MO DEWJI ANYAKUA TUZO YA MWAKA YA MFANYABIASHARA ANAYESAIDIA ZAIDI JAMII

MO DEWJI ANYAKUA TUZO YA MWAKA YA MFANYABIASHARA ANAYESAIDIA ZAIDI JAMII

September 17, 2015
IMG_9463
Mkurugenzi Mtendaji wa CNBC Africa, Roberta Naicker akimkabidhi tuzo ya '2015 Philanthropist of the year-East Africa' Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji katika sherehe zilizofanyika hoteli ya DusitD2 jijini Nairobi.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
IMG_9492
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akizungumza kwenye hafla ya tuzo za All Africa Business Leaders Awards 2015 (AABLA). Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa CNBC Africa, Roberta Naicker.
IMG_9595
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akipozi katika picha ya kumbukumbu na Mkurugenzi Mtendaji wa CNBC Africa, Roberta Naicker.
IMG_9627
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akiwa ameshikilia tuzo yake.
IMG_9608
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akibadilishana mawazo na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa jijini Nairobi ambapo pia walimpongeza.
IMG_9587
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji katika picha ya kumbukumbu na mmoja wa wageni waalikwa kwenye hafla ya tuzo za All Africa Business Leaders Awards 2015 zilizofanyika kwenye hoteli ya Dusit D2 jijini Nairobi.
IMG_9655
Mohammed Dewji, CEO of MeTL Group....2015 Philanthropist of the Year-East Africa.
Na Mwandishi Wetu
BILIONEA anayemiliki kampuni kubwa ya Mohammed Enterprises nchini (MeTL), Mohammed Dewji `Mo’ ameshinda Tuzo ya Mfanyabiashara wa Mwaka anayejitoa zaidi kuisaidia jamii kunufaika kutokana na biashara zake, akiwa mshindi wa Afrika, Kanda ya nchi za Afrika Mashariki katika tuzo zilizofanyika juzi jijini Nairobi, Kenya.
Katika tuzo hiyo ya heshima kwa wafanyabiashara Afrika inayoratibiwa na Kituo cha Biashara cha Televisheni ya CNBC Afrika, Dewji alishindanishwa na mabilionea raia wa Kenya, Ashok Shah wa kampuni ya Apollo Investment Limited na Damaris Too-Kimondo anayemilikia kampuni ya Shrand Promotions.
Katika sherehe hizo zilizofana, Dewji alikabidhiwa tuzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa CNBC Africa, Roberta Naicker.
Ushindi wake umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha Dewji ambaye pia ni mwanasiasa aliyekuwa mbunge wa Singida Mjini kwa miaka kumi, kujihusisha na misaada yenye lengo la kupambana na umasikini kupitia sekta mbalimbali kama elimu, maji, watu wenye ulemavu na pia uwezeshaji kiuchumi, matukio ambayo yamelenga na kubadili hali ya watu maskini zaidi katika jamii.
Washindi hao wa Kanda ya Afrika Mashariki watashindanishwa na washindi wengine kutoka Kanda ya Kusini mwa Afrika na Afrika Magharibi Novemba 13, mwaka huu huko Sandton, Johannesburg nchini Afrika Kusini ili kupata mshindi wa jumla wa bara la Afrika.
Akizungumza mara baada ya kutunukiwa tuzo yake hiyo yenye heshima kubwa, aliwashukuru waandaaji, jarida la Forbes na majaji kwa kumuona anastahili kwa tuzo hiyo ya kipekee.
Alisema, kwake ni faraja kubwa kupata heshima huyo na amekuwa na ndoto za kusaidia watu wa Tanzania kukabiliana na changamoto wa kasi ya maendeleo barani Afrika na kwamba ili kuendana na kasi hiyo, miongoni mwa juhudi zinazotakiwa ni kuwawezesha kupata elimu bora, hasa wa maeneo ya vijijini.
“Ninaamini tukiunganisha nguvu, nchi za Afrika zina nafasi kubwa ya kuwa na wataalamu wake watakaosaidia kusukuma gurudumu la kiuchumi Afrika na hivyo kuboresha hali za maisha za watu wa bara hili,” alisema bilionea huyo kijana aliyeanzishwa taasisi yake ya Mo Dewji Foundation kwa lengo la kuisaidia jamii.
Alisema kwamba hilo ni tukio kubwa sana kwake na kumnukuu Maya Angelou, akisema: “Ukisoma, fundisha. Ukipata, toa.” Aliongeza kuwa, kwa kuwa amebarikiwa na Mungu kupata vyote, anakusudia kuendelea kuuelimisha umma juu ya kufanya mapinduzi ya kielimu, afya, na maeneo mengine ya ustawi wa jamii, huku akiahidi kusaidia kwa kila atakachojaliwa.
Dewji mwenye umri wa 40 ambaye kwa sasa ndiye bilionea kijana zaidi Afrika kwa vijana wasiozidi umri huo, akiwa pia miongoni mwa mabilionea 55 wanaoongoza kwa utajiri Afrika, anaongoza kampuni yenye makampuni yaliyojikita katika sekta za kilimo, fedha, uzalishaji, usambazaji wa bidhaa na kadhalika, huku akitajwa kuajiri zaidi ya watu 20,000.

MSAFARA WA SUGU WASHAMBULIWA KWA MAWE AKIELEKEA KATIKA KAMPENI ZAKE ZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA MBEYA

September 17, 2015
Gari la Mgombea Ubunge jimbo la Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi Sugu likiwa kituo cha Polisi kati jijini Mbeya mara baada ya kushambuliwa kwa mawe na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM

Sugu akiwa kituo cha Polisi na wafuasi wake.Picha Kenneth Ngelesi Mbeya .

(JAMIIMOJABLOG MBEYA )


Na Emanuel Kahema ,Mbeya

MGOMBEA ubunge  kupitia chadema jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi leo  amejikuta katika wakati mgumu baada ya msafara wake kushambuliwa na mawe na wafuasi wanaosadikiwa kuwa ni wa chama   cha mapinduzi CCM na kwamba katika tukio hilo watu wawili wamejeruhiwa akiwemo dereva aliyekuwa akimuendesha mgombea huyo  .


Tukio hilo la kushambuliwa kwa msafara huo, limetokea majira ya saa 11 za jioni katika eneo  la barabarani lililopo katika Kata ya Ghana mtaa wa Mbata jijini hapa  ambapo inasemekana mgombea huyo alikuwa  katika harakati za kampeni kuomba kura kwa wananchi wa Iziwa  ambapo mgombea huyo alikuwa ndani ya gari yake yenye namba za usajili T161 CPP Toyota  Land Cruser VX .


Awali, wafuasi wa chama cha mapinduzi CCM, walikuwa katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea wao ngazi ya Udiwani katika kata ya Ghana iliyopo ndani ya Jiji la Mbeya, hivyo wakiwa kwenye harakati hizo inasemekana walishangaa kuona msafara wa sugu ukipita katikati ya mkutano huo hivyo kushindwa kuvumilia na kuanza kurusha mawe huku wengine wakishikana mithili ya kutaka kupigana.



Katika vurugu hizo gari aliyokuwa amepanda mgombea huyo  lilipasuliwa kioo cha mbele na gari ya chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Mbeya, ikipasuliwa kioo cha mbele .

Aidha Vurugu hizo zimesababisha   majeruhi wawili ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya akiwemo dereva wa mbunge huyo na mfuasi mmoja wa chadema.


Kutokana na hali hiyo  mgombea huyo wa ubunge mbeya mjini kwa tiketi ya Chadema alilazimika kuikatisha zoezi lake la kuongea na wakazi wa Kata ya Iziwa iliyopo Jijini Mbeya kwa muda, kutokana na kulazimika kuripoti katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.


Mgombea huyo ilimlazimu kufika kituoni na kuchukuliwa maelezo na baada ya hapo aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa lakini gari yake yenye namba za usajili T161 CPP aliyokuwa akiitumia katika kampeni zake ikibaki polisi.




Hata hivyo, mgombea huyo alipomaliza kutoa maelezo  katika kituo cha polisi cha kati cha Wilaya ya Mbeya, aligoma kuzungumza na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa kwenye eneo la tukio na kuwataka wafike katika mkutano kwani ndipo atakapotolea ufafanuzi wa suala hilo hilo.


Mwisho.

KIAMA CHA MAJANGILI CHAJA, BATHAWK YAZINDUA NDEGE MAALUM KUPAMBANA NAO ​

September 17, 2015

Ndege aina ya Super Bat DA-50

Na Daniel Mbega, Mkomazi
NI majira ya saa tatu asubuhi Jumatano, Septemba 16, 2015 wakati tunawasili kwenye uwanja mdogo wa ndege (air strip) katika eneo la Kisima ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi inayotenganisha mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Uwanja unaonekana mweupe, hakuna ndege! Nikashangaa kwa sababu wenyeji wetu kampuni ya Bathawk Recon wametuambia tunakuja kushuhudia uzinduzi wa ndege maalum zinazopambana na ujangili.
Kilichoonekana mbele yetu ni hema kubwa ambalo mbele yake kulionekana minara midogo iliyosimikwa kama fimbo. Kwenye banda kubwa ikaonekana ndege ndogo aina ya Twin otter. Nikadhani ndiyo inayozinduliwa, lakini Idrisa Jaffary, mwenyei wetu tuliyekuwa naye kwenye gari akasema, hapa siyo hiyo.
Mshangao ukanipata baada ya gari kusimama wakati nilipokiona kifaa mfano wa ndege kikiwa kimeegeshwa kwenye bomba maalum kana kwamba ndege inataka kupaa.
Kama nisingekuwa nazifahamu ndege hizi maarufu kama drones, ningeweza kusema kwamba huo ni mdoli ambao mwanangu angefurahia kama ningempelekea akauchezea.
Kwa siku za karibuni zimekuwa maarufu kwani zinatumika kupeleka misaada mbalimbali hata katika maeneo hatari ya vita ambako hakufikiki kirahisi.
“Hii ndiyo ndege yenyewe,” Idrisa akatueleza. “Hee! Ndiyo hii?” tukajiuliza kwa mshangao. Kwamba Tanzania tumeanza kuitumia teknoloia hii yanaweza kuwa maendeleo mengine mapya.
Mshangao wetu ulimalizika wakati Phil Jones, ofisa mwendeshaji wa mitambo hiyo kutoka kampuni ya MartinUAV ya Marekani iliyotengeneza ndege hiyo aina ya Super Bat DA-50 UAV, alipoanza kutuelezea namna ‘ndege’hiyo (drone) inavyofanya kazi huku akituonyesha kila sehemu na kazi yake.
“Hii ni ndege ambayo haihitaji kuwa na rubani, inaongozwa kwa kompyuta maalum, ina antenna mbili, ina kamera maalum ambazo zinaweza kupiga picha usiku na hata mchana,” akatueleza.
Akasema ndege hiyo ina uwezo wa kuruka urefu wa futi 20,000 kutoka usawa wa bahari na kwenda katika nusu kipenyo cha kilometa 35 kutoka ilipo mitambo ya kuiongoza.
Jones, ambaye baadaye alinieleza kwamba yeye rubani wa zamani wa ndege za kijeshi katika Jeshi la Uingereza aliyestaafu mwaka 2014 ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, akasema ndege hiyo inayorushwa kwa mtindo wa manati (catapult launch system), inaweza kuruka mfululizo kwa muda wa saa 10 ikiwa angani kabla ya kutua na kujazwa mafuta tena.
“Ina mfumo maalum wa kamera ambazo zina uwezo wa kupiga picha hata usiku wa manane na kutambua mienendo ya viumbe wenye damu ya moto kama hayawani na binadamu, hivyo ni rahisi kubaini kama kuna majangili,” akafafanua.
Baada ya maelezo ya takriban nusu saa, hatimaye yeye na wasaidizi wake wakaamua kuirusha ndege hiyo baada ya kuiwasha. Ilichomoka kwa kasi ya ajabu na kuelekea angani ikaanza kuzunguka.
Hapo ndipo tukasogezwa kwenye hema kubwa ambako tuliwakuta wasaidizi wake – Austin Howard na Kory Ferguson – wakiendesha kompyuta hizo na tukashuhudia mazingira halisi ya hifadhi katika eneo husika pamoja na kuona wanyama mbalimbali.
“Sasa hapa unaweza kuona kama kuna wavamizi (majangili) na inakuwa rahisi kuwasiliana na askari wa wanyama pori na kwenda kwenye eneo husika kuwakamata,” anasema Jones.
Hata ilipotua, ilikuja kama ndege za kawaida zinavyokuja, tofauti yake tu yenyewe haina magurudumu. Naam, unaweza kuwa ufumbuzi mwingine wa kupambana na ujangili nchini, tatizo ambalo haliko Tanzania tu, bali katika nchi nyingi barani Afrika.
Taasisi mbalimbali za ndani na nje zikiwemo serikali za mataifa makubwa zimekuwa zikijitahidi kusaidia mapambano hayo kama alivyofanya Rais Barack Obama wa Marekani alipoahidi kutoa Dola milioni 10 (sawa za Shs. 20 bilioni) ili kuimarisha mapambano hayo nchini.
Takwimu zinaonyesha kuwa Bara la Afrika mwaka 1930 lilikuwa na tembo 50 milioni na kwamba hadi kufikia mwaka 2013 tembo waliobakia katika bara zima ni  500,000.
Aidha, takwimu hizo zinaonyesha kwamba katika miaka ya 1960 Tanzania kulikuwa na tembo kati ya 250,000 hadi 300,000 na kwamba wanyama hao walipungua hadi kufikia 130,000 mwaka 2002 na idadi ya tembo hapa nchini imeendelea kupungua kwa kasi ambapo hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa inakadiriwa kuna tembo wasiozidi 55,000.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wastani wa tembo 30 huuawa kijangili kila siku ikiwa ni sawa na tembo 850 kwa mwezina zaidi ya tembo 10,000 wanauawa kila mwaka,hali ambayo inatishia uwepo wa wanyama hao wakubwa zaidi duniani kwa sasa.
Kwenye Hifadhi ya Tarangire, jumla ya tembo 104 waliouawa katika kipindi cha miaka mitatu tu kutoka mwaka 2007 hadi 2009 na katika Hifadhi ya Serengeti idadi ya tembo imepongua kutoka 2,500 mwaka 1985 hadi kufikia 500 mwaka 2012 huku nyati wakipungua kutoka 70,000 hadi 40,000 ujangili huo ukiua faru wengi kutoka 1,000 waliokuwepo mwaka 1985 hadi 20 tu.
Kwenye Pori la Akiba la akiba la Selous inaelezwa kwamba hadi kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo zaidi ya 70,000 lakini idadi hiyo imeshuka hadi tembo 30,000 tu kufikia mwaka 2012.
Kasi ya ujangili inayoongezeka kila mwaka inachangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo kukua kwa uchumi wa nchi ya China na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia kama Hong Kong, Vietnam na Philippines.  
Juhudi mbalimbali zimefanywa na wadau wa sekta ya utalii na maliasili, lakini inaoenakana tatizo hilo linazidi kuota mizizi huku taasisi za kimataifa zikiendelea kulipigia kelele bila mafanikio.
Kampuni ya Bathawk Recon Limited ya Tanzania imeitikia kwa vitendo mapambano ya vita dhidi ya ujangili nchini, ambapo leo hii Septemba 16, 2015 ikaamua kuzindua ndege hizo maalum zinazoweza kupambana na ujangili.
 “Haya ni majaribio ya tatu, tulifanya majaribio mara ya kwanza katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa kutumia ndege maalum aina ya DT 16, lakini hayakuonyesha matokeo mazuri,” anasema Michael Chambers, Mkurugenzi wa Mikakati na Mawasiliano wa Bathawk.
Chambers, ambaye amekuwepo nchini Tanzania kwa takriban miaka 20 sasa, anasema jaribio la pili lilifanyika katika Pori la Selous mwezi Mei 2015 kwa kutumia ndege aina ya DT 26 iliyotengenezwa Ufaransa, lakini iliharibika na haikuweza kutoa matokeo mazuri.
Anaibainisha kwamba, katika kipindi cha siku tano cha majaribio tangu Septemba 11, 2015, ndege hiyo mpya aina ya Super Bat DA-50 UAV iliyotengenezwa na kampuni ya MartinUAV ya Marekani, imeonyesha mafanikio makubwa.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi na muasisi wa kampuni hiyo, Tom Lithgow, anasema baada ya majaribio yao kuonyesha mafanikio, sasa wataandaa ripoti yao na kuiwasilisha kwenye taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) pamoja na kwenye Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ili kama wataridhia, basi waweze kuona namna gani yakuanza utekelezaji kuhakikisha tembo na wanyama wengine wanalindwa.
“Tumefanya kazi kwa ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, hususan Tanapa na Idara ya Wanyamapori, tunaamini baada ya mafanikio haya, nao wataangalia ni kwa namna gani tunaweza kuanza kuitumia,” anasema Tom, Mtanzania ambaye ana uzoefu mkubwa wa mazingira ya porini na utalii kwa ujumla.
Hata hivyo, Mike Chambers anasema, teknolojia hiyo itakuwa ya kwanza kutumia nchini Tanzania katika suala zima la kubaini na kudhibiti ujangili na ni ya gharama nafuu zaidi kwani ndege hizo hazitumii rubani ndani yake, zinatumia mafuta kidogo na kuruka kwa muda mrefu.
“Mbali ya kupambana na ujangili, lakini pia teknolojia hii itasaidia suala zima la uhifadhi kwa kutambua hata idadi ya wanyama waliopo (scouting),” anafafanua Chambers.
Herman van Rooyen na Johnson Makere ni vijana waliohitimu stashahada ya Uhifadhi Wanyamapori katika Chuo cha Wanyamapori cha Mweka mkoani Kilimanjaro, ambao kwa sasa wameelekezwa namna ya kurusha na kuongoza ndege hizo kwa ustadi mkubwa.
Ingawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo maalum na muhimu, lakini wanaielezea teknolojia hiyo kwamba inafaa sana katika suala zima la uhifadhi wanyamapori.
Wanasema, kutokana na tatizo la uhaba wa watumishi na vitendea kazi pamoja na miundombinu duni ndani ya hifadhi na mapori ya akiba, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa ikiwa serikali itaikubali na kuitumia.
“Teknolojia hii inasaidia kuwakamata majangili wakiwa wanafanya uharamia wao ndani ya hifadhi na hivyo kuondoa malalamiko yaliyopo sasa kwamba majangili wanaokamatwa wanakuwa wanasingiziwa,” anasema Makere.
Makere anaongeza: “Hivi sasa utaratibu unaotumiwa ni kama wa mbwa kufuata nyayo na harufu kwani majangili mara nyingi wanakuwa wanakamatwa wakiwa majumbani mwao, lakini hapa watakamatwa humo ndani na hivyo kuukazia ushahidi kwani picha zipo na watakuwa na vidhibiti.”
Kampuni ya Bathawk Recon inajipambanua kwamba kwa kuja na teknolojia hiyo ya utambuzi inaweza kuwa suluhu ya janga la ujangili kwa kuwa inao uwezo wa kutambua majangili hata kama wakijificha, labda kama watachimbia ardhini.
“Na kama watajichimbia basi itakuwa faida zaidi, kwa sababu hawawezi kufanya lolote bila kuonekana,” anaongeza Jones, ambaye kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa rubani wa ndege za kivita kwenye Jeshi la Kifalme (Royal Armed Forces).
Ofisa uhifadhi kutoka Hifadhi ya Tarangire, Marandu, ambaye alimwakilisha Mhifadhi katika uzinduzi huo, anasema anaamini teknolojia hiyo ni nzuri na inaweza kusaidia kuwahifadhi wanyama.
“Katika mapambano dhidi ya ujangili na ustawi wa maliasili, mbinu yoyote yenye kuleta matokeo chanya ni vizuri ikapokelewa na kujaribiwa, kama inafaa basi itakuwa msaada mkubwa kwa taifa,” anasema.
Sera ya Taifa ya Wanyamapori ya mwaka 1998 inaelekeza kuwa aina zote za viumbe hai zihifadhiwe, wanyamapori wasitumiwe kiasi cha kuifanya idadi yao ipungue na kuwa katika hatari ya kutoweka na kuhakikisha Taifa linaendelea kumiliki wanyamapori na kusimamia kwa niaba ya wananchi.

Ndege zilizojaribiwa

DT-18 ilijaribiwa Tarangire

Hii ilitengenezwa Ufaransa. Ni ndogo sana, inaweza kuruka kwa saa mbili tu katika nusu kipenyo cha kilometa 15 kutoka ilipo mitambo.

DT-26 ilijaribiwa Selous

Imetengenezwa Ufaransa na kampuni ya Delair Tech. Hii ni kubwa kidogo, ina uwezo mkubwa na inatumia viwango vya satelaiti za kijeshi vya mawasiliano kutumana kupokeataarifa pamoja na namna ya kuongozwa kwake.

Superbat DA 50 – Imejaribiwa Mkomazi

Imetengenezwa Marekani na kampuni ya MartinUAV. Inaitwa MLB Super-Bat DA-50. Inatumia injini yenye mapigo mawili na uwezo wa 50cc ikiwa na genereta la Watts 75 pamoja na mafuta. Urefu wake ni futi 8.5 x 5.3 x 2.25 inapokuwa imeunganishwa, lakini ikiwa bado haijaungwa ina urefu wa futi 3.5 x 1.25 x 1.5. Kasi yake ni kati ya 40 hadi 70kts, inakaa angani kwa saa 10 mfululizona inaruka kimo cha futi 15,000 hadi 20,000 bila kupoteza mawasiliano.


0656-331974

TUZO ZA SANAA YA UCHORAJI TINGATINGA

September 17, 2015

 Balozi wa China nchini Tanzania Dr. Lu Younq ing akiongea na baadhi ya wasanii wa sanaa ya uchoraji  wa Tingatinga katika hafla ya utoaji wa  Tuzo  la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam. Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China. Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga akiongea  katika hafla ya utoaji wa  Tuzo  la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam.Tuzo hizo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China ambapo washindi wawili wataelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana utamaduni
 Mmoja wa wachoraji  wa sanaa ya Tingatinga akionyesha cheti chake cha ushindi katika hafla ya utoaji wa Tuzo  la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam,wa kwanza aliyekaa kulia ni  Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga.Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China ambapo washindi wawili wataelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana utamaduni.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga akimpongeza mmoja wa washindi wa uchoraji wa Sanaa ya Tingitinga katika utoaji wa Tuzo la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam, Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Prof. Hermas Mwansoko. Tuzo hizo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China ambapo washindi wawili wataelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana utamaduni.
  Balozi wa China nchini Tanzania Dr. Lu Younq ing akimkabidhi mmoja wa washindi wa  uchoraji wa sanaa ya tingatinga katika utoaji wa Tuzo la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam. Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China. ambapo washindi wawili wataelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana utamaduni.
 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni  na Michezo  Prof. Hermas Mwansoko akimkabidhi  mmoja wa washindi wa  uchoraji wa sanaa ya tingatinga katika utoaji wa Tuzo la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam. Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China. ambapo washindi wawili wataelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana utamaduni.
 Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania Bw. Adrian Nyangamale akiongea na  baadhi ya wasanii wa sanaa ya uchoraji  wa Tingatinga katika hafla ya utoaji wa  Tuzo  la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam. Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China. Tuzo hizo zimetolewa kwa  ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China.
Mwenyekiti  wa  Tingatinga Arts Co-operation Society akiongea na  baadhi ya wasanii wa sanaa ya uchoraji  wa Tingatinga katika hafla ya utoaji wa  Tuzo  la Mashindano ya Kimataifa ya Uchoraji wa Tingatinga Tanzania iliyofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam. Tuzo hizo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China. ambapo washindi wawili wataelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana utamaduni. (Picha na Benjamin Sawe- WHVUM)

ARUSHA YAONGOZA MICHUANO YA WAZI TENISI KWA VIJANA.

September 17, 2015

Na Woinde Shizza,Arusha
Jiji la Arusha limeendelea kuwa kinara katika mchezo wa tenisi baada ya wachezaji wake kuibuka kidedea kwa kutwaa ushindi katika umri tofauti tofauti ,mashindano yaliyomalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Arusha Tenisi gymkhana klabu.

Mashindano hayo yalidhaminiwa na Jubilee tyres ikiwa ni mwaka wa tatu sasa, yalishirikisha jumla ya wachezaji 90 ambao 28 kati yao ni wasichana kutoka Dar es salaam gymkhana klabu,Kijitonyama tenisi klabu kutoka Dar es salaam,Morogoro tenisi klabu, ISM –Moshi campus, AICC klabu –Arusha pamoja na Arusha tenis gymkhana klabu.

Katika umri wa miaka 6 kwa wasichana Schaefer Swantje kutoka ISM Moshi campus alifuatiwa na Suhana  Patel kutoka Arusha gymkhana klabu,huku kwa  upande wa wavulana wa umri huo Sahil Shah kutoka ISM moshi campus na kufuatiwa na Yuvraj Sidhu kutoka Arusha gymkhana klabu.

Wasichana walio na umri wa miaka 8 Asha Ali aliibuka mshindi na nafasi ya pili kumwendea Bahati Mdee wachezaji wote kutoka klabu ya AICC na kwa upande wa wavulana mika 8 Johnson Peter alibuka mshindi na kufuatiwa na Yasin Yusuph wote kutoka klabu ya AICC na kwa wasichana walio na umri wa miaka 10 Vanessa Emmanuel kutoka AICC aliibuka kidedea na kufuatiwa na Caroline Mwangata wa ISM Moshi campus, huku kwa wavulana miaka hiyo Rashid Abdallah kutoka Arusha gymkhana klabu na kufuatiwa na Abdumarik Kudra kutoka Morogoro klabu.

Kwa umri wa miaka  12 wasichana Shana Martin aliongoza na kufuatiwa na  Fei Amon wote kutoka Arusha gymkhana klabu na wavulana Damas Felex na nafasi ya pili kumwendea Benjamini Laurance wote kutoka AICC ,Huku kwa umri wa miaka 14 kwa wasichana Jackline Kayuga kutoka kijitonyama Tenisi klabu na nafsi ya pili Anikaa Aggarwal  kutoka Arusha Gymkhana klabu na kwa wavulana wa umri huo Deogratius Felex  na kufuatiwa na Yusufu Laurance wote kutoka AICC.

Jackline Kayuga kutoka  Kijitonyama Tennis klabu alishika nafasi ya kwanzana kufuatiwa Hawa Yahya kutoka Dar es salaam gymkhana klabu katika umri wa miaka 16 kwa  wasichana  na kwa  wavulana Omari Sulle Arusha Gymkhana klabu na kufuatiwa na Hassan Hamisi - AICC Club Arusha.

Kwa upande wa umri wa miaka 18 kwa wasichana hawakuwepo ,na walicheza wavulana pekee ambapo Emmanuel Mallya- Arusha Gymkhana Club alifuatiwa na -  Frank Menard -Arusha Gymkhana Club.

Nicholaus Leringa Kocha mkuu  wa klabu ya AGC alisema kuwa  mashindano hayo hufanyika kila mwaka yakiwa na lengo  la kuwaimarisha vijana katika dhana nzima ya  kunyanyua vipaji vyao.
UGEUGEU NA UPAPARA WA KUPATA FEDHA UNAKWAMISHA VIJANA

UGEUGEU NA UPAPARA WA KUPATA FEDHA UNAKWAMISHA VIJANA

September 17, 2015
_MG_1920
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akiingia katika ukumbi wa mkutano hoteli ya Double Tree by Hilton kwa ajili ya warsha ya vijana na ajira iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Na Mwandishi wetu
VIJANA nchini Tanzania wanatakiwa kujitambua, kuacha kuwa kigeugeu na kufanya papara ya kupata fedha kama wanataka kuendelea na kufanikiwa kibinafsi na kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewea jana na Meneja Ajira za Kifundi kwa vijana na Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga kwenye warsha ya wadau wa kitaifa ya kujadili suala la ajira kwa vijana Tanzania .
Kauli yake hiyo kwa vijana hao waliojumuika katika hoteli ya DoubleTree by Hilton, Dar es salaam, ilitokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika nchini ambazo zinaonesha kwamba vijana wengi hawana msimamo wa maisha, hawana maono, hawana malengo binafsi wala kutambua matarajio.
Amesema: “ Usipojitambua, leo nikija nikakueleza habari za kuanzisha biashara ya matofali utachangamkia. Kesho akija mtu mwingine akakueleza kuhusu uchimbaji wa madini utaacha kutengeneza tofali na kukimbilia machimboni”.
Akizungumza kwa ufasaha kabisa kuhusu vijana na ajira, alisema kila mmoja ana nafasi yake katika kuleta maendeleo yake na taifa na kwamba lazima kujituma na si kubweteka na kulalamika tu.
Akizungumza kwa mfano alimzungumzia kijana mmoja Joseph ambaye alikuwa mwadilifu sana na mwenye kumwamini Mungu. Anasema Kila siku Joseph aliamka asubuhi na kumuomba Mungu amsaidie aondokane na umaskini alionao.
Alifanyakazi hivyo kwa miaka 30 lakini maombi yake hayakumsaidia kuondokana na umaskini.
Siku moja, alisema, Mungu alimuona Joseph akiwa na masikitiko makubwa akamuuliza kulikoni, Joseph akamjibu: “Mungu ni miaka 30 leo tangu nianzie kukuomba uniwezeshe nishinde bahati nasibu. Mimi nimeishi maisha yangu kwa uadilifu nawe wajua . Lakini mbona maombi hayatimii?”
_MG_1976
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akifungua warsha ya vijana na ajira iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC). Kushoto ni Meneja Ajira za Kifundi kwa vijana na Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga na kulia ni Kiongozi Mpango wa Ukuaji na Ajira wa Taasisi wa Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) Dk. Arjan de Haan.
Naye Mungu akatabsamu akamwambia, Joseph, si ununue tiketi basi?
Dk Kiaga alisema kwa kuzingatia hadithi yake kila mmoja anatakiwa kufanya kitu na Joseph alisahau kwamba huwezi kushinda bahati nasibu bila kununua tiketi.
“Kumbuka haitoshi kuwa na elimu na ujuzi kama hutaweza kuweka elimu hiyo au ujuzi ulionao katika vitendo” alisema na kuongeza kuwa Joseph alikuwa anajua anahaitaji fedha ya kianzio lakini hakuchukua hatua ya kupata hela hiyo.
Alisema pamoja na ukweli kuwa asilimia 40 ya watu wasio na ajira duniani ni vijana, kwa maana ya kwamba kuna vijana wapatao milioni 75 duniani kote wanatafuta ajira huku vijana wa kike wakiwa na changamoto kubwa zaidi, ipo shida kubwa ya vijana kukata tamaa.
Aidha alisema kwamba hali ya kukata tamaa imewapeleka vijana kuongezeka katika soko la vijana wanaopata kazi zisizo na staha.
Alisema pamoja na sera zilizopo vijana wanatakiwa kuwa na shauku na kazi na pia kujitambua.
“Vijana wa siku hizi hawana mitazamo sahihi kuhusu ajira. Kwamba vijana hawana shauku na kazi na wana mitazamo hasi (ili mradi kazi..mkono uende kinywani?) . Matokeo yake ni kwamba vijana hawatumii ubunifu wowote katika kuboresha uwezekano wao wa kupata kazi zenye staha” alisema.
Amesema mtaji unahitaji kujiboreshea seti ya ujuzi katika kutafuta kazi ikiwa ni pamoja na uwezo, uzoefu na elimu.
_MG_2014
Meneja Ajira za Kifundi kwa vijana na Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga akizungumza kwenye warsha ya vijana na ajira iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Alisisitiza kuwa vijana waliowengi hawajitambui na kujiuliza ‘mimi ni nani’ au hawana malengo binafsi na matarajio mimi nataka kuwa nani na kusema bila kuyafanyia kazi mambo hayo mawili ya shauku ya kazi na kujitambua hakutakuwepo na mabadiliko.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Tausi Kida, akifungua warsha hiyo alisema pamoja na taifa kuwa mstari wa mbele kushughulikia ajira kwa vijana kwa kutunga sera zilizolenga kukidhi haja ya ajira,ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 na na mpango wa utekelezaji wa sera ya taifa ya ajira kwa vijana iliyo chini ya mtandao wa ajira unaofadhiliwa na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, changamoto bado zipo.
Aliwataka washiriki wa warsha hiyo wakiwemo vijana waliofanikiwa kueleza siri za fursa na kujiajiri ili kutoa mwanga kwa wenzao.
Pamoja na warsha hiyo kutoa nafasi kwa vijana kujadili namna ya kutambua na kutumia fursa za kuichumi zilizopo nchini, kutoa ujuzi kwa vijana wa namna ya kuingia katika soko la ajira ikiwa ni pamoja na kujiajiri, kukuza ujasiriamali na kuendeleza biashara, Dk Kida aliwasihi vijana kujitafutia riziki yake na kushiriki ipasavyo katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.
Aliwataka kujijengea uwezo wa kufanyakazi pamoja na kubaini na kuzitumia fursa za kiuchumi na kibiashara zilizopo nchini.
Warsha hiyo iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) ilikutanisha vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania na kuwezeshwa kwa sehemu kubwa na Taasisi ya tamasha ambapo Mkurugenzi wake Mtendaji Richard Mabala alikuwa Mchokozaji mkuu.
Akiwasilisha salamu kutoka IDRC, kiongozi Mpango wa ukuaji na ajira wa taasisi hiyo. Dk Arjan de Haan alisema kwamba taasisi hiyo ya serikali ya Canada imekuwa ikitoa ushirikiano katika tafiti zilizolenga kuangalia utatuaji wa tatizo la ajira kwa namna inavyofaa.
_MG_2200
Mtafiti Mwandamizi ESRF, Dk. Georgina Ole Saibul akiwasilisha mada katika semina ya vijana na ajira.
Alisema kwamba kwa kawaida taasisi yake husaidia pale inapoona utafutaji wa mbinu za kutatua tatizo unashirikisha na wahusika ili kupata suluhu endelevu ya tatizo husika.
Alisema ameridhishwa na kuona kwamba warsha hiyo imezingatia kanuni za IDRC za kutaka kutatua tatizo la ajira kwa kushirikisha vijana wenyewe, kuangalia na kushauri namna bora ya kukabili tatizo la ajira ambao kwa sasa ni changamoto kubwa duniani.
Alisema kwamba ipo haja ya kubadili baadhi ya sera kulingana na mahitaji ya sasa ili kuwezesha vijana wengi zaidi kuingia katika soko la ajira.
Wakati wa utambulisho na kuelezea kero zao katika ajira wengi wa vijana waligusia kuwapo kwa sera ambazo si rafiki zinazotengeneza urasimu mkubwa katika kusaidiwa.
Ingawa wengi walisema fursa zipo, walizungumzia kutopata ushirikiano kutoka kwa wazazi , viongozi na taasisi mbalimbali zinazodai kupambana na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Aidha vijana wengine walisema kwamba ni kweli kuna mtazamo hasi kwa vijana hasa kukata tamaa na pia kutaka maendeleo ya kasi huku wakikosa ubunifu.
Joachim Fanuel kutoka singida Youth Entrepreneurs and Consultants Cooperative Society (SYECLOS) alisema kwamba ingawa wao wanaendesha miradi ya kuku wa kienyeji na asali kama fursa zilizopo wanakabiliwa na tatizo la kukata tamaa kutokana na kuona kwamba inachukua muda mrefu kupata vitu wanavyotaka.
Aidha alisema kwamba wamekuwa hawasikilizwi na serikali na taasisi mbalimbali kwa kuwa hawana mali za kuwakilisha kama dhamana katika mambo mbalimbali.
 
_MG_2213
Johari A. Sadik kutoka kampuni inayotengeneza nguo za kitamaduni Binti Africa, akitoa ushuhuda kwamba vijana wanaweza kama watajitambua katika warsha ya siku mbili vijana na ajira inayofanyika hoteli ya DoubleTree by Hilton.
Kijana Musa Mohammed kutoka Zanzibar alisema kwamba japo wana fursa za usindikaji wa vyakula, mizizi na matunda wamekuwa na tatizo la ujuzi katika uchakataji, sera duni zisizojibu mahitaji yao na kuwalinda katika soko.
Binti mmoja kutoka Binti Africa Kampuni inayotengeneza nguo za kitamaduni alisema kwamba kuna shida ya kukata tamaa miongoni mwa vijana lakini pia hawajali kutafuta taarifa wanazohitaji wakisubiri kutafuniwa.
Vijana wengine walizungumzia ugumu wa mitaji, ukosefu wa taaluma na mfumo wa elimu kwuatengeneza kupata ajira katika serikali na taasisi zake.
Mshiriki Leticia Mango kutoka Kigoma alisema kwamba ipo shida ya vijana wenye vipaji ambao hawana elimu vijijini kudharaulika na kutothaminiwa kwa kile kinachoonekana sio wasomi.
Alisema vijana wasomi wakiunganika na wenye vipaji wanaweza kuwa mbali zaidi na kusisitiza ipo haja vijana kuwa pamoja kwa maendeleo yao.
_MG_2221
Joachim Fanuel kutoka Singida Youth Entrepreneurs and Consultants Cooperative Society (SYECCOS) akionesha chupa ya asali kutoka kwa mradi wa kikundi cha vijana ambao waliamua kujiajiri katika warsha ya vijana na ajira.
_MG_2220
Joachim Fanuel kutoka Singida Youth Entrepreneurs and Consultants Cooperative Society (SYECCOS) akizungumza na washiriki wa warsha ya vijana na ajira.
_MG_2178
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida (kushoto) akiwa na Kiongozi Mpango wa Ukuaji na Ajira wa Taasisi wa Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC), Dk. Arjan de Haan wakiwa katika warsha ya vijana na ajira.
_MG_2226
Vijana wakishiriki kazi za vikundi kwenye warsha hiyo.
_MG_2229
_MG_2138
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akiwa katika picha ya pamoja na vijana walioshiriki warsha ya vijana na ajira hoteli ya Double Tree by Hilton jijini Dar.

HIVI NDIVYO MAGUFULI ALIVYOITEKA KIGOMA UWANJA WA KAWAWA

September 17, 2015

-- Ahmad Issa Michuzi Editorial Director P.O BOX 9033, DAR ES SALAAM. issamichuzi.blogspot.com www.michuzijr.blogspot.com othmanmichuzi.blogspot.com Phone:0713 422 313/ 0783 422 313 Tanzania- East Africa.