MBUNGE MGIMWA ATUMIA MAMILIONI KUBORESHA SEKTA YA ELIMU NA AFYA JIMBONI KWAKE

February 26, 2018
 MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 12 vitakavyotumika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu na afya jimboni humo
 MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akikabidhi sim tanki ya lita 500 kwa viongozi 
  MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 12 vitakavyotumika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu na afya jimboni humo
  MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa bati na rangi kwa baadhi ya viongozi waliojitokeza kuja kuchukua masaada huo
  MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akimkabidhi diwandi makopo ya rangi 

Na Fredy Mgunda,Mufindi.

MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 12 vitakavyotumika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu na afya jimboni humo.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo Mgimwa alisema kuwa ametoa mabati 280, mifuko 310 ya saruji, rangi za maji na mafuta na sim tenki la lita mia tano (500) za kuhifadhia maji.

“Nilifanya ziara katika vijiji vya kata hizo nikaona wananchi wanavyojitoa kuboresha  sekta ya elimu na mimi kama mbunge wao nikaamua kuwaunga mkono kwa kuchangia vifaa hivyo” alisema Mgimwa


Mgimwa alizitaja kata zinazonufaika na msaada huo ni kata ya Mapanda, Kibengu, Ihanu na Sadani na akavitaja vijiji vinavyonufaika na msaada huo kuwa ni pamoja na Ihimbo, Ukami na Chogo katika kata ya Mapanda; na Kipanga, Igeleke, Kibengu, Usokami na Igomtwa katika kata ya Kibengu.

Vingine ni kijiji cha Lulanda katika kata ya Ihanu na katika kata ya Sadani Mgimwa sehemu ya msaada huo inakwenda kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mgalo.

Aidha Mgimwa alisema kuwa ataendelea kusaidia maendeleo kwenye vijiji ambavyo vinafanya maendeleo katika jimbo lake

Akiongea kwa niamba ya halmashauri ya wilaya ya Mufindi na vijiji vyote vilivyonufaika na msaada huo, Makamu Mwenyekiti Asheri Mtono alisema kuwa jimbo la Mufindi Kaskazini linakabiliwa na changamoto nyingi za ujenzi wa majengo mbalimbali hivyo msaada alitoa utapunguza changamoto zilizopo kwa kiasi Fulani

“halmashauri hii ina changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu ya shule na kwa msaada huu wa mbunge mazingira hayo yatakwenda kuboreshwa” alisema Mtono

 Mtono ambaye pia ni diwani wa kata ya sadani alisema pamoja na mchango wa mbunge huo na wadau wao wengine, wananchi wa vijiji hivyo na vingine vyote katika halmashauri hiyo wanahitajika kuendelea kuchangia shughuli zao za maendeleo.

 Nao baadhi ya viongozi wa vijiji wamempongeza mbunge Mgimwa  kuwa kutoa vifaa vya ujenzi kwenye vijiji vyake vyote vya jimbo la Mufindi Kaskazini ambavyo vitachochoe kuleta maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.

Mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isupilo, Onorata Mwanuke alisema kwa msaada waliopatapata wanakwenda kukamilisha ujenzi wa nyumba moja ya mwalimu.

“Mahitaji ya nyumba za walimu ni tisa zilizopo ni tatu na mbunge ametoa msaada wa mifuko 30 ya saruji kusaidia kukamilisha nyumba ya nne ya mwalimu. Tunategemea mbunge ataendelea kutuunga mkono”alisema Mwanuke

Kabla ya jana mbunge mgimwa alishakuwa ametoa jumla ya bati mia tano tisini (590) na saruji mifuko mia mbili ishirini (220) kwa ajili ya ujenzi  na ukarabati wa madarasa ya shule,zahanati na nyumba za wafanyakazi wa zahanati na walimu wa shule zilizopo katika kata ya Ihalimba huku lengo likiwa kuboresha sekta ya elimu na afya kwa wananchi.

Na alifanya kazi kwa kushirikiana na wananchi  wa kijiji cha Kibengu wametumia jumla ya shilingi milioni mia moja kumi na tisa na laki mbili (119,200,000) katika ujenzi wa madarasa ya shule,zahanati na nyumba za wafanyakazi wa zahanati na walimu wa shule zilizopo katika kijiji hicho lengo likiwa katika kuboresha sekta ya elimu na afya kwa wananchi.


 IGP SIRRO AWATAKA ASKARI KUTENDA HAKI KWA WANANCHI WANAOWAHUDUMIA

IGP SIRRO AWATAKA ASKARI KUTENDA HAKI KWA WANANCHI WANAOWAHUDUMIA

February 26, 2018
1
Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro (wapili kushoto), akikagua baadhi ya vielelezo katika kituo Kikuu cha Polisi wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kuzungumza na maofisa na askari mkoani humo, IGP Sirro amewataka askari kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi pamoja na kutenda haki kwa wananchi wanaowahudumia. Picha na Jeshi la Polisi.
2
Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro, akipokea salamu ya heshima kutoka kwa askari wa kikosi maalum cha Jeshi hilo wakati alipowasili Bariadi mkoani Simiyu kwa ziara ya kikazi IGP Sirro pia aliwataka askari kutojihusisha na vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi wanaowahudumia. Picha na Jeshi la Polisi.
3
Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro, akiweka saini kwenye kitabu cha wageni wakati alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu kwa lengo la kuzungumza na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo (hawapo pichani), kulia ni Mkuu wa mkoa huo Mhe. Antony Mtaka. Picha na Jeshi la Polisi.

WATANZANIA KUPENYA SOKO LA KENYA

February 26, 2018
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akifafanua jambo kwa washiriki wa kikao cha kujadili maandalizi ya wiki ya Tanzania nchini Kenya mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Kuia ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dk. Pindi Chana na katikati ni Mtendaji Mkuu wa TANTRADE Edwin Rutageruka.
Baadhi ya washiriki wa kikao cha kujadili maandalizi ya wiki ya Tanzania nchini Kenya wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa - MAELEZO

Jonas Kamaleki- MAELEZO.
Serikali imetoa wito kwa  wafanyabiashara wa Tanzania kupeleka bidhaa zao katika soko la Kenya ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kikao cha Maandalizi ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya.
Prof. Mkenda alisema kuwa ni nia ya Serikali kuhakikisha watanzania wanapenya katika masoko ya kimataifa ili kuongeza pato la mtu binafsi na la Taifa kwa ujumla.“Hali ya biashara kwa sasa ni nzuri sana, hivyo vikwazo visiwepo kabisa kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki”, alsiema Prof. Mwaikenda.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema kuwa watanzania inabidi wathubutu na kuingia katika soko la Afrika Mashariki hususan soko la Kenya.Amesema kuwa wafanyabiashara wa Kitanzania wasiogope kuingia katika masoko ya nje ya nchi, wajitahidi ili waweze kuongeza vipato kutokana na ukubwa wa soko lililopo nchini na Kenya kwa ujumla.
“Mkifanya biashara Kenya mtaongeza mitaji, ajira na kipato kwa ujumla kwani nchi hizi mbili zina zaidi ya watu milioni 90”, na hii inaendana na falsafa ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli ya Uchumi wa Viwanda, hivyo hatuna budi kufuata maono ya Kiongozi wetu na kutengeneza na kuuza bidhaa za viwandani nje ya nchi”, alisema Balozi Pindi Chana.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Ali Juma amesema wazo la kufungua soko la Kenya ni zuri na kumpongeza Balozi Pindi Chana kwa ubunifu huo.
Aliongeza kuwa anafahamu kuwa zipo changamoto ndogo ndogo katika masoko lakini zinafanyiwa kazi ili kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Kenya inaenda vizuri.Bwana Juma alisisitza kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini inabidi ziwe na ubora na kuwa na vifungashio bora ili kumvutia mteja kununua.
Naye  Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Edwin Rutageruka amesema watanzania waende Kenya wakijiamini kwani bidhaa zao zinahitajika sana.Aliwataka wafanyabiashara kujenga maghala mipakani ili kutunza bidhaa zao humo na kuziuza kwa bei nzuri wakati muafaka.
Akichangia mada katika kikao cha maandalizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye aliwaomba seka binafsi wajitokeze ili kupeleka bidhaa zao nchini Kenya na kuitumia hiyo fursa katika kukuza biashara zao.
Simbeye aliiomba Serikali kuwapeleka waambata wa kibiashara kwenye balozi za Tanzania Duniani ili washughulikie suala la masoko na fursa nyingine za kibiashara.Kikao hiki cha maandalizi kimetokana na maono ya Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana ambaye amebuni wazo la kufanya wiki ya Tanzania nchini Kenya kwa ajili ya kutafuta soko la bidhaa za Tanzania ambayo itafanyika 26 Aprili, 2018 na itadumu kwa wiki moja.

DC SHINYANGA AFANYA MKUTANO KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI BUGAYAMBELELE

February 26, 2018
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga amewataka maafisa watendaji wa vijiji na kata kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi pamoja na wenyeviti wa vitongoji,mitaa,vijiji na kata kufanya mikutano kwa ajili ya kutatua kero zinazowakabili wananchi.

TANESCO TANGA YAWAPA TAHADHARI WANUNUZI WA NYUMBA

February 26, 2018
WANUNUZI wa nyumba na wapangaji mkoani Tanga wame tahadharishwa kuzikagua mita zao za umeme kabla ya kuishi ili kuepukana na kuingia gharama wasizotarajia wakati wa ukaguzi na wanaofanya ili kuwabaini wahujumu.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa Tanga Mhandisi Aloyce Shayo wakati akitolea ufafanuzi wa operesheni wanayoendelea nayo ili kuweza kubaini vitendo vya uhujumu
vinavyofanywa na wateja.

Alisema operesheni hiyo imekuwa ikilenga kukagua na kuangalia mita  na iwapo zinakutwa na makosa mbalimbali ikiwemo kuchezewa wanalazimika kusitisha huduma hiyo.

Aidha alisema kuwa operesheni inayoendelea Mkoani hapa ni ya kuwabaini wale wanaolihujumu Shirika kwa kuzichezea mita ambapo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa kulipa deni hilo kwa wakati kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kaimu Meneja huyo alisema wamegundua pia matatizo kwa baadhi ya wateja wao wanaponunua nyumba au kupangisha hawana utaratibu wa kuhakiki mita zao kupitia mafundi wao ili waweze kujiridhisha kama ziko salama badala yake wanasubiri mpaka wanapokuja kukaguliwa na kuadhibiwa.

Alisema hivi sasa ifike wakati wa jamii nzima kuelewa na kutekeleza wajibu wao wa kimsingi wa kuomba mafundi kutoka katika Shirika hilo kwa ajili ya ukaguzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo wanaohitaji kupangisha au kununua kabla ya kukutana na mkono wa sheria.

Hata hivyo alisema shirika hilo litaendelea na operesheni yake kwamkoa mzima na wale watakao bainika kuharibu miundombinu ya umeme sheria ziko wazi na kuongeza zoezi hilo ni endelevu ili kudhibiti uharibifu na uingiaji wa hasara kwa shirika usio tarajiwa.

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AAGIZA WAKURUGENZI KUPANDISHWA KIZIMBANI JIJINI MWANZA, NI KWA KUTOJISAJILI NA WCF

February 26, 2018




NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mwanza

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde, (pichani juu), ameagiza waajiri ambao hawajajisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kufanya hivyo, vinginevyo wafikishwe mahakamani mara moja.

 Mhe. Mavunde ametoa agizo hilo Jumatatu Februari 26, 2018 baada ya kufanya ziara ya kushtukiza jijini Mwanza, kubaini waajiri ambao bado hawajatekeelza takwa la kisheria kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi, Sura 263 marejeo ya mwaka 2015, ambayo inamtaka kila mwajiri kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania bara awe amejisajili na kuwasilisha michango kwenye Mfuko huo.



Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo, Bw. Anslem Peter,  jiji la Mwanza pekee lina waajiri 1228, lakini kati ya hao ni waajiri 482 tu ndio waliojisajili na Mfuko huku waajiri wengine 746 wakiwa bado hawajajisajili. Hali hiyo ndiyo iliyomfanya Mhe. Naibu Waziri kufanya ziara hiyo ya ghafla.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi huo wa kushtukiza, Mhe. Mavunde pia ameiagiza WCF kuwafikisha mahakamani mara moja, waajiri wa kampuni ya ujenzi ya JASCO, (Mkurugenzi Mtendaji Bw.Karan Bachu),

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Airco Holdings  inayotoa huduma za kusogeza vifurushi na mizigo uwanja wa ndege wa Mwanza na hoteli ya Belmonte ya jijini humo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli hiyo, Bw. Philemon Tei, amejikuta matatani.

"Naagiza  waajiri hao kulipa michango yote ya nyuma (tangu tarehe 1 Julai 2015 tangu Mfuko ulipoanza kutekeelza majukumu yake au siku mwajiri aliyoanza kazi zake iwapo ni baada ya tarehe 1 Julai 2015).

Mhe. Mavunde ameagiza waajiri hao kufanya mawasiliano na watendaji wa Mfuko haraka iwezekanavyo ili kuweza kubaini kiwango cha riba kila mwajiri anachopaswa kulipa kutokana na kuchelewesha michango katika Mfuko. “Ni kosa la jinai kwa mwajiri kutotekelza takwa hilo la kisheria na kifungu cha 71(4) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kimeweka wazi kuwa mwajiri wa aina hii, anaweza kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni 50,000, kifungo kisichozidi miaka 5 jela au adhabu zote kwa pamoja, kwa hivyo nitoe wito kwa waajiri hao, hakuna sababu ya kushurutishwa kutekeleza sheria.
"Tutatekelza agizo la Mhe. Waziri kama alivyolitoa, na nitoe rai tu kwa waajiri kote nchini (Tanzania Bara), kutekeleza takwa hilo la kisheria, kwani hakuna kichaka cha kujificha tutawafikia." Alisisitiza Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo, Bw. Anslem Peter katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde(kushoto), akiwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, 9WCF), Bw. Anslem Peter,  akitoa maagizo ya kufikishwa mahakamani mara moja mkurugenzi mtendaji wa Belmonte Hotel ya jijini Mwanza leo Februari 26, 2018 kwa kushindwa kutekeleza takwa la kisheria linalomtaka kujisajili na Mfuko huo. Naibu waziri ameonya waajiri wote nchini kuttekeleza wajibu wao kwani hakuna mahala pa kujificha na operesheni hiyo inaendelea mikoa mingine.
 
 NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde, (wakwanza kushoto), Mkurugenzi wa Uenmdeshaji (Director of Operations), Anslem Peter,  Afisa Kazi Mfawidi Mkoa wa Mwanza, Khadija Hersi, wakipitia nyaraka za Hoteli ya Belmonte ya jijini Mwanza kuona jinsi uongozi wa hoteli hiyo unavyotekeleza Sheria ya Fidia Kwa wafanyakazi, kwa kujisajili na Mfuko huo. Naibu Waziri alifanya ziara ya kushtuikiza kwenye kampuni kadhaa jijini Mwanza ambapo hoteli hiyo ilibainika kutojisajili na aliamuru Mkurugenzi wake kupelekewa mahakamani mara moja. Wakwanza kulia aliyesimama ni Mkuu wa KItengo cha Mawasiliano na Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge.
 Naibu waziri akiongozana na Bw. Anslem Peter na afisa mwingine kutoka jijini Mwanza mara baada ya kukagua ofisi za huduma za vifuriushi na mizigo uwanja wa ndege wa Mwanza, Airco Holdings.
Mkurugenzi wa Belmonet Hotel ya jijini Mwanza, Bw.Philemon Tei
Naibu Waziri Mvunde, akizungumza na wafanyakazi wa Airco Holdings ya uwanja wa ndege wa Mwanza. Kushoto ni Bw. Anslem Peter

 Naibu Waziri akiwa kwenye ofisi za Airco Holdings uwanja wa ndege wa jijini Mwanza
 Naibu Waziri akitoa maelekezo kwa uongozi wa Belmonte Hotel



 Maafisa wa WCF, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anslem Peter, (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Bi. Laura Kunenge, wakitoka kwenye kiwanda cha kuchakata samaki jijini humo baada ya ukaguzi huo wa kushtukiza.
 Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya JASCO, ya jijini Mwanza Bw. Karan Bachu, akijieleza mbele ya Naibu Waziri Mvunde, (hayupo pichani)
 Mhe. Mavunde, (kushoto), akizungumza mbele ya Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya JASCO, ya jijini Mwanza Bw. Karan Bachu
 Mhe. Mavunde, akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya JASCO ya jijini Mwanza baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza leo Februari 26, 2018.
 Mhe. Mavunde na maafisa wa WCF wakiwa ofisi za kampuni ya kuchataka samaki jijini Mwnaza
 Mhe. Naibu Waziri akipitia nayaraka za kampuni ya kuchakata samaki ya jijini Mwnaza wakati wa ukaguzi wake.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa WCF, Bw. Anslem Peter akimuonyesha nyaraka za kampuni ya uchakataji samaki jijini Mwanza, ambayo imeanza kuwasilisha michango, lakini bado haijajisajili na Mfuko, ambapo aliagiza watekeeleze takwa hilo haraka.
-- Khalfan Said Photojournalist K-VIS MEDIA P.o.box 77807 Dar es Salaam, Tanzania Mobile: +255-784-646-453/+255-653-813-033 Blog: khalfansaid.blogspot.com

MASHINDANO YA POOL TABLE TANGA KUCHEZWA KUCHUYA PUB

February 26, 2018
MASHINDANO ya ndani ya mchezo wa Pool Table mkoa wa Tanga yanatarajiwa kuanza kutimumia  Machi 3 mwaka huu kwenye ukumbi wa Kichuya Pub itakayohusisha timu zinazomaliza Ligi ya mkoa msimu uliopita na kufanikiwa kuingia sita bora.

Ukumbi huo upo wilayani Korogwe ambapo msimu huu wamepaanga kuchezesha timu sita  badala ya kumi kama ilivyokuwa miaka iliyopita kutokana na makubaliana yao na mfadhili ambaye atadhamini mashindano hayo.

Akizungumza na Tanga Raha Blog,Katibu wa Chama cha Mchezo wa Pool Table mkoa wa Tanga(TARPA) Shabani Kibelo alisema msimu huu wamepanga mashindano hayo kuchezwa kwa siku tatu.

Alisema katika mashindano hayo ambayo yamefadhiliwa na mdau mmoja mkoani Tanga yatafanyika kwa ufanisi mkubwa huku kila timu shiriki ikigharamiwa fedha za usafiri wa kwenda na kurudi.

Kibelo alisema katika mashindano hayo mshindi wa kwanza kwa timu ataapata sh.500,000 mshindi wa pili sh.300,000 mshindi wa tatu akipata sh.200,000.

Alisema pia kwa washindi mmoja mmoja ambapo kwa upande wa wanaume mshindi wa kwanza atapata sh.300,000 mshindi wa pili sh.200,000 huku mshindi wa tatu akipata sh.100,000.

Hata hivyo aliongeza kwa upande wa wanawake mshindi mmoja mmoja wa kwanza sh.200,000 mshindi wa pili atapata sh.100,000 na mshindi wa tatu atapata sh.50,000.

Tigo Yamwaga Smatifoni Kwa Washindi wa promosheni ya Nyaka Nyaka Bonus

February 26, 2018
Mshindi wa Simu aina ya Tecno R6 katika promosheni inayoendelea  Nyaka Nyaka Bonus, Rajabu Saidi Yote (kulia), ambaye ni mkaazi wa Tandika Dar es Salaam,  akipokea zawadi yake kutoka kwa balozi wa promosheni hiyo inayoendeshwa na kampuni ya Tigo, Mina Ali (kushoto) pamoja na Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael (katikati). Jumla ya washindi 156 wamejinyakulia simu katika promosheni hiyo. 


Mshindi wa Simu aina ya Tecno R6 katika promosheni inayoendelea  Nyaka Nyaka Bonus, Tinna Sharon Masatu (kulia), ambaye ni mkaazi wa Mbezi Beach akipokea zawadi yake kutoka kwa balozi wa promosheni hiyo inayoendeshwa na kampuni ya Tigo, Mina Ali (kushoto) pamoja na Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael (katikati). Zaidi ya simu 900 bado zinashindaniwa katika promosheni hiyo. 


Mshindi wa Simu aina ya Tecno R6 katika promosheni inayoendelea  Nyaka Nyaka Bonus, Margareth Martin Hiza (kulia), ambaye ni mkaazi wa Ubungo, Dar es Salaam akipokea zawadi yake kutoka kwa balozi wa promosheni hiyo inayoendeshwa na kampuni ya Tigo, Mina Ali (kushoto) pamoja na Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael (katikati). Jumla ya washindi 156 wamejinyakulia simu katika promosheni hiyo. 



Add caMshindi wa Simu aina ya Tecno R6 katika promosheni inayoendelea  Nyaka Nyaka Bonus, Daniel Joseph Swai  (kulia), ambaye ni mkaazi wa Iala, Dar es Salaam akipokea zawadi yake kutoka kwa balozi wa promosheni hiyo inayoendeshwa na kampuni ya Tigo, Mina Ali (kushoto) pamoja na Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael (katikati). Zaidi ya simu 900 bado zinashindaniwa katika promosheni hiyo.  



Baadhi ya washindi zaidi ya 84 waliojinyakulia simu aina ya Tecno R6 katika promosheni inayoendelea ya Nyaka Nyaka Bonus wakiwa katika picha ya pamoja na balozi wa promosheni hiyo inayoendeshwa na kampuni ya Tigo, Mina Ali (kati) wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi hizo kwa washindi. Jumla ya washindi 156 wa simu tayari wamepatikana katika promosheni hiyo ambapo zaidi ya simu 900 bado zinashindaniwa.  


  • Wateja 156 wa Tigo wajinyakulia smartphone za TECNO R6 4G

  • Zaidi ya simu 900 na bonasi za internet bado zinashindaniwa!
Dar es Salaam, Februari 26, 2018 – ‘Kwa sasa mama yangu anatumia simu ya kawaida ambayo haituwezeshi kuwasiliana kikamilifu kwa njia ya mtandao. Kwa mfano siwezi kumtumia picha za wajukuu wake. Ndio maana  nitampa zawadi ya simu hii mpya niliyoshinda kutoka Tigo leo ili iturahisishie mawasiliano yetu na kumfanya awe sehemu ya ulimwengu wa kisasa wa mawasiliano.’ Haya ni maneno ya Margareth Martin Hiza, mfanyabiashara na mkaazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye aliibuka moja wa washindi wa simu mpya za kisasa senye uwezo wa 4G aina ya Tecno R6 4G katika promosheni ya Nyaka Nyaka Bonus inayoendeshwa na Tigo Tanzania.

Wateja wa Tigo Tanzania wanazidi kupata faida lukuki ikiwemo bonasi za hadi GB 1 bure kwa matumizi yao ya intaneti pamoja na fursa ya kushinda mojawapo ya simu janja 900 ambazo bado zinashindaniwa katika Nyaka Nyaka Bonus, promosheni murwa inayowazawadia wateja wa Tigo wanaounua vifushi vya kuanzia TZS 1,000 vya intaneti kupitia menu iliyoboreshwaya *147*00#.

Akikabidhi zawadi kwa washindi wa wiki hii, Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kuwa bado kuna zaidi ya simu 900 aina ya Tecno R6 zenye uwezo wa 4G ambazo zinashindaniwa na wateja watakaonunua vifurushi vya intaneti vya kuanzia TSH 1,000 kupiita menu *147*00#.

‘Washindi wetu wote 156 tuliowapata kufikia sasa wanatoka sehemu mbali mbali za nchi, kwa hiyo ninawashauri wateja wetu kote nchini washiriki ili wajishindie bonasi za data bure pampoja na mojawapo ya simu zaidi ya 900 za Smartphones ambazo bado zinashindaniwa,’ Woinde alisema.
Kupitia promosheni ya Nyaka Nyaka Bonus, Tigo itaongeza idadi ya watumiaji wa simu za kisasa pamoja na matumizi ya data nchini.




DK. KIGWANGALLA ATOA MIEZI TISA KWA WANANCHI KULIPWA FIDIA WAPISHE HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE NA PORI LA AKIBA MKUNGUNERO

February 26, 2018

Na Hamza Temba-WMU-Manyara
........................................................................

Serikali italipa fidia na vifuta jasho kwa vitongoji ambavyo vipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ili viweze kupisha maeneo hayo yaendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambao ulihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya za Simanjiro, Kiteto na Kondoa.

Alisema fidia hiyo italipwa kwa vitongoji viwili vya kijiji cha Irkishbo vya Maasasi na Lumbenek  vilivyopo katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ambavyo vilikutwa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero wakati pori hilo linaanzishwa mwaka 1996 kwa Tangazo la Serikali Na. 307.

"Tutafanya tathmini, tutawaomba wananchi mshirikiane na Serikali ili muweze kulipwa fidia mpelekwe maeneo mengine, jukumu letu sisi ni kugharamia zoezi la tathmini na kulipwa fidia ili muweze kuondoka katika maeneo haya ya hifadhi," alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kimotorok ambao wameanzisha makazi kimakosa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero hawatalipwa fidia na badala yake watafanyiwa tathmini na kulipwa kifuta jasho na kupelekwa maeneo mengine.

"Kimsingi ukimkuta mtu yupo katika eneo lako hupaswi kulipa fidia, hapa tumekuwa waungwana na kutumia roho ya kibinadamu, vinginevyo tungeweza kusema leo hapa tusione mtu na tungevunja kwa sababu ni eneo halali la hifadhi na hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria mtu kuishi ndani ya hifadhi.

"Kwa sasa hatutatumia nguvu, lakini tukikamilisha zoezi la tathmini tukalipa watu fidia yao, tutatoa muda maalum wa watu kuondoka na watu watapaswa kuondoka, ilimradi tutajiridhisha kwamba tulimtendea haki kila mwananchi anayeishi katika eneo hili," alisema Dk. Kigwangalla.

Akizungumzia moja ya zahanati iliyojengwa ndani ya kitongoji hicho cha Kimotorok ambayo nayo itabomolewa baada ya zoezi la kulipa vifuta jasho, aliiagiza TANAPA kujenga zahanati nyingine katika eneo jipya litakalopangwa Halmashauri husika kwa ajili ya wananchi hao kuhamia.

Alisema zoezi la tathmini pamoja na wananchi kulipwa fidia na vifuta jasho linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa ijayo kuanzia mwezi Machi, 2018. 

Akizungumzia hatma ya makazi mapya kwa wananchi watakaondolewa kwenye maeneo hayo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla ameziagiza Halmashauri husika za Kiteto, Kondoa na Simanjiro kupanga maeneo mengine mbadala ya kuwahamishia wananchi hao punde baada ya kulipwa fidia zao.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori inayosimamia Pori la Akiba Mkungunero kusaidia jamii jirani na maeneo hayo ya hifadhi kwa kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi, kuendeleza eneo la malisho na kuchimba mabwawa ya maji ya kunywesha mifugo ili kujenga misingi ya urafiki na ujirani mwema.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla amefuta mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame ambayo imeingia kimakosa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero na kumuagiza Meneja wa Pori hilo, Emmanuel Bilaso kuweka ulinzi mkali katika eneo hilo.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula alisema watasimamia utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali ili kuhakikisha mgogoro huo wa muda mrefu unapatiwa ufumbuzi. 

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Manyara, Waziri Kigwangalla alitembelea na kukagua eneo la Ranchi ya Manyara ambayo pia ni sehemu ya mapito ya wanyamapori,  eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ambapo alitoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha maeneo hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo hifadhi hiyo jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara. 

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyeshwa mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na viongozi wa hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo ya mapito ya wanayamapori na mipaka ya hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makuta wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi katika Kijiji cha Kimotorok mkoani Manyara jana. Wanaoshuhudia kushoto Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa.