WIZARA YA NISHATI KUBORESHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - KAPINGA

November 17, 2023


*Nishati Safi si anasa, kaya zote kufikiwa*

Wizara ya Nishati imelenga kuboresha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kutokana na umuhimu wa afya za Watanzania na Mazingira. Inakadiriwa Watanzania zaidi ya asilimia 80 wanatumia  vyanzo vya nishati ya kupikia  ambavyo si salama na vyenye madhara ya kiafya, kiuchumi na kimazingira. 

Akimuwakilisha Mgeni rasmi  Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko,  wakati wa kukabidhi hundi za takribani Shilingi Bilioni 9 za Kitanzania fedha za ruzuku zinazofadhiliwa  na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU)  kupitia mfuko wa *CookFund* kwa wajasiriamali 44 wanaojihusisha na Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia leo Novemba 17, 2023. Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesema, jitihada zinazofanyika zitasaidia kupunguza utegemezi wa Nishati zisizo safi na kuunga mkono jitihada za  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alihimiza uwepo wa programu endelevu za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia zinalenga kusaidia Wananchi na kujikwamua katika hali za kiuchumi.

"Kwa kweli kwa niaba ya Wizara tunapenda kuwapongeza  Umoja wa Ulaya (EU), kwa mradi huu kabambe wa kuboresha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia, lakini vilevile mradi ambao unachagiza maendeleo katika Sekta ya Nishati nchini," amesema Kapinga. 

Aidha, ameongeza kuwa programu hiyo ni muhimu kwa Wizara na washirika kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya fedha ambao kwa pamoja wameendelea kuboresha mnyororo wa thamani kutokana na umuhimu wa Nishati safi ya kupikia kwa ustawi wa Taifa. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) Cèdric Merel amesema, suala la Nishati safi ya kupikia lisichukuliwe kuwa ni la anasa na kwamba hitaji hilo lifikie kila kaya bila kujali hali ya kipato kwani inasaidia kuokoa muda, ni rahisi kutumia na inalinda mazingira. 

"Maono ya Serikali ni kuhakikisha inafikia lengo lake la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya kupikia mpaka ifikapo mwaka 2033, nishati hii safi ya kupikia pia ipatikane kwa urahisi, na kwa ufanisi na kwa gharama nafuu," Cèdric Merel

Awali, Meneja Mradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la (UNCDF), Emmanuel Muro amesema, utekelezaji wa mradi huo umeingia mwaka wa pili na unalenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na kwamba asilimia 80 ya Watanzania wanahama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo safi na kuwataka wadau kuendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha lengo. 

Mradi huo wa Nishati Safi ya kupikia  unafadhiliwa na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU), ukitekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali (UNCDF), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati.

Hafla hiyo ya utoaji wa hundi kwa wajasiriamali wa Nishati Safi ya Kupikia (44) imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, Mkuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya  (EU) Cèdric Merel, Wataalam kutoka (UNCDF) na Wizara ya Nishati.

Wafanyakazi Benki ya CRDB waadhimisha Siku ya Wanaume Duniani

November 17, 2023

 

Katika kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, Benki ya CRDB imefanya semina ya siku moja kwa wafanyakazi wake wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami.

Semina hiyo iliendeshwa na madaktari pamoja na wanasaikolojia, na kufanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 

Licha ya kuwajengea wafanyakazi uwezo wa kusimamia mambo yao binafsi, pia imelenga kuongeza morali na kuwatia moyo wa kujituma zaidi kila wanapowahudumia wateja ili kukidhi mahitaji na matarajio yao ya kifedha.

Siku ya Wanaume Duniani huadhimishwa kila ifikapo Novemba 19 ya kila mwaka ili kutoa nafasi kwa wanaume kujadili maendeleo yao binafsi pamoja na ya familia zao na kutafuta suluhu ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, wafanyakazi wa Benki ya CRDB wamepitishwa kwenye mada kadhaa ikiwamo afya ya akili, afya ya uzazi, familia na malezi pamoja na saikolojia ya jamii.

Mjadala huo umelenga kuwajengea uwezo wa kurahisisha maisha yao ndani ya ndoa, maisha binafsi pamoja na jinsi wanavyochangamana na jamii bila kusahau maisha yao wakiwa kazini.
Mtaalamu wa Masuala ya Saikolojia nchini, Dkt. Ellie Waminian akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ambaye ni Afisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Timothy Fasha akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 









Benki ya CRDB yafungua tawi wilayani Magu mkoani Mwanza kusogeza huduma kwa wananchi

November 17, 2023

Magu. Tarehe 17 Novemba 2023: Siku chache baada ya kubeba tuzo za huduma bora na mtandao mpana wa mashine za kutolea fedha zinazotoa huduma, Benki ya CRDB imefungua tawi lake jipya wilayani Magu mkoani Mwanza.
 
Tawi hilo linaloifanya Benki ya CRDB kufikisha matawi 262 nchini kote, lilizinduliwa na Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mheshimwa Hassan Masala ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Ilemela akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Amos Makalla.
 
Mheshimiwa Masala amesema jitihada za Benki ya CRDB kutanua wigo wake wa huduma zinaonekana na mchango wake utakuwa na tija kubwa kwenye jamii ya taifa zima kwani maendeleo ya kiuchumi yanategemea sana huduma za fedha.
“Tawi hili linaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya matawi 19 yanayotoa huduma mkoani mwetu hivyo nawasihi wananchi wenzangu wilayani Magu kulitumia vyema ili kujiinua kiuchumi. Hapa mtatunza fedha zenu kwa usalama zaidi, mtakopa kwa ajili ya biashara au malengo mengine binafsi hivyo kukamilisha mipango yenu kwa wakati. Nawashukuru Benki ya CRDB kwa kuja wilayani hapa, naamini wananchi watanufaika na fursa zenu bunifu zikiwamo za Programu ya Imbeju,” amesema Masala.
 
Akizungumza kwa niaba ya menejimenti, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa amesema wateja watapata fursa ya kufungua akaunti zinazoendana na mahitaji yao halisi, mikopo binafsi, ya ujasirimali na biashara,  huduma za bima, kuunganishwa na mifumo ya kidijitali, pamoja na ushauri wa masuala ya fedha na uwekezaji.
 
Tangu ilipoanzishwa mwaka 1996, Rutasingwa amesema Benki ya CRDB imetanua mtandao wake wa huduma kutoka matawi 19 yaliyokuwepo mpaka 262, ukuaji unaoakisi dhima ya dhati ya benki hiyo kusogeza huduma karibu zaidi na Watanzania bila kujali wanaishi mjini au vijijini. 
“Tunakidhi mahitaji ya watumshi na wafanyakazi, wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara. Kwa vijana na wanawake, tunayo Programu ya Imbeju inayotoa mtaji wezeshi. Programu hii ni mahsusi kwa makundi haya mawili hasa kwa wale ambao hawajakidhi vigezo vya benki. Ninawakaribisha wana Magu mje kupata huduma zetu,” amesema Rutasingwa.
 
Kwa wapenda michezo hasa mpira wa miguu, Rutasingwa amewaambia wana Magu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa wateja waliopo na wale watakaofungua akaunti hivi sasa watapewa TemboCard itakayowapa fursa ya kushiriki kampeni ya 'Tisha na Tembocard Tukakiwashe AFCON' itakayowapeleka wateja 8 nchini Ivory Coast kushuhudia fainali za Michuano ya Mataifa Huru ya Afrika (AFCON).
 
“Safari znima italipiwa na Benki ya CRDB. Washindi watalipiwa kiingilio cha uwanjani na hoteli watakayolala itakuwa ni kwa gharama za Benki. Tunafahamu Watanzania wanapenda michezo hivyo huu ni wakati wao wa kuzitumia kadi zao ili washinde safari hiyo ya nchini Ivory Coast,” amesema Rutasingwa.
Wiki iliyopita, Benki ya CRDB ilishinda tuzo tatu kutoka Consumer Choice Awards Africa (CCAA) 2023 katika vipengele vya huduma kwa wateja, benki yeny emtandao mpana wa mashine za kutolea fedha (ATM) zinazofanya kazi pamoja na mkurugenzi mwenye usahawishi zaidi. 
 
Licha ya matawi yake yaliyoenea nchi nzima, Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 25,000 wanaotoa huduma mtaani walipo wananchi nchi nzima, ATM 550 na matawi 21 yanayotembea. Vilevile, inazo mashine za ununuzi ya kadi (POS) zaidi ya 6,000 huku ikishirikiana na asasi ndogo washirika (microfinance) zaidi ya 500.
 
Kwa wanaopenda kulipa kidititali, Benki ya CRDB inayo programu ya Simbanking pamoja na huduma kupitia mtandao wa internet “Internet banking.”