FCC :YABAINI ASILIMIA 3.4 YA MAKONTENA HAYAJAFATA SHERIA YA ALAMA YA BIDHAA BANDARINI
Na Hamida Ramadhan , Dodoma
MKURUNGEZI Mkuu wa Tume ya Ushindani FCC William Erio amesema wameendelea kufanya Kaguzi ili kubaini wanaoingiza bidhaa nchini zilizo kiuka Sheria ya alama za bidhaa.
Pia FCC imefanya kaguzi ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu (ICDs) ambapo 3.4% ya jumla ya makasha (containers) yaliyokaguliwa yenye thamani ya kiasi cha Shilingi Bilioni 20.8 yalikutwa na bidhaa zilizokiuka Sheria ya Alama za Bidhaa .
Mkurungezi huyo ameyasema hayo leo Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendajiwa majukumu ya FCC ambapo ameeleza Kaguzi za kushtukiza (Dawn Raids) zilifanyika bidhaa zenye thamani ya Shilingi Billioni 4.7 zilizokiuka Sheria ya Alama za Bidhaa zilikamatwa na hatua stahiki zilichukuliwa.
Amesema Kaguzi hizo zilifanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Songwe, Kilimanjaro, Pwani, Mwanza, Arusha, Katavi na Mbeya.FCC imefanya uharibifu wa bidhaa bandia zilizokamatwa katika Mikoa ya Mbeya, Iringa na Ruvuma.
Amebainisha bidhaa zilizoharibiwa ni pamoja na wino wa printa katoni 432 na kilo 1,302 za vifungashio.Kaguzi hizi zinapunguza madhara ya bidhaa bandia ambazo pamoja na mambo mengine, zinaweza kutokuwa salama kwa walaji, zinaikosesha serikali mapato, na zinaweza kuathiri biashara na uwekezaji halali.
"Walaji wanatakiwa kufahamu kuwa, watengenezaji wa bidhaa bandia huwa wanazalisha bidhaa hizi kwenye brands ambazo zinauzika kwa urahisi na zenye kukubalika zaidi sokoni (reputable brands)," Amesema Mkurungezi huyo
Na kuongeza"Hivyo ni vizuri walaji wajifunze mbinu za kuzitambua bidhaa bandia kwa kufanya milinganisho ya bei (kati ya bandia na isiyo bandia) pamoja na kufuata maelekezo ya alama za bidhaa zinazotolewa na kampuni husika inayomiliki nembo ya bidhaa halali," amesema.
Katika kipindi Julai, 2022 hadi Juni, 2023; FCC imefanikiwa kutekeleza na imeidhinisha maombi 56 ya miungano ya kampuni kutoka katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, uzalishaji, madini, mawasiliano, mafuta na Gesi.
Amesema Maombi 51 yalipitishwa bila masharti na maombi matano (5) yalipitishwa kwa masharti. Kwa mujibu wa Sheria, maombi ya miungano yanatakiwa kushughulikia ndani ya siku 90, lakini yamekuwa yakishughulikiwa kwa wastani wa siku 75.
Amesema FCC imetoa msamaha katika mkataba mmoja (1) uliokuwa ukififisha ushindani “exemption to agreement” kati ya Precision Air Services Plc na Kenya Airways Plc kwa lengo la kuendeleza Sekta Ndogo ya Usafiri wa Anga Nchini.
Ameeleza FCC imefanya uchunguzi wa mashauri 20 yanayohusu miungano ya kampuni ambayo haikuidhinishwa na FCC (unnotified mergers).
"Kati ya mashauri haya 4 yameshafungwa na yaliyobaki yako katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa. FCC imechunguza Mashauri nane (8) yanayohusu uwezekano wa kuwa na matumizi mabaya ya nguvu ya soko (abuse of market power) ambapo moja limefungwa na mengine yako katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa," amesema.
MAFANIKIO YA TUME YA USHINDANI KWA UJUMLA
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (mwaka 2020 - 2023), FCC iliridhia kununuliwa kwa kampuni 14 zenye jumla ya thamani ya bei ya mauziano inayofikia Shilingi Bilioni 49.4 katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuruhusu kampuni hizo kuongeza wigo zaidi sokoni, kuongeza mitaji na kupunguza uwezekano wa kampuni hizo kuondoka sokoni.
Kampuni hizi ni pamoja na Mtanga Foods Limited (yenye biashara zake Iringa), kampuni ya uzalishaji wa Parachichi ya Rungwe Avocado Company Limited, kampuni ya uchenjuaji mpunga (mchele) ya MW Rice Millers Limited na Mring’a Estates Limited.
Mwisho
MKUTANO WA MAAFISA HABARI WAFANYIKA ZANZIBAR.
Na Rahima Mohamed, Sheha Sheha Maelezo 1/8/2023
Maafisa habari wametakiwa kutumia vyombo vya habari vya serikali kutoa taarifa za utekelezaji katika taasisi zao kwa jamii.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Habari na Matukio kutoka shirika la Utangazaji Zanzibar Salum Ramadhan kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo katika mkutano wa maafisa habari, mawasiliano na uhusiano wa taasisi za Serikali huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mkoa wa Mjini Unguja.
Amesema maafisa kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi wa taasisi za umma kutumia vyombo vya habari ili wananchi wajue maendeleo yanayofanywa na serikali yao.
Aidha amesema maafisa habari wanatakiwa kutumia njia mbalimbali kutoa taarifa katika taasisi zao ikiwemo kuandaa Makala, matangazo na vipindi mbali mbali vinazotoa uchambuzi zinazoeleza maendeleo ya nchi.
Vilevile, amewashajihisha maafisa habari hao kuvitumia vipindi vya asubuhi njema na dira vinavyoendeshwa na shirika hilo ambavyo vinatoa nafasi kwaviongozi wa taasisi mbali mbali kuzungumza na Wananchi.
Mkurugenzi Salum ameipongeza Idara ya habari Maelezo kwa kusimamia sera ya habari na kuwakutanisha pamoja maafisa hao kwa lengo la kujua maendeleo wanayoyafanya na changamoto wanazokumbana nazo katika majukumu yao ya kila siku.
Mkurugenzi wa idara ya Habari Maelezo amewataka wakuu wa taasisi mbalimbali kuwashirkisha maafisa Habari katika kazi zao ili jamii iweze kuhabarika juu ya kazi hizo.
Aidha amewataka maafisa habari kuwa wabunifu katika kuandaa kazi zao za kihabari na kuendana na kasi teknolojia ya habari na mawasiliano.
Kwa upande wao maafisa habari kutoka taasisi mbali mbali, wamesema kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo zinarejesha nyuma majukumu yao ipasavyo ikiwemo ufinyu wa bajeti na ushirikishwaji mdogo.
Afisa Habari wa ZRA Makame Khamis akitoa Taarifa ya Jumuia ya Maafisa Habari wa Serikali katika Mkutano wa Maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano uliofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Zanzibar.
RAIS WA ALGERIA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA WAZIRI TAX
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune amekutana Kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipomtembelea Ikulu Jijini Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria unaofanyika kuanzia tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023.
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kirafiki na kidiplomasia ili kuweza kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya nchi zao.
Aidha, katika kuendelea kuimarisha ushirikiano Waziri Tax pamoja na majukumu mengine, atazindua Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 2 Agosti 2023 Jijini Algiers.
Uzinduzi wa ubalozi huo, ni hatua muhimu hasa wakati huu ambapo viongozi hao wamekubaliana kuinua sekta za uchumi ambazo ni pamoja na biashara, uwekezaji, nishati, madini, elimu, sayansi na teknolojia, afya na utalii.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipomtembelea Ikulu Jijini Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.