WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amechukua fomu za kuomba kuwania Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Waziri Mkuu Pinda alikabidhiwa
fomu hizo leo (Ijumaa, Juni 12, 2015), saa 4:03 asubuhi kutoka kwa
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Oganaizesheni), Bw. Mohammed Seif
Khatib na saa 4:05 akaweka saini kwenye daftari la kupokea nyaraka ili
kuthibitisha kuwa amezipokea.
Saa 4:07 alikabidhiwa mkoba wenye
nyaraka hizo na Bw. Khatibu na saa 4:08 akaunyanyua juu mbele ya
waandishi wa Habari waliokuwepo kwenye ukumbi wa Katibu Mkuu wa CCM
kushuhudia akipokea fomu hizo. Kisha saa 4:15 aliingia ukumbi wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kukutana na wanahabari.
Akizungumza na waandishi wa habari
na wanaCCM waliofika ukumbi wa NEC kumsikiliza mara baada ya kuchukua
fomu hizo, Waziri Mkuu alisema endapo atafanikiwa kuteuliwa na CCM
awanie kiti cha Urais atasimamia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa
Maendeleo ya Uchumi ili unufaishe makundi mengi zaidi ya jamii.
“Ukuaji wa uchumi uko vizuri
lakini umaskini unapungua kwa kiasi kidogo, kasi yake hairidhishi… hii
ni kwa sababu ukuaji huo umegusa sekta zisizogusa maisha ya watu moja
kwa moja kama za ujenzi, utalii, uchukuzi na nyinginezo,” alisema.
“Wataalamu wa mataifa
yaliyoendelea wanatuambia ukuaji wa uchumi hauonekani sana kwa sababu
unagusa maisha ya watu wachache, sasa hivi wanataka jitihada ziongezwe
kwenye jamii kubwa zaidi ambazo ni wakulima, wavuvi, wafugaji,
wajasiriamali na warinaasali,” alisema.
“Mimi naamini tukiwagusa hawa impact
kubwa itaonekana, ajira zitapatikana kwani viwanda vya usindikaji
vitakuwepo; kilimo kikiboreshwa kwa kutumia zana za kisasa wengi
watafanya kazi hiyo ambayo hivi sasa kila mtu anaikimbia kwa sababu ya
shuruba za kazi yenyewe.”
Alisema Mpango wa Kwanza wa
Maendeleo na Ukuzaji Uchumi ulilenga kuimarisha miundombinu zikiwemo
barabara, bandari na ndani yake kulikuwa na mpango wa kuunganisha makao
makuu ya mikoa yote kwa barabara za lami ifikapo mwaka 2018.
Alisema mpango huo ulioasisiwa na
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ni wa miaka 25 (2000-2025) lakini ilibidi
Rais Kikwete augawanye katika awamu tatu za miaka mitano mitano kuanzia
kwama 2011 -2015 sababu muda uliobakia ulikuwa ni miaka 15 tu.
“Kwa maoni yangu kazi iliyokwisha
kufanyika ni nzuri lakini tusibweteke. Chini ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo ya Uchumi, mambo yatabadilika na ikiwezekana hatutafika 2025
kwa sababu maji, elimu, afya vitakuwa vimeboreshwa tayari,” aliongeza.
Akigusia kuhusu Ilani ya CCM,
Waziri Mkuu alisema hawezi kuiongelea kwa sababu bado haijatoka. “Lakini
ninaahidi, pindi ikitoka na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM, na Mungu
akijalia nikapitishwa na chama, sitashindwa kuitekeleza Ilani hiyo.
Nina uzoefu wa Ilani zote zilizopita,” alisisitiza.
Alisema kufanya kazi kwa karibu
zaidi na Marais wote wanne na uwepo wake kwenye Serikali za Mitaa kwa
muda mrefu ni turufu pekee anayoamini itamuwezesha kuwahudumia
Watanzania vizuri zaidi kwani anaifahamu nchi kwa undani pamoja na
matatizo yanayowakabili Watanzania walio wengi.
Alisema anaamini Mungu peke yake
ndiye ajuaye nani amemuandaa kwa ajili ya kuiongoza nchi hii na kwamba
hata yeye bado anamtumaini Mungu amuongoze katika safari hiyo. “Mungu
peke yake ndiye anajua nani amemuandaa kwa nafasi hii, ni siri yake.
Kadri itakavyompendeza, atampa nafasi hiyo yeye amtakaye,” alisema.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, JUNI 12, 2015.