TRA YAJIZATITI KUONGEZA IDADI YA WALIPAKODI

January 04, 2018



Na: Veronica Kazimoto, 04 Januari, 2018, 
Dar es Salaam. 

Mwaka huu wa fedha wa 2017/18, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imedhamiria kuongeza idadi ya walipakodi kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu kupunguza kutegemea misaada kutoka kwa wahisani. 

Lengo kuu la kuongeza walipakodi ni kupanua wigo na kuongeza makusanyo ambayo hutumika katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi wa nchi. 

TRA ina mikakati mbalimbali ambayo imechukuliwa na inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa, walipakodi wanaongezeka na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. 

Mikakati hiyo ni pamoja na kusajili walipakodi ambapo Mamlaka imezindua kampeni ya usajili wa walipakodi nchi nzima ili kuhakikisha kwamba kila mfanyabiashara anasajiliwa na kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi  (TIN) kwa urahisi na haraka. 

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Kamishna wa Kodi za Ndani Elijah Mwandumbya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania alisema, usajili wa walipakodi ni chanzo cha kuongeza idadi ya walipakodi na mapato kwa ujumla. 

"Moja ya majukumu ya msingi ya TRA ni Usajili wa Walipakodi ambao huongeza idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi, makusanyo pamoja na kutoa taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa na kutozwa kodi ili kuchangia Pato la Taifa", Alisema Mwandumbya. 

Mwandumbya alisisitiza kuwa, walipakodi wadogo wanaostahili kulipa kodi kwa njia ya makadirio, watalipa robo ya kwanza ndani ya siku tisini (90) kuanzia waliposajiliwa tofauti na utaratibu uliokuwepo kwa kulipa kodi hiyo hata kabla mfanyabishara hajaanza kufanya biashara husika. 

"Wananchi wanaostahili kusajiliwa kama walipakodi ni watu wote wanaotarajia kuanzisha biashara, kumiliki vyombo vya usafiri kama vile gari na pikipiki, wanaostahili kulipa kodi ya majengo, wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi na wanaotarajia kupata leseni za udereva", alifafanua Mwandumbya. 

Aidha, Mwandumbya aliyataja mahitaji ya usajili kuwa ni Mkataba wa pango au uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua ya mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ikiwa na muhuri na namba ya simu ya mwenyekiti wa mtaa husika, kitambulisho cha mhusika kama vile hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura na mhusika ni lazima aende mwenyewe kwenye ofisi za TRA kwa ajili ya kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole. 

Kamishna Mwandumbya, amewatahadharisha wananchi kuwa makini na vishoka kwa kuwa usajili huo hufanyika bila malipo na hufanyika katika ofisi za TRA na katika vituo maalum ambapo wananchi watatangaziwa kupitia vyombo vya habari na kwenye maeneo husika. 

"Napenda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi wote wanaostahili kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi kuwa makini na vishoka wanaoweza kutumia mwanya huo na kuharibu nia njema ya kampeni hii kwasababu hakuna wakala yeyote aliyepewa jukumu la kusajili au hata kutoa fomu ya usajili", ametahadharisha Mwandumbya. 

Elijah Mwandumbya amesema endapo mtu atapata changamoto yoyote katika kusajili na kupata namba ya mlipakodi anashauriwa kuwasiliana na Ofisi ya TRA iliyopo karibu au kupiga simu bure katika Kituo cha Huduma kwa namba 0800 750075 au 0800 780078 au kutuma barua pepe huduma@tra.go.tz au services@tra.go.tz. 

Hatua nyingine ni uwepo wa mifumo mbalimbali ya kielektroniki ya kusajili walipakodi ambayo imerahisisha ulipaji kodi na hivyo kuongeza ulipaji kodi kwa hiari. 

Mifumo hii imepunguza muda wa usajili ambapo kabla ya kutumia mifumo hii ya kielektroniki kazi ya kusajili walipakodi mpaka kukamilika ilikuwa inachukua takribani siku 7 lakini baada ya kuanza kutumia mifumo hii, usajili hufanyika ndani ya dakika 30 tu. 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ndugu Richard Kayombo akizungumza ofisini kwake alisema TRA imejiwekea lengo la kusajili walipakodi wakubwa, wa kati na wadogo wapatao milioni moja (1,000,000) kwa mwaka huu wa fedha 2017/18. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya walipakodi na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. 

Kayombo alisema kuwa, mamlaka ina mpango wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanakuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kuongeza ufanisi wa zoezi la usajili kwa kutumia Mfumo wa Vitalu - Block Management System ambao utawezesha kutambua walipakodi wanaostahili kusajiliwa na kulipa kodi. 

Aidha, ameongeza kwamba, mamlaka ina mkakati wa kuongeza idadi ya walipakodi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Halmashauri au Manispaa mbalimbali ili kuhakikisha kila mfanyabiashara katika maeneo hayo anakuwa na namba ya TIN. Namba hii husaidia kumtambua kila mfanyabiashara mahali anapofanyia biashara yake na kiasi cha kodi anachotakiwa kulipa. 

"Kama mamlaka, tuna mpango wa kuwarahisishia wafanyabiashara muda wa kufanya usajili kwa kupeleka vifaa vya usajili karibu na mahali wanapofanyia biashara kwa ajili ya kuokoa muda wanaoutumia kwenda kwenye ofisi zetu kufanya usajili", amesema Kayombo. 

Kupitia mkakati huu, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania itaweza kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara waliopo kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwapatia Kadi ya Utambulisho. Wafanyabiashara hao ni kama vile wenye maduka ya reja reja hasa wenye ma fremu, wamachinga, washereheshaji, wachimbaji wadogo wa madini n.k. 

Uwepo wa idara cha Huduma na Elimu kwa Walipakodi kilichopo ndani ya Mamlaka, ni hatua nyingine ya kuongeza idadi ya walipakodi ambapo idara hi inajishughulisha na kutoa elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi, kujibu hoja mbalimbali pamoja na kuwakumbusha walipakodi kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati muafaka kupitia ujumbe mfupi wa maneno. 




Mikakati na hatua zote zilizobainishwa hapo juu zitaongeza idadi ya walipakodi, uhiari wa kulipa kodi na mapato ya Serikali kwa ujumla.

TPA YANUNUA VIFAA VYA KISASA BANDARI YA MTWARA

January 04, 2018
 Mkuu wa bandari ya Mtwara, Nelson Mlali (Kulia) akitoa maelezo kwa Wakurugenzi wa Bodi wa TPA wa Kamati za TEHAMA na Utekelezaji pamoja na ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara mara baada ya wajumbe wa kamati hizo kufanya ziara ya kikazi bandari ya Mtwara hivi karibuni.
Mkuu wa bandari ya Mtwara, Nelson Mlali (Kulia) akitoa maelezo kwa Wakurugenzi wa Bodi wa TPA wa Kamati za TEHAMA na Utekelezaji pamoja na ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara mara baada ya wajumbe wa kamati hizo kufanya ziara ya kikazi bandari ya Mtwara hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imenunua vitendea kazi vipya na vya kisasa kwa ajili ya bandari ya Mtwara ili kuongeza ufanisi.
Vifaa hivyo ambavyo tayari baadhi vimeshawasili bandarini hapo ni pamoja na mzani wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 ambao tayari unatumika.
Vifaa vingine vilivyonunuliwa na vinavyotarajiwa kuwasili kuanzia mwezi Januari, 2018 ni pamoja na ‘Reach Stalker’ mbili mpya zenye uwezo wa kubeba tani 40 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko ameyasema hayo wakati wa majumuisho ya ziara za Kamati za Bodi za Wakurugenzi wa TPA zinazoshughulikia TEHAMA na Utelekezaji na ile ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara.
Wakurugenzi wa Bodi za Kamati hizo ambazo ziliongozwa na Mwenyekiti, Dkt. Jabiri K. Bakari, ni pamoja na Jayne K. Nyimbo, Renatus Mkinga, Aziz M. Kilonge na Jaffer S. Machano.
Kamati hizo zilitembelea miradi mbalimbali iliyopo Bandari za Mtwara na Lindi na kutoa maelekezo kadhaa ambayo ni muhimu katika kuendeleza bandari hizo ili kuongeza huduma zake.
Akizungumzia vifaa vipya vilivyowasili na vinavyotarajiwa kuwasili hivi karibuni, Mhandisi Kakoko amesema ununuzi wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa mipango ya kuifanya bandari hiyo kuwa ya kisasa zaidi.
“Ununuzi wa vifaa tunaofanya sasahivi utasaidia kuboresha na kuimarisha zaidi utendaji kazi wa bandari ya Mtwara na kuongeza ufanisi zaidi,” amesema Mhandisi Kakoko.
Mhandisi Kakoko ameongeza kwamba vifaa vingine ambavyo mchakato wa manunuzi umeshafanyika ni pamoja na mzani mwingine wa pili wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 pia.
Amevitaja vifaa vingine kuwa ni pamoja na boti maalum za kuhudumia mafuta ‘Mooring Boat’ moja na boti moja ya ulinzi ‘Pilot Boat’.
Mbali ya vifaa hivyo, bandari ya Mtwara pia itapokea ‘Terminal Tractors’ 9 - matrekta maalumu yanayovuta ‘matrela’ yaliyopakiwa kontena au makontena yakiwa bandarini.
Bandari ya Mtwara pia inatarajia kupokea mashine maalum ya kubebea makontena ‘Empty Container Handler’, folklift mbili moja ya tani 16 na nyingine tani 20 pamoja na ‘Automatic Glab moja ya tani 15. 
Kama sehemu ya ziara hiyo, Mhandisi Kakoko pia alifanya kikao na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mtwara na kuwaagiza kukutana na Mawakala wa Forodha wa Mtwara ili kuwaelimisha umuhimu wa kutoa mizigo ya wateja kwa wakati.
Awali akitoa maelezo kwa Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi wa TPA inayoshughulikia TEHAMA na Utelekezaji, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA (Miundombinu) Mhandisi Karim Mattaka amesema vifaa hivyo vitawasili bandari ya Mtwara kuanzia mwezi ujao.
“Tunatarajia kuanza kuwasili kwa vifaa hivyo hapa Mtwara kuanzia mwezi ujao (Januari, 2018) ili kuharakisha mpango kazi wetu wa kubadili bandari hii,” amesema.
Naye Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nelson Mlali amesema kwamba kuna ongezeko la mizigo la wastani wa asilimia 16.5 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
“Katika mwaka 2016/2017, Bandari ya Mtwara imehudumia wastani wa tani 377,590 za mizigo ambazo ni sawa na asilimia 93 ya uwezo wa bandari, ambapo uwezo wake ni kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka” amesema.
Bw. Mlali amesema kwamba ongezeko hilo limechangiwa zaidi na ongezeko la uzalishaji wa Korosho ambalo ndilo zao kuu la biashara kwa mikoa ya kusini.
Amesema kwamba zao la Korosho ambalo hulimwa zaidi na wakazi wa mikoa ya kusini hupitishwa katika bandari ya Mtwara na kusafirishwa moja kwa moja kwenda nchi za Vietnam na India.
Kwa mwaka huu pekee bandari ya Mtwara ambayo ina uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu hadi wa mita 211 imefanikiwa kusafirisha wastani wa tani 160,000 za Korosho hadi kufikia Disemba, 2017.
Mkuu huyo wa bandari ya Mtwara amepongeza juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kuagiza Korosho zote zisafirishwe kupitia bandari ya Mtwara.
Mbali ya Korosho bandari ya Mtwara pia uhudumia shehena nyingine za mizigo kama vile, saruji, vifaa mbalimbali na mafuta.

MBUNGE WA LUSHOTO AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA KUSAIDIA SEKTA YA AFYA JIMBONI KWAKE

January 04, 2018
Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika Kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola wilayani Lushoto ambapo pamoja na kusikiliza kero zao aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuijali kata hiyo kwa kupeleka fedha milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya cha Kisasa katika Kata ya Mlola ambapo kati ya hizo milioni 300 kwa ajili ya kununulia vifaa wakati kituo hicho kitakapomalika huku milioni 400 zikiwa tayari wameingiziwa tayari kwa ajili ya ujenzi huo
 Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika Kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola wilayani Lushoto ambapo pamoja na kusikiliza kero zao aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuijali kata hiyo kwa kupeleka fedha milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya cha Kisasa katika Kata ya Mlola ambapo kati ya hizo milioni 300 kwa ajili ya kununulia vifaa wakati kituo hicho kitakapomalika huku milioni 400 zikiwa tayari wameingiziwa tayari kwa ajili ya ujenzi huo
Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia akizungumza katika mkutano wa hadhara kushoto ni Diwani wa Kata ya Mlola
Diwani wa Kata ya Mlola (CCM) akizungumza katika mkutano huo kabla ya kumkaribisha mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia aliyekaa kulia
Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia aliyekaa kulia akiwa na diwani wa Kata ya Mlola wakifuatilia kwa umakini maswali ya wananchi katika mkutano huo wa hadhara
Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia aliyekaa kulia akiandika baadhi ya kero alizoelezwa na wananchi hao ili kuweza kuona namna ya kuzipatia ufumbuzi.
 Sehemu ya wananchi wakimsikiliza Mbunge wao
 Mkazi wa Kijiji hicho Kata ya Mlola wilayani Lushoto akimuuliza swali Mbunge huyo

 Mmoja kati ya wakazi wa Kijiji hicho akimuuliza Mbunge huyo swali kuhusu kuwasaidia vijana na ajira za mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga
 Mkazi wa Kijiji hicho akimuuliza swali Mbunge wa Jimbo hilo
 Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia katikati akiagana na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kata ya Mlola wilayani Lushoto,Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi,Elmerick Joseph mara baada ya kumalia mkutano wa hadhara katikati ni diwani wa kata hiyo
 Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia akisalimiana na wakina mama wa Kijiji hicho mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara

 Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia kushoto akimsikiliza kwa umakini Mwenyekiti wa CCM kata ya Mlola
 Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia katikati akiwasilikiliza wananchi wa Kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara
Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia akiteta jambo na wananchi wa Kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola wilayani Lushoto mara baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara

Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia wa pili kutoka kushoto akimuelza jambo diwani wa kata ya Mlola (CCM) mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo uliofanyika makao makuu ya Kijiji cha Lwandai Kaya hiyo

WAZIRI MPANGO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA GAVANA MTEULE WA BoT

January 04, 2018

Gavana mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, akisaini kitabu cha wageni alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwa katika mazungumzo na Gavana mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)


RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AKUTANA NA MJUMBE MAALUM WA RAIS WA UGANDA YOWERI MUSEVENI, WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA UGANDA SAM KUTESA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

January 04, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mjumbe maalum wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Mjumbe maalum wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Ujumbe Maalum uliotoka kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na kuwasilishwa kwake na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiufungua na kuusoma Ujumbe huo maalum uliotoka kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na kuwasilishwa kwake na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mjumbe maalum wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam

Mjumbe maalum wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje kwa upande wa Tanzania Balozi Dkt. Augustine Mahiga Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU