WACHEZAJI WAWILI VPL, FDL WAPIGWA FAINI,CHANONGO AFUNGIWA MECHI MITATU

January 20, 2015
Release No. 004
                     TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Januari 20, 2015
                                                                                                                 
WACHEZAJI WAWILI VPL, FDL WAPIGWA FAINI
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewapiga faini na  kuwafungia mechi wachezaji wawili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kufanya vitendo kinyume na kanuni zinazotawala ligi hizo.

Mshambuliaji Haruna Chanongo wa Stand United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga teke mwamuzi wa mechi dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Januari 3 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu.

Kipa Amani Simba wa Oljoro JKT amepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kukataa kupeana mkono na viongozi wakati wa kusalimia kabla ya kuanza mechi kati ya timu yake na Toto Africans iliyofanyika jijini Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14 ya FDL.

Timu ya Polisi Mara imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi ya FDL dhidi ya Mwadui ya Shinyanga iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Pia Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 40 dhidi ya Geita Gold, adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 41.

12 WAPELEKWA KAMATI YA NIDHAMU YA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapeleka wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na matukio mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake.

Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na Nassib Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za FDL.

Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Rhino Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Oljoro JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi akiba (fouth official) Mussa Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kocha wa Polisi Tabora, Kim Christopher analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Msimamizi wa Kituo cha Musoma, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona naye anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.

Kwa upande wake, Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.

Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje mchezo.

Naye Gunda analalamikiwa kwa kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

SDL KUANZA MZUNGUKO WA PILI JANUARI 31
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) sasa utaanza Januari 31 mwaka huu, badala ya Januari 24 mwaka huu kama ilivyopangwa awali ili kutoa fursa kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia usajili wa dirisha dogo.

Timu zinazocheza ligi hiyo katika makundi manne tofauti ni; Milambo FC, Mji Mkuu FC (CDA), Mvuvumwa FC, Singida United, na Ujenzi Rukwa (Kundi A),  Arusha FC, Bulyanhulu FC, JKT Rwamkoma FC, Mbao FC, na Pamba SC (Kundi B).
Nyingine ni Abajalo FC, Cosmopolitan, Kariakoo Lindi, Kiluvya United, Mshikamano FC, na Transit Camp (Kundi C), wakati Kundi D ni Magereza Iringa, Mji Njombe, Mkamba Rangers, Town Small Boys, Volcano FC, na Wenda FC.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

“MALAIKA KUANZA SHOW ZA MIKOANI MWEZI UJAO”

January 20, 2015

 
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.

BENDI ya Mziki wa dansi ya Malaika Band inatarajiwa kuanza kupiga show zao katika mikoa mbalimbali hapa nchini wakianzia na mikoa ya kanda ya kaskazini

Akizungumza na TANGA RAHA BLO, Meneja wa Malaika Band, Abajalo Juma alisema  kuwa maandalizi ya show hizo yanaendelea vizuri na zitaanza mwezi ujao ambapo wataanzia na mkoa wa Tanga.

Alisema kuwa licha ya bendi hiyo kujiandaa na show hizo lakini wataendelea kutoa burudani kwenye jiji la Dar es Salaam kama kawaida ambapo Ijumaa wiki hii watapiga show ukumbi wa Mango Garden Kinondoni.

Aidha alisema kuwa Jumamosi watakuwa kwenye tamasha la Lidaz Bongo Fleva na mabendi mengi ambapo watafanya kubwa ili kuweza kuendeleza historia yao kama kawaida yao.

Hata hivyo alisema siku ya Jumapili watakuwa kwenye ukumbi wa TTC Chang’ombe  kutakapokuwa na bonanza CDS Masudi  ambaye anatimiza miaka 10 bendi mchanganyiko ya malaika.

KILIMANJARO FC YANUSA UBINGWA MKOA WA K'NJARO...

January 20, 2015
NA MWANDISHI WETU,MOSHI

KLABU ya Kilimanjaro FC ya Pasua, inayocheza ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa wa Kilimanjaro, imepiga hatua moja mbele katika harakati zake za kutwaa ubingwa wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuifunga Afro Boys ya majengo, goli 1-0.

Goli la Kilimanjaro FC katika mchezo huo mkali wa raundi ya pili,
hatua ya sita bora, uliopigwa juzi kwenye uwanja wa Ushirika, mjini Moshi, lilipatinana katika dakika 48, kipindi cha pili, likifungwa na
Jackson Obadia "Messi" kwa shuti kali, akiunganisha pasi ya Ayubu
Lipati.

Kwa ushindi huo sasa, Kilimanjaro FC, maarufu Mpira Pesa, inahitaji kushinda mchezo mmoja tu kati ya michezo yake miwili iliyosalia ili kutangazwa bingwa wa msimu 2014/2015.

Mpaka sasa timu hiyo, imeshajikusanyia Pointi 19, ambapo inahitaji
mchezo mmoja mmoja tu kati yake na Polisi Kilimanjaro, utakaopigwa siku ya Ijumaa, ambao utaifanya ifikishe pointi 22 ambazo hamna timu yoyote inayoweza kufikisha.

Msimamo wa ligi hiyo unaotarajiwa kumalizika, Februari mosi mwaka huu, unaonesha kuwa Kilimanjaro FC inaongoza kwa pointi 19, ikifuatiwa na Hai City, yenye pointi 15 sawa na Afro Boys, iliyoko katika nafasi ya tatu, zikizidiana kwa tofauti ya magoli.

Nafasi ya nne ni Polisi Mwanga yenye pointi 13 na mchezo mmoja
mkononi, nafasi ya tano ni Polisi Kilimanjaro yenye pointi 4 huku
Sango FC isiyokuwa na Pointi hata moja ikiridhika na nafasi ya mwisho.

Best regards;

MSEMAJI WA KILIMANJARO FC

FADHILI ATHUMANI

0756038214/0654724337

MAFUNZO KWA WATOA HUDUMA WA MRADI WA KFW YAANZA JANA WILAYANI KOROGWE

January 20, 2015
MENEJA WA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA MKOA WA TANGA,ALLY MWAKABABU AKIZUNGUMZA KABLA YA KUANZA MAFUNZO KWA WATOA HUDUMA WA MRADI WA KFW WILAYANI KOROGWE JANA

KATIBU TAWALA WILAYA YA KOROGWE,STANLEY LAMECK AKIZUNGUMZA NA WASHIRIKI WA MAFUNZO KWA WATOA HUDUMA WA MRADI WA KFW KUTOKA HALMASHAURI MBALIMBALI MKOANI TANGA JANA KUSHOTO KWAKE NI MWAKILISHI WA MKURUGENZI MKUU WA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA,DAUDI BUNYINYIGA

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Daudi Bunyinyiga akisisitiza jambo jana wakati ufunguzi wa mafunzo kwa watoa huduma wa mradi wa KFW wilayani Korogwe uliohusishwa Halmashauri Mbalimbali mkoani hapa.




Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini,Steven Ngonyani "Maji Marefu akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watoa huduma wa mradi wa KFW jana kushoto kwake ni Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga,Ally Mwakababu

Washiriki kutoka halmashauri mbalimbali wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwakilishwa jana