SEKRETARIETI YAPELEKA WANNE MAADILI

January 15, 2018
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF imewapeleka kwenye kamati ya Maadili viongozi wanne kwa kughushi na udanganyifu. 
 
Viongozi walioshtakiwa kwenye Kamati ya Maadili ni msimamizi wa Kituo cha Mtwara Dunstan Mkundi, Katibu wa Chama cha soka mkoa wa Mtwara Kizito Mbano, Muhasibu msaidizi wa klabu ya Simba Suleiman Kahumbu na Katibu msaidizi wa Klabu ya Ndanda FC ya Mtwara Selemani Kachele. 
 
Sekretarieti inawashtaki viongozi hao kwa makosa ya kughushi pamoja na udanganyifu wa mapato kwenye mchezo namba 94 kati ya Ndanda FC ya Mtwara dhidi ya Simba ya Dar es Salaam iliyochezwa Disemba 30, 2017 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
 
Kwa tuhuma hizo viongozi hao watatakiwa kufika mbele ya kamati Januari 18, 2018.
 
Kamati ya maadili iko chini ya mwenyekiti Wakili Hamidu Mbwezeleni, Makamu Mwenyekiti Wakili Steven Zangira, Wajumbe ni Glorious Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhresa

SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA HUDUMA KWA WAGENI WANAOINGIA NCHINI KUPITIA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA DAR ES SALAAM (JNIA)

January 15, 2018



Na Hamza Temba-Dar es Salaam
...................................................................................
SERIKALI kupitia wizara zake nne tofauti imedhamiria kukabiliana na changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere (JNIA) jijijini Dar es Salaam.
Changamoto hizo ni pamoja na msongamano na joto katika eneo la kuchukulia mizigo, muda mrefu wa upatikanaji wa hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani hapo.
Mawaziri wa Wizara hizo ambao wamefanya ziara ya pamoja katika uwanja huo jana na kukagua shughuli za utoaji huduma ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk.Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk.Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.

Akizungumza uwanjani hapo, Dk. Kigwangalla alisema wamefikia hatua ya kukutana mawaziri hao baada ya wageni hasa watalii wanaiongia nchini kulalamika kuwa wanatumia muda mwingi kuhudumiwa katika eneo la uwanja huo kiasi cha kuwapotezea muda.
Dk.Kigwangala amesema kutokana na malalamiko hayo ya muda mrefu na mengine kadhaa hatua mbalimbali zimechukuliwa tangu Agosti 8 mwaka 2017 manaibu waziri wa wizara hizo nne walipofanya ziara uwanjani hapo kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi changamoto hizo na kwamba kukutana kwao jana ni muelendezo wa kushughulikia kero hizo ambapo mafanikio yameanza kuonekana.
Dk.Kigwangala amesema ipo haja ya kuweka mikakati ya kuboresha huduma katika viwanja vya ndege nchini ukiwamo JNIA huku akisisitiza umuhimu wa watendaji na watoa huduma katika nafasi mbalimbali kuwa wakarimu kwa wageni.
Amesema ni vema hata Polisi walioko uwanjani hapo wakimkamata mgeni basi badala ya kutumia nguvu wawe na ukarimu kwani ni muhimu kumdhibiti mgeni bila kutumia nguvu ili ikibainika hana kosa aachiwe na asiwe na malalamiko ya kunyanyaswa.
Dk.Kigwangala amesema kuna haja kwa wageni wanapokuja Tanzania wakirudi makwao wasimulie ukarimu na uzuri wa nchini yetu. 
Ameongeza anatamani kuona kuanzia uwanjani hapo hadi hotelini ambako mgeni anakwenda anatumia muda mchache, anapata nafasi ya kuona picha za viongozi mbalimbali ambazo zitakuwa uwanjani, picha za wanyama na video ambazo zinaonesha utalii wa Tanzania.

Amesema kumpokea mgeni jambo moja lakini namna ya kumhudumia ni jambo jingine na ndilo muhimu zaidi na akafafanua hata teksi ambayo mgeni ataitumia kusafiri dereva awe na ukarimu hata wa kumsalimia na wakati mwingine kutabasamu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya ndani Ndani Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza baada ya ziara hiyo alisema jitihada mbalimbali zinafanywa kutatua changamoto hizo.

Ametaja hatua ambazo wizara yake inachukua ni kuharakisha utoaji huduma wa hati za kusafiria kwa njia ya kieletroniki.

Pia wameamua kuongeza idadi ya madawati ya kutolea huduma kwa wageni ikiwa sambamba na kuongeza watoaji huduma ili kurahisisha utoaji huduma wa muda mfupi.
“Taarifa zinaonesha kuwa kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma kwani badala ya saa tatu ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda wa utoaji huduma umeshuka hadi saa moja, lengo letu ni kushuka zaidi.
“Mbali ya kuboresha huduma tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi na usalama katika viwanja vyetu vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye nia ovu na nchi yetu.

“Tunafahamu mataifa mengi yameitikia mwito wa uwekezaji nchini hasa katika mikakati ya kufikia Serikali ya Viwanda na uchumi wa kati.
“Hivyo wageni wanakuja kwa nia njema ya kuwekeza lakini hatutaki wale wenye nia mbaya kutumia mwanya huo.Hivyo tutaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika viwanja vyetu,”amesema.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba amesema wanaridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa changamoto zinazoelezwa kuwapo uwanjani hapo.

Amesema wizara yao inatamani kuona idadi ya wageni inaongezeka zaidi na wakati huo huo wakifurahia huduma ambazo wanazipata wakifika nchini kwetu. Alisema Wizara yake itaendelea kuitangaza Tanzania na vitutio vyake ili idadi ya watalii iweze kuongezeka.
“Tumefanya ziara na binafsi niseme tu nimeridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa changamoto hizo,”amesema Dk.Kolimba.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema wizara yao tayari imechukua hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya kufunga viyoyozi (AC) kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.

“AC zilizopo ni za muda mrefu kwani ziliwekwa tangu majengo ya uwanja huo yalipojengwa. Hivyo tayari zimeanza kufungwa AC mpya na ndio maana joto limepungua” amesema.
 Pia amesema wamepata kampuni ambayo itakayofanya ukarabati kwa kuongeza eneo la kukaa wageni wanaosubiri huduma mbalimbali kabla ya kutoka uwanjani.

Amesema kuna jitihada mbalimbali Serikali inafanya jitihada za kuondoa msongamano wa wageni ikiwamo ya kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la kusafiria wageni la Terminal III ambalo litahudumia watu milioni sita badala ya jengo la sasa ambalo wakati linajengwa  lengo lake lilikuwa kuhudumia watu milioni moja.

“Ujenzi wa jengo jipya umekamilika kwa asilimia 70 na litakapokuwa tayari kwa asilimia 100 litaanza kutumika kwa kuwa kasi ya ujenzi inakwenda vizuri,’amesema.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA jana kwa ajili ya kukabiliana nazo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba (wa nne kulia).
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiteta jambo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa tatu kushoto) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) .
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kulia) akiteta jambo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (kulia) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia).


-- Khalfan Said Photojournalist K-VIS MEDIA P.o.box 77807 Dar es Salaam, Tanzania Mobile: +255-784-646-453/+255-653-813-033 Blog: khalfansaid.blogspot.com

MNEC SALIM ASAS AMWAGA MAMILIONI YA FEDHA KATA YA KIHESA KWA AJILI YA MAENDELEO

January 15, 2018
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas,diwani halali wa kata ya kihesa  Jully Sawani na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) manispaa ya Iringa wakifurahia kukabidhiwa kwa hati kwa diwani wa chama hicho tukio hilo lilifanika katika ofisi ya kata ya kihesa likihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na mamia ya wananchi na wanachama wa chama hicho.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas,diwani halali wa kata ya kihesa  Jully Sawani wakizungumza na wananchi waliohudhulia tukio hilo
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas,diwani halali wa kata ya kihesa  Jully Sawani wakiwapokea wanachama wapya kutoka chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) wa kata ya kihesa 
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas akiongea na wananchi walijitokeza kushudia tukia na kupewa cheti diwani wa kata hiyo Jully Sawani

Na Fredy Mgunda,Iringa.

KATA ya kihesa manispaa ya Iringa imeanza kupata neema ya mamilioni ya fedha za kimaendeleo mara baada ya kumpata diwani mpya kupitia chama cha mapinduzi (CCM) baada ya kupita bila kupigwa kutoka na vyama vingine vya siasa kutoweka wagombea.

Akikabidhiwa hati ya utambulisho wa kuwa ndio diwani halali wa kata ya kihesa,Jully Sawani alielezea mikakati ya kimaendeleo ya kata hiyo ambayo ataanza nayo ni kukarabati miundombinu ya barabara kwenye baadhi ya mitaa ya kata hiyo.

“Ukipita kwenye mitaa yetu utagundua kuwa mtaa kama mtaa wa mafifi miundombinu ya barabara sio nzuri kabisho akahidi kuwa ndani ya wiki hii atapeleka kata pila lianze kazi ya kuzikarabati bara bara hizo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wake kwa kuwa wamemtuma kufanya kazi” alisema Sawani

Sawani aliongeza kwa kusema kuwa amejianda kuhakikisha anatatua kero za wananchi kwa kushirikiana na serikali ya manispaa ya Iringa ambayo inatekeleza sera za chama cha mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 huku ikiwa na kauli mbiu inayosema kuwa hapa kazi tu.

“Naomba niseme ukweli wananchi wangu wote wa kata ya Kihesa sasa ni wakati wa kufanya kazi na sio mchezo mchezo mliokuwa mnaufanya nimeomba kuwa diwani kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi wa kata hii anafanya kazi kwa kuhakikisha kuwa familia yake haiwi masikini,ninasema kuwa kila ukilala hakikisha unaukataa umasikini kwa kuutamka wakati unalala tena kwa zaidi ya mara tisa hapo ndio utafanya kazi” alisema Sawani

Aidha Sawani alitoa kilio chake cha kwa kuomba msaada wa kimaendeleo kwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas ambapo alimwambia kuwa wananshida ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Kihesa na kusaidiwa kumalizia ujenzi wa jingo la kibiashara ambalo lipo jirani na ofisi za kata ya hiyo.

“Mheshimiwa MNEC Salim Asas nipo hapa naomba utusidie msaada wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Kihesa na jingo hili ambalo lipo mbele yetu unaliona linahitaji kumaliziwa ili kuweza kuongeza ajira kwa wananchi wa kata yangu hivyo naomba sana msaada wako kukamilisha hivi vyote kwa awamu hii ya kwanza” alisema Sawani

Akihutubia mamia ya wananchi walijitokeza katika hafla hiyo ya kukadhiwa cheti cha kuwa diwani wa kata hiyo Jully Sawani, MNEC Salim Asas alisema kuwa atatoa mifuko miambili ya saruji kwa ajili ya kutatua kero hiyo ya ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Kihesa na kuahidi kuwa ataitembelea shule hiyo kujua changamoto nyingine.

“Leo naanza kwa kutoa mifuko miambili ya saruji lakini nitakuja hapo shule kujionea changamoto nyingine za shule hiyo ili niweze kuzitatua kabisa na kuwaacha wananfunzi wakisoma kwa uhuru kwa lengo la kukuza kizazi chenye elimu bora na kuja kusaidia taifa katika kuleta maendeleo wote tunajua kuwa bila elimu huwezi kupata maendeleo hivyo nitasaidia sana kwenye elimu” alisema Asas

Asas aliwakata viongozi wa kata hiyo kuandaa bajeti ya kumalizia jingo hilo ambalo litaongeza ajira kwa wananchi wa kata hiyo ambao kwa sasa hali zao za kiuchumi zimedolola hivyoa atafanya linalowezekana kuhakikisha kuwa wananchi wa kata hiyo wanabadili na kuacha kuishi kimazoea.

“kata ya Kihesa anayoijua yeye ni ile yenye vijana wengi wasio na ajira ambao kwa bahati mbaya wamekuwa wakishughulishwa kwenye siasa badala ya kuhamasishwa kufanya shughuli za maendeleo” Alisema Asas


Asas alisema vijembe na malumbano ya kisiasa katika kata hiyo yanatosha na akawataka vijana hao kuunda vikundi vya ujasiriamali vitakavyowawezesha kufikiwa kirahisi na mipango mbalimbali ya maendeleo 

SERIKALI KUPITIA DAWASA KUJENGA MITAMBO MITATU YA KISASA YA KUCHAKATA MAJI TAKA JIJINI DAR ES SALAAM

January 15, 2018

 Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, (DAWASA), Bi. Modester Mushi(kushoto), akifafanua jambo leo Januari 15, 2018 kwa kutumia ramani ya mradi wa ujenzi wa mitambo mitatu ya kuchakata maji taka jijini Dar es Salaam, kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, jijini, Mhe. Ali Hapi, wakati alipotembelea eneo la Kilongawima, Mbezi Beach jijini ambako patajengwa moja kati ya mitambo hiyo. Katikati ni Meneja Uhusiano wa Umma wa DAWASA, Bi. Neli Msuya.


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

WIZARA ya Maji na Umwagiliaji, kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, Dar es Salaam (DAWASA), inajiandaa kujenga mitambo mitatu ya kisasa ya kuchakata maji taka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha hali ya mazingira jijini.
Hayo yamesemwa leo Januari 15, 2018 na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa DAWASA, Bi. Modester Mushi wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mitambo hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinodnoni jijini Dar es Salaam, Mhe. Ali Hapi, wakati alipotembelea moja ya maeneo ya mradi huo huko Kilongawima, Mbezi Beach.
“Ujenzi wa mitambo hii utakwenda sambamba na ujenzi wa mfumo wa ukusanyaji maji taka katika jiji la Dar es Salaam ambapo lengo ni kulaza jumla ya kilomita 563 za mabomba ya ukubwa mbalimbali ya ukusanyaji na usafirisha maji taka kutoka sehemu mbalimbali za jiji na kuyamwaga kwenye mitambo mikubwa mitatu itakayojengwa hapa Kilongawima,(Mbezi Beach), Jangwani na Kurasini.” Kaimu Mkurugenzi huyo amemueleza Mkuu wa Wilaya Mhe. Hapi.
Kuhusu ukubwa wa mitambo hiyo, Bi. Modester alisema, Mtambo wa Kilongawima (Mbezi Beach) utakapokamilika, utakuwa na uwezo wa kuchakata maji taka yenye mita za ujazo 16,000 kwa siku, wakati ule wa Jangwani utakuwa na uwezo wa kusafisha (kuchakata) maji taka yenye lita za ujazo 200,000 kwa siku na ule wa Kurasini utakuwa na uwezo wa kuchakata maji taka yenye lita za ujazo 11,000 kwa siku.
“Ujenzi wa mitambo hii utaanza muda wowote mwaka huu wa 2018 na utagharimu kiasi cha dola za Kimarekani Milioini 65.” Alisema.
Akifafanua zaidi jinsi mitambo hiyo ya kisasa itakavyofanya kazi, Bi.Modester Mushi alisema, mitambo hiyo pia itazalisha gesi asilia na umeme kwa ajili ya kujiendesha, na hivyo kupunguza matumizi na gharama za umeme.
“Lakini pia maji yatakayokuwa yamesafishwa yatauzwa na kutumika katika shughuli mbalimbali kama vile kupoozea mitambo na umwagiliaji wa bustani wakati tope litakalobaki baada ya mchakato huo wa usafishaji maji taka litaweza kutumika kama mbolea kwa ajili ya kilimo lakini pia kuendesha bustani za miti ya kivuli na hivyo kulipendezesha jiji.” Alifafanua Bi. Modester na kuongeza,
Katika eneo la Jangwani , bustani ya kisasa itakayokuwa na miti ya kivuli, maua  na viti vya kupumzikia itajengwa ili kuboresha taswira ya eneo hilo la Jangwani na hiyo itakuwa ni mchango wa DAWASA katika kuunga mkono harakati za Serikali za kuboresha usafi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Mhe. Ali Hapi, aliwapongeza DAWASA kwa hatua wanazochukua hususan kazi ya kuanza mradi huo na kuwataka waharakishe utekelezaji wa mradi. “Changamoto kubwa ambayo tubnakabiliana nayo sisi viongozi wa serikali hatuelewi sana ni ucheleweshwaji wa mradi,tunatamani kuona vitu vinatokea na hasa mnapotuhakikishia kuwa fedha zipo, kama mnachangamoto zozote ni vizuri kuzifikisha kwenye mamlaka zinazohusika ili ziwasaidie kutatua changamoto hizo ili kwa pamoja tuweze kuwaletea wananchi maendeleo.” Alisema Mhe. Hapi.
Mheshimiwa Hapi pia alitembelea kituo cha kusukuma maji taka cha Shoppers Plaza, Mikocheni pamoja na kutembeelea maeneo korofi yanayovuja maji taka kwenye eneo la Mikocheni na Mwenge na kuitaka Kampuni inayosimamia uendeshaji wa kuondoa maji taka DAWASCO kuhakikisha wahandisi wake wanatoka maofisini na kukagua maeneo korofi ili kuchukua hatua za kuyarekebisha.
“Nasisitiza tena Wahandisi watembelee maeneo ambayo kazi zao zipo, watembelee barabara zetu, Halmashauri zinatumia fedha nyingi kurekebiusha barabara zetu, zikirekebisha baada ya mwezi mmoja chemba zinapasuka na kuharibu barabara, hatuwezi kuendelea na utaratibu huu, ni lazima tutafute suluhu.” Alisema. 
 Mhe. Hapi akizungumza kwenye moja ya maeneo korofi ya chemba ya maji taka Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara hiyo.
 Mhe. Hapi akizunghumza kwenye eneo korofi la chemba ya maji Taka Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara hiyo.
 Mhe. Hapi (kushoto), akitazama ramani hiyo.

 Mkuu wa Wilaya Mhe. Ali Hapi, (kulia), akifafanua jambo wakati alipotembelea eneo lililopangwa kujengwa mtambo wa kuchakata maji taka huko Kilongawima, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, leo Januari 15, 2018. Kulia ni Meneja Uhusiano wa Umma wa DAWASA, Bi. Neli Msuya.
 Bi. Modester akimsikilkiza kwa makini Mkuu wa Wilaya Mhe. Ali Hapi (hayupo pichani).
 Mkuu wa Wilaya Mhe. Hapi, (kulia), akibadilishana mawazo na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa DAWASA, Bi. Modester Mushi, (kushoto) na Meneja Uhusiano wa Umma, Bi., Neli Msuya.
 Mhe. Hapi akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwenge jijini Dar es Salaam, Bw.Bashiri Hoza, (kulia) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwenge, alipotembelea kuona maeneo korofi ambayo chemba za mitaro ya maji taka hufumuka mara kwa mara kwenye eneo hilo jirani na soko la Mwenge.
 Mhe. Hapi akizungumza mbele ya wananchi alipotembelea maeneo korofi ambayo chemba za maji taka hufumuka mara kwa mara eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Hapi, akitoa maelekezo alipotembelea eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam kuona miundombinu ya maji taka.
-- Khalfan Said Photojournalist K-VIS MEDIA P.o.box 77807 Dar es Salaam, Tanzania Mobile: +255-784-646-453/+255-653-813-033 Blog: khalfansaid.blogspot.com

MBUNGE RITTA KABATI ATOA MSAADA WA MAFUTA MAALUM YA KUPAKA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI MKOA WA IRINGA

January 15, 2018
Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi box la mafuta hayo katibu wa Tas mkoa wa Iringa bwana Leo Sambala katika ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa  
 Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi boxi  la mafuta hayo katibu wa Mufindi bwana Andrea Kihwelo
 Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi  mafuta hayo moja ya walemavu wa ngozi
 Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi boxi la mafuta hayo mwenyekiti wa wilaya ya Kilolo ndugu Anna Masasi 


Na Fredy Mgunda,Iringa

JAMII imetakiwa kuwalea, kuwatunza na kuwajali watu wenye ulemavu wa ngozi albino kwa kuhakikisha kwamba wanaishi katika mazingira mazuri, yenye usalama na sio kuwanyanyapaa pale wanapohitaji mahitaji yao ya msingi.

Aidha Chama cha walemavu wa ngozi (TAS) mkoa wa Iringa kimeshauriwa kuendelea kushirikiana na serikali, ili walemavu hao pia waweze kupata elimu juu ya afya ya usalama wa ngozi pamoja na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili katika maisha yao.


Hayo yalisemwa na mbunge wa viti maalum Ritta Kabati wakati alipokuwa akitoa msaada wa mafuta maalum ya kupaka watu wenye ulemavu wa ngozi albino katika hafla fupi iliyohudhuriwa na walemavu hao ambayo ilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa


“Nampongeza Mwenyekiti wa TAS mkao wa Iringa kwa jitihada zake alizozifanya juu ya namna ya kupata mafuta haya, kama chama endeleeni kuwa wabunifu namna ya kulisaidia kundi hili tete la walemavu kwa kuwalea na kuwatunza katika mazingira mazuri”, alisisitiza mbunge Kabati 

Vilevile Kabati  aliongeza kwa kuwataka viongozi wa chama hicho kutumia fursa waliyopewa na wanachama wao, kuhakikisha kwamba wana ainisha matatizo waliyonayo walemavu wa mkoa wa Iringa na kuyafikisha katika ofisi za serikali ili yaweze kufanyiwa kazi.

Kabati alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inahakikisha kuwa inafakiwa kutatua matatizo ya wananchi wa ikisha maisha yao yanaboreshwa.

“Hata haya mafuta yamenunuliwa na serikali kupitia wizara ya afya ,maendeleo ya jamii ,jinsia ,wazee na watoto na yanasambazwa nchi nzima hivyo sisi viongozi kazi yetu ni kwasaidia usafiri walememavu hawa” alisema Kabati


Awali akitoa maelezo mafupi juu ya changamoto zinazowakabili albino katika mkoa wa Iringa huo, Mwenyekiti wao Hellen Machibya  alisema kuwa wanashindwa kuwafikia wanachama wake kwa urahisi kutokana na kukosa usafiri na rasilimali fedha, kwa ajili ya kuwatimizia mahitaji yao ya msingi. 

Machibya alifafanua kuwa kukosekana kwa fedha kunakwamisha utendaji kazi na uendeshaji wa shughuli husika, hivyo wanaiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kwa kutatua kero zinazowakabili ili kundi hilo tete liweze kusonga mbele kimaendeleo.

Machibya alisema kuwa kazi aliyoifanya mbunge huyo ni kuokoa maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwa watakuwa wanajikinga na mionzi ya jua.

Machibya alisema kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi wamekuwaathirika wakubwa wa ugonjwa wa kasa kutokana na ngozi zao kushambuliwa na jua na kusababisha kuiathiri ngozi hivyo msaada uliotolewa na serikali umeokoa sana maisha.

“Jamani sisi watu wenye ulemavu tunapenda sana kufanya kazi tatizo mionzi ya jua inatuathiri sana na kusababisha kushindwa kufanya kazi zetu kwa uwezo wetu hivyo tunaomba serikali na wadau kama mbunge Ritta Kabati waendelee kutusaidia maana mafuta haya dukani ni gharama sana hivyo watu wenye ulemavu wa ngozi hatuzimudu” Machibya

Lakini Chama cha walemavu wa ngozi (TAS) mkoa wa Iringa wamemshukuru mbunge wa viti maalum Ritta Kabati kwa kuwasidia kuwafikishia mafuta ya kujipaka mwilini kwa ajili ya kujikinga na mionzi ya jua ambayo imekuwa ikiwasababishia kupata ugonjwa wa kansa.

NAIBU WAZIRI WA MADINI MHE BITEKO AUTAKA UONGOZI WA CHUO CHA MADINI DODOMA KUJITATHIMINI

January 15, 2018
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akisikiliza kwa makini maelezo kuhusu mashine zilizotolewa na wafadhili pasina kutumika kwa muda mrefu wakati alipotembelea Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akiwasili Chuo cha Madini Dodoma kwa ajili ya ziara ya kikazi, leo 15 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizuru katika Chumba cha uchenjuaji madini wakati alipotembelea Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akikagua mashine mbalimbali wakati alipotembelea Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018.

Na Mathias Canal, Dodoma

Uongozi wa Chuo cha Madini Dodoma kilichopewa ithibati kamili ya kutoa mafunzo ya umahiri yaani Competence Based Education and Training System (CBET) umetakiwa kujitathmini ikiwemo kutatua changamoto zinazokikabili chuo hicho ndani ya wiki mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko Leo 15 Januari 2018 alipotembelea chuoni hapo na kujionea hali ya ufanisi wa chuo hicho huku akikerwa na uduni wa utunzaji wa vifaa katika chumba cha maabara ya uchenjuaji wa madini.

Mhe Biteko alisema kuwa pamoja na changamoto lukuki walizoainisha katika taarifa ya chuo iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Ndg Vincent Willium Pazzia ikiwa ni pamoja na uchache wa bajeti, uhaba wa wakufunzi katika fani za uhandisi na usimamizi wa mazingira migodini na upungufu wa ofisi za watumishi, wanatakiwa kuwa na mikakati ya kukabiliana nazo ndani ya wiki mbili zitakazofika ukomo mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli haitatoa fedha mahali ambapo hakuna matokeo ili ziliwe na watu wasiokuwa na matakwa mema na Taifa.

Aliongeza kuwa katika Wizara ya madini kumekuwa na malalmiko mengi kuliko utendaji jambo ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu haraka litabakisha usugu na uvivu wa kufikiri kwa baadhi ya watendaji na kusalia kufanya kazi kwa mazoea pasina kuwa na ubunifu.

Naibu Waziri wa Madini Mhe Biteko alisema kuwa wakati Taifa likiwa linaelekea kuwa katika uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda huku rasilimali za madini zikipewa umuhimu mkubwa ni lazima watendaji wakubali kukabiliana na changamoto mbalimbali kwani tiba ya changamoto hizo ni pamoja na kuzikabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.

Aidha, ameutaka uongozi wa chuo hicho cha madini kuhakikisha kuwa kinazalisha wataalamu wengi katika sekta ya madini ambao watalisaidia Taifa kutekeleza majukumu muhimu ya serikali ikiwemo uzalendo na ulinzi wa mali za umma.

Alisema kuwa watendaji wote serikalini wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu kubwa moja la kuhakikisha kuwa wanatekeleza kwa ubora na umakini mkubwa maelekezo rasmi ya serikali ambayo yamebainishwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2015-2020.

SEKTA YA MADINI LAZIMA IWE NA MCHANGO MKUBWA KWENYE PATO LA TAIFA: MHE DOTTO BITEKO

January 15, 2018
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Stanislaus Nyongo akizungumza jambo kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri mwenzake katika Wizara hiyo Mhe Dotto Mashaka Biteko kuzungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018.

Na Mathias Canal, Dodoma

Sekta ya Madini inachangia kati ya asilimia 3.5 mpaka 4 katika Pato la Taifa ukilinganisha na sekta zingine ambazo zimejitutumua kwa kiasi kikubwa katika mchango mahususi wa pato la Taifa nchini Tanzania.

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko amebainisha kuwa kiasi cha kati ya asilimia 3.5 mpaka 4 ni kidogo sana ukilinganisha na umuhimu wa sekta hiyo nchini hivyo Wizara ya Madini imekusudia kuongeza tija katika mchango wa pato la Taifa kupitia sekta hiyo muhimu ya Madini.

Mhe Biteko amebainisha hayo Leo Januari 15, 2018 wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na watumishi wa Wizara ya Madini ofisi Kuu Mjini Dodoma huku akiwataka watumishi wote kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uzalendo mkubwa kwa manufaa ya Taifa.

Alisema kuwa sekta ya Madini ni muhimu nchini kutokana na rasilimali Madini ilizonazo hivyo watumishi wote wanapaswa kufikiria namna ya kufanya kazi kwa tija ili kuwa na ongezeko la mchango mkubwa katika pato la Taifa.

"Natamani nione kwenye taarifa ya robo mwaka ya BOT ikisoma kwamba sekta ya madini inachangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa kuliko ilivyo hivi sasa na hilo naamini linawezekana kwa ushirikiano wa pamoja" Alisisitiza Mhe Biteko

Mhe Biteko alisema kuwa hakuna mtu yeyote ambaye atatutumua mabega kwamba ni mkubwa katika Wizara badala yake ukubwa wa cheo na umri utaonekana katika matokeo muhimu na makubwa katika utendaji kazi.

"Mimi kuwa Naibu Waziri hapa So What... kama sitofanya kazi yenye matokeo makubwa kutokana na imani niliyopewa na Rais nitakuwa si lolote, hivyo kwa ushirikiano wenu pekee tutaweza kutimiza utendaji uliotukuka na wenye manufaa makubwa" Alikaririwa Mhe Biteko wakati akizungumza na watumishi wa Wizara ya Madini

Mhe Biteko alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli anafanya kazi nzuri kwa manufaa makubwa ya watanzania wote hivyo watumishi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo pasina kurudisha nyuma makusudi na matakwa ya utekelezaji wa ilani ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwaka 2015-2020.

Asubuhi siku ya Jumatatu Januari 8, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli alimuapisha Mhe Dotto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa madini, Ikulu Jijini Dar es salaam.