Baada ya kumalizika kwa mradi wa SCMS, USAID yaahidi kuendelea kuisaidia Tanzania

Baada ya kumalizika kwa mradi wa SCMS, USAID yaahidi kuendelea kuisaidia Tanzania

June 01, 2016
Baada ya kufanyika nchini kwa miaka 10, mradi wa SCMS ambao ulikuwa ukisimamiwa na John Snow Incorporated (JSI) kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) limeiahidi serikali ya Tanzania kuwa litaendelea kuisaidia katika misaada mbalimbali ya afya licha ya kumalizika kwa mradi huo.
Hayo yamesemwa na Naibu Mkurugenzi wa USAID nchini, Tim Donnay katika mkutano ambao ulikutanisha wadau mbalimbali wa afya ili kujadili mradi wa SCMS ambao umefikia tamati baada ya kufanyika nchini kwa miaka 10.
Bi. Donnay alisema serikali ya Marekani kupitia USAID imejipanga kuendelea kuisaidia Tanzania katika sehemu mbalimbali ambazo zinahusu Afya.
“USAID itaendelea kuisaidia Tanzania ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya upatikanaji wa huduma bora wa kiafya ... kumalizika kwa mradi huu hukutafanya kusitishwa kwa huduma ambazo zinatolewa kwa sasa,” alisema Bi. Donnay.
DSC_3159
Naibu Mkurugenzi wa USAID nchini, Tim Donnay akiwasilisha ujumbe kwa niaba ya serikali ya Marekani katika mkutano wa hitimisho wa mradi wa SCMS.
Nae mgeni rasmi katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr. Mpoki Ulisubya alisema kufanyika kwa mradi huo nchini kumewezesha kusaidia kuboreshwa kwa kasi huduma za afya tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Mradi huu umetusaidia sana awali hata utolewaji wa dawa kwa waathirika wa UKIMWI ulikuwa ni laki na nusu kwa mwaka ila kwa sasa kuna upatikanaji wa dawa hadi laki nane kwa mwaka,
“Mbali na hiyo pia wametujengea maghala ambayo yanatumika kuhifadhi dawa na hata kusaidia kuweza kuwasogezea huduma wananchi ambazo awali hazikuwa zikitolewa,” alisema Ulibusya.
Na Rabi Hume, MO Dewji Blog
DSC_3179
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr. Mpoki Ulisubya akitoa neno la shukrani kwa niaba ya serikali katika mkutano wa hitimisho la mradi wa SCMS uliotolewa na USAID na kusimamiwa utekelezaji wake na John Snow Incorporated (JSI) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya. (Picha zote na Rabi Hume, MO DewjiBlog)
DSC_3165
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dr. Juma Malik Akil akitoa neno la shukrani kwani niaba ya serikali ya Zanzibar baada ya kumalizika kwa mradi wa SCMS.
DSC_3149
Mfamasia wa Serikali, Henry Irunde akielezea utaratibu wa usambazaji wa dawa nchini uliotumika wakati ambao mradi huo ulikuwa ukifanyika nchini.
DSC_3142
Baadhi ya wadau wa sekta ya afya walioshiriki mkutano huo.
DSC_3130
DSC_3129
DSC_3143
Mkurugenzi wa John Snow Incorporated (JSI), Deo Kimera akizungumzia Mradi wa SCMS.DSC_3103
Baadhi ya wafaidika wa mradi wa SCMS wakielezea jinsi mradi huo umeweza kuwasaidia wao binafasi na katika sehemu ambazo wanafanyia kazi.DSC_3105
Baadhi ya wahudhuriaji wa mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere wakiwasikiliza wafaidika wa mradi wa SCMS.
DSC_3121
Muonekano wa kazi ambazo zimefanywa na mradi wa SCMS kwa kipindi cha miaka 10 tangu ulipoanza mwaka 2005.
DSC_3192
Baadhi ya waandaji wa mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja.

SERIKALI YATOA UFAFANUZI UBORESHAJI WA MASLAHI YA POLISI NA MAFUNZO YA JKT

June 01, 2016


 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson akiongoza kikao cha 34 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo mjini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifurahia jambo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye ndani ya Ukumbi wa Bunge kabla ya kuanza kwa kikao cha 34 cha Mkutano wa 3 wa Bunge mjini Dodoma.

 Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Moga iliyoko jijini Dar es salaam wakifuatilia shughuli za kikao cha 34 cha Bunge mjini Dodoma. Wanafunzi 90 wa shule hiyo wamelitembelea Bunge hilio kujifunza namna linavyoendeshwa.
 Baadhi ya Mawaziri na Wabunge wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge wakati wa kikao cha 34 mjini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Mhe. Ramo Makani akijibu maswali ya Wabunge yaliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa kipindi cha Maswali na majibu leo, Dodoma.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Muhagama akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa Serikali ndani ya ukumbi wa Bunge leo mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 leo mjini Dodoma. Wizara hiyo inaliomba Bunge lipitishe kiasi cha shilingi Trilioni 8.7 kwa ajiri ya matumizi ya kawaida na matumizi mengine.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji wakiandika maoni ya Wabunge waliokuwa wakichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara Fedha na Mipango kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 leo mjini Dodoma.
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(kulia) akimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina nje ya Ukumbi wa Bunge leo.
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(kushoto) akisalimiana na Mbunge wa Kilolo Mhe. Venance Mwamoto nje ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma.
 Baadhi ya Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Moga iliyoko jijini Dar es salaam wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Ukumbi wa Bunge mara baada ya kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge kufuatilia shughuli za kikao cha 34.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto) akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba (kulia) kwenye viwanja vya Bunge, Dodoma. 

Na. Aron Msigwa- DODOMA.
SERIKALI imesema kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi na kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mkakati wa Serikali wa kuboresha maslahi ya Askari wa Jeshi hilo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bungeni mjini Dodoma leo
Amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza Mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba za Polisi 4136 ambao utakwenda sambamba na ujenzi wa vituo vya Polisi.

Amesema Serikali imechukua hatua za haraka kulishughulikia suala la ukosefu wa nyumba za askari hao katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yenye ukosefu wa nyumba hizo.

Amelieleza Bunge kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa maslahi ya Askari Polisi yanaimarishwa ikiwemo malipo ya Posho ya pango kwa askari wasio na nyumba ambayo ni asilimia 15 ya mishahara yao ili waweze kulipia gharama hizo.

Ameongeza kuwa  askari wenye utalaam maalum wakiwemo madereva na madaktari wamekuwa wakilipwa posho ya asilimia 15 ya mishahara yao na kuongeza kuwa askari wanaoajiriwa katika ajira mpya kama madaktari wamekuwa wakilipwa mishahara sawa na madaktari wengine bila kujali vyeo vyao.

“Serikali tumefanya jitihada kubwa sana kuboresha maslahi ya askari wetu, kama Serikali tumetoa posho za nyumba, posho za utalaam maalum kwa askari wote ambayo ni asilimia 15 ya mshahara wa kila Polisi hii yote ni kuwafanya askari wetu waweze kumudu gharama za maisha” Amesisitiza Mhe. Mpina.
Ameeleza kuwa kwa askari wanaofanya kazi katika mazingira magumu wakiwemo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamekuwa wakipewa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu (Hardship allowance) kiasi cha shilingi laki moja (100,000) kila mwezi.
Mhe. Mpina amebainisha kuwa askari wote wanaohitimu mafunzo yao wamekuwa wakikatiwa Bima ya Afya kwa asilimia 100 na Serikali pamoja na udhamini wa mikopo mbalimbali katika taasisi za kifedha ili waweze kupewa mikopo na taasisi hizo.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali imewapandishia kiwango cha Posho ya katikati ya mwezi (Ration Allowance) kutoka shilingi 180,000 za awali hadi 300,000 ambazo wanalipwa kwa sasa nchi nzima.
Katika hatua nyingine Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetoa ufafanuzi kuhusu vijana wa kidato cha nne kutochukuliwa kujiunga na  Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi  amesema kuwa hatua ya kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa haiwezekani kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali.
Amesema kuwa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea kwa sasa ni 5000 hadi 7000 kwa mwaka kulingana na bajeti inayotolewa na kuongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha na kujenga kambi zaidi za mafunzo ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga  na mafunzo hayo kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kwa upande wa wahitimu wa kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na JKT kwa mujibu wa Sheria Mhe. Mwinyi amesema Serikali imewachukua vijana 14,000 na inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kuchukua vijana wengi zaidi.
Amesema Serikali inakusudia kujenga majengo ndani ya makambi ili kuwezesha vijana wote wanaohitimu kidato cha sita kupitia JKT kabla ya kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini.
Aidha, Amefafanua kuwa kwa wale wanaojiunga na JKT kwa kujitolea ambao idadi yao inafikia 5000 sio wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na kuongeza kuwa ni asilimia 71 ndio hupata ajira kwenye vyombo hivyo huku waliobaki wakilazimika kurudi nyumbani.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia utaratibu wa kuwawezesha vijana hao ili wanaporudi uraiani waweze kupatiwa mitaji ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe.

NAIBU WAZIRI MASAUNI ATUA MKOANI TANGA, AZUNGUMZA NA WAKUU WA VYOMBO VYA ULINZI, ATEMBELEA MSITU WA MAPANGOPORI YA AMBONI

June 01, 2016

 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akichungulia pango lililopo katika msitu wa Mapangopori ya Amboni linalodaiwa kuwa ni njia kuu ya watu wanaohofiwa majambazi waliofanya mauaji katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Tarafa ya Chumbageni, jijini Tanga.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akitoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo (kulia), mara baada ya kutoka ndani ya pango lililopo katika msitu wa Mapangopori ya Amboni linalodaiwa kuwa ni njia kuu ya watu wanaohofiwa majambazi waliofanya mauaji katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Tarafa ya Chumbageni, jijini Tanga. Katikati ni Mkuu wa Kikosi Maalum kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia Makao Makuu Dar es Salaam, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, William Mwampagale.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) akiwa na vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotoa ulinzi katika msitu wa Mapangopori ya Amboni mkoani Tanga. Naibu Waziri alifanya ziara ya kutembelea mapango hayo ambayo yalikuwa makazi ya watu wanaohofiwa majambazi waliofanya mauaji katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Tarafa ya Chumbageni, jijini Tanga. Kushoto ni Mkuu wa Kikosi Maalum kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia Makao Makuu Dar es Salaam, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, William Mwampagale.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto meza kuu) akizungumza katika Kikao cha Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga. Kulia meza kuu ni Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigella. Watatu kushoto ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu (wapili kushoto). Viongozi hao wamekutana  mkoani humo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akimsalimia Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kabla ya kwenda katika msitu wa Mapangopori ya Amboni mkoani Tanga. Naibu Waziri alifanya ziara ya kutembelea mapango hayo ambayo yalikuwa makazi ya watu wanaohofiwa majambazi waliofanya mauaji katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Tarafa ya Chumbageni, jijini Tanga. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI.