UCHUMI UKIIMARIKA, RIBA BoT YASALIA ASILIMIA 6

July 04, 2024

 •⁠ ⁠Mfumuko wa bei wapungua, Utayari wananchi kulipa kodi waongezeka huku Akiba fedha za kigeni ikiwa ya kutosha


Na Leandra Gabriel,Dar es Salaam

UCHUMI Wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi unaotarajiwa kuimarika kwa siku zijazo kutokana jitihada za uboreshaji wa miundombinu hususani reli, barabara na bandari, upatikanaji wa uhakika wa umeme, hali nzuri ya hewa kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na sera za programu za maboresho.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT,) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC,) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Tanzania iliyoketi Julai 3, 2024 na kuamua Riba ya Benki Kuu (CBR,) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024.

Amesema, Katika kutathimini mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati hiyo ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza ya mwaka na pili ya mwaka 2024.

" Mfumuko wa bei umeendelea kupungua pamoja na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani na benki kuu katika Nchi nyingi kuanza kupunguza viwango vya riba....Bei ya mafuta ghafi ilipungua licha ya kuongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi juni 2024, Bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama njia mbadala ya uwekezaji katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani, Na matarajio ni uchumi wa dunia kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024 na 2025 licha ya kuwepo kwa hatari kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mizozo ya kibiashara." Ameeleza.

Pia amesema, Tathmini iliyofanywa na kamati hiyo kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba, Utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2024 umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia 5.

"Maamuzi ya kamati pia yanazingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia ambapo matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika Nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani na kushuka kwa bei ya bidhaa katika soko la Dunia. Na Kamati inatarajia uchumi wa ndani utaendelea kukua kwa kasi sambamba na upatikanaji wa chakula cha kutosha, kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni yaliyotokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula." Amesema.

Akieleza kuhusu maeneo mahususi ya mwenendo wa uchumi yaliyofanyiwa tathmini na kamati hiyo amesema ni pamoja na ukuaji wa uchumi ambao ulikua kwa asimilia 5.1 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka 2022 ambapo ukuaji huo ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini na mawe, ujenzi na shughuli za kifedha hususani ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi.

Aidha shughuli za utalii zimeendelea kuchangia kuimarika kwa uchumi ambapo kamati hiyo imekadiria ukuaji wa uchumi kuwa takribani asilimia 5 na 5.4 katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024.

" Uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara, mwaka 2023 ulikua kwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2022 na mwenendo huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, chakula na uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi na mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na 2025." Amefafanua

Pia mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu na chini ya lengo la Taifa la chini ya asilimia 5, Mwezi Aprili na Mei 2024 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3 na 3.1 mwenendo uliosababishwa na kupungua kwa mfumuko wa bei ya chakula kufuatia uwepo wa chakula cha kutosha nchini na kwa upande wa Zanzibar mfumuko wa bei umeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 5 kutokana na kupungua kwa bei za chakula na bidhaa zisizo za chakula na mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki ndani ya wigo wa asilimia tatu hadi nne katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na kuendelea.

Dkt. Yamungu amesema, utekelezaji bajeti ya Serikali umeendelea kuwa wa kuridhisha huku ukichagiza utekelezaji sera ya fedha ambapo; mapato ya Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia asilimia 95 ya lengo na Zanzibar mapato yakivuka lengo kwa asilimia 0.3 kulikosababishwa na maboresho katika usimamizi wa kulipa kodi na kuongezeka kwa utayari wa wananchi kulipa kodi.

Akifafanua kuhusu akiba ya fedha za kigeni amesema akiba iliendelea kuwa ya kutosha ya zaidi ya dola bilioni 5 zinazotosheleza uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya Nchi kwa zaidi ya miezi minne huku matarajio yakiwa ni kuongezeka zaidi kwa fedha za kigeni nchini kupitia mapato yatokanayo na shughuli za utalii, mauzo ya madini, bidhaa asilia na usafirishaji wa chakula kwenda Nchi jirani.

Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT,) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC,) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Tanzania iliyoketi Julai 3, 2024 na kuamua Riba ya Benki Kuu (CBR,) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024.

 Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

BENKI YA NMB YAIPIGA TAFU SHULE MBILI ZA SEKONDARI DAR, YAKABIDHI MEZA 90 NA VITI 90 VYENYE THAMANI YA SH.MILIONI 10

July 04, 2024



Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB imekabidhi meza 90 na viti 90 venye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 kwa mbili mkoani Dar es Salaam zikiwa ni Shule ya Sekondari ya Uhamiaji iliyopo Wilaya ya Temeke na Shule ya Sekondari iliyopo wilaya ya Temeke ikiwa ni utekelezaji wa azma ya benki hiyo kuboresha ya elimu .

Samani hizo zitapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upungufu wa madawati kwa walimu na wanafunzi na ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Uwekezaji kwa Kijamii (CSI) unaolenga kusaidia jamii ambapo benki hiyo inafanya kazi.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi meza na viti hivyo Jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona alisema uboreshaji wa sekta ya elimu ni miongoni mwa vipambule muhimu kwa benki yake huku alisisitiza dhamira ya benki hiyo kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote ikiwemo Serikali katika kuinua maendeleo ya sekta ya elimu nchini kote.

"Kama benki, tunatambua kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha ndiyo maana kwa miaka mingi tumewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuinua ukuaji wa sekta ya elimu. Kwa hakika, sekta ya elimu ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika mkakati wetu wa CSI. Tumekuwa tukitenga asilimia moja ya Faida Baada ya Kodi (PAT) kila mwaka ili kuchangia mipango mbalimbali ya maendeleo,” alisema.

Mpona aliongeza, “Tunaamini samani tunazotoa leo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu,”
Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo aliipongeza benki hiyo kwa moyo wake wa ukarimu na kusisitiza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuendeleza maendeleo ya sekta ya elimu.

“Tunafahamu kuwa shule nyingi za Wilaya ya Temeke bado zinakabiliwa na changamoto nyingi na zinahitaji msaada zaidi kutoka kwa wadau wa elimu kwa kuwa tuna bajeti ndogo. Naishukuru Benki ya NMB kwa kuunga mkono jambo hili zuri na nachukua fursa hii kutoa wito kwa wadau wengine wa ushirika kuungana na azma yetu ya kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu,” Mapunda alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo wakati wa hafla ya kukabidhi meza 50 na viti 50 vilivyotolewa na benki ya NMB kwa Shule ya Sekondari Mchikichini alishukuru benki ya NMB kwa kuendelea kuunga juhudi za serikali za kuboresha sekta ya elimu.

“Tunashikia faraja kwa benki yetu kwa kuendele kuwa karibu na wananchi. Mheshimiwa rais ameshaleta fedha za kujenga ghorofa katika shule hii ya Mchikichini na matundu ya vyoo. Kitendo cha benki ya NMB kutoa meza na vitu ni jitihada njema za kuunga mkono serikali na siku zote wamekuwa wakituunga mkono kwa vitendo,” alisema.

Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Uhamiaji, Christopher Mtabutu alibainisha kuwa shule yake ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati ya walimu akionyesha matumaini kuwa madawati yaliyotolewa na benki ya NMB kwa kiasi kikubwa yatasaidia kukabiliana na upungufu huo.

“Mchango huu umekuja wakati muafaka kwani tumekuwa tukikabiliwa na upungufu wa madawati ya walimu. Ninaamini kuwa madawati na meza ambazo benki ya NMB imetupatia leo vivitasaidia tu kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu mbali na kuboresha usalama wa mali zao pia,” aliongeza.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mchikichini Nelson Nestory alisema, “Msaada wa meza 50 na viti 50 utasaidia sana. Kabla ya kuomba msaada huu tulikuwa na upungufu wa meza na viti 150 na meza 50 ambapo Mkurugenzi alituletea viti 100 na meza 100. Tulikuwa na upungufu wa meza 50 na viti 50. Tunaishukuri benki ya NMB kwa kutupatia meza 50 na viti 50 na kwa sasa tumemaliza tatizo la wanafunzi kukosa meza na viti.

Aliahidi shule yake kuendelea kutunza msaada huo vyema ili kusaidia vizazi vijavyo.




BENKI YA NMB YAELEZA UWEZO WA KUKOPESHA ZAIDI YA BILIONI 5/= KWA MKUPUO MMOJA.

July 04, 2024

  Kupitia Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania, yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Benki ya NMB imeeleza ina uwezo wakukopesha hadi Sh.Bilioni 515 kwa mkupuo mmoja  ‘single borrower limit’ kwa sababu yakufanya vizuri kwenye soko la Tanzania.


Hayo yamesemwa na Meneja wa NMB Tawi la Sabasaba, Bi. Kidawa Masoud, katika banda la benki hiyo kwenye Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, na kwamba tangu Julai 2023 hadi Mei 2024, NMB imetoa mikopo ya zaidi ya Sh. Bilioni 585.

Tunayo mizania wa zaidi ya Sh. Trilioni 12.2, jambo ambalo unaowahakikishia uimara na uwezo wa kukopesha hadi Sh. Bilioni 515.

Uimara huo kiuchumi, unawapa uhakika wa kuendana na kasi ya Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeweka mazingira wezeshi kibiashara kama inavyoakisi kaulimbiu ya Maonesho ya Sabasaba mwaka huu; ‘Tanzania ni Sehemu Bora kwa Biashara na Uwekezaji.’
 
 “Tuko imara kuhudumia kada zote za wateja wadogo, wa kati, wakubwa na mashirika ama kampuni, ambazo zinaweza kukopa kwetu hadi Bilioni 515 kwa mkupuo mmoja na nguvu hii inatokana na ongezeko la silimia 26 ya Faida Baada ya Kodi tuliyopata mwaka 2023 ya Sh. Bilioni 542.

“Mpango Mkakati tulionao kwa ni kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia mifumo ya kidijiti, ambayo imeonesha mafanikio makubwa sana, kwani asilimia 94 ya miamala iliyofanyika kwa mwaka jana, imefanywa nje ya matawi 231 ya benki yetu kote nchini.

“Katika kufanikisha hili, tunazo akaunti za NMB Pesa zinazofunguliwa kwa Sh. 1,000 tu, NMB Kikundi inayojumuisha wanachama wa vikundi mbalimbali vya kijamii, lakini pia tunao mkakati wa Huduma za Kibenki Vijijini ‘Rural Banking’ yenye lengo la kuvifikia vijiji 1,000 Tanzania,” alisema.

Bi. Kidawa alifafanua ya kwamba, ‘Rural Banking’ ni mkakati unaolenga kufungua akaunti Miloni 1.5 kwa wakazi wa maeneo yasiyo na huduma za kibenki vijijini, kupitia mawakala wa benki hiyo waliotapakaa kila kona ya nchi.

Aidha, wakati kalenda ya Mwaka wa Fedha wa Serikali wa 2024/25 inayoanzia Julai 1 ikianza kutumika, NMB imetambia mafanikio katika makusanyo ya Mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzaibar (SMZ), ilikofanyia maboresho mifumo yao na serikali zote.

Bi. Kidawa amesema: “Mwaka huu tunaendeleza mashirikiano yetu na Serikali zote za Bara na Visiwani, katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato, ambako tumeweza kukusanya zaidi ya Sh. Trilioni 9.8 tangu mwaka 2018 kupitia NMB Wakala, NMB Mkononi na matawi yetu.”

Aliongeza ya kwamba, kama taasisi ya fedha kinara nchini, wanajivunia mafanikio yaliyowawezesha sio tu kutoa gawio kubwa zaidi la Sh. Bilioni 57.3 kwa Serikali ya Tanzania ambayo inamiliki asilimia 31.8 ya Hisa za Benki ya NMB, bali kutwaa Tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa mwaka wa 11 mfululizo.

“Ni mwaka ambao tulipata pia Tuzo ya Benki Bora Tanzania tuliyopewa na Jarida la Euromoney, lakini pia tukapata idhini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CSMA), kuwa wakala wa madalali wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).