BENKI YA TPB YATOA MSAADA WA MASHUKA NA VYANDARUA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA YA KAHAMA

October 13, 2017


Mkurugenzi wa uendeshaji na Teknohama kutoka makao makuu ya benki ya Posta (TPB) Jema Msuya (wa pili kutoka kushoto) akikabidhi mashuka na vyandarua kwa afisa takwimu wa halmashauri ya mji wa Kahama Flora Sangiwa ambaye alimwakilisha mkurugenzi.
*****
Takriban wagonjwa elfu 24 hadi elfu 30 wanapokelewa kila mwezi katika hospitali ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga idadi ambayo inatajwa kuwa ni kubwa ukilinganisha na miundombinu ya hospitali hiyo.

Hayo yamesemwa leo na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dr. Fredrick Malunde wakati akipokea msaada wa mashuka 100 na vyandarua 50 vyenye thamani ya shilingi milioni mbili vilivyotolewa na Benki ya TPB.

Amesema kutokana na wingi wa wagonjwa wadau wanapaswa kuguswa kutoa misaada ya vifaa ili kukabiliana na changamoto hizo.

Naye Mkurugenzi Uendeshaji na Teknohama kutoka makao makuu ya Bank ya TPB Jema Msuya amesema Benki hiyo itaendelea kusaidia kuchangia miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali huku akiwaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia sekta za afya.

Afisa Takwimu wa Halmashauri yam Mji wa Kahama, Flora Sangiwa ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo amesema halmashauri hiyo itaendelea kuthamani michango ya wadau wa maendeleo na kuipongeza benki ya TPB kwa msaada huo.

Wafanyakazi wa Benki ya TPB wakisomba vyandarua na mashuka mara baada ya kufika katika hospitali ya wilaya ya Kahama.
Afisa mawasiliano wa Benki ya TPB Moves Moses akiwaonyesha waandishi wa habari ubora wa vyandarua walivyovitoa katika hospitali hiyo. 
Wafanyakazi wa Benki ya TPB wakiteta jambo muda mchache kabla ya kuanza kwa zoezi la ugawaji wa mashuka na vyandarua.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Kahama Fredrick Malunde akiteta jambo na meneja wa tawi la TPB Kahama wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo.
Waziri Kalemani Ataka Umeme Wa Dharura Mtwara

Waziri Kalemani Ataka Umeme Wa Dharura Mtwara

October 13, 2017
PICHA NA 1
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akielezea mikakati ya usimamizi wa miradi ya umeme nchini mbele ya Watendaji kutoka Wizara ya Nishati,  Shirika la  Umeme  Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati  Vijijini (REA), Kampuni ya Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) Wakandarasi wa Miradi ya Umeme pamoja na Wasambazaji wa nyaya, tansfoma na nguzo (hawapo pichani) Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi  Innocent Luoga
PICHA NA 2
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akifafanua jambo katika kikao hicho. Wengine kutoka kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi  Innocent Luoga, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
PICHA NA 3
Sehemu ya washiriki wa kikao hicho wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani. (hayupo pichani).
………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha linashughulikia haraka tatizo la kukatika kwa umeme katika mkoa wa Mtwara ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.
Waziri Kalemani alitoa  agizo hilo jana (tarehe 12 Oktoba, 2017)  alipofanya kikao na Watendaji wa Wizara ya Nishati, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wa Shirika la  Umeme  Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) na Kampuni ya Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).
Wengine waliohudhuria kikao hicho walikuwa ni pamoja na Naibu  Waziri, Subira Mgalo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi  Innocent Luoga, wakandarasi wa miradi ya usambazaji wa umeme  vijijini inayosimamiwa na TANESCO na REA pamoja na wasambazaji wa nyaya, nguzo na  transfoma nchini.
Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujitambulisha, kujadili namna  ya kutekeleza miradi ya  umeme nchini pamoja na changamoto zake.
Alisema kumekuwepo na tatizo la kutopatikana kwa umeme wa uhakika katika mkoa wa Mtwara ambapo ndio chanzo cha gesi asilia inayotumika kuzalisha umeme.
Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dkt. Tito Mwinuka kuhakikisha unapatikana umeme wa dharura kwa namna yoyote na kuongezwa  katika mkoa wa Mtwara hivyo kumaliza  tatizo la kukatika kwa umeme kwa mara kwa mara.
Alisema mbali na kuweka umeme wa dharura, shirika hilo linatakiwa kuhakikisha mitambo iliyoharibika inakarabatiwa mapema ipasavyo na kuendelea na mchakato wa ununuzi wa mitambo mipya kwa kasi kubwa ili hatimaye tatizo la umeme katika mkoa wa Mtwara liwe historia.

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA UTALII

October 13, 2017

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa kufungua Maonyesho ya Tatu ya Kimataifa ya Utalii yanayojulikana kwa jina la Swahili linalofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Maonyesho ya ya Tatu ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili uliofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi kinyago maalum Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANAPA Jenerali Mstaafu George Waitara kama ishara ya shukrani kwa kuwa mmoja wa wadhamini wa Maonyesho ya Tatu ya Utalii ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Bw. Allan Kijazi mara baada ya kupokea kinyago maalum ikiwa ni shukrani kwa kuwa mmoja wa wadhamini wa Maonyesho ya Tatu ya Utalii ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili. 
   Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi kinyago maalum Naibu Mhifadhi (Uhifadhi, Maendeleo ja Jamii na Utalii) wa Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Maurus Msuha kama ishara ya shukrani kwa kuwa mmoja wa wadhamini wa Maonyesho ya Tatu ya Utalii ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

WIZARA YA AFYA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA MAMA NA MTOTO KUFIKIA 2020

October 13, 2017

 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu katikati akiongea na wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali  hawapo pichani wa Wizara ya afya kuhusiana na kuimarisha huduma bora za afya nchini  leo jijini Dar es salaam, wa kwanza kushoto ni Naibu wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndungulile na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya. Wakati wa kikao chake na wakuu hao.

NA WAMJW-DAR ES SALAAM
WIZARA ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imejidhatiti kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto mpaka kufikia 2020 ili kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga .
Hayo yamesemwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipokutana na Wakuu wa Idara na vitengo Mbalimbali kwa ajili ya utambulisho wa Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndungulile  katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.
“Vifo vya wajawazito vimekua tishio nchini hivyo ni lazima tuimarishe huduma za afya ya mama na mtoto ili tufikie malengo ya kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi mpaka kufikia 2020 ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora” alisema Waziri ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa katika kuboresha hilo amewaagiza wakuu wa idara wizara ya afya kushirikiana na mfuko wa bima ya afya nchini(NHIF) kuona kama kuna uwezekano wa kuanzisha bima ya afya kwa wajawazito kwa bei nafuu hadi kufikia Julai mosi 2018.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa wanamipangilio ya kutokomeza kabisa tatizo la dawa nchini kwa kuweka mpango mkakati kati ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na vituo  vitoavyo huduma za afya  ili kuepuka tatizo hilo lisijirudie mara kwa mara .
Kwa upande wake Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndungulile amesema kuwa ameshukuru kwa kupewa dhamana hiyo na atashirikiana vyema na Waziri pamoja na watendaji wa Wizara hiyo ili kuleta ufanisi na Huduma bora za afya nchini.
“Nitashirikiana na Waziri wangu pamoja na nyinyi watendaji wenzangu katika kusimamia na kutekeleza sera ya afya ili kuweza kutoa huduma bora za afya kwa watanzania wote bila ya kujali rika,jinsia wala umri” alisema Dkt. Ndungulile.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa wamepokea maagizo hayo amabayo baadhi  wameanza kuyatekeleza na mengine  atawahimiza watendaji wake kuendana na kasi ya awamu ya tano ya HAPA KAZI TU ili kuifikisha nchi katika afya bora.
 Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto Dkt.  Faustine Ndungulile wa kwanza kushoto akiongea na wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya hawapo pichani kuhusiana na kuimarisha huduma bora za afya nchini  leo jijini Dar es salaam, katikati ni Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu na kulia ni Katibu Mkuu Wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya. Alipokutana na wakuu hao.
 Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na watoto wakifuatilia kwa makini maelezo kutoka kwa Waziri mwenye dhamani hiyo  Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile hawapo pichani wakati wa kikao na wakuu wa idara hizo leo jijini Dar es salaam.
 Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na watoto wakimpongeza Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndungulile hayupo pichani mara baada ya kuwapa maelezo wakati wa kikao na wakuu wa idara hizo leo katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es salaam.

MAMA JANETH MAGUFULI NA MAMA SHEIN WATEMBELEA VITUO VYA WATOTO YATIMA NA WAZEE ZANZIBAR LEO

October 13, 2017

 Mama Janeth Magufuli na Mama Mwanamwema Shein wakiwa na baadhi ya watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha yatima cha Mazizini Unguja ambako wake hao wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar walitembelea ambapo Mama Magufuli alitoa msaada wa vyakula mbali mbali na mafuta ya kupikia na sukari leo Oktoba 13, 2017.




 Mama Janeth Magufuli akiwa ameongozana na Mama Mwanamwema Shein katika kituo cha yatima cha SOS eneo la Mombasa mjini Unguja ambako wake hao wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar walitembelea ambapo Mama Magufuli alitoa msaada wa vyakula mbali mbali na mafuta ya kupikia na sukari leo Oktoba 13, 2017.
 Mama Janeth Magufuli akiwa na Mama Mwanamwema Shein wakimsalimia Bibi anayelelewa katika kituo cha Wazee eneo la Welezo ambako wake hao wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar walitembelea ambapo Mama Magufuli alitoa msaada wa vyakula mbali mbali na mafuta ya kupikia na sukari leo Oktoba 13, 2017.
 Mama Janeth Magufuli akiwa ameongozana na Mama Mwanamwema Shein wakisalimia baadhi ya wazee wanaolelewa katika kituo cha Welezo Unguja wakati wake hao wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar walitembelea ambapo Mama Magufuli alitoa msaada wa vyakula mbali mbali na mafuta ya kupikia na sukari.
 Mama Janeth Magufuli akiwa ameongozana na Mama Mwanamwema Shein akikabidhio msaada wa vyakula kwa ajili ya wazee wanaolelewa kituo cha Welezo Unguja wakati wake hao wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar walitembelea ambapo Mama Magufuli alitoa msaada wa vyakula mbali mbali na mafuta ya kupikia na sukari leo Oktoba 13, 2017. 


 Mama Janeth Magufuli akiwa ameongozana na Mama Mwanamwema Shein wakiwa katika kituo cha kulelea Wazee cha Sebleni Unguja wakati wake hao wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar walitembelea ambapo Mama Magufuli alitoa msaada wa vyakula mbali mbali na mafuta ya kupikia na sukari leo Oktoba 13, 2017.

DKT ANGELINA MABULA AAHIDI WATAALAMU WA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI SINGIDA.

October 13, 2017
 Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na wataalamu wa ardhi, viongozi na watendaji wa halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Singida [hawapo pichani], Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
 Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Massaka.
 Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi wa Wilaya ya Iramba Lugano Sanga kuhusu utuzanji wa nyaraka za idara hiyo.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi hati ya kumiliki kiwanja chake kilichopo Mjini Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeahidi kutoa timu ya wataalamu watakao suluhisha mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida na Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.

Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Singida katika kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama ambapo amesema Wizara yake itatoa wataalamu watakaoweza kutatua mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.

“Kwakuwa pande zote mbili za Mkalama na Hanang’ zimekutana mara kadhaa bila mafanikio, nitaleta wataalamu wafike eneo la mpaka ili wataalam hao wawasomee alama moja baada ya nyingine, kila mmoja wenu afahamu eneo lake mwisho ni wapi, nadhani hapo tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu”, amesema Dkt Mabula.

Amesema wananchi wa Kijiji hicho cha Singa wasiwe na wasiwasi endapo baada ya kuonyesha mpaka wao mashamba yao yakionekana yapo wilaya ya Hanang’ wataruhusiwa kuendelea kuyamiliki ila watatakiwa kwenda kujitambulisha katika Uongozi wa Wilaya hiyo.

Aidha Dkt Mabula amesema timu hiyo ya wataalamu itahakikisha inasuluhisha migogoro yote ya mipaka ya wilaya hiyo ambayo ngazi ya wilaya imeshindikana kutatuliwa.

Amewashauri wananchi hao kutouza au kugawa ardhi yao ovyo ovyo kwakuwa ardhi ni mali na mtaji popote pale hata kama ni vijijini hivyo watunze ardhi yao na kuiongezea thamani kwa kuipima na kuwa na hati ya umiliki.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walitoa malalamiko kwa Naibu Waziri huyo huku wakimueleza kuwa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu umesababisha baadhi yao kupelekwa mahakamani kwa madai ya kuvamia mashamba.

Mzee Anaftali Amosi Majii amemueleza Naibu waziri kuwa taarifa za mgogoro huo zilitolewa muda mrefu na kuongeza kuwa wananchi wamechoka kushitakiwa kwa makosa ya uvamizi wa mashamba wakati wao wanaamini wanayamiliki kwa uhalali jambo ambalo linawachelewesha kimaendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama Mhandisi Geofrey Sanga amesema Wilaya ya Mkalama ina migogoro ya mipaka kwa wilaya tano zinazowazunguka.

Mhandisi Sanga ameeleza kuwa Mkalama ina migogoro ya mipaka kati yake na Wilaya za Mbulu, Iramba, Hanang’ na Wilaya ya Singida jambo ambalo linawafanya baadhi ya wananchi kukwepa kuchangia shughuli za maendeleo wakidai wao sio wa Wilaya hiyo.

Wakati huo huo Naibu Waziri Dkt Angelina Mabula amefanya ziara Wilaya ya Iramba na kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika masijala ya Ardhi ya Wilaya hiyo ambapo hakuridhishwa na utunzaji wa nyaraka pamoja na utendaji usioridhisha unaosababisha wananchi kuchelewa kupata hati za viwanja.

Dkt Mabula pia hakuridhishwa na kasi ndogo ya upimaji viwanja na utoaji wa hati wilayani humo huku akiwataka kuacha kukusanya kodi mbalimbali za ardhi kwa utendaji wa kimazoea bali wafanye kazi bidii.

Wateja wa Tigo Mbeya wapata huduma za bidhaa kwa bei nafuu msimu huu wa Tigo Fiesta

October 13, 2017
Msimamizi msaidizi wa Duka la Tigo mkoani Mbeya, Elifazi Mtwale akitoa huduma kwa wateja waliofika dukani hapo kupata huduma mbalimbali kwa bei nafuu msimu huu wa Tigo Fiesta leo.

Mtoa huduma wa Duka la Tigo mkoani Mbeya, Janeth  Rwanga akitoa huduma kwa wateja waliofika dukani hapo kupata huduma mbalimbali kwa bei nafuu msimu huu wa Tigo Fiesta leo.