HABARI

SIASA

ELIMU

Recent Posts

TANROADS KUFUNGA BARABARA YA TANGA–SEGERA KWA SAA NNE UKARABATI MADARAJA YA HALE, MAGUZONI

October 18, 2026 Add Comment







Na Oscar Assenga, TANGA

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga unatarajia kufanya ukarabati wa madaraja ya Hale na Maguzoni yaliyopo katika barabara kuu ya Tanga–Segera, kwa lengo la kuimarisha usalama na kulinda miundombinu hiyo dhidi ya athari za mvua kubwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya wataalamu wa TANROADS kufanya ukaguzi wa barabara na madaraja mkoani humo kufuatia taarifa za uwepo wa mvua nyingi za El Niño nchini, ambapo walibaini changamoto zinazohitaji kushughulikiwa katika madaraja hayo.

Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama K Msama alisema ukarabati huo utahusisha maeneo ya chini ya madaraja yanayopitisha maji pamoja na vyuma vilivyopo katika sehemu za juu za madaraja ambavyo vimeathiriwa na kutu.

Alisema wamebaini kuwa maji ya mvua yanapita katika baadhi ya maeneo ya madaraja na kusababisha vyuma kupata kutu na kuharibika, hali inayohitaji hatua za haraka ili kuzuia uharibifu zaidi na kuhakikisha madaraja yanaendelea kutekeleza majukumu yake.

Alisema ukarabati huo unalenga kuimarisha uimara wa madaraja hayo na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, wakiwemo wasafiri na wasafirishaji wanaotumia njia hiyo muhimu.

Alifafanua kuwa ili kuruhusu kazi hiyo kufanyika kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa, barabara ya Tanga–Segera itafungwa kwa muda wa saa nne, kuanzia asubuhi hadi saa sita mchana, Jumanne, Oktoba 20.

Alisema TANROADS imejipanga kuhakikisha mitambo na vifaa vinavyohitajika vinafika eneo la kazi ili ukarabati ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuruhusu magari kuendelea na safari zake.

Meneja huyo aliwataka wasafiri na wasafirishaji kupanga safari zao mapema kwa kuzingatia muda wa kufungwa kwa barabara hiyo ili kupunguza usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa kazi hizo.

Barabara ya Tanga–Segera ni kiunganishi muhimu cha usafiri na usafirishaji, inayohudumia magari yanayotoka Dar es Salaam kupitia Chalinze kuelekea Segera na kuendelea Tanga, pamoja na magari yanayotoka mikoa ya Singida, Arusha na Kilimanjaro.

Aidha, barabara hiyo hutumiwa na magari yanayohudumia shughuli za Bandari ya Tanga pamoja na usafirishaji unaotoka eneo la Horohoro mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Kosani alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha madaraja na barabara vinaendelea kuwa salama kwa matumizi ya wananchi na wadau wa usafirishaji.


UGUNDUZI MPYA WA GESI ASILIA MNAZI BAY KUONGEZA AKIBA YA GESI NCHINI - DKT.HOMERA

October 18, 2026 Add Comment



Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam


Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema zoezi la uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara limekamilika kwa mafanikio makubwa, ambapo imegunduliwa gesi asilia inayotarajiwa kuongeza kiasi cha nishati hiyo kutoka futi za ujazo trilioni 57.54 zilizopo sasa.

Amesema Serikali inatarajia kuzindua visima hivyo wiki ijayo katika Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara, ambapo pia itatangaza kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa kutokana na shughuli hizo za uchimbaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 18, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Mhe. Homera amesema visima hivyo, viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti, vimechimbwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na mwekezaji, kampuni ya M&P.

Amesema ugunduzi huo unazidi kuiwezesha Serikali kuwa na nishati ya gesi asilia kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.

Mhe. Homera ameongeza kuwa Serikali kupitia TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.

Ameeleza kuwa shughuli za uchukuaji wa data za mitetemo zinaendelea katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na zinatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku maandalizi ya uchorongaji wa kisima cha uzalishaji na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yakiendelea katika Kitalu cha Ntorya.

Kuhusu maendeleo ya Kitalu cha Ntorya, Mhe. Homera amesema ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka Ntorya hadi Madimba umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kuanza mapema mwaka 2027 na kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku.

Ameeleza kuwa TPDC inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi katika usambazaji wa gesi asilia majumbani na kwenye magari (CNG), ambapo hadi Septemba 2026, jumla ya vituo 22 vilikuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma.

Katika hatua nyingine, Homera amesema wiki ijayo Serikali inatarajia kusaini na kukabidhi leseni mpya za utafutaji mafuta na gesi asilia (PSA) kwa TPDC, hatua itakayoliwezesha shirika hilo kuendelea na shughuli za utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali hizo nchini ambapo Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi atakuwa mgeni rasmi.

Akizungumzia sekta ya umeme, Mhe. Homera amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka na kufikia Megawati 4,646 kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia, jua na nishati nyingine mbadala, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo huo hadi Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Amesema katika kuimarisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu, Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Kishapu II wenye uwezo wa Megawati 100 ukiendelea.

Aidha, miradi mingine yenye uwezo wa zaidi ya Megawati 600 ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi.

Kuhusu miundombinu ya usafirishaji umeme, Waziri huyo amesema Serikali imekamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma tangu Septemba 2026, ambao umeimarisha ubora na kiwango cha umeme kinachofika katika mikoa ya Magharibi na Kaskazini mwa nchi.

Ameongeza kuwa Mradi wa Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwa Novemba 2026 na kuunganisha Mkoa wa Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza, huku Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga ukitarajiwa kuwashwa Februari 2027 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na maeneo ya viwanda ya Mkuranga.

Aidha, amesema utekelezaji wa Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa na kuondoa changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.



RAIS SAMIA AAGIZA WAKULIMA WADOGO WALINDWE DHIDI YA WAJANJA,UKODISHAJI WA SHAMBA LA SERIKALI MBARALI

October 18, 2026 Add Comment

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ameweka wazi msimamo wa Serikali kuhusu shamba la Highland Estate wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, lililofanyiwa uthamini wa Shilingi bilioni 30, akisisitiza kuwa fedha hizo zinazotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hazipaswi kugeuka fursa ya kujinufaisha kwa watu wachache wenye nguvu za kiuchumi, huku wakulima wadogo waliokusudiwa kusaidiwa wakiendelea kuteseka.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa ziarani Rujewa mkoani Mbeya, Makamu wa Rais amesmea Serikali tayari imetoa Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya malipo ya shamba hilo, lenye takribani hekari 6000, kwa lengo la kulirejesha chini ya usimamizi wa Serikali na kuwawezesha wakulima wadogo kulikodi kwa gharama nafuu, badala ya kuendelea kulipa kati ya Shilingi 600,000 na 700,000 kwa ekari katika maeneo mengine.

 


Katika hatua inayoonyesha kutoridhishwa na uwezekano wa wajanja kupenyeza majina yao kwenye orodha ya wanufaika, Makamu wa Rais amemwelekeza Waziri wa Kilimo kushirikiana na viongozi wa Mkoa, Wilaya, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Taasisi za Serikali kuwabaini wakulima halisi wanaostahili kunufaika na shamba hilo, huku akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya yeyote atakayebainika kuhujumu mchakato huo. 

Amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuwaonea huruma watu wanaotumia nafasi zao kujinufaisha wakati wananchi wa kawaida wanaendelea kuteseka, akionya pia dhidi ya watu wanaoweza kukodi mashamba hayo kwa bei nafuu kutoka Serikalini na kisha kuwakodishia wakulima wadogo kwa gharama kubwa.

Aidha, amemtaka Waziri wa Kilimo kuweka ukomo wa muda wa kukamilisha ugawaji wa maeneo hayo, akisisitiza kuwa wakulima wana familia za kuhudumia, watoto wa kusomesha na maisha yanayohitaji kuendelea.

Akijibu maelekezo hayo, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya malipo ya shamba hilo na inatarajia kukamilisha awamu mbili zilizosalia ndani ya miezi miwili, huku akiahidi kuimarisha utaratibu utakaohakikisha wakulima wadogo ndio wanaonufaika. Amesema shamba hilo halitagawiwa kwa wananchi kama umiliki wa moja kwa moja, bali litaendeshwa kwa mfumo wa ukodishaji wa msimu kwa gharama nafuu chini ya usimamizi wa Serikali.

Hata hivyo, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa kasi ya utekelezaji lazima iendane na uadilifu, ili dhamira ya Rais Samia ya kuwasaidia wakulima waliopoteza maeneo yao kufuatia mabadiliko ya mipaka ya hifadhi isije ikatekwa na watu wenye maslahi binafsi, na kuwaacha walengwa halisi wakiendelea kusubiri haki yao.

 


Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

18 Oktoba 2026

Rujewa.

TANZANIA YAIMARISHA URATIBU WA KITAIFA KUKUZA KISWAHILI KIMATAIFA

October 18, 2026 Add Comment

Tume ya Taifa ya UNESCO yakutana na BAKITA, BAKIZA na TATAKI kujadili ushirikiano wa maendeleo ya Kiswahili

Dar es Salaam, 16 Oktoba 2026

Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na viongozi na wataalamu kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), kwa lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano wa kitaasisi katika kukuza nafasi ya lugha ya Kiswahili katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Kikao hicho cha pamoja cha kiofisi kimewakutanisha wawakilishi wa taasisi hizo nne kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika masuala yanayohusu maendeleo ya Kiswahili, kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha juhudi za kitaifa na kutumia fursa zinazopatikana katika majukwaa ya kimataifa.

Katika mazingira ambayo lugha zina nafasi muhimu katika mawasiliano, utamaduni na ubadilishanaji wa maarifa, uratibu wa kitaifa ni nyenzo muhimu katika kuendeleza nafasi ya Kiswahili na kuongeza mwonekano wake katika majukwaa mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Kupitia kikao hicho, washiriki walikubaliana kuendelea kutumia mifumo na fursa zilizopo za kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza nafasi ya Kiswahili, sambamba na kuzingatia misingi rasmi ya usanifishaji na maendeleo ya lugha hiyo.

Ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya UNESCO, BAKITA, BAKIZA na TATAKI unaunganisha majukumu na utaalamu wa taasisi hizo katika masuala ya lugha, taaluma, utafiti na maendeleo ya Kiswahili. Ushirikiano huo ni muhimu katika kuweka msingi wa uratibu wa pamoja kuhusu fursa zinazoweza kuchangia kukuza lugha hiyo katika ngazi ya kimataifa.

Aidha, hatua hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa taasisi za kitaifa katika kuendeleza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, maarifa na utamaduni, huku ikiimarisha juhudi za kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kupata nafasi katika mazingira yanayozidi kuunganishwa kupitia mawasiliano ya kimataifa.

Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa katika kutekeleza majukumu yake yanayohusiana na maeneo ya UNESCO, ikiwemo mawasiliano na taarifa, kwa kuzingatia fursa za ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Tume ya Taifa ya UNESCO — Kuimarisha ushirikiano wa kitaifa kwa maendeleo ya lugha, maarifa na utamaduni.

TAIFA GAS YADHAMINI NA KUTOA MAFUNZO YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KWA WATU WENYE ULEMAVU

October 18, 2026 Add Comment

  


Afisa Masoko wa Kampuni ya Taifa Gas, Santina Ngaponda (katikati), akipokea cheti cha udhamini wa semina ya matumizi ya nishati safi kwa watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam. Pembeni yake ni Mwakilishi wa Kampuni ya Badson Group, Francis Ngonga, na Mkurugenzi wa Tupo Sawa Organization, Jackline Mtaita, aliyeketi kwenye kiti cha magurudumu. Semina hiyo iliandaliwa na Tupo Sawa Organization na kudhaminiwa na Taifa Gas.

BARRICK BULYANHULU YAFANIKISHA UJENZI WA SHULE MPYA YA MSINGI KIJIJINI BUSHINGWE

October 18, 2026 Add Comment

Sehemu ya jengo la Shule ya Msingi Bushingwe iliyojengwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa gharama ya Sh. milioni 388.3 kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bushingwe, iliyojengwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa gharama ya Sh milioni 388.3 kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), wakifuatilia masomo katika mazingira bora, salama na rafiki kwa ujifunzaji.

***
#Imeondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.


Katika Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga, utekelezaji wa miradi ya elimu kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu, kuimarisha usalama wa wanafunzi na kufungua fursa mpya, huku ukiwapa wananchi matumaini ya maisha bora.

WANAFUIKA WA TASAF WILAYANI MISUNGWI WAIPONGEZA SERIKALI KUBADILISHA MAISHA

October 18, 2026 Add Comment
*Wasema kwa sasa mambo safi ,wanamudu gharama za maisha 

SERIKALI KUTUMIA MILIONI 600 KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA MAKAMBAKO -PROF.SHEMDOE

October 18, 2026 Add Comment



Na: OWM–TAMISEMI, Makambako

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali itapeleka shilingi milioni 600 katika Halmashauri ya Mji wa Makambako kabla ya Desemba 2026 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kitandililo, hatua itakayosaidia kusogeza huduma bora za matibabu karibu na wananchi.


Prof. Shemdoe ameyasema hayo Oktoba 17, 2026, akiwa Makambako, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na OWM-TAMISEMI kuboresha huduma za afya ya msingi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika wakati wa ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Njombe.


“Mhe. Makamu wa Rais, tumeshapata shilingi milioni 600 ambazo tutazileta hapa Makambako kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kitandililo kabla ya Desemba, ili wananchi wapate huduma bora za matibabu kwa wakati,” amesisitiza Prof. Shemdoe.


Kuhusu ombi la Mbunge wa Makambako ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, la kujenga zahanati mbili, Prof. Shemdoe amesema ofisi yake inaendelea kulifanyia kazi kwa kutafuta fedha ili zitakapopatikana zitumike kujenga zahanati hizo na kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.


Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema anatambua jitihada zilizofanywa na Naibu Waziri wa OWM-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. Dkt. Festo Dugange, pamoja na Waziri wa Nchi, OWM-TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, wakati akiwa Katibu Mkuu, katika kusimamia ujenzi wa Shule ya Mkoa ya Wasichana ya Sayansi ya Vipaji Maalumu iliyojengwa Wanging’ombe.


Ujenzi wa Kituo cha Afya Kitandililo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto, gharama za matibabu na usafiri, huku ukiimarisha afya ya jamii, kuongeza tija na uzalishaji, na kujenga rasilimali watu yenye afya kwa maendeleo endelevu ya taifa.




WAZIRI MKUU KUMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA KATIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA NORMAN E. BORLAUG MAREKANI

October 18, 2026 Add Comment





WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameondoka nchini leo, Jumamosi, Oktoba 17, 2026, kuelekea jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, nchini Marekani, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), utakaofanyika kuanzia Oktoba 20 hadi 22, 2026.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu anatarajiwa kutoa hotuba kuu na kushiriki majadiliano kuhusu maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula na matumizi ya teknolojia katika kuongeza tija, huku akieleza vipaumbele vya Tanzania na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Waziri Mkuu pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Taasisi ya Tuzo ya Chakula Duniani (World Food Prize Foundation) na Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA), pamoja na wadau wa biashara na uwekezaji katika kilimo.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuvutia uwekezaji na teknolojia katika kilimo ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

TBS YAWATAKA WAZALISHAJI WA BIDHAA ZA CHAKULA KUZINGATIA VIWANGO

October 17, 2026 Add Comment
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa bidhaa za chakula nchini kuzingatia viwango na ubora katika uzalishaji ili kulinda afya na usalama wa watumiaji, pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

KAMATI YA BUNGE YATAKA MABORESHO YA USIMAMIZI WA DAMPO LA PUGU

October 17, 2026 Add Comment
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeelekeza kuwepo kwa mpango madhubuti wa kudhibiti na kusimamia Dampo la Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam, ili kupunguza athari za kimazingira na kulinda afya za wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.

MAKAMU WA RAIS AKERWA NA UDANGANYIFU TANROADS MBEYA

October 17, 2026 Add Comment
Na Mwandishi Wetu,Mbeya

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi, amekerwa na uzembe na taarifa za kupotosha kuhusu ufunguaji wa barabara ya njia nne mkoani Mbeya, kuwapunguzia adha watumiaji wa barabara hiyo, baada ya kurejea kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika eneo la Kabwe.

MOOT COURT: WANAFUNZI WA SHERIA WAPATA JUKWAA LA KUONESHA UWEZO

October 17, 2026 Add Comment
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa TRA Paul Walalaze, ameeleza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikishirikiana VIctor's Hub Limited waandaaji wa mashindano (Moot Court Competition) tangu hatua za awali, ikiwemo kutoa ufadhili ili kufanikisha shughuli hiyo.
WALIMU WA UFUNDI TANZANIA KUNUFAIKA NA UTAALAMU WA CHINA

WALIMU WA UFUNDI TANZANIA KUNUFAIKA NA UTAALAMU WA CHINA

October 17, 2026 Add Comment
Na WyEST,Tianjin, China
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zimesaini hati ya makubaliano ya kuimarisha Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi (TVET), kwa lengo la kuboresha ubora wa mafunzo, kuimarisha ushirikiano na viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Hati hiyo imesainiwa Oktoba 17, 2026, jijini Tianjin, na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb), kwa niaba ya Tanzania, na Naibu Waziri wa Elimu wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China China, Mhe. Wang Guangyan.
Makubaliano hayo yanatoa kipaumbele katika kuanzisha Karakana (Luban Workshop], kituo cha mafunzo ya ufundi kinachotumia teknolojia za kisasa pamoja na kuimarisha programu za uhandisi wa ujenzi, upimaji na uchoraji ramani, reli, barabara na madaraja. China pia imeahidi kutoa msaada wa kitaalamu kupitia mafunzo kwa walimu, uendelezaji wa mitaala ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ubadilishanaji wa wataalamu na matumizi ya mbinu za kisasa za ufundishaji.
Aidha, makampuni ya Kichina nchini Tanzania, hususan katika Sino–Tan Industrial Park na sekta za reli, nishati, madini na ujenzi, yamehimizwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi,  Serikali ya Tanzania itateua taasisi zitakazotekeleza  makubaliano hayo na kuhakikisha programu zinaendana na Mfumo wa Kitaifa wa Sifa na Tuzo  (TQF), ili kuimarisha ubora na uendelevu wa mafunzo.
Mbali na makubaliano hayo, Tanzania imenufaika na ushiriki wake katika Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na nchi nyingine kuhusu uboreshaji wa mitaala, viwango vya mafunzo na uhusiano kati ya elimu na mahitaji ya soko la ajira.
Katika mkutano huo, Tanzania imeunga mkono Kiunzi cha Kimataifa cha Viwango vya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (Framework of World Vocational and Technical Education Standards), kinachotoa rejea ya hiari ya kulinganisha viwango huku kikiheshimu mifumo ya elimu ya kila nchi. Akizungumza kuhusu mfumo huo, Mhe. Ameir alisema unaendana na mageuzi ya elimu nchini yanayotekelezwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, linalolenga kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi na umahiri.
Tanzania pia imependekeza vipaumbele vinne vya utekelezaji wa kiunzi hicho, ambavyo ni utambuzi wa pamoja wa sifa, upatikanaji wa ufadhili na vifaa vya kisasa, ubadilishanaji wa walimu na mafunzo, pamoja na tathmini ya hiari kwa ajili ya kujifunza kwa pamoja. Hatua hiyo inaipa nchi nafasi ya kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu viwango vya mafunzo na kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, ikiwemo na China.
Akizungumza katika kikao maalumu cha majadiliano Oktoba 16, 2026, Mhe. Ameir amesema elimu ya ufundi ni nyenzo muhimu ya kuunganisha nguvu kazi ya vijana wa Afrika na maendeleo endelevu ya kiuchumi. Alisisitiza umuhimu wa kuwaandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto katika sekta za reli, nishati, madini, kilimo, gesi na viwanda.
Ushiriki huo na makubaliano yaliyosainiwa yanatarajiwa kusaidia Tanzania kuboresha mafunzo ya ufundi, kuongeza uwezo wa wakufunzi na fursa za mafunzo kwa vitendo. Hatua hizo zinalenga kuandaa vijana wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, kuwawezesha kujiajiri na kuchochea ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

MKUYU AFRICA YAWATAKA MADALALI KUJITAMBUA, KUEPUKA KUCHUKULIWA KAMA ‘VISHOKA’

October 17, 2026 Add Comment

 

DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya Mkuyu Africa imewataka madalali wa nyumba na ardhi nchini kuzingatia maadili ya kazi, kujiendeleza kitaaluma na kujiunga na mifumo rasmi ya usajili ili kujenga uaminifu kwa wateja na kurejesha heshima ya taaluma hiyo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, wakati wa mkutano uliowakutanisha madalali na wadau wa sekta hiyo kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na umuhimu wa kuanzisha mfumo rasmi wa kuwatambua na kuwasimamia.

Juneid alisema sekta ya nyumba, ardhi na ujenzi ina mchango mkubwa katika maisha ya wananchi, hivyo inahitaji watu wenye uaminifu, weledi na uwajibikaji ili kulinda maslahi ya wateja na kuimarisha imani ya umma.

Alisema licha ya kuwepo kwa madalali wengi wanaofanya kazi kwa uaminifu, baadhi ya watu wamekuwa wakijihusisha na shughuli za udalali bila utambulisho rasmi wala mfumo wa kuwawajibisha wanapokiuka maadili, hali inayochangia malalamiko na kuharibu taswira ya taaluma hiyo.

“Tatizo linapotokea kwa mtu mmoja, wakati mwingine jamii inawaona madalali wote kama vishoka. Hali hii inawanyima heshima wale wanaofanya kazi kwa uaminifu na weledi,” alisema Juneid.

Alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Bodi ya Madalali itakayoweka viwango vya kitaaluma, kusimamia maadili na kusaidia kutambua madalali wanaofanya kazi kihalali ndani na nje ya nchi.

Alisema mfumo huo utasaidia pia kuwalinda wateja dhidi ya utapeli na migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa kununua, kuuza au kupanga nyumba na ardhi.

“Tunapokwenda kwa daktari, wakili au mkandarasi, kuna mifumo inayotuwezesha kutambua na kufuatilia wataalamu hao. Madalali nao wanahitaji mfumo utakaowatambua na kuwaweka katika viwango vinavyokubalika,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha madalali nchini, Emmanuel Machibya, alisema kuanzishwa kwa bodi hiyo kutasaidia kuwaunganisha madalali na kuweka msingi wa kutambuliwa kisheria.

Alisema wazo la kuanzisha bodi hiyo limepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali baada ya Mkuyu Africa, kupitia jukwaa la Miliki Mali, kuibua umuhimu wa kuwa na chombo kitakachosimamia taaluma hiyo.

Machibya alisema bodi hiyo inatarajiwa kusaidia kulinda haki na maslahi ya wateja pamoja na wanunuzi, huku ikiwapa madalali mfumo wa kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji.

Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Leonida Sudi Ibrahim, aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwatambua na kuwarasimisha madalali ili waweze kufanya kazi katika mfumo unaotambulika kisheria.

Alisema chama hicho kimejipanga kutoa elimu na mafunzo kwa madalali katika maeneo mbalimbali nchini, kwa msisitizo maalumu kwa wanawake, ili kuwajengea uwezo, kujiamini na kuzingatia misingi ya taaluma.

Ibrahim alisema kupitia mwamvuli wa TBAB, wanatarajia kuanzisha mfumo maalumu wa utambulisho wa madalali na kuendesha mafunzo yatakayowasaidia kuboresha utendaji wao na kuelewa wajibu wao kwa wateja.

Aliwataka madalali wanawake kutokata tamaa kutokana na changamoto wanazokutana nazo, akisema wana uwezo wa kushindana katika sekta hiyo iwapo watajiamini, kujitambua na kutumia fursa zilizopo.

Aliongeza kuwa umoja na urasimishaji wa shughuli zao unaweza kuwasaidia madalali kupata fursa za huduma za kifedha na mikopo kutoka taasisi husika, hatua itakayochangia kuimarisha biashara zao na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.




MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR KUTUA SML AWARDS 2026

October 17, 2026 Add Comment


Tuzo hizo kulenga kukuza usafirishaji, ugavi na uwekezaji


DAR ES SALAAM. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo za Supply Chain, Mobility & Logistics Awards (SML Awards 2026), zinazolenga kutambua ubunifu, ubora na mchango wa wadau katika sekta za ugavi, usafirishaji na lojistiki.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Oktoba 23, 2026, katika ukumbi wa Superdome, Masaki, jijini Dar es Salaam, ikitarajiwa kukutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Mkurugenzi wa SML, Amon John Mtonyi, amesema tuzo hizo zinalenga kutambua mchango wa wadau katika sekta za ugavi, usafirishaji na lojistiki, huku zikitoa fursa ya kuimarisha ubunifu, ushindani na uwekezaji katika sekta hizo.

Miongoni mwa viongozi wengine wanaotarajiwa kushiriki katika hafla hiyo ni Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa; Waziri wa Uchukuzi na Ujenzi wa Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed; Waziri wa Biashara wa Zanzibar, Omar Said Shaaban; pamoja na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Dkt. Nasra Nassor Omar.

Ushiriki wa viongozi hao unatarajiwa kutoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, hususan katika kuboresha mifumo ya usafirishaji, kuongeza ufanisi wa huduma za ugavi na kuvutia uwekezaji.

Kwa makampuni yanayojihusisha na usafirishaji, bandari, biashara, utalii na huduma za lojistiki, hafla hiyo inaweza kuwa jukwaa la kujenga mahusiano ya kibiashara, kutafuta masoko mapya na kuimarisha ushirikiano na wawekezaji pamoja na taasisi za umma.

Aidha, utambuzi wa makampuni yanayofanya vizuri unaweza kuchochea ubunifu, ushindani wenye tija na uboreshaji wa viwango vya huduma, hatua zinazoweza kuongeza ushindani wa biashara za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa wananchi, maendeleo ya sekta za usafirishaji na ugavi yana umuhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuboresha upatikanaji wa huduma na kupanua fursa za ajira na biashara.

Hata hivyo, manufaa ya jukwaa hilo yatategemea namna mahusiano yatakayojengwa yatakavyogeuzwa kuwa uwekezaji, miradi na maboresho yenye matokeo yanayopimika kwa wafanyabiashara na wananchi.


SML Awards 2026 inalenga kuwa zaidi ya hafla ya utoaji wa tuzo kwa kuwaunganisha wadau muhimu na kutambua mchango wao katika sekta zinazosaidia kurahisisha biashara, kuunganisha masoko na kuchochea ukuaji wa uchumi.


Wadau wanaotaka kushiriki katika hafla hiyo wanaweza kupata tiketi kupitia tovuti rasmi ya tuzo hizo: https://smlaward.com/ticket/

SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 218 KATIKA ELIMU,AFYA NA BARABARA MBEYA-PROF.SHEMDOE

October 17, 2026 Add Comment




Na: OWM–TAMISEMI, Mbeya


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia kutolewa kwa shilingi bilioni 75 mkoani Mbeya ambapo sehemu ya fedha hizo zilitumika kujenga shule mpya 57, madarasa 1,100 na nyumba za walimu 23. 


Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imetenga shilingi bilioni 5.2 ambapo sehemu ya fedha hizo zitatumika kujenga madarasa 1,100 ili kujiandaa kuwapokea wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 kupitia mfumo wa double cohort.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Oktoba 16, 2026, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na OWM–TAMISEMI kutatua kero na changamoto za wananchi wa Jiji la Mbeya, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanjelwa, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Mbeya.

“Mwaka huu tuna shilingi bilioni 5.2 ambazo zitatumika kujenga madarasa 1,100 ili kujiandaa kupokea wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na darasa la sita, watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 kwa mfumo wa double cohort, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa mtaala mpya,” amesema Prof. Shemdoe.

Katika sekta ya afya, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza shilingi bilioni 47 mkoani Mbeya kati ya mwaka 2021 na 2026, ambapo sehemu ya fedha hizo zimetumika kujenga zahanati 287, vituo vya afya 33 na hospitali tatu za halmashauri. 

Kwa upande wa barabara, Prof. Shemdoe amesema Serikali imewekeza shilingi bilioni 96 katika Jiji la Mbeya kati ya mwaka 2021 na 2026, ambapo sehemu ya fedha hizo zilizotumika kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 96, zikiwemo kilomita 12.3 zilizojengwa kupitia mradi wa TACTIC, na kwa mwaka huu wa fedha imetenga shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini.

Uwekezaji huo wa shilingi bilioni 218 mkoani Mbeya katika elimu, afya na barabara, uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni hatua muhimu katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuimarisha huduma za kijamii, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.