Rais Jakaya Kikwete Aunda Tume kuchunguza mwenendo wa Operesheni Tokomeza

May 05, 2014
Rais aunda Tume kuchunguza mwenendo wa Operesheni Tokomeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameunda Tume ya Uchunguzi (Commission Inquiry) Kuhusu Vitendo vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni Tokomeza.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam jioni ya Ijumaa, Mei 2, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Kutokana na hatua yake ya kuunda Tume hiyo, Rais Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji na Balozi Mstaafu Hamisi Amiri Msumi kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Aidha, Rais Kikwete amewateua Mheshimiwa Jaji Mstaafu Stephen Ernest Mtashiwa Ihema na Mheshimiwa Jaji Mstaafu Vincent Kitubio Damian Lyimo kuwa Makamishna. Rais pia amemteua Ndugu Frederick Manyanda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa Katibu wa Tume hiyo.
Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa uteuzi huu ulianza jana, Alhamisi, Mei Mosi 2014.
Taarifa ya Balozi Sefue iliyataja majukumu ya Tume hiyo yatakuwa yafuatayo:
Kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.

Kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza.

Kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni Tokomeza.

Kuchunguza na kubaini kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.

Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.

Uteuzi huo wa Tume hiyo unatekeleza ahadi ya Rais Kikwete ambayo aliitoa wakati anahutubia Bunge Novemba 18, mwaka jana, 2013 mjini Dodoma.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

DAR CITY CENTER KUFANYIKA MEI 24

May 05, 2014
Na Father Kidevu Blog
SHINDANO la Miss Dar City Center limezinduliwa rasmi jana na linatarajiwa kufanyika mei 24 kwaka huu katika ukumbi ambao utatangazwa baade, huku likishirikisha warembo 15.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana, mratibu wa shindano hilo, Judith Charles alisema kuwa, mwaka huu shindano hilo litambapwa na vionjo tofauti tofauti ili kulifanya kuwa la aina yake.

Judith alisema kwamba, wameangalia changamoto zilizotokea kwa waandaaji wa waliopita wa shindano hilo, ili kuweza kulifanya kuwa na ubora wa hali ya juu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea.

“Tumetumia changamoto ya waandaaji waliopita wa shindano hili na sisi tumeamua kuliboresha zaidi na hivyo tunaamini kabisa kwamba litakuwa katika kiwango cha juu zaidi tofauti na uilivyokuwa hapo mwanzo,” alisema Judith.

Aidha aliongeza kusema kwamba, ana aimani kubwa kwamba Miss Dar City Center ndiko atakakotokea Miss Tanzania 2014, kwani wamejiandaa kwa ukamilifu wa hali ya juu.

Judith alisema kwamba ana imani kubwa na matron ambaye pia ndie mwalimu wa warembo wa shindano hilo, Eshe Rashid kuwa atawapa mafunzo mazuri zaidi yatakayowezesha kuwa bora zaidi jukwaani.

Pia aliongeza kusema kwamba, zawadi kwa washindi wa shindano hilo zitakuwa zimeboreshwa zaidi na hivyo ana imani zitavutiwa zaidi na warembo hao.

Aidha Judith alisema, shindano hilo kwa kiasi kikubwa linafadhiliwa na  Prima, Zanzi, Sky light band, Clouds FM, Dimond Bureu De Change LTD, gazeti la Jambo leo, Klabu Maisha ambako warembo wanafanyia mazoezi, blog ya Wananchi, blog ya Father Kidevu, Hoteli ya JB Belmont na Machapta Production

WILAYA YA MUHEZA YAANZA JITIHADA ZA KUKABILIANA NA TATIZO LA MAJI.

May 05, 2014
NA OSCAR ASSENGA, MUHEZA.

WILAYA ya Muheza imeanza kuchukua jitihada mbalimbali za kukabiliana na tatizo la maji Muheza mjini hapa ikiwemo kuchimba kisima cha Polisi Mangenya na kuendeleza kisima cha kitisa kilichokuwa kinatumiwa na mamlaka ya Mkonge.

Mkuu wa wilaya hiyo, Subira Mgalu aliyasema hayo hivi karibuni ambapo alisema visima virefu tisa vimechimbwa maeneo ya Muheza mjini, Lusanga na Kitisa vyote vina uwezo wa kutoa maji.

Mgalu alisema utaratibu wa upimaji wa ubora wa maji umeandaliwa ili maji hayo yaanze kutumika ambapo mradi huo ulijengwa mwaka 2013 na chanzo chake ni kisima kirefu chenye kina cha mita 57 na uwezo wake ni lita 5000 kwa saa.

Alisema kisima hicho kilichimbwa na wizara ya mambo ya ndani mnamo mwaka 1998 na baadaye kuhujumiwa na watu wasiojulikana ambapo mwaka 2010 kisima hicho kilisafishwa kwa jitihada za halmashauri ya wilaya ya Muheza na kujengewa chemba yenye mfuniko na kufuli.

Aliongeza kuwa kutokana na kero kubwa iliyopo katika wilaya ya Muheza mjini ilipatikana fedha kutoka wizara ya maji mnano jaunari 2013 jumla y ash.milioni 100. kwa ajili ya kuendeleza kusima cha Polisi.

Mradi huo umekamilika na unatoa huduma kwa wananchi wa muheza mjini hususani katika eneo la genge ya zamani,kituo cha polisi na shule ya sekondari Chifu Mangenya.

Katika hatua nyengine, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza,Hans Patrick  alisema kiasi cha sh.bilioni 13.4 zinahitaji ili kuweza kutatua kero ya maji wilaya ya Muheza mjini kutokana na huduma kutokuwa ya uhakika hali ambayo inapelekea baadhi ya wananchi kutafuta huduma hiyo umbali mrefu.

Patrick alisema kuwa gharama hizo zitatumika kwa ajili ya kutoa maji mto zigi kwa ajili ya kusambaza maeneo yote yaliyopo mijini ambayo yanakabiliwa na changamoto ya kutokupatikana maji kwa uhakika

Alisema hivi sasa wanajitahidi kutafuta wafadhili mbalimbali ambao wataunganisha nguvu zao na fedha kutoka serikalini ili kuweza kuanza mradi huo ambao utakuwa ni mkubwa yenye lengo la kuondoa kero ya maji kwenye wilaya hiyo ambayo imekuwa kubwa.

Mhandisi huyo alisema mradi huo tayari ulishapata baraka kutoka wizara husika ambao awali walishapelekea mhandisi mshauri kwa ajili ya kwenda kuuangalia ambapo utakapokamilika utahudumia wakazi wa vijiji vya Kisongeni, Kisiwa Ngumba na Mto zigi.

Alieleza kuwa wananchi wa Misongeni, Ubembe,Mikwamba,Kwemhosi,Masimbani na Mamboleo wanapata maji yam to mgobe ambao mradi wake ulitumia kiasi cha sh.milioni 839 na tayari ulishakamilika ikiwemo kuanza kazi.

WAGOSI WA KAYA KUJA NA MWANAUME KUSHUGHULIKA SOON.

May 05, 2014
NA OSCAR ASSENGA, TANGA.
KUNDI la Mziki wa Bongo Fleva Mkoani Tanga la ‘Wagosi wa Kaya”linatarajiwa kuachia wimbo wake mpya hivi karibu utakaoitwa “Mwanaume Kushughulika” waliomshirikisha nguli za mziki wa Taarabu nchini Khadija Koppa.

Akizungumza na TANGA RAHA BLOG LEO mmoja wa wanasanii wanaounda kundi hilo,John Simba “Dr.John”alisema waliamua kuungana tena pamoja mara baada ya kufikia makubaliana ya kufanya kazi pamoja lakini watakuwa chini ya uangalizi kwa ajili ya kusimamia kazi zao za kundi hilo ili kusiwe na malalamishi ambayo yanaweza kujitokeza ndani yao.

Dr.John alisema wimbo huo utakuwa gumzo kutokana na kuwepo kwa vionjo mbalimbali hivyo kuwataka mashabiki wao kukaa mkao wa kula kwani wamepania kufanya mapinduzi kwenye mziki huo.

Alisema miongoni mwa nyimbo ambazo tiyari walishazitoa ni pamoja na "Tiza Uya Kaya"ambayo ina misemo ya kisambaa wenye maana tumerudi nyumbani wakiwa wameshirikisha Lady Jay Dee na Gahawa ambazo zinatarajiwa kufanya vizuri.

Akizungumzia mziki wa kizazi kipya hapa nchini maarufu kama bongofleva,Dr.John alisema kwa sasa unalipa sana hivyo kuwataka wasanii kuendelea kukaza buti kwa kutunga tungo zenye jumbe nzuri kwa jamii.

UKOSEFU WA UZALENDO WASABABISHA KUTEKETEA KWA MSITU WA BOMBO WEST

May 05, 2014







Viongozi wa vijiji vya Bombo majimoto, Bombo Mtoni,Kijungumoto na Kwetonge vilivyopo kata ya Mashewa wamelalamikiwa kukosa uzalendo na kutuhumiwa kushirikiana na raia
  wanaosadikiwa kutoka nchi jirani ya Kenya kuvuna msitu wa asili wa miti ya Mkarambati unaozunguka vijiji hivyo kwa ajili ya kuchongea vinyago ambavyo huuzwa kwa Watalii  nchini Kenya.
Hayo yamebainishwa juzi na baadhi ya Wananchi wa vijiji hivyo waliokutwa katika msitu huo wakikusanya kuni wakati wa operesheni maalum iliyolenga kuwakamata waharibifu wa  msitu huo ambayo  iliendeshwa na kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya ya Korogwe kwa kushirikiana na wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) na Halmashauri ya wilaya ya Korogwe.
Akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama mkazi wa Bombo majimoto Shaban Said alisema kuwa mara nyingi wameshajaribu kutoa taarifa kuhusu uhalifu unaoendelea katika msitu huo ngazi ya kijiji lakini wamekuwa wakidhihakiwa kuwa wana vyeo gani serikalini hata walisemee suala hilo na hivyo imekuwa ngumu kwao kama Wananchi kukomesha ujangili huo wa msitu.
“Ili mhakikishe kuwa wanashirikiana ndiyo maana hata hawatembelei msitu mara kwa mara kwani wangeshachukua hatua kabla ya nyie kuja kutokana na uharibifu mkubwa uliofanyika humu ndani ya msitu, lakini sisi tukipeleka taarifa tunaulizwa tuna vyeo gani.” Alisema  Said.
 Kwa upande wake diwani wa kata ya Mashewa inayozungukwa na msitu huo Seif Hillaly,   alisema yeye binafsi na uongozi wa kata walishafanya doria katika msitu huo na kufanikiwa  kuwakamata wahalifu lakini hata hivyo  waliachiwa huru baada ya kulipa faini  kulingana na sheria za nchi,hivyo  alitoa rai kwa watunga Sheria kutunga Sheria kali zenye adhabu itakayowatofautisha wazawa na wageni ili kukomesha kabisa tabia ya raia wa nchi nyingine kuingia Tanzania na kuharibu misitu.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wanafanya juhudi kama Serikali kwa ushirikiano na idara ya uhamiaji kuwatia nguvuni watu hao wanaosadikiwa kuingia nchini kinyemela na kufamya uhalifu huo na kwamba atatumia vyombo vya dola kuchunguza na kuwabaini viongozi wanaoshirikiana nao,pia  alitoa wito kwa Watanzania kuwa Wazalendo na kulinda nchi yao wao wenyewe kwani msitu huo unawafaidisha Watanzania hivyo kuathirika kwake ni hasara kwa Watanzania huku wakenya wakibaki salama na nchi yao.
Awali akitoa taswira ya uharibifu wa msitu huo, Afisa Misitu Msaidizi wa TFS Mbwelwa Kimweri alisema msitu huo wenye ukubwa wa hekta 3500 umekwishaharibiwa kwa asilimia 90 na sababu kubwa ikiwa ni ukosefu wa uzalendo kwani TFS na Halmashauri wameshatoa elimu ya kutosha kwa wanajamii hao kuhusu umuhimu wa msitu huo na jinsi ya kuuhifadhi huku wakiendelea kufaidika nao.
Operesheni hiyo ilifanikisha kukamatwa kwa mtu mmoja anayedhaniwa kuwa  raia wa Kenya ambaye alifikishwa katika kituo cha polisi wilayani Korogwe na hatua za awali za kufunguliwa mashtaka zimekwishafanyika. 
Kamati ya Ulinzi na Usalama ikijipanga katika makundi kuingia Msituni kusaka waharibifu wa Msitu.
 
Safari kuelekea Msituni
Kikosi kazi kilipovamia kambi ya Majangili hao wa Msitu na kukuta wametoroka,hata hivyo kikosi hicho kilimpata mmoja wao ambaye anashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani Korogwe
Mgambo wakitoka na Shehena ya vinyago Msituni vilivyokuwa vikiendelea na matengenezo kabla ya msitu kuvamiwa na Kamati ya Ulinzi.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe(mwenye shati jekundu) ikiwahoji baadhi ya Watanzania waliokutwa  msituni kuhusu uharibifu unaoendelea katika msitu huo.