Watumishi wa Serikali Mkoa wa Tanga kuchuana katika bonanza kesho Jumamosi.

Watumishi wa Serikali Mkoa wa Tanga kuchuana katika bonanza kesho Jumamosi.

April 19, 2013

Na Burhan Yakub,Tanga.

WATUMISHI wa serikali kutoka idara mbalimbali mkoani hapa kesho jumamosi watachuana katika michezo mbalimbali ikiwamo ya soka na netiboli katika bonanza litakalofanyika uwanja wa shule ya Sekondari
ya Tanga Ufundi.

Mkufunzi wa michezo mkoa wa Tanga,Daniel Mabena alisema jana kuwa bonanza hilo litaratibiwa na Afisa Michezo mkoani hapa, Digna Tesha na kufanyika asubuhi ambapo pia wadau wengine wa michezo wanaruhusiwa
kushiriki.

Alisema michezo itakayochezwa katika bonanza hilo kuwa ni riadha,mazoezi ya viungo,kuvuta kamba,netiboli,soka ambapo watacheza wanawake na wanaume.

Mkufunzi huyo pia alisema katika bonanza hilo kutakuwa na semina fupi juu ya umuhimu wa michezo kwa afya ambayo mafunzo yatatolewa na wataalamu kutoka idara ya afya mkoa wa Tanga.

MWISHO

LIGI YA MABINGWA WA MIKOA KUANZA MEI 12

LIGI YA MABINGWA WA MIKOA KUANZA MEI 12

April 19, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
 
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kutafuta timu tatu zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza(FDL) msimu ujao chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaanza Mei 12 mwaka huu.

 Mwisho wa mikoa kuwasilisha majina ya mabingwa wao ni Mei 1 mwaka huu wakati ratiba ya ligi hiyo itapangwa mbele ya waandishi wa habari Mei 3 mwaka huu kwenye ofisi za TFF.

Uwasilishaji wa jina la bingwa wa mkoa unatakiwa kufanyika pamoja na ulipaji ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000. Mfumo wa ligi hiyo ni bingwa wa mkoa X kucheza na bingwa wa mkoa Y nyumbani na ugenini ambapo mshindi ndiye anayesonga mbele katika hatua inayofuata.

Usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika hatua ya mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.

Mwisho.
 
KILA LA KHERI AZAM FC

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam FC katika mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayochezwa kesho (Aprili 20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Azam FC ina fursa nzuri ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Emile Fred kutoka Shelisheli kutokana na maandalizi iliyofanya, lakini vilevile tunatoa mwito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono.

Makocha wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat wamezungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi hiyo, kuwa wamejiandaa kuibuka na ushindi.

Kocha Ongala amesema wamepata DVD za mechi tatu za mwisho za AS FAR Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al Nasir ya Libya ambayo waliitoa katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na nyingine mbili za ligi ya Morocco ambazo wanazifanyia kazi kuhakikisha wanashinda kesho.

Naye Ouadani amesema hawaifahamu vizuri Azam, lakini wanaujua mpira wa Tanzania baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na Stars kushinda mabao 3-1.

Baadhi ya wachezaji ambao Azam inatarajia kuwatumia kwenye mechi ya kesho ni pamoja na Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars kilicho chini ya kocha Kim Poulsen.

AS FAR Rabat ina wachezaji sita kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji hao ni mabeki Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.

Mwisho.

Mh.Diwani nami napanda miti.

April 19, 2013
Mh.Diwani akishiriki kwenye upandaji wa miti kwenye uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na wananchi pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi wilayani hapa,Picha na Mwandishi Wetu,Mkinga.

TUNAPANDA MITI

April 19, 2013
Afisa Tarafa  ya Mkinga, Qegen Mkinga akishiriki kwenye uzinduzi wa upandaji miti ambapo jumla ya miti 100 ilipandwa kwenye kata ya Duga Maforoni wilayani Mkinga,Picha na Mwandishi wetu.

PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI YA UPANDAJI MITI LEO KATA YA DUGA MAFORONI MKINGA

April 19, 2013

TUPO MAKINI KUKUSIKILIZA

April 19, 2013
WANAFUNZI pamoja na wanafunzi wa shule za msingi wilayani Mkinga wakimsikiliza Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo leo.

UZINDUZI SIKU YA UPANDAJI MITI MKINGA LEO

April 19, 2013
Afisa Tarafa ya Mkinga, Qegen Mkinga ambaye alimuwakilisha Mkuu wa wilaya ya Mkinga,Mboni Mgaza akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya upandaji miti wilayani humo ambapo kiwilaya ilizinduliwa kata ya Duga maforoni,Picha na Mwandishi wetu
DC MGAZA aagiza viongozi wa vijiji na kata kuendelea kuhimiza upandaji miti kwenye maeneo yao.

DC MGAZA aagiza viongozi wa vijiji na kata kuendelea kuhimiza upandaji miti kwenye maeneo yao.

April 19, 2013
Na Oscar Assenga, Mkinga.

MKUU wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgazi amewaagiza viongozi wa vijiji na kata kuendelea kuwahimiza wananchi kupanda miti kwenye maeneo yao na kuhakikisha wanaitunza ili iweze
kukua na kutumika kw malengo yanayotarajiwa.

Agizo la Mkuu wa wilaya alilitoa leo wakati wa uzinduzi wa wiki ya kupanda miti kiwilaya iliyofanyika kwenye kata ya Duga Maforoni wilayani humo katika hotuba yake ambayo ilisomwa na Afisa Tarafa  ya Mkinga, Qegen Mkinga ambapo amesema wiki hiyo ya kupanda miti ililengwa makusudi ya kuwahimiza wananchi kushiriki katika mchakato huo wa upandaji na kutunza mazingira katika maeneo yao.

Mgaza amesema mabadiliko mbalimbali ya tabia ya nchini ambayo yanachangiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji miti usiozingatiwa urushiaji huleta madhara mbalimbali ikiwemo kupata mvua zisizo za uhakika, ongezeko la joto duniani na upungufu wa rasilimali zinazotokana na miti pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji.

Amesema licha ya kuleta madhara hayo huchangia pia ongezeko la magonjwa ya mlipuko pamoja na kuongezeka kina cha bahari hivyo kuwataka wananchi kutoruhusu ukataji wa miti ovyo kwenye maeneo yao kwani athari watakazo kumbana nazo ni kubwa kuliko wanavyodhani.

Aidha amesema kutokana na upungufu wa miti ya asili jamii imehamishia matumizi kwenye miti ya matunda kama vile mikorosho, miembe, minazi na mifenesi ambayo sasa inapasuliwa mabo kwa matumizi mbalimbali ambapo aliwataka wananchi wafuate ushauri wa kitaalamu na sio kujichukulia sheria mikononi za kuikata.

  “Ni jukumu letu sisi wananchi wote kuona kwamba haya ni matatizo makubwa yenye madhara na ni vyema kukemea visababishi vya madhara haya na kuchukua tahadhari “Alisema DC Mgaza huku akisisitiza umuhimu wa kutunza mazingira.

Mkuu huyo wa wilaya amesema wilaya hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wilayani humo wanajukumu la kutoa elimu ya upandaji wa miti kwa wananchi wa kuanzia ngazi za vijiji na kata pamoja na kukemea uharibifu wa mazingira.

Pamoja na hayo alisema wilaya hiyo imepanga kupanda miti 810,000 hasa katika maeneo yote yenye vyanzo vya maji ikiwemo kuwahimiza wananchi kuisimamia na kuilanda ili iweza kukua na kutunza mazingira yao siku zijazo.

Alisema hata hiyo wanajukumu la kuongeza kasi ya upandaji miti ili kukabiliana na upungufu wa miti uliopo na mabadiliko ya tabia ya nchi vile vile kufikia lengo lililowekwa na Taifa la kila wilaya kupanda miti 1,000,000 kila mwaka.

Katika uzinduzi huo jumla ya miti 100 ilipandwa katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa vyanzo vya maji ambapo zoezi hilo linatarajiwa kuendelea wiki nzima.

Mwisho.