Mhandisi
wa Mahakama ya Tanzania, Khamadu Kitunzi akielezea teknolojia
inayotumika kujenga jengo la kituo cha mafunzo cha mahakama leo jijini
dar es salaam.
Kaimu
jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa na
Mwakilishi wa Benki ya dunia nchini, Bella Bird (kulia) na kulia ni jaji
kiongozi wa mahakama kuu ya Tanznaia Mhe. Ferdinand Wambali
walipotembelea ujenzi wa kituo cha mafunzo cha Mahakama leo jijini Dar
es salaam
Picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo.
Na Mohamed Ali-Mahakama.
MAHAKAMA
ya Tanzania inakusudia kuanzisha kituo cha Mafunzo kwa ajili ya
watumishi wake pamoja na wadau ili kuwaongezea ujuzi utakaosaidia
kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama.
Kituo
hicho kinachojengwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es
salaam kitawaunganisha watumishi wa Mahakama na wadau katika mafunzo kwa
njia ya video (video conferencing).
Akizungumzia
Kituo hicho, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma
amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya Maboresho ya huduma za
Mahakama ambacho pia wadau wa Mahakama watakuwa ni sehemu ya mafunzo
yatakayokuwa yakitolewa.
Amesema
badala ya Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau wa Mahakama kwenda
kupata baadhi ya mafunzo kwenye chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto
(IJA), baadhi ya mafunzo watakuwa wakiyapata katika kituo hicho.
Naye
Mratibu wa Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na maboresho ya Huduma za
Mahakama Mhe. Zahara Maruma alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji
wa nguzo ya tatu ya mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya
Tanzania ambapo kupitia nguzo ya pili ya Mpango huo, Majaji na Mahakimu
hupatiwa mafunzo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa
wakati.
Akizungumzia
nguzo ya tatu ya Mpango huo, Mhe. Maruma alisema nguzo hiyo inahusiana
na urejeshaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa
wadau katika shughuli za Mahakama ambapo kupitia kituo hicho wadau wa
Mahakama watahusishwa kwenye Mafunzo mbalimbali ili kurahisisha suala la
upatikanaji wa Haki.