na ujangili kwa ajili ya biashara haramu ya meno ya Tembo”.
“Kutokana na Ripoti ya Sensa ya TAWIRI 2014 Miaka hamsini iliyopita, kulikuwa na Tembo 300,000 nchini Tanzania. Mwaka 2009, kulikuwa na Tembo 109,000. Leo, inakadiriwa kuna Tembo 43,000 tu waliobaki – upungufu wa asilimia 60 ndani ya miaka mitano tu”, alisema Mwarabu.
Aliendelea kusema wanatambua hatua zilizofanyika kukabiliana na tatizo la ujangili. Uundaji wa mikakati ya kitaifa dhidi ya ujangili, juhudi za Kikosi Kazi cha National and Transnational Serious Crimes Investigation Unit (NTSCIU) na kuongeza rasilimali kwa mamlaka ya wanyamapori ni hatua muhimu.
Alisisitiza, “Nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa Tembo hapo kabla. Mwaka 1989, Tanzania iliongoza jitihada za kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo ulimwenguni tulipochukua hatua kukomesha mauaji ya Tembo, dunia nzima ilituunga mkono. Ni lazima turejeshe upya dhamira yetu kwa ahadi tuliyojiwekea kwa hatua ya kimataifa zaidi ya miaka ishirini iliyopita, na kuleta ukomo wa biashara yote ya meno ya Tembo”.
“Tunaiomba serikali kuwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo nchini, bila kujali utaifa, hadhi au mamlaka, kuteketeza hadharani ghala ya meno ya Tembo Tanzania – inayosadikika kuwa kubwa kuliko yote ulimwenguni kwani ni gharama kutunza na kulinda ghala la meno ya Tembo Tanzania”.

MTOTO WA MWAKA MMOJA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUTUMBUKIA KISIMANI MBEYA

November 12, 2015
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi.


Na EmanuelMadafa,Mbeya

Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba  Promis Dank mkazi wa bwawani wilaya ya chunya alifariki dunia njiani akiwa anapelekwa hospitali baada ya kutumbukia kisimani.

Tukio hilo limetokea Novemba  112  majira ya saa 12 asubuhi huko kitongoji cha railway,  kata ya bwawani, wilaya ya chunya, mkoa wa mbeya.

Inadaiwa kuwa, mtoto huyo baada ya kutumbukia kwenye kisima hicho ambacho kilikuwa wazi, aliokolewa akiwa hai lakini alifariki dunia akiwa njiani kuelekea hospitali teule ya mwambani kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya  Ahmed z. Msangi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini hasa kwa kuweka uangalizi wa kutosha kwa watoto wadogo ili kuepuka madhara yanayoweza kuepukika.

Aidha anatoa wito kwa jamii kufunika visima vilivyowazi, kufukia mashimo yenye maji kwani ni hatari kwa watoto wadogo hasa katika msimu huu wa mvua za vuli.

Wakati huo 
mwisho. 
(JAMIIMOJABLOG MBEYA )
DKT. YAMUNGU KAYANDABILA: “SAYANSI NI MUHIMU SANA KATIKA KUYAFIKIA MALENGO YA AGENDA 2030”

DKT. YAMUNGU KAYANDABILA: “SAYANSI NI MUHIMU SANA KATIKA KUYAFIKIA MALENGO YA AGENDA 2030”

November 12, 2015
DSC_1572
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Yamungu Kayandabila akizungumza na wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia katika mkutano maalum wa siku ya Sayansi Duniani. Kushoto kwake ni Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO- Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam Novemba 10. 2015. (Picha zote na Andrew Chale, Modewjiblog).
Na Andrew Chale, Modewjiblog
[DAR ES SALAAM-TANZANIA] Tanzania kupitia wadau wa Sayansi nchini imedhamilia kupiga hatua zaidi katika kufikia malengo ya Agenda 2030 kwa kuchangamkia fursa za maendeleo katika Sayansi.
Hayo yameelezwa jijini hapa wakati wa wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, walipokutana katika majadala wa Siku ya Sayansi Duniani kwa ajili ya Amani na Maendeleo (World Science Day for Peace and Development).
Akisoma neno, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Yamungu Kayandabila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), katika kukuza Sayansi nchini.
Dkt. Yamungu ameelezea kuwa, nchi yoyote ile ilikuendelea, inategemea Sayansi hivyo kwa Tanzania ni wakati wa kuchangamkia fursa ili kufikia malengo na Agenda 2030.
“Tanzania tuna fursa nyingi na za kutosha. Tuna Nyuklia na hii ni uchumi tosha tutakapofanyia kazi kwa malengo tutafika mbali kwani inahitaji Sayansi ya kina.
Navipongeza vyuo mbalimbali vilivyopo nchini ikiwemo DIT, Nelson Mandela cha Arusha, Chuo cha Sayansi Mbeya na vingine vingi” ameeleza Dk. Yamungu.
Aidha, Dkt. Yamungu ametaka Sayansi kuendana na suala la ulinzi wa chakula na miundombinu mingine ikiwemo suala la maji huku akihimiza wanafunzi kuyapenda na kuyasoma masomo ya Sayansi na suala la umuhimu wa Sayansi na namna inavyoweza kuathiri maisha ya watu kila siku.
DSC_1570
Afisa Utawala na Fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha ambaye alimwakilisha Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa UNESCO- Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues akisoma ujumbe maalum wa siku ya Sayansi Duniani wakati wa mkutano huo wa wadau wa Sayansi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia Prof. Evelyn Mbede amepongeza wadau wa Sayansi na Teknolojia kwa kujimuika katika maadhimisho ya siku hiyo ya Sayansi Duniani ambapo ameelezea kuwa Wizara yake milango ipo wazi kwa wadau wote katika kuhakikisha wanapiga hatua katika kukuza na kuendeleza Sayansi hapa nchini.
Kwa upande wake, Afisa Utawala na Fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha ambaye alimwakilisha Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO- Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutilia mkazo suala la Sayansi na Teknolojia na kufanya suala hilo kuwa mtambuka kwa maendeleo ya vizazi vya sasa na baadae.
Akisoma ujumbe maalum kutoka UNESCO, Bw. Bokosha alieleza kuwa kupitia Sayansi na Teknolojia na ubunifu, maendeleo ya Taifa endelevu, uimarishaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa maandalizi kwa ajili ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na madhara yake hivyo Sayansi inahitajika kwa kiwango kikubwa juu ya hilo.
Aidha, ameeleza kuwa, UNESCO imekuwa mstari wa mbele katika kuanzishwa kwa moduli za elimu ya Mazingira katika shule za Sekondari.
DSC_1565
Profesa John Kondoro Mkuu wa Chuo cha Teknolojia cha jijini Dar es Salaam – (DIT) akitoa mada katika mkutano huo wa wadau wa Sayansi wakati wa maadhimisho ya siku ya Sayansi.
Akinukuu ujumbe maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Bi Irina Bokova katika ujumbe alieleza:
“Hii ni siku ya Sayansi Duniani kwa amani na Maendeleo na imekuja miezi miwili baada ya makubaliano ya Agenda 2030 ya maendeleo endelevu.
Hivyo Serikali zote zitambue nguvu ya Sayansi ya kutoa majibu muhimu kwa usimamizi mzuri wa maji kwa ajili ya hifadhi na matumizi endelevu ya bahari, ulinzi wa mazingira na viumbe hai, ilikukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na majanga na kuendeleza uvumbuzi na kuondokana na umasikini na kupunguza tofauti” alieleza katika nukuu hiyo.
DSC_1557
Afisa kutoka UNESCO NAT.COM, Bw. Joel Samuel akitoa mada katika mkutano huo wa wadau siku ya Sayansi Duniani.
DSC_1580
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, akifafanua jambo wakati wa mjadala huo juu ya maendeleo ya Sayansi na Teknolojia nchini katika mkutano uliowakutanisha wadau wa Sayansi katika maadhimisho ya Siku ya Sayansi Duniani.
DSC_1584
Wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa siku ya Sayansi Duniani.

WAENDELEA KUJITOKEZA KUCHUKUA FOMU ZA USPIKA

November 12, 2015

 Ndugu Julius Pawatila (kulia)akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib
 Mbunge mteule wa Jimbo la Kongwa Ndugu Job Ndugai akijaza maelezo kwenye kitabu maalum cha kujisajili kabala ya kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib (kushoto)akimkabidhi fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbunge wa Jimbo la Kongwa Ndugu Job Ndugai.
 Ndugu Simon Rubugu (kulia) akirejesha fomu za kuwania Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  Katibu
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib.
 Balozi Philip Marmo(kulia) akirejesha fomu za kuwania Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Balozi Philip Marmo akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kurejesha fomu ambapo aliwaambia kuwa amejipanga kuendesha bunge kisasa linaloendana na wakati na teknolojia.
Dr.Tulia Arkson (kulia) akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib
 Ndugu Watson Mwakalila (kulia) akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib
 Dr. Didas Masaburi (kulia)akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib
Mbunge wa Jimbo la Chato Medadi Majogolo Kalemani (kulia) akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib
Ritta Mlaki akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib.
 Veraikunda Urio akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni,  Ndugu Mohamed Seif Khatib
(Picha na Bashir Nkoromo)
Haya ndio majina ya waliochukua fomu leo;
Ndugu Julius Pawatila
Ndugu Job Ndugai
Dk. Tulia Arkson
Dk. Medadi Majogolo Kalemani
Dk. Didas Masaburi
Ritta Mlaki
Veraikunda Urio

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Ataka kauli za “njoo kesho” zikome

November 12, 2015

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kushoto) akijadiliana jambo na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise (katikati). Wa kwanza kulia ni Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James Andilile.
Wajumbe wa kikao wakimsikiliza katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi (kushoto) akizungumza wakati wa kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi- EWURA, Profesa Jamidu Katima.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia) akipokea nyaraka mbalimbali kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi- EWURA, Profesa Jamidu Katima. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi.

Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini zimeagizwa kutochelewesha kushughulikia maombi ya wawekezaji pale wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanapoonesha dhamira ya kuwekeza. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati wa kikao chake na Watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo.

Mhandisi Chambo aliwaagiza watendaji hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake wazingatie Sheria na maadili ya kazi zao, kutokana na ukweli kwamba sekta ya Nishati ni sekta nyeti inayohitaji watendaji waadilifu na wabunifu.

“Akitokea mwekezaji ambaye ameonesha nia ni vema ajibiwe haraka bila kuchelewa iwe amekubaliwa au kukataliwa ombi lake; hakuna sababu ya kumzungusha mwekezaji; tuzidishe kasi ya uwajibikaji,” alisema Mhandisi Chambo.

Alisema lengo la Serikali ni kuongeza uwekezaji hususan kwenye sekta za Nishati na Madini na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha uwekezaji kwani fursa za uwekezaji zilizopo nchini ni nyingi.

Aliwaasa EWURA na Taasisi nyingine kuacha tabia ya woga, na kusema kwamba endapo itatokea mwekezaji akatuma maombi ya kuwekeza nchini, wanapaswa kupitia maombi husika, kujiridhisha na kutoa maamuzi kwa haraka na kwa kujiamini.

“Tufikie mahali tufanye maamuzi. Msiwe na woga kwenye kutekeleza jambo lenye maslahi mapana ya Kitaifa; majibu ya njoo kesho hatutayavumilia,” alisema.

Vilevile Mhandisi Chambo alisema ni vyema taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini zikashirikiana na Wizara katika kufanya upembuzi yakinifu wa miradi katika maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji. Aidha, aliwaagiza watendaji kukaa pamoja kujadili maeneo ya kipaumbele ili upembuzi yakinifu ufanyike kwa lengo la kurahisisha majadiliano na wawekezaji.

Alisema ni vyema ikaundwa timu ya wataalamu kutoka katika Taasisi na Wizara ambao watahusika moja kwa moja na suala la kubaini maeneo pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi yenye tija na manufaa na hivyo kufikia mwafaka mapema na kuanza utekelezaji wa mradi husika pale mwekezaji anapojitokeza.

“Ikitokea mwekezaji akaonesha dhamira ya kuwekeza kwenye maeneo husika ni vema taarifa za awali zikawepo. Hii itavutia wawekezaji wengi zaidi lakini pia itaharakisha majadiliano,” alisema. Aidha, Mhandisi Chambo aliwapongeza EWURA kwa kufanya vizuri kwenye masuala ya mafuta na kuwaasa kujitahidi kufanya vizuri katika majukumu mengine yaliyo chini yao. Naye Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi aliahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu pamoja na kumpatia ushirikiano wa kutosha. Kikao hicho ni mwendelezo wa vikao vya Katibu Mkuu huyo na Menejimenti pamoja na Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili.