JAMII YAASWA KUTOA USHIRIKIANO KWA JESHI LA POLISI.

JAMII YAASWA KUTOA USHIRIKIANO KWA JESHI LA POLISI.

August 30, 2013
Na Amina Omari,Tanga
Jamii imeaswa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi badala ya kuwaona ni kama maadui kwao hasa wanapofuatilia taarifa za uhalifu  ili kuhakikisha wanashirikina katika kulinda na kuzuia vitendo vya kihalifu  vinavyofanyika miongoni mwa jamii .
Ushauri huo umetolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Costantine Massawe  wakati  wa maadhimisho ya siku ya polisi ambapo kwa mkoa wa Tanga wameadhimisha kwa kutembelea kituo cha waathirika wa madawa ya kulevya  SOBAR HOUSE pamoja na kituo cha kulelea watoto yatima na kutoa misaada ya kijamii.
Alisema jamii imekuwa ikilichukulia jeshi hilo kama sehemu ya maadui jambo ambalo sio kweli kwani  nia ya uwepo wao ni kuhakikisha wanalinda mali za wananchi pamoja na kuzuia uhalifu wa aina yoyote usitokee miongoni mwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Lengo la maadhimisho ya siku ya polisi ni kufanya kazi ambazo zitaonyesha tupo karibu na jamii ikiwemo kama kufanya usafi kwenye hospitali  kwa Tanga tumeamua kutembelea ndugu zetu walioathirika na madawa ya kulevya pamoja na watoto yatima “alisema Kamnda Massawe.
Awali akiwa SOBAR HOUSE aliwataka waathirika hao kuhakikisha hawarudi tena kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya baada ya kupona na kuwahamasisha wenzao kutotumia madawa hayo kwa kuwaeleza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizo
“Nawaomba baada ya kupona msikubali kurudi tena kwenye utumiaji wa madawa hayo kwani yanarudisha nyuma maendeleo yenu na taifa kwa ujumla kwani  mnapoteza muda mwingi kwenye matibabu yake na nguvu kazi ya taifa inapotea bure”aliwaasa Kamanda.
Hata hivyo akiwa kwenye kituo cha watoto yatima cha Abdillah bin Omari  aliiasa jamii ya wanatanga  kutowatenga watoto hao  bali  kuwatambua ni  sehemu yao   kwa kuwaonyesha upendo ili wajiihisi nao ni wajamii kama wengine
Jumla ya msaada wenye thamani ya sh Laki saba ulitolewa kwa vituo hivyo ikiwemo fedha taslim sh laki tanona katoni nne za maji ya matunda  kwa  kituo cha SOBAR HoUSE pamoja na mchele kilo 50 ,mafuta ya kupikia lita 10  na maji ya matunda katoni sita kwa ajili ya kituo cha Abdi Abdulrahmani

TFF, AZAM MEDIA ZASAINI MKATABA WA BIL. 5.5/-

August 30, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kampuni ya Azam Media leo (Agosti 30 mwaka huu) wamesaini mkataba wa haki za kipekee za televisheni (exclusive rights) utakaoiwezesha Azam TV kuonesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

Mkataba huo wa miaka mitatu wenye thamani y ash. 5,560,800,000 umesainiwa kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani amesaini kwa niaba ya TFF wakati aliyesaini kwa upande wa Azam Media ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Thys Torrington.

Ligi Kuu ya Tanzania sasa itakuwa ikipatikana kupitia kisimbuzi (decorder) cha Azam TV kitakachokuwa na chaneli zaidi ya 50. Mechi hizo zinatarajiwa kuoneshwa moja kwa moja wakati wowote kuanzia mwezi ujao.

Makamu wa Rais wa TFF, Nyamlani amesema udhamini huo wa televisheni ni fursa pana kwa klabu kwani zitaweza kujitangaza zaidi huku wachezaji nao wakipata soko zaidi za mpira wa miguu.

KOCHA KIM AONGEZA MMOJA TAIFA STARS

August 30, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameongeza kwenye kikosi chake beki David Mwantika kwa ajili ya mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.

Mwantika ameitwa kwenye kikosi hicho kuziba nafasi ya beki Kelvin Yondani ambaye ni majeruhi. Wachezaji ambao ni majeruhi na Kim amewaondoa kwenye kikosi hicho ni waweze kushughulikia matibabu yao ni Athuman Idd, Shomari Kapombe na John Bocco.

Taifa Stars imeingia kambini jana (Agosti 29 mwaka huu) na imeanza mazoezi leo jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager pia itakuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa.