TBS yatoa elimu kwa wananchi kwenye Maonesho ya Nanenane Mwanza

August 06, 2023
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa limeshiriki maonesho ya wakulima Nanenane 2023 katika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza, kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu udhibiti na ubora wa bidhaa mbalimbali.

Meneja TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka amesema shirika hilo limetumia fursa ya maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa mazao ya chakula yatokanayo na kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi ili kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazokidhi viwango.

“Kaulimbiu mwaka huu inasema ‘vijana na wanawake ni msingi imara wa uendelevu katika uzalishaji wa mifumo ya chakula’, hivyo TBS tuna jukumu la kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinakidhi matakwa ya viwango na ni salama kwa matumizi ya bindamu” amesema Kanyeka.

Kanyeka ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo, TBS pia inatoa elimu kwa wananchi ili kutambua bidhaa zenye ubora, zinazofaa kwa matumizi na zilizopigwa marufuku ikiwemo vipodozi ili kuepuka matumizi yake kwani zina madhara makubwa kiafya.

Naye Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala amesema pia wanatoa elimu kwa wazalishaji na wauzaji wa bidhaa za vipodozi na chakula ili kuhakikisha wanadhibiti ubora wa bidhaa zao na kuepuka kuuza bidhaa zilizopigwa marufuku, zilizoisha muda huku pia wakizingatia utunzaji bora wa bidhaa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa watumiaji/ walaji.

Mayala ameeleza kuwa pia TBS inawahamasisha wajasiriamali kusajili bidhaa zao na kupata nembo ya ubora huku akiwatoa hofu kwamba Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwainua wajasiriamali wadogo kwa kuwapa fursa ya kupata nembo ya ubora bure kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Tunalenga kuwainua wajasiriamali wadogo kutoka hali ya chini kwenda hali ya juu ambapo Serikali imetoa utaratibu wa kuwasaidia kufanya shughuli zao kwa miaka mitatabu bila kulipia gharama za nembo ya ubora. Pia tunatoa mafunzo ya aina mbalimbali kuhusu namna ya kuandaa bidhaa zenye ubora na kudhibiti madhara yanayoweza kuwapata watumiaji” amesema Mayala.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TBS kwenye maonesho ya Nanenane Nyamhongolo jijini Mwanza ni David Maduhu ambaye ameshauri shirika hilo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa bidhaa zinazozalishwa ama kuingizwa nchini ili kuhakikisha wazalishaji wanazingatia ubora uliokusudiwa.

“Nafurahi pia wamenipa vipeperushi vyenye orodha ya bidhaa ambazo hazipaswi kuwa sokoni. Nashauri waendelee kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa bidhaa zinazosajiliwa na kupewa nembo ya ubora ili kuhakikisha wazalishaji wanazingatia ubora ule ule uliokusudiwa” amesisitiza Mayala.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka akieleza kuhusu ushiriki wa shirika hilo kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kanda ya Ziwa Magharibi kwenye uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza yakishirikisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Meneja TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Nyamhongolo jijini Mwanza.
Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala akieleza namna shirika hilo linavyowasaidia wajasiriamali kuboresha bidhaa zao ili kukidhi viwango na kupata nembo ya ubora.
David Maduhu ambaye no mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TBS kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza akiwa na vipeperushi mbalimbali vyevye elimu kuhusu bidhaa zenye ubora na zilizopigwa marufuku sokoni.
Wananchi wakipata elimu kwenye banda la TBS kwenye Maonesho ya Nanenane 2023 Nyamhongolo jijini Mwanza.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (katikati) na Afisa Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala (kushoto) wakitoa elimu kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonesho ya Nanenane Nyamhongolo jijini Mwanza.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamuge waliotembelea banda la shirika hilo.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (wa pili kushoto waliokaa) na Afisa Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala (wa kwanza kushoto waliokaa) wakitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamuge.
Wanafunzi wakipata elimu kwenye banda la TBS kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza yakishirikisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 08, 2023.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

DKT SIMEO: MICHEZO NI NGUZO MUHIMU YA UTULIVU NA USALAMA KWENYE NCHI

August 06, 2023
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo akizungumza wakati alipozindua zoezi la wanachama,wapenzi na mashabiki wa timu ya Simba kuchangia damu katika Zahanati ya Kisosora Jijini Tanga kulia ni Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Tanga Edgar Mdime

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo akizungumza wakati alipozindua zoezi la wanachama,wapenzi na mashabiki wa timu ya Simba kuchangia damu katika Zahanati ya Kisosora Jijini Tanga kulia ni Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Tanga Edgar Mdime
Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Tanga Edgar Mdime akizungumza kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo
MKUU wa Idara ya Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo Sinde Mtobu akieleza umuhimu wa uchangiaji damu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kulia ni Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Tanga Edgar Mdime

Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Tanga Edgar Mdime akichangia damu



Na Oscar Assenga, TANGA.

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Tanga Japhet Simeo leo amezindua zoezi la wanachama,wapenzi na mashabiki wa timu ya Simba kuchangia damu katika Zahanati ya Kisosora Jijini Tanga huku akieleza kwamba michezo ni moja ya nguzo muhimu katika utulivu na usalama kwenye nchi.

Simeo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba kwenye uzinduzi huo alisema kwamba michezo ina tija sana katika maisha ya binadamu ikiwemo kuwaunganisha jamii na kutengeneza undugu.

Alisema kwamba uchangiaji wa damu ni muhimu ili kuokoa maisha ya wagojwa wahitaji wa damu wakiwemo waluopata ajali, wakina mama wajawazito na watoto waliopo katika hospital mbalimbali mkoani Tanga.

Mganga Mkuu huyo aliwapongeza wanachama hao kwa utayari wao wa kuona umuhimu wa kuchangia damu ambayo itakwenda kusaidia jamii yenye uhitaji huku akizitaka Taasisi, Vikundi na watu binafsi kuendelea kuwa na utamaduni huo ili kuweza kuokoa maisha ya watu wanaofika hospital kupata huduma hiyo.

"Nawapongeza mashabiki wa timu ya Simba SC kwa utayari wenu kuja kuchangia damu mimi nawaambia hii ni sadaka na thawabu kubwa sana mliyoitoa kwa wenzenu wenye uhitaji wa damu " Alisema Simeo.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Matawi ya Klabu ya Simba SC Edgar Mdime alisema kwamba zoezi la uchangiaji wa damu imekuwa ni utaratibu waliojiwekea kila mwaka lengo likiwa kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kuokoa maisha ya wahitaji.

Alisema bado wanasukumwa kuchangia damu katika hospitali wakitambua kuwa uhitaji wa damu ni mkubwa kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu hivyo licha ya kushiriki siku hiyo adhimu kwao bado wanaendelea kuhamasishana kujitoa kwa pamoja katika zoezi hilo.

Aidha alisema walianza na zoezi la usafi kubwa zaidi ilikuwa ni kuchangia damu na hamasa kubwa sana ambayo imetokea kwa mkoa huo kwa wana Simba na matawi yote wameungana kwa pamoja kwa ajili ya zoezi hili la kuchangia damu

Hata hivyo alisema kwamba wanajua damu ni muhimu sana kwa kila mmoja hasa ukizingatia wapo wakina mama wanaojifungua katika hospitali ikiwemo ajali zinatokea watu wanahitaji kuwekewa damu kwa hiyo wao wamehamasika kama wanajamii ukiachana na suala la michezo.

Tambo 

Mwenyekiti huyo alisema kwamba dhamira yao kubwa msimu huu lazima timu yao ichukue Ubingwa kutokana na uwepo wa kikosi kipana kulingana na usajili mkubwa uliofanyika wakiamini lazima timu hiyo ifanye makubwa katika mashindano ya ndani na hata kimataifa pia.

Katika hatua nyengine, Mdime alituma salamu kwa watani zao timu ya wananchi Yanga kuelekea mechi za Ngao ya jamii zitakazo chezwa Mkwakwani Tanga ambapo ametamba kwa kusema kuwa hawatakuwa tayari ngao hiyo aichukue tena mtani mbele yao.

Mchezo huo unatarajiwa kucheza Agosti 9 mwaka huu katika uwanja wa CCM Mkwakwani Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ngao ya jamii watakutana na matajiri wa Chamanzi Azam FC huku Simba SC wao wakiminyana na Singida Fountain Gate katika hatua ya nusu fainali timu zote zikitafuta nafasi ya kuanza vyema msimu 2023/2024 .