WADAU WAPONGEZA MIF KWA KUSAIDIA MTOTO WA KIKE ZANZIBAR, WAJITOKEZA KUCHANGIA

June 18, 2022

 


Na John Mapepele. 

Wadau mbalimbali wa kupigania maendeleo ya mtoto wa kike nchini wamejitokeza  kuchangia takribani  shilingi  bilioni moja  kwenye  taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) iliyopo Zanzibar inayojishughulisha na kumkwamua mtoto wa kike katika elimu ili kutimiza ndoto zake. 

 Wadau hao wametoa michango  hiyo katika  halfa maalum ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na taasisi ya (MIF) usiku wa kuamkia leo Juni 19, 2022 Zanzibar  kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na mfuko huo  katika suala zima la  kuwasaidia Watoto wa kike kufikia malengo  yao hivyo kuendesha maisha yao.


Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Mhe. Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na mtetezi wa haki  za vijana na wanawake amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea  kuchangia ili kuwasaidia Watoto wa kike  waweze kutimiza ndoto zao.


 “Naomba kuchukua  fursa hii kushukuru sana isiwe mwanzo wala mwisho naomba iwe mwanzo na tuendelee kuchangia  mfuko wetu wa Mwanamke Initiative ili kuona kwamba mtoto wa kike anasimama  na anaweza kushindana katika ulimwengu” amefafanua,  Mhe Wanu.


Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti tofauti kuhusu kuanzishwa kwa mfuko huo, wamepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na MIF kwa kuwasaidia watoto wa kike Zanzibar huku wakitoa rai kwa wadau wengi zaidi  kushiriki kwenye jitihada hizo za kuwakomboa Watoto wa kike kwa kuchangia kwa hali na mali katika mfuko huo ili lengo liweze kutimia. 


“Tumefarijika sana na kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na mfuko huu, tunaomba na wadau wengine waendelee kujitokeza kuchangia kwa  kuwa ukimsaidia mtoto wa kike aweze kujikwamua umesaidia taifa”aliongeza Tuli Mwambapa ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya CRDB nchini.

Benki ya CRDB imechangia shilingi milioni mia tatu ambapo wadau wengine pia waliweza kuchangia kwenye hafla hiyo.

Katika hafla hiyo mbali na wageni mbalimbali waliohudhuria   pia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ambaye ni mume wa Wanu alishiriki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan. leo,  Juni 19, 2022 anatarajiwa kuuzindua rasmi mfuko huo.

WAZIRI MCHENGERWA AIPONGEZA TIMU YA KRIKETI KUTWAA UBINGWA RWANDA, AMSHUKURU RAIS SAMIA

June 18, 2022

 

 

Na John Mapepele


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa pongezi kwa  Timu ya Tanzania ya  Wanawake ya Kriketi kwa  kutwaa Ubingwa leo Juni 18, 2022 kwenye mashindano ya Kwibuka Cup nchini Rwanda, yaliyoshirikisha nchi nane ( Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Botswana , Nigeria, Brazil na Ujerumani) bila kufungwa na timu yoyote. 

Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa anaoutoa katika michezo.

Amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha michezo kwa kuweka mikakati  kabambe chini ya uongozi wa Samia imeleta matokeo chanya kwenye sekta za michezo na sanaa hapa nchini.

Amesema taarifa ya hali ya uchumi wa nchi iliyosomwa bungeni hivi karibuni imeonesha kuwa sanaa na burudani zimechangia kwa asilimia 19.4 katika kipindi cha mwaka 2021 na kuziacha kwa  mbali sekta mbalimbali.

Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuifanya michezo kuwa uchumi badala mazoe ya kuifanya michezo kama  kitu cha burudani pekee.

Aidha, amesema Serikali tayari inazigharimia timu zote za taifa zinazojiandaa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kwa kuziweka kambini kuanzia mwanzo wa mwaka huu.

Hivi karibuni Mhe. Mchengerwa amekaririwa vyombo vya habari akisisitiza kuwa michezo na sanaa ni uchumi  hivyo wanamichezo na wasanii wanapaswa kutambua kuwa vipaji walivyonavyo ni mtaji wa maisha yao.

Ujumbe wa Klabu ya Southampton uliokutana na Mhe. Waziri Mchengerwa na kufanya mazungumzo ya kuinua michezo ulioongozwa na Mkuu wa Idara ya Biashara ya klabu hiyo David Thomas pia ulimpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye michezo na kumzawadia jezi ambayo ilipokelewa kwa niaba yake na Mhe. Mchengerwa.

UWEKEZAJI MKUBWA KUFANYWA NA SERIKALI KATIKA SEKTA YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI– MNDOLWA

June 18, 2022

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa akiongea na waandishi wa Habari baada ya mkutano na watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wahandisi wa Umwagiliaji wa Mikoa, uliofanyika Jijini Dodoma mapema leo.

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa na Baadhi ya watumishi wa Tume hiyo pamoja na wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa



Baadhi ya watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakifuatilia kikao kilichofanyika jijini Dodoma mapema leo.






Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa amesema, kutakuwa na kilimo cha umwagiliaji cha uhakika kutokana na uwekezaji mkubwa wakihistoria unaofanywa na serikali ya awamu ya sita katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji.

Bw,Mndolwa ameyasema hayo mbele ya Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dodoma mara baada ya kufungua kikao kazi kilichowahusisha watumishi wote wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kuongeza kuwa, kutokana na majukumu makubwa iliyopewa na serikali Tume ya Taifa ya Umwagiliaji “niliona ni muhimu sana tukutane watumishi wote ili tujipange,tuweze kutekeleza majukumu hayo”.

“Tume tuna juku la kuwasaidia wakulima waweze kulima kutokana na kilimo wanacholima ili waweze kupata maji katika mazao wanayolima hili ni sehemu ya majukumu yetu, kutokana na hali yakuwa na upungufu wa mvua serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kilimo cha umwagiliaji kwa matarajio yajayo”.

Tunataka Wananchi na Wakulima waliokata tamaa ya kulima warudi shambani, kwasababu tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewezeshwa na inakuja kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo cha Umwagiliaji.

Akizungumzia suala la Bajeti kubwa iliyoelekezwa na Serikali ya awamu ya sita katika Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, Mkurugenzi Mndolwa ameongeza kusema kuwa, Tume imeelekeza nguvu katika miradi iliyokwisha buniwa na miradi hiyo ndiyo ya kipaumbele, baada ya miradi hiyo ya mwaka huu hatua itakayofuata ni kujenga miradi mingine ya umwagiliaji nchini katika maana ya mikoa yote itakayotekeleza kilimo cha umwagiliaji na aina gani ya miradi ifanyike katika kuhakikisha kila Mkoa na Wilaya inapata miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji.

Alisema wana panga upya kuhakikisha kwamba mwaka wa fedha unaofuata yaani 23/24 watakuwa na mkakati ambao utaenea nchinzima.

Mwaka wa fedha huu 22/23 watarekebisha Skimu thelathini (30) za kilimo cha umwagiliaji lakini Wahandisi wa umwagiliaji wa mikoa watafanya mapitio ya miradi iliyokwisha kwa lengo la maboresho kulinga na na bajeti yetu.

“Nina ahidi kwamba maboresho yatakuwa makubwa ili kila mwananchi anayetaka kulima aweze kulima.”Alisisita Kikao cha leo ni majumuisho ya siku yapili ya kikao kilichohusisha watumishiwa Tume Makao makuu na Wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa kilichojadili, Mpango mkakati wa miaka mitano wa utekelezaji wa shughuli zaTume.