Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

KARNE YA AI: 'SADC BADO KUNA PENGO LA MAWASILIANO YA SAYANSI'

December 02, 2025 Add Comment




Na Veronica Mrema - Pretoria 

Ulimwengu wa sayansi na teknolojia unasonga kwa kasi ya ajabu. Mataifa makubwa duniani yanawekeza kwenye ubunifu, utafiti wa kisayansi, na teknolojia za kisasa.

Teknolojia kama akili unde, kilimo cha kisasa na tiba za kibunifu zaidi zinabadilisha maisha katika mataifa makubwa duniani.

Karne ya akili unde [AI], roketi zinavuka anga, kuna uvumbuzi na gunduzi nyingi katika teknolojia mpya kwa kasi ambayo dunia haijawahi kushuhudia.

Mataifa makubwa yanawekeza, yanashirikiana, na yanapasha habari za sayansi kwa umma wao kwa kasi.

Lakini upande mwingine wa dunia, ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika [SADC], bado kuna pengo kubwa katika mawasiliano ya sayansi. 

Watafiti wanagundua, Serikali zinafanya miradi, taasisi zinavumbua, lakini taarifa 'hazitembei' kwa kasi inayohitajika.

Bado haziwafikii vema wananchi wake, hazijengi uelewa na hazifanyi sayansi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Ndani ya SADC, bado kuna pengo kubwa kati ya maendeleo ya ki-sayansi na jinsi ambavyo taarifa hizo zinavyowafikia wananchi.

"Kwa sababu nchi nyingi za SADC bado hazina mkakati wa mawasiliano katika masuala ya sayansi,".

Yameelezwa hayo na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Afrika, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (DSTI), Afrika Kusini Mwampei Chaba.

Ni wakati alipokuwa akifungua mdahalo wa siku moja wa waandishi wa masuala ya sayansi kutoka nchi 18 wanachama wa SADC.

Amesema kutokana na pengo lililopo katika upashanaji habari kuhusu maendeleo ya sayansi katika nchi hizo, ndiyo maana DSTI iliona vema kuwaleta pamoja waandishi wa habari na kufanya mdahalo huo.

Ni katika mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za masuala ya sayansi [WCSJ2025] unaofanyika Pretoria nchini Afrika Kusini.

Akifungua mjadala huo, aliweka wazi changamoto kubwa wanazokutana nazo waandishi wa sayansi katika ukanda huu.

“Nchi nyingi katika SADC bado hazina mkakati wa ushirikiano katika mawasiliano kuhusu sayansi. Hiyo ndiyo sababu upashanaji habari za sayansi unakumbwa na changamoto nyingi.”

Ameongeza "Ukosefu wa mkakati huo unawafanya waandishi wengi kukosa ushirikiano wanaohitaji kutoka kwa Serikali zao.

"Mnashindwa kuwa karibu na watafiti, mnakosa mazingira rafiki ya kupata habari, pamoja na fursa za ufadhili au mwaliko kwenye matukio muhimu yanayohusu sayansi na uvumbuzi.

Amesisitiza "Kwa hivyo, katika nchi yako na unataka kupata ushirikiano kutoka Serikali [kuandika kuhusu habari fulani inayohusu sayansi] au unataka watambue kazi yako.

"Unataka kufadhiliwa kwa baadhi ya kazi zako. Unataka kualikwa kwenye matukio [kwa wengi wenu], itakuwa ngumu kwa kuwa hawana mkakati wa ushirikiano kuhusu hilo," amesema.

"Mkirudi nchini mwenu kafuatilieni hili kwa undani, nendeni mkaulize wizara [zinazohusika na masuala ya] sayansi, wizara za mawasiliano [iwapo] wameandaa mkakati?.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za sayansi, afya, mazingira na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mdahalo huo kwa ajili ya waandishi wa habari kutoka SADC ulilenga kuwaleta pamoja kujadiliana namna gani watasukuma mbele masuala ya sayansi ndani ya nchi zao kwa upashanaji habari.

"Hii ni warsha ya mafunzo yenye umuhimu mkubwa kwetu. wazo hili lilikuja kwetu mwaka 2022 tulipoandaa Mkutano wa Sayansi Duniani (World Science Forum).

"..,, ambao ulikuwa wa kwanza kuandaliwa barani Afrika. Kwa hivyo, tulitengeneza historia mwaka 2022 kwa kuandaa mkutano wa Sayansi Duniani barani Afrika. 

"Kisha tukaamua kuwa kuleta fursa kama hii barani Afrika bila waandishi, waandishi wa sayansi kuwa kwenye chumba, kungekuwa kupoteza. 

Ameongeza "Tunawezaje kuwasilisha kile tunachofanya katika mkutano, kama idara, kama serikali barani Afrika, kama taasisi zinazofanya utafiti, ikiwa hatuna uandishi wa sayansi kwenye chumba?

"Pia tuligundua kuwa waandishi wa sayansi bado hawana uwezo wa kutosha kuhusiana na uandishi na kuandika makala za sayansi. 

"Hivyo basi, tuliona hitaji la kuunda ushirikiano. Na Stellenbosch alishirikiana nasi kwa kiwango kikubwa. 

Amesema walianza kupanga warsha ya mafunzo, yenye vipengele vingi, ambayo itasaidia kujenga uwezo wa waandishi wa habari katika kuwasilisha kazi tunazofanya kwa ufanisi zaidi. 

"UNESCO ilifadhili baadhi ya wajumbe mwaka 2022, na imeendelea kuwa mshirika wetu tangu wakati huo. 

"Sekretari ya SADC pia imekuwa mshirika wetu, na tunashukuru sana michango waliyotoa kwa waandishi wa SADC kuungana nasi. 

"Chama cha Waandishi wa Sayansi wa Afrika Kusini (SASJA) pia kimeungana nasi, na sisi pia tuko kwenye mshirika mkubwa katika mkutano mwingine wa kihistoria," amebainisha,

Amesema mkutano wa WCSJ2025 walioandaa mwaka huu unatengeneza historia mpya nyingine na walitaka kuwa sehemu ya historia hiyo.

Amesema Afrika Kusini waliunda mkakati wa mawasiliano na ushirikiano katika masuala ya sayansi tangu mwaka 2015 na kwamba walichelewa mno kuunda.

"Taasisi yetu ilianzishwa Juni 2004, hivyo karibu miaka 11 baadaye, tu wakati huo tu tulikuwa na mkakati wa ushirikiano wa sayansi unaotekelezwa kwa sasa, na mchakato wa ukaguzi upo.

Amebainisha "Mwaka huu SADC ilishiriki katika G20. Tulikuwa Rais wa G20 na GSTI ilipanga kile kinachoitwa Wiki ya Utafiti na Ubunifu [Research and Innovation Week]. 

"Pia tulipitisha hati maalumu inayoitwa Azimio la Ushirikiano wa Sayansi wa G20 (G20 Science Engagement Resolutions). 

"Hati hiyo inahimiza nchi za G20 kuweka sayansi kati-kati ya jamii inahimiza kuongeza ufahamu katika jamii zetu kuhusu thamani ya sayansi, na kuwasilisha sayansi kwa njia jamii zinaweza kuelewa.

"Kwa nini tunapaswa kufanya hivyo? Ni kwa nini hii ni muhimu? Sayansi haifadhiliwi vya kutosha, na hili ni changamoto katika jamii nzima.

Amesisitiza "Ikiwa thamani ya sayansi haifahamiki, ikiwa athari ya sayansi haijulikani kwa serikali zetu, jamii zetu, wafadhili wetu na wachangiaji.

"Basi mpango wa kufafanua ni ninyi walioko hapa. Ninyi ndio midomo yetu. Ninyi ndio mabalozi wetu wa kuwasilisha sayansi kwa jamii. 

"Mara sayansi itakapofahamika, mara thamani ya sayansi itakapothibitishwa kwenye hatua za vitendo, kwenye jamii, kwenye vijiji.

"Basi mna nafasi nzuri ya kupata ufadhili kutoka Serikalini, ufadhili kutoka kwa wafadhili na kadhalika. 

"Kwa hivyo, jukumu lenu ni muhimu sana, na tunategemea ninyi kusaidia kuunganisha pengo," amesema na kuongeza, 

"Napenda kuwahimiza kwamba katika wiki hii, mchukue fursa ya warsha nyingi zinazofanyika kuhamasisha sayansi. 

"Matumizi ya data, sita-sita kusema kwamba sayansi inapaswa kuwa kati-kati ya jamii, elimu, viwanda, ili kuendesha maendeleo kwa ujumla. 

"Na haiwezi kuwa katikati ikiwa ninyi hufahami jinsi ya kuwasilisha sayansi. Nami naamini hatuhitaji kuwa wanasayansi ili kuelewa sayansi. 

"Sayansi inapaswa kufafanuliwa kwa mtu wa miaka 85 na mtoto wa miaka 5. Bila kutumia maneno magumu. 

Amesisitiza "Ikiwa mtu hawezi kueleza, ikiwa mwanasayansi unayemhoji hawezi kueleza sayansi yao kwa njia unayoielewa, basi hawafanyi kazi nzuri. 

"Na pia unapaswa kuwa na uwezo wa kuhimiza wanasayansi kuzungumza na kuwasilisha sayansi kwa njia kila mtu anaweza kuelewa.

Amehoji "Je, unajua waandishi mashuhuri wa sayansi barani Afrika? Kwa nini haingewezekana iwe wewe?

"Kwa nini haingewezekana iwe wewe?” aliuliza, akiwahimiza washiriki kuwa wao wenyewe wanaweza kuwa waandishi mashuhuri wa sayansi Barani Afrika. 

“Kuna waandishi wa sayansi mashuhuri duniani kote, lakini sio barani Afrika. Afrika inahitaji sayansi kwa maendeleo zaidi kuliko kanda nyingine yoyote duniani. 

"Hivyo basi, tufanye lengo letu kuwa na waandishi mashuhuri wa sayansi katika jamii zetu, nchi zetu, ndani ya SADC na barani kote. 

Amesisitiza "Vinginevyo, mbona mko hapa? Kwa nini mko hapa ikiwa hatutumiwe kile tulicho nacho kuwasilisha sayansi na kuifanya iwe ‘fashionable’?”

Amehimiza waandishi wa habari kutumia vema majukwaa ya kidigitali kama fursa ya kufikisha taarifa muhimu zinazohusu sayansi kwa kundi la vijana ambalo kubwa lipo kwenye majukwaa hayo.

"Kila mtu yupo TikTok, kila mtu yupo YouTube, lakini lazima tuone maudhui ya sayansi pia kwenye TikTok au YouTube. 

"Tumia majukwaa haya maarufu kuwasilisha sayansi. Tuwafikie vijana walipo kwenye YouTube, Instagram na mitandao mingine na kuwapa elimu ya sayansi kwa njia wanayoielewa.”

Picha zote kwa hisani ya DSTI

WAZIRI MCHENGERWA ATOA SIKU 21 ZA KUANDALIWA KWA WITO WA KUVUTIA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA NCHINI

WAZIRI MCHENGERWA ATOA SIKU 21 ZA KUANDALIWA KWA WITO WA KUVUTIA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA NCHINI

November 25, 2025 Add Comment




Na WAF – Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ametaka ndani ya siku 21 Wizara ya Afya kupitia Idara ya Huduma za Dawa na ofisi ya Mfamasia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kuandaa wito wa uoneshaji wa nia (Call of Expression of Interest) ili kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.

Akizungumza mbele ya Wataalam wa Sekta ya Afya Novemba 24, 2025 katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam, Waziri Mchengerwa amesema hatua hiyo inalenga kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

“Tuandae ‘Call of Expression of Interest’na tuwaonyeshe yale ambayo tunaweza kushirikiana nao katika utengenezaji wa dawa lakini pia tuwakaribishe katika uwekezaji wa viwanda vingi vya dawa na vifaa tiba hapa nchini” amesisitiza Waziri Mchengerwa huku akitoa siku 21 kwa wito huo kuwa umeandaliwa na kutolewa.

Amesema kuwa uwekezaji wa viwanda vya dawa hapa nchini utairahisishia Serikali katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa kwa usalama wa afya za Watanzania huku pia kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kununua bidhaa za afya kutoka nje ya nchi.



BALOZI YAKUB APONGEZA MUHIMBILI KUPELEKA WATOA HUDUMA ZA KIBINGWA WENGI NCHINI COMORO

October 01, 2025 Add Comment


Balozi wa Tanzania nchini Comoro Saidi Yakub ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kupeleka idadi kubwa ya madaktari bingwa bobezi katika kambi ya matibabu nchini humo  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati wa ziara yake visiwani humo.

Akizungumza hii leo katika mahojiano maalumu na Afisa Habari kutoka Idara ya Habari ya MNH,  Balozi Yakub amesema hospitali hiyo imepeleka jumla ya madaktari bingwa saba wa mgonjwa mbalimbali ukilinganisha na taasisi nyingine zinazoshiriki kambi hiyo.

" Hospitali ya Muhimbili imetuletea zaidi ya madaktari saba na katika wataalam hao watakuwa katika mgonjwa ya figo, ngozi, macho, meno,  masuala ya uzazi kwa akina mama pamoja na magonjwa ya kinamama"



Aidha, Balozi Yakub ameongeza kuwa licha ya kambi ya matibabu kuanza kuanza Oktoba 04, 2025, tayari  zaidi ya watu 1000 wamekwisha kujisajili ili kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE WAIMARIKA

September 27, 2025 Add Comment




📌 *Wapanda kutoka asilimia 95 hadi 96.16 katika kipindi cha robo mwaka*

📌 *Mhandisi Mramba asema ongezeko hilo linaakisi utoaji wa huduma kwa wananchi*

📌 *Apongeza Taasisi kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa Wananchi.*

📌 *Asisitiza mitandao ya kijamii kutumika ipasavyo utoaji elimu Nishati Safi ya kupikia.*

Imeelezwa kuwa, utendaji kazi wa Wizara ya Nishati kupitia Taasisi inazosisimamia umezidi kuimarika na kufikia asilimia 96.16 katika kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025.

Hayo yamefahamika wakati wa kikao cha Tano cha Tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa robo nne ya mwaka 2024/2025 kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba.Tathmini hiyo ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati imeonesha kuwa katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati umeimarika kwa zaidi ya asilimia 96 kutoka asilimia 95 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025.

Kufuatia tathmini hiyo, Mha. Mramba amewapongeza Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi kupitia utekelezaji wa miradi na utoaji huduma kwa wananchi hali inayoleta matokeo chanya katika Sekta ya Nishati.“Tathmini hizi zinaakisi kile tunachokitekeleza kwani huduma zimeendelea kuboreshwa pamoja na kuimarika zaidi, sisi kama Wizara tumeendelea kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora kwa wananchi”.Ameeleza Mha. Mramba

Katika kikao hicho, Mha. Mramba amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati jambo ambalo limeleta ongezeko la kuimarika kwa utoaji huduma.Aidha, kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, amesisitiza kutumia mitandao ya kijamii katika kuitangaza nishati hiyo hususani matumizi ya majiko yanayotumia umeme kidogo akieleza kuwa mitandao ya kijamii inanguvu kubwa ya kufikisha habari kwa watu wengi na kwa muda mfupi lengo likiwa ni kutimiza adhma ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wananchi wanahama kutoka matumizi ya Nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Vilevile,amekipongeza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Wizara ya Nishati kwa kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi huku akisisitiza kuwa Kitengo hicho kipewe ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Idara, Vitengo na Taasisi zinawasilisha taarifa za utendaji kazi kwa wakati ili kitengo hicho kiongeza ufanisi zaidi katika kazi ya tathmini na hivyo kuboresha utendaji kazi.Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amezipongeza Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Nishati kwa utendaji kazi wenye kuleta matokeo chanya kama ambavyo tathmini ya utendaji kazi ilivyoonesha kuwa ufanisi wa kazi umeendelea kuboreshwa na kuimarika zaidi.

Awali, Akiwasilisha taarifa ya tathmini ya utendaji kazi kwa Wizara na Taasisi zake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Wizara ya Nishati, Bi. Anita Ishengoma alisema kuwa kutoka zoezi la tathmini lianze kufanyika, limeleta ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na mipango ya Wizara kwani utendaji kazi wa Taasisi umeongezeka.Amesema kuwa Idara/Vitengo zilizofanya vizuri zaidi katika tathmini iliyofanyika katika Wizara ya Nishati kwa kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025 ni Idara ya Umeme na Nishati Jadidifu (nafasi ya kwanza), Kitengo cha Manunuzi -(Nafasi ya Pili) na - Kitengo cha Tehama ( Nafasi ya Tatu).

Aidha, Taasisi zilizofanya vizuri zaidi katika utendaji kazi kwa tathmini iliyofanyika katika kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025 ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) - nafasi ya kwanza), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) -nafasi ya Pili) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA)- nafasi ya Tatu).

Mikoa ya Kitanesco iliyofanya vizuri katika utendaji kazi kwa tathmini iliyofanyika katika kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025 ni Manyara (nafasi ya kwanza), Kinondoni Kusini ( nafasi ya Pili) na Simiyu ( nafasi ya Tatu).

Ilielezwa kuwa utendaji kazi wa mikoa ya kitanesco kwa ujumla umeimarika kwani hamna mkoa ambao utendaji wake umekuwa chini ya asilimia 91.83.

Katika Kikao hicho pia Taasisi ziliweza kuwasilisha taarifa za utendaji kazi wake.

kikao hicho kilihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakurugenzi wa Vitengo Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara mbalimbali, Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake pamoja na Mameneja wa Kanda wa TANESC
MUHAS  YAPEWA JUKUMU KUU KUANDAA WATAALAMU BINGWA WA MOYO NA MISHIPA YA DAMU

MUHAS  YAPEWA JUKUMU KUU KUANDAA WATAALAMU BINGWA WA MOYO NA MISHIPA YA DAMU

September 22, 2025 Add Comment

 

Na.Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) utakuwa chachu ya kukuza ujuzi wa wataalamu wa afya nchini.

Prof. Nombo alitoa kauli hiyo Septemba 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Uendeshaji ya mradi huo, kilichofanyika katika Kituo cha Umahiri kilichopo Mloganzila. Alieleza kuwa mradi huo ni ushahidi wa wazi wa namna Serikali inavyowekeza katika kuimarisha elimu ya afya na kuhakikisha taifa linapata wataalamu mahiri wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

“MUHAS ni taasisi inayotoa utaalamu wa kisayansi na kuandaa wataalamu wa afya kwa kiwango cha juu. Kituo hiki ni mahali pa kufundisha mabingwa na bobezi katika sayansi ya moyo na mishipa ya damu. Tunaona vifaa vinavyotumika ni vya kisasa, hivyo tunatarajia wananchi kunufaika kwa kiwango kikubwa kupitia huduma zitakazotolewa hapa,” alisema Prof. Nombo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Appolinary Kamuhabwa, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kilichopo Mloganzila, pamoja na ushirikiano wa kimataifa uliowezesha chuo hicho kupata ufadhili wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia.

Prof. Kamuhabwa amesema kuwa mchango wa Serikali na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali umeimarisha uwezo wa MUHAS katika kutoa mafunzo ya kibingwa na kuendeleza tafiti za kisayansi.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kitaalamu wa MUHAS katika kutoa mafunzo ya vitendo na huduma za kibingwa, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kisasa kwa ajili ya tafiti na mafunzo ya afya ya moyo na mishipa ya damu.

DKT. BITEKO AZINDUA TEKNOLOJIA YA KUONDOA UVIMBE MWILINI BILA UPASUAJI

August 27, 2025 Add Comment




📌 Ni kwa mara ya kwanza kufanyika Afrika Mashariki na Kati


📌 Aipa kongole Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 kwa wagonjwa 50 wa kwanza


📌 Asema Serikali itaendelea kuweka msukumo ushirikiano na Sekta binafsi


📌 Awaasa Watendaji Wizara ya Afya kutoogopa kujifunza pale Sekta binafsi inapofanya vizuri


📌 Wagonjwa 300  wanufaika na teknolojia ya utoaji uvimbe bila upasuaji


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameziindua teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayofahamika kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU) katika Hospitali ya Kairuki ikiwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kuzinduliwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Akizindua huduma hiyo Agosti 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko amepongeza Watendaji wa hospitali ya Kairuki pamoja na muasisi wake Hubert Kairuki na Mkewe kwa uthubutu wao katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma hiyo ya HIFU ambayo imeiweka Tanzania katika rekodi ya kutoa uvimbe bila kufanya upasuaji  barani Afrika suala ambalo pia litaongezea nchi mapato.

Ameeleza kuwa awali huduma ya HIFU barani Afrika likuwa ikipatikana katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.

Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 la gharama za matibabu ya utoaji uvimbe bila upasuaji kwa wagonjwa 50 wa kwanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo ikiwa ni kielelezo cha Watendaji wa hospitali hiyo kuonesha utu kwa Watanzania, kuacha alama njema na kuunga  mkono dhamira ya Serikali ya kutoa huduma kwa watanzania kwa gharama nafuu.

Dkt. Biteko amesema kuwa kufanyika kwa tukio hilo muhimu  ni kielelezo cha Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa msukumo sekta binafsi na kuikuza ili kutoa huduma za matibabu kwa wananchi kwa ufanisi na kusogeza karibu huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani ndani ya nchi hivyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono Sekta binafsi.

·Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kuanzisha Idara ya huduma za dharura ambayo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9,000 kwa mwaka. 

Katika hatua, nyingine, Dkt. Biteko amewataka Watendaji katika Wizara ya Afya kutoogopa kujifunza kutoka Sekta binafsi pale inapofanya vizuri na wawape ushirikiano wakati wote siyo nyakati za ukaguzi tu kwani lengo la Serikali ni kufikisha huduma bora kwa wananchi kwa ushirikiano wa Serikali na sekta hiyo.


Kuhusu ombi la Hospitali ya Kairuki la kujengewa barabara ya lami ya mita 300 kuelekea kwenye hospitali hiyo ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi ameelekeza Manispaa ya Kinondoni kufanyia kazi ombi hilo.

Dkt. Mwinyikondo Amir, kutoka Wizara ya Afya akimwakilisha Waziri wa Afya, amesema kuwa tukio hilo ni ishara ya ushirikiano uliopo kati ya sekta binafsi na Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema Wizara ya Afya imekuwa na ushirikiano mkubwa na Hospitali ya Kairuki katika masuala mengi ikiwemo matumizi ya Bima ya Afya na kwamba pande zote mbili zinatambua kuwa zina wajibu wa kutekeleza dira ya maendeleo ya 2050 inayoelekeza uwepo wa jamii yenye afya bora.


Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Afya na Elimu Kairuki, Kokushubila Kairuki ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.


Amesema sekta ya afya imekuwa na maendeleo makubwa chini ya uongozi wa  Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba  hospitali hiyo itaendelea kuunga  mkono juhudi hizo hasa ikiwa ni utekelezaji wa Dira 2050 inayolenga kujenga Taifa lenye uchumi imara na afya bora.


Amesema gharama za kuweka teknolojia hiyo ya HIFU ni shilingi Bilioni 12 na milioni 300.

 

Aidha amesema kutoka huduma ya HIFU ianze kutolewa tayari wananchi 300 wamepata huduma za uchunguzi huku 298 wakipata matibabu.


 Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kairuki,  

Dk. Onesmo Kaganda alisema uzinduzi wa HIFU ni tukio la kihistoria kwakuwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo  kuzinduliwa  katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Amesema teknolojia hiyo barani Afrika  imeanzishwa katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.


Ameeleza kuwa HIFU ni Teknolojia ya kisasa inayotumia Mawimbi Sauti (Sound Waves) b kutibu aina mbalimbali za uvimbe mwilini bila upasuaji, ikiwemo uvimbe wa saratani na usiokuwa wa saratani katika maeneo kama Matiti, Kongosho, Kizazi kwa Wanawake, na Tezi Dume kwa wanaume.


Ameeleza  faida za huduma hiyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na kovu kwa kuwa hakuna upasuaji, mgonjwa hawekewi nusu kaputi na mgonjwa hupona kwa muda mfupi na kurejea katika shughuli zake, matibabu hayahitaji kumwongezea damu mgonjwa hata kwa wagonjwa wenye upungufu wa damu, pia kupunguza gharama za kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.


Ameongeza kuwa, faida nyingine ya HIFU ni pamoja na tiba shufaa ambayo husaidia dawa za saratani kufanyakazi vizuri mwilini, kufubaza kukua kwa saratani mwilini (slowdown disease progression) na kupunguza maumivu kwa wagonjwa wa saratani. 


Amesema mtambo huo ulianza kufanya kazi desemba 2023 ambapo mpaka sasa wagonjwa 303 wamefanyiwa uchunguzi na 298 kupatiwa matibabu na kumekuwa na matokeo chanya ya wagonjwa hao.

Amesema kuwepo kwa teknolojia hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya za kuifanya  Tanzania kuwa kitovu cha utalii Tiba Kusini mwa jangwa la Sahara.

Pia, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira wezeshi ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi Binafsi.

Kuhusu Idara ya Huduma za Dharura iliyozinduliwa katika Hospitali ya Kairuki amesema itakuwa  na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9000 kwa mwaka na pia imejizatiti kwa magonjwa ya dharura pindi yatakapotokea.


Mwisho